Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
التَّخْيِيْرُ في الطَّلَاقِ
Kumpa Mke Chaguo La Kati Ya Kubaki Kwenye Ndoa Au Kujiendea Zake
02: Mke Akiamua Kuachia Ndoa Yake, Je, Itakuwa Ni Talaka Moja Rejea, Au Talaka Mtengano"بَيْنُوْنَةٌ", Au Talaka Tatu?
Tumefahamu kutokana na Hadiyth hizo mbili za ‘Aaishah kwamba ikiwa mtu amemkhiyarisha mkewe, na mkewe akaamua kujitoa kwenye ndoa, basi hapo itakuwa ni talaka isiyohitajia mume kuitamka kwa tamko la talaka. Kwa muktadha huu, ‘Ulamaa wamekhitilafiana katika kauli tatu kuhusiana na talaka itakavyohesabika.
Kauli Ya Kwanza:
Itakuwa ni talaka moja rejea. Ni madhehebu ya Ash-Shaafi'iy na Ahmad. Imesimuliwa pia toka kwa 'Umar, Ibn Mas-'uwd, 'Aaishah, Jaabir, 'Abdullaah bin 'Amri na wengineo.
Kauli Ya Pili:
Itakuwa ni talaka mtengano (baain). Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, na pia ni kauli ya Ibn Shubrumah.
Kauli Ya Tatu:
Itakuwa ni talaka tatu kwa aliyeingiliwa. Ni madhehebu ya Maalik.
Ninasema:
“Kauli ya kwanza iko karibu zaidi na usahihi kuliko mbili zingine, ingawa linaloonekana katika aayah tukufu:
"إِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا فَتَعَالَيْنَ أُمَتِّعْكُنَّ وَأُسَرِّحْكُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا "
“Ikiwa mnataka uhai wa dunia na mapambo yake, basi njooni nikupeni kitoka nyumba na nikuacheni huru, mwachano mzuri”, ni kwamba kule tu yeye mke kuchagua kuondoka hakuwi ni talaka, bali ni lazima mume aitamke talaka, kwani Kauli Yake Allaah Ta'aalaa: “Basi njooni nikupeni kitoka nyumba na nikuacheni huru, mwachano mzuri”, inaashiria baada ya mke kufanya uamuzi wa kuachia ndoa.
Kwa muhtasari, mume kumchaguzisha mkewe hakuwi ni talaka, ni sawa mke akiamua kubakia au kuondoka mpaka mume atamke talaka. Ni msimamo wa Abu Muhammad bin Hazm, nao uko karibu zaidi na dalili iliyopo kwenye aayah.
Je, Ni Lazima Mke Atoe Uamuzi Wake Haraka Au Anaweza Kuutoa Baada Ya Muda?
Maswahaba, Taabi'iyna na 'Ulamaa wengi wanaona kwamba ni lazima mke atoe uamuzi wake hapo hapo, na kama hakuutoa wakati utakiwao, basi hatakuwa tena na khiyari baada ya hapo.
Hili linaashiriwa na 'Aaishah aliposema:
"لَمَّا أُمِرَ النَبِىُّ صلى الله عليه وسلم بِتَخْيِيرِ أَزْوَاجِهِ بَدَأَ بِي فَقَالَ: إِنِّي لَمُخْبِرُكِ خَبَرًا، فَلاَ عَلَيْكِ أَنْ لاَ تَسْتَأْمِرِي أَبَوَيْكِ، ثُمَّ تَلاَ هَذِهِ الآيَةَ: يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُلْ لأَزْوَاجِكَ إِنْ كُنْتُنَّ تُرِدْنَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا إِلَى قَوْلِهِ جَمِيلاً، فَقُلْتُ: أَفِي هَذَا أَسْتَأْمِرُ أَبَوَىَّ فَإِنِّي أُرِيدُ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ وَرَسُولَهُ وَالدَّارَ الآخِرَةَ، قَالَتْ: ثُمَّ فَعَلَ أَزْوَاجُ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم مِثْلَ مَا فَعَلْتُ"
"Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoamuriwa kuwakhiyarisha wakeze, alianza na mimi akiniambia: Mimi nitakueleza habari ya hakika, basi usiharakie (kufanya uamuzi) bali kwanza watake ushauri wazazi wako. Kisha akasoma aayah hii: "Ee Nabiy! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka uhai wa dunia na mapambo yake, basi njooni nikupeni kitoka nyumba na nikuacheni huru, mwachano mzuri“. Nikamwambia: Hili ni la kuwashauri wazazi wangu! Kwa hakika mimi ninamtaka Allaah na Rasuli Wake pamoja na Nyumba ya Aakhirah. Kisha ‘Aaishah akasema: Halafu wakeze Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakafanya kama nilivyofanya mimi (bila kuchelewa)". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (4786) na Muslim (1475)]