SWALI:
Assalama Aleykum
Namshukuru Alla Kwa Kutujaalia Kuipata Website Yenye Kutunyoosha Juu Ya Dini Yetu. Baraka Za Allah Ziwaendee Wote Wenye Kujihusisha Na 'website Hii'Kila Mmoja Kwa Kiwango Apendacho Allah.
Sual Langu Kwa Leo Ni Hili: - Nini Hekima Ya Kumswalia Mtume. Nahangaishwa Na Mawazo Yangu Kwamba Mtume Ni Mjumbe Wa Mnwenyeenzi - Mungu Na Ameshamtakasa Na Kila Ovu Na Ameshamwahidi Pepo Yake Kila Zuri Yeye Ni Kiongozi Huko Akhera. Ameshatakasika - Sasa Kwa Nini Tunahitaji Kumuombea-ombea Kila Wakati Na Wengine Hata Hatuna Kauli Njema Nini Kumtaja-taja Kipenzi Cha Allah. Nadhani Sisi Ndio Tuko Njia Panda, Hatujijui, Tunahitaji Kuombeana Kila Wakti.
Naomba Mafahamisho. Juu Ya Hekima Iliyopo.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kauli yako uliyosema kuwa Mtume (SwallaAllaahu 'alayhi wa aailihi wa sallam) ameshatakaswa na maovu na ameshaahidiwa Pepo na kadhalika, na kwamba sisi ndio tunaohitaji kuombeana yote hayo ni kweli kabisa. Lakini bila shaka umetatizwa kufahamu hikma ya kumswalia Mtume (SwallaAllaahu 'alayhi wa aailihi wa sallam). Kwa hiyo, tutakufahamisha kwa kadiri tunavyoelewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anajua zaidi.
Kwanza tutambue kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hatuhitaji sisi tumuombee au tumswalie Mtume (SwallaAllaahu 'alayhi wa aailihi wa sallam) ikiwa sisi hatutapenda kufanya hivyo. Bali sisi ndiye wenye kumhitaji Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa kutaraji Neema na Rehma Zake na kutupa fadhila kama hizo za kumswalia Mtume (SwallaAllaahu 'alayhi wa aailihi wa sallam). Kwa hiyo ikiwa tutampenda Mtume (SwallaAllaahu 'alayhi wa aailihi wa sallam) au hatutampenda, vile vile Mola wetu hatuhitaji sisi tumpende Mtume Wake kwani Yeye Mwenyewe pamoja Malaika Wake Wanampenda na wamekwishatangulia kumswalia kabla ya kutuamrisha sisi:
Anasema Allaah سبحانه وتعالى
((إِنَّ اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا))
((Hakika Allaah Anamteremshia Rehma Mtume; na Malaika Wake (wanamuombea du'aa kwa vitendo vizuri alivyovifanya), Enyi mlioamini! Mswalieni (Mtume - muombeeni Rehma) na muombeeni amani) [Al-Ahzaab: 56]
Sababu za kumswalia Mtume (SwallaAllaahu 'alayhi wa aailihi wa sallam) ni nyingi mno na zinaweza kuandaliwa katika makala na vitabu. Lakini tutafupisha kama ifuatavyo:
-
Kumswali Mtume ni kumtukuza Mtume wa mwisho
Kumswalia Mtume (SwallaAllaahu 'alayhi wa aailihi wa sallam) ni kumtukuza kwani yeye ndiye Mtume wa mwisho, na hii ni neema kwa Ummah wetu wa Kiislamu kujaaliwa kuwa yeye ndiye Mtume wetu. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametusifu kuwa sisi ni Ummah bora kabisa. Na bila ya Mtume (SwallaAllaahu 'alayhi wa aailihi wa sallam) tusingeliweza kupata uongofu kamili kwani ameletwa ili pia atufafanulie Qur-aan.
Na ikiwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Mwenyewe Amemtukuza kwa kumtofautisha na Mitume wengineo, hivyo basi kumswalia kwetu ni njia mojawapo ya kumtukuza. Tunaona kwamba Allaah amewaita Mitume wote wengine katika Qur-aan kwa majina yao, isipokuwa Mtume Muhammad (SwallaAllaahu 'alayhi wa aailihi wa sallam). Yeye Amemwita ima 'Ee Nabii' au ‘Ee Mtume’.
