Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
طَلَاقٌ رَجْعِي
Talaka Rejea
17: Talaka Rejea "طَلَاقٌ رَجْعِي":
Hii ni talaka ambayo kwayo mume anaweza kumrejea mkewe katika kipindi chake cha eda bila ndoa mpya na hata bila ya ridhaa yake. Na hii inakuwa ni baada ya talaka ya kwanza au ya pili isiyo mtengano "بَائِنٌ"ikiwa mume atamrejea mkewe kabla ya kumalizika eda. Eda ikimalizika, basi talaka inakuwa ni talaka mtengano " بَائِنٌ", na mume hatakuwa na uwezo wa kumrejea mkewe ila kwa ndoa nyingine mpya na kwa mahari mapya.
Asili ya suala hili ni Kauli Yake Ta'aalaa:
"الطَّلَاقُ مَرَّتَانِ ۖ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ"
"Talaka ni mara mbili. Hivyo kuzuia kwa mujibu wa shariy’ah au kuachia kwa ihsaan". [Al-Baqarah: 229]
Muradi wa "Kuzuia kwa mujibu wa shariy'ah" hapa ni kumrejesha kwenye ndoa na kutangamana naye kwa wema.
Na Allaah Amesema:
"وَالْمُطَلَّقَاتُ يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ ثَلَاثَةَ قُرُوءٍ ۚ وَلَا يَحِلُّ لَهُنَّ أَن يَكْتُمْنَ مَا خَلَقَ اللَّـهُ فِي أَرْحَامِهِنَّ إِن كُنَّ يُؤْمِنَّ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ وَبُعُولَتُهُنَّ أَحَقُّ بِرَدِّهِنَّ فِي ذَٰلِكَ إِنْ أَرَادُوا إِصْلَاحًا"
"Na wanawake waliotalikiwa wabakie kungojea zipite hedhi (na twahara) tatu. Na wala si halali kwao kuficha Aliyoumba Allaah katika matumbo yao ikiwa wao ni wenye kumwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na waume zao wana haki kuwarejea katika muda huo ikiwa watataka suluhu". [Al-Baqarah: 228]
Tunapata kufahamu hapa kwamba waume wa wanawake waliotalikiwa, wana haki ya kuwarejea wake zao katika kipindi cha eda, lakini kwa sharti ya kutodhamiria kuwadhuru au kuwasumbua na kadhalika.
Na aayah hii tukufu inaonyesha wazi kwamba waume wote wa wanawake waliowataliki, wana haki ya kuwarejelea bila kuwepo tofauti kati ya talaka rejea "رَجْعِيْ" au talaka mtengano "بَائِن". Lakini katika mahala kwengine, Allaah Ta'aalaa Ameashiria kwamba talaka mtengano "بَائِن" haimruhusu mume kumrejea mkewe Aliposema:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا"
"Enyi walioamini! Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kujimai nao, basi hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu. Basi wapeni kitoka nyumba na waacheni huru, kwa mwachano mzuri". [Al-Ahzaab: 49]
Talaka kabla ya kumuingilia mke inakuwa talaka mtengano "بَائِن", kwani mwanamke anakuwa hana eda kwa mume. Kumrejea kunakuwa katika kipindi cha eda kabla haijamalizika (ikiwa aliingiliwa).
Nyuma tumeieleza Hadiyth ya Ibn 'Umar ambaye baada ya kumtaliki mkewe akiwa kwenye hedhi, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia 'Umar (baba yake) amwamuru amrejeshe.
Jopo la 'Ulamaa wote wanasema kwa sauti moja kwamba muungwana akimtaliki mkewe chini ya talaka tatu na mtumwa chini ya talaka mbili, basi wote wawli wana haki ya kuwarejea wake zao katika kipindi cha eda. Al-Mughniy (7/515), Al-Ifswaah (2/185) na Al-Badaai'u (3/181)]
Hikma Ya Uhalali Wa Talaka Rejea:
Bila shaka, iko haja kubwa ya kuwepo talaka hii, kwa kuwa mume anaweza kumtaliki mkewe (kutokana na sababu isiyo na uzito), kisha akaja kujuta kwa hatua hiyo kama Alivyoashiria Allaah Ta'aalaa Aliposema:
"لَا تَدْرِي لَعَلَّ اللَّـهَ يُحْدِثُ بَعْدَ ذَٰلِكَ أَمْرًا"
"Hujui. Huenda Allaah Atatokezesha jambo jingine baada ya haya". [At-Twalaaq: 01]
Na kabla ya kufikia hatua hiyo ya kujuta, anapata nafasi ya kuwahi mambo na kumrejea mkewe. Isingelikuwepo, basi ingebidi afunge ndoa mpya ambayo mwanamke anaweza akaikataa. Hivyo basi, talaka hii imewekwa kwa ajili ya kuyaweka mambo sawa kati ya wanandoa wawili. Ni hikma ya Kimola Aliyetukuka na Mbora kuliko wote katika kuweka hukumu ya mambo kwa ajili ya maslaha ya viumbe.