Skip to main content

11A-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha كتاب الفرق بين الزوجين - Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Talaka Kutengana Mke Na Mume: Hukmu Za Kimakalifisho Kwa Talaka (Ni Haramu, Ni Makruhu, Ni Mubaah, Ni Mustahabu, Ni Waajib?)

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

الطَّلَاقُ

Talaka

Alhidaaya.com 

02: Hukmu Za Kimakalifisho Kwa Talaka (Ni Haramu, Ni Makruhu, Ni Mubaah, Ni Mustahabu, Ni Waajib?)

Waislamu tokea enzi ya Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) wamekubaliana kwa itifaki moja kwamba talaka inaruhusiwa. Lakini hata hivyo, 'Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na hukmu za kimakalifisho kwa talaka.

Jumhuwr ya 'Ulamaa wanaona kwamba asili ya talaka ni jambo halali, lakini lililo bora ni kutoitoa isipokuwa kwa dharura au kwa sababu zisizoweza kuepukika.  Inaweza kutoka nje ya asili hii katika hali na mazingira tofauti. 

'Ulamaa wengineo wanaona kwamba asili yake ni marufuku, na inaweza kutoka nje ya marufuku hii katika hali na mazingira tofauti. Dalili yao ni Hadiyth ambayo ni dhwa'iyf isemayo:

"أَبْغَضُ الحَلَالِ إِلَى اللهِ الطَّلَاقُ"

"Halali inayochukiza zaidi kwa Allaah ni talaka".  [Hadiyth Dhwa'iyf.  Imechakatwa na Abu Daawuwd (2177- 2178), Al-Bayhaqiy (7/322), Ibn Abiy Shaybah (5/253) na wengineo.  Angalia Al-'Ilal cha Ibn Abiy Haatim (1/431), At-Takhliyswa (3/205) na Al-'Ilalul Mutanaahiyah (2/638)]

Pamoja na kukhitilafiana huku, Mafuqahaa hatimaye wamekuja kukubaliana kwamba talaka inaguswa na hukumu tano za kimakalifisho kwa mujibu wa mazingira na hali kama ifuatavyo:

1-  Inakuwa Haramu: 

Kama kumtaliki mke akiwa kwenye hedhi, au kumtaliki katika hali ya utwahara baada ya mume kumuingilia.  Hii ni talaka ijulikanayo kama talaka ya bid'a "طَلَاقُ البِدْعَةِ" (iliyokiuka sharia).  Uharamu wake umekubaliwa na wote.  Pia talaka inakuwa haramu endapo mume atahofia kuzini kama atamtaliki mkewe.

2-  Inakuwa Makruhu (Yenye Kuchukiza): 

Ni wakati mke na mume wanapokuwa wako vizuri katika ndoa yao bila matatizo yoyote.  Baadhi ya Mafuqahaa wanasema talaka katika hali hii inakuwa ni haramu. 

Ninasema:  "Ukaraha na uharamu, unaweza kutolewa dalili kwa Hadiyth ya Jaabir aliyesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

"إِنَّ إِبْلِيسَ يَضَعُ عَرْشَهُ عَلَى الْمَاءِ ثُمَّ يَبْعَثُ سَرَايَاهُ فَأَدْنَاهُمْ مِنْهُ مَنْزِلَةً أَعْظَمُهُمْ فِتْنَةً، فيَجِيءُ أَحَدُهُمْ فَيَقُولُ: فَعَلْتُ كَذَا وَكَذَا، فَيَقُولُ: مَا صَنَعْتَ شَيْئًا، قَالَ: ثُمَّ يَجِيءُ أَحَدُهُمْ فَيَقُولُ: مَا تَرَكْتُهُ حَتَّى فَرَّقْتُ بَيْنَهُ وَبَيْنَ امْرَأَتِهِ، قَالَ: فَيُدْنِيهِ مِنْهُ وَيَقُولُ: نِعْمَ أَنْتَ"‏ 

"Hakika Ibliys hukisimamisha kiti chake cha enzi juu ya maji (ya bahari), kisha hutuma vikosi vya askari wake.  Atakayekuwa na cheo kikubwa zaidi kwake ni yule atakayefitinisha zaidi watu. Atamjia mmoja wao atamwambia:  Nimefanya kadha wa kadha.  Atamwambia: Hukufanya kitu wewe.  Kisha atakuja mwingine na kumwambia:  Sikumwacha mpaka nikaweza kumtenganisha yeye na mkewe.  Hapo humkumbatia na kumwambia:  Wewe ndiye mwenye kazi nzuri zaidi kushinda wote".  [Hadiyth Swahiyh.  Muslim]