-
Kumswali Mtume Ni ibada kwetu
Kwa sababu ni amri kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama tulivyoona katika Aayah hiyo ya juu, na ndio maana tunamswalia mpaka kwenye Swalah zetu za fardhi na za Sunnah, bila ya kumswalia Swalah haikamiliki.
-
Rahma kwetu kupata fadhila na thawabu zaidi
Binaadamu kila siku ana makosa hata awe anafanya ibada vipi, kwa hiyo ni neema kwetu kuzidishiwa fadhila kwa kutekeleza vitendo vya Sunnah fulani ili kujiongezea thawabu na daraja ya Pepo kwani hakuna mtu asiyependa ziada ya neema.
-
Fadhila ya Kuswaliwa na Allaah سبحانه وتعالى mara kumi
عنْ عبد اللَّه بن عمرو بن العاص ، رضي اللَّه عنْهُمَا أنَّهُ سمِع رسُول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم يقُولُ : (( من صلَّى عليَّ صلاَةً ، صلَّى اللَّه علَيّهِ بِهَا عشْراً)) رواهُ مسلم
Imetoka kwa 'Abdullah ibn 'Amru ibn Al'Aasw رضي اللَّه عنْهُمَا kwamba kamsikia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم anasema, ((Atakayeniswalia Swalah moja Allaah Atamswalia mara kumi)) [Muslim]
Maana ya Swalah ya Allaah سبحانه وتعالى na Malaika Wake:
Swalah ya Allaah سبحانه وتعالى kwa waja Wake ni: Rahma na kuwasifu kwa malaika.
Swalah ya Malaika kwa waumini ni:
Du'aa na kuwaombea maghfirah.
-
Kupata daraja ya Pepo karibu naye Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :
عن ابن مسْعُودٍ رضي اللَّه عنْهُ أنَّ رسُول اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال : (( أَوْلى النَّاسِ بي يوْمَ الْقِيامةِ أَكْثَرُهُم عَليَّ صلاةً)) رواه الترمذي وقال : حديثٌ حسنٌ
Imetoka kwa ibn Mas'uud رضي اللَّه عنْهُ kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
amesema, ( (watu wa mwanzo kwangu (watakaokuwa karibu yangu) siku
ya Qiyaamah ni wale wanaoniswalia sana)) [At-Tirmidhy na kasema ni Hadiythi Hasan]
Vile vile kumuombea Du'aa, mfano du'aa baada ya adhaan ni fadhila kwetu kuwa atakayefanya hivyo atakuwa miongoni mwa atakayeombewa Shufaa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم siku ya Qiyaamah.
-
Kudhihirisha mapenzi yetu kwake
Muumini ni yule mwenye kumpenda khaswa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kabla ya kupenda chochote hata nafsi yake kwani ilipoteremka aya hii:
((النَّبِيُّ أَوْلَى بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنفُسِهِمْ))
((Nabii ni bora zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao)) [Al-Ahzaab:6].
'Umar رضي الله عنه alisema kuwa yeye anampenda Mtume kuliko chochote ila nafsi yake. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akamuambia 'Umar kuwa hadi ampende hata kuliko nafsi yake ndipo yatakapothibitika mapenzi yake, naye 'Umar akakubali kuwa anampenda kuliko hata nafsi yake. Kwa hiyo na sisi waumini tuwe na mapenzi makubwa ya kumpenda na dalili mojawapo ni kupenda kumswalia.
-
Kumswalia kwetu ni thawabu alizokwishaahidiwa.
Allaah سبحانه وتعالى Amekwishamuahidi Mtume Wake kuwa atapata malipo mengi yasiyokatika:
((وَإِنَّ لَكَ لَأَجْرًا غَيْرَ مَمْنُونٍ))
((Na kwa hakika wewe una malipo yasiyokatika)) [Al-Qalam: 3]
Mbali ya kuwa ni malipo yake kwa sababu ya utume wake na kufikisha ujumbe kwa tabu na maudhi, vile vile kumswalia kwetu kila siku kama katika Swalah kila mara na kuswaliwa na Umma mzima wa Kiislamu tokea utume wake hadi siku Qiyaamah ni mojawapo ya kuthibitisha kauli ya Allaah سبحانه وتعالى hiyo.
Mwisho kama ulivyosema kuwa sisi ndio tuliokuwa njia panda na tunaohitaji kuombeana, bila shaka tunahitaji kufanya hivyo, na kwa hiyo pia kumswalia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ni kutuzidishia uzito wa mizani zetu za mambo mema na kufanya nyepesi mizani za mambo maovu.
Wa Allaahu A'alam