Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
التَّخْيِيْرُ في الطَّلَاقِ
Talaka Kumpa Mke Chaguo La Kati Ya Kubaki Kwenye Ndoa Au Kujiendea Zake
01: Taarifu Yake Na Uhalali Wake:
Ni mume kumchaguzisha mkewe kati ya kubaki naye au mke afanye jambo fulani (na ndoa ivunjike). Ni kama kumwambia: "Chagua moja; ima uache kazi unayofanya tuendelee kuishi pamoja, au tuachane (uendelee na kazi yako)". Hapa mke anaweza akachagua moja ya hayo mawili.
Asili ya hili ni Kauli Yake Ta'aalaa:
"يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ إِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا فَتَعَالَيْنَ أُمَتِّعْكُنَّ وَأُسَرِّحْكُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا • وَإِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَالدَّارَ الْآخِرَةَ فَإِنَّ اللَّـهَ أَعَدَّ لِلْمُحْسِنَاتِ مِنكُنَّ أَجْرًا عَظِيمًا"
"Ee Nabiy! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka uhai wa dunia na mapambo yake, basi njooni nikupeni kitoka nyumba na nikuacheni huru, mwachano mzuri • Na ikiwa mnamtaka Allaah na Rasuli Wake na nyumba ya Aakhirah, basi hakika Allaah Amewaahidi wanawake watendao wema miongoni mwenu ujira adhimu". [Al-Ahzaab: 28-29]
Na kwa mujibu wa rai ya Jumhuwr ya 'Ulamaa, kumchaguzisha mke kati ya moja ya mawili hakuzingatiwi kuwa talaka.
Mke Akichagua Kubaki Na Mumewe:
Ikiwa mwanamke atachagua kubaki na mumewe na kuacha hiyo kazi kwa mfano au jambo jingine, basi hakuna kitu, na ndoa yao itaendelea kama kawaida. Hii ni rai ya 'Ulamaa wengi wakiwemo Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi'iy, Ahmad, Ath-Thawriy, Ibn Al-Mundhir na wengineo. Imesimuliwa pia toka kwa 'Umar, Ibn Mas-'uwd, Ibn 'Abbaas na 'Umar bin 'Abdul-'Aziyz. Dalili zao ni:
1- Hadiyth ya 'Aaishah (Radhwiya Allaah 'anhaa):
"خَيَّرَنَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَاخْتَرْنَا اللَّهَ وَرَسُولَهُ، فَلَمْ يَعُدَّ ذَلِكَ عَلَيْنَا شَيْئًا"
"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitukhiyarisha, nasi tukamkhitari Allaah na Rasuli Wake, na yeye halikuhesabiwa khiyarisho hilo kuwa talaka kwetu". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5262) na Muslim (1477)]
2- Toka kwa Masruwq, amesema:
"سَأَلْتُ عَائِشَةَ عَنِ الخِيَرَةِ فَقَالَتْ: خَيَّرَنا النَّبيُّ صلى الله عليه وسلم، أَفَكَانَ طلاقاً؟، فَقَالَ مَسْرُوْقٌ : مَا أُبَالي أَخَيَّرْتُها واحِدَةً أَوْ مِائةً، بَعْدَ أَنْ تَخْتَارَني"
“Nilimuuliza 'Aaishah kuhusu kuchaguzishwa kwao (kati ya kubaki na Rasuli au talaka), akasema: Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitupa chaguo. Je, unadhani chaguo hilo lilikuwa ni talaka?! (La hasha). Masruwq akasema: Kama ni hivyo, basi sijali tena ikiwa nimemkhiyarisha mke wangu mara moja au mara mia, baada ya kuchagua kubaki nami”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5263) na Muslim (1477)]