Toka kwa 'Amri bin Diynaar, amesema:

"طلَّقَ ابنُ عُمَرَ امْرَأَةً لَهُ، فَقَالَتْ لَهُ: هَلْ رَأَيْتَ منِّيْ شَيْئًا تَكْرَهُهُ؟ قَالَ: لا، قَالَتْ: فَفِيْمَ تُطَلَّقُ المَرْأَةُ العَفِيْفَةَ المُسْلِمَةَ؟ فَارْتَجَعَهَا" 

"Ibn 'Umar alimtaliki mkewe.  Mkewe akamuuliza:  Je, umeona lolote baya kwangu?  Akasema:  Hapana. Akamuuliza:  Ni kwa jambo gani mwanamke mtakasifu wa Kiislamu anatalikiwa? Akamrejea".  [Isnaad yake ni Swahiyh.  Imechakatwa na Sa'iyd bin Mansuwr katika Sunanih (1099)]

3- Inakuwa Mubaah (Kuitoa Au Kutoitoa Ni Sawa): 

Ni wakati inapohitajika kutolewa kutokana na tabia mbaya ya mke, au mume kupata madhara ya kuendelea kuishi naye, au kushindikana kupatikana malengo ya ndoa kati yao.

4-  Inakuwa Mustahabbu (Kuitoa Ni Vizuri Zaidi Kuliko Kutoitoa): 

Ni wakati mke anapozembea kutekeleza haki za Allaah zinazompasa kama swalah na mfano wake, na mume akawa hana uwezo wa kumlazimisha.  Au mke akawa hajatulia, kwa kuwa kuendelea kuishi naye ni doa kwa dini ya mume, mbali na uwezekano wa kumchafulia kitanda na kumzalia watoto wa nje.  Allaah Ta'aalaa Amesema:

"وَلَا تَعْضُلُوهُنَّ لِتَذْهَبُوا بِبَعْضِ مَا آتَيْتُمُوهُنَّ إِلَّا أَن يَأْتِينَ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ"

"Na wala msiwazuie kwa inda ili mpokonye baadhi ya vile mlivyowapa isipokuwa wakiwa wamefanya uchafu bayana".  [An-Nisaa: 19]

Tabia hizi tajwa zinaweza pia kuifanya talaka kuwa ni lazima.

5-  Inakuwa Ni Lazima: 

Ni kama kwa mume aliyemwapia mkewe kwamba hatomuingilia kwa miezi minne (akafanya "Iylaa" "إِيْلاءُ"), kisha akakataa kumrudia baada ya muda huo kumalizika. Hapa talaka inakuwa ni lazima, na hii ni kauli ya Jumhuwr ya 'Ulamaa.

Au talaka ya waamuzi wawili katika kuamua mgogoro kati ya mke na mume ikishindikana kuleta suluhu kati yao, na waamuzi wakaona kwamba talaka ndio suluhu ya mwisho.

Mume Ndiye Mwenye Mamlaka Na Talaka:

Allaah Ta'aalaa Amempa mume haki ya kumwacha mkewe likipatikana jambo lenye kuhitajia kufanya hivyo.  Hakuiweka talaka mikononi mwa mwanamke ingawa mwanamke huyu ni mshirika mkuu katika mkataba wa ndoa.  Na hii ni kwa ajili ya kulinda maisha ya ndoa, lakini pia kuepusha hatari ya kuvunjika ndoa haraka bila kutarajia.  Mwanaume alivyo kimaumbile, ana uwezo wa kukadiria matokeo ya maamuzi ya mambo, na yuko mbali kufanya vitendo vya papara au maamuzi ya kukurupuka.  Ama mwanamke, yeye zaidi anakuwa ni mwenye kutawaliwa na hisia na mihemko, na kama angekuwa na mamlaka ya kutoa talaka, basi talaka nyingi zingetolewa kwa mambo madogo madogo sana. 

Isitoshe, talaka hufuatiwa na gharama ambazo zinamfanya mwanaume kuvuta subira, lakini mwanamke anakuwa hapati madhara yoyote ya kimali kwa talaka.  Kwa picha hii, angekuwa hana simile katika kuitoa kutokana na hasira zake za haraka.

Talaka inaweza kutolewa na mtu mwingine kwa niaba ya mume, pia kadhi katika baadhi ya kesi kutokana na udharura.