017-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kuondosha Munkari Kwa Mkono Au Ulimi Au Kuchukia Moyoni

 

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 17

 

Kuondosha Munkari Kwa Mkono Au Ulimi Au Kuchukia Moyoni

 

 

 

 

عن أبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيُّ (رضي الله عنه) قال: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم):  ((مَنْ رَأَى مِنْكُمْ مُنْكَرًا فَلْيُغَيِّرْهُ بِيَدِهِ فَإِنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَبِلِسَانِهِ فَإِنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَبِقَلْبِهِ وَذَلِكَ أَضْعَفُ الإيمَانِ)) رواه مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه) amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) anasema: ((Atakayeona munkari [uovu] basi aubadilishe kwa mkono wake, na asipoweza basi kwa ulimi wake, na asipoweza basi kwa moyo wake [achukizwe] na huo ni udhaifu wa Iymaan)) [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Wajibu wa Muislamu kuamrisha mema na kukataza munkari kwa hali yoyote ile. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفلِحُونَ ﴿١٠٤﴾

Na watokeze kutoka kwenu umati wa watu unaolingania kheri na unaoamrisha mema na unaokataza munkari. Na hao ndio waliofaulu. [Aal-‘Imraan (3: 104)]

 

Na pia Rejea: Aal-‘Imraan (3: 110), At-Tawbah (9: 71,  112), Al-Hajj (22: 41).

 

 

2. Kuamrisha mema na kukataza munkari ni jukumu la kila Muislamu na jamii, kwani ni fardhi kifaayah (ya kutosheleza). Walilaaniwa Ahlul-Kitaab wasiotimiza amri hii kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

لُعِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَىٰ لِسَانِ دَاوُودَ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ ۚ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوا وَّكَانُوا يَعْتَدُونَ ﴿٧٨﴾

Wamelaaniwa wale waliokufuru miongoni mwa wana wa Israaiyl kwa lisani ya Daawuwd na ‘Iysaa mwana wa Maryam. Hivyo ni kwa sababu ya kuasi kwao na walikuwa wakitaadi.

كَانُوا لَا يَتَنَاهَوْنَ عَن مُّنكَرٍ فَعَلُوهُ ۚ لَبِئْسَ مَا كَانُوا يَفْعَلُونَ ﴿٧٩﴾

Walikuwa hawakatazani munkari waliyofanya. Uovu ulioje waliyokuwa wakiyafanya. [Al-Maaidah (5: 78-79)]

 

 

3. Imesemwa na ‘Ulaama kuwa Hadiyth hii ni thuluthi ya Dini. Na imesemwa pia kuwa Uislamu wote umo humo, kwani vitendo katika Shariy’ah ima ni vyema vinavyowajibika kutendwa au vitendo vya munkari vinavyowajibika kujiepusha navyo. Na baadhi ya ‘Ulamaa wameona kwamba lau ingelikuwa fardhi za Kiislamu zaidi ya sita, basi mojawapo ingelikuwa ni kuamrishana mema na kukatazana maovu. Na wengine wameongezea katika nguzo za Kiislamu.

 

 

 

4. Muislamu hatakiwi kuchangia katika maovu, bali kusaidia katika mema na uchaji Allaah. Rejea: Al-Maaidah (5: 2).

 

 

 

5. Waislamu wako tofauti katika uwezo wa kukataza maovu.

 

 

6. Iymaan ziko katika daraja tofauti. Inaongezeka katika kumtii Allaah (سبحانه وتعالى) na inapunguka katika kumuasi Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

7. Muumin ni yule anayekataza maovu na asipoweza achukie kwa moyo wake au sivyo atakuwa katika hatari ya kupotoka, kupata adhabu na kutokukubaliwa du’aa yake. Hadiyth: ((Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, hakika mtaamrishana ma’ruwf [wema] na mtakatazana munkari [maovu], au Allaah Atakuleteeni adhabu, kisha mtamuomba wala Hatokuitikieni)) [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan]

 

 

 

Share