Skip to main content

11A-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha كتاب الفرق بين الزوجين - Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Talaka Kutengana Mke Na Mume: Masharti Ya Talaka: Masharti Ya Mtoa Talaka

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

الطَّلَاقُ

Talaka

Alhidaaya.com 

03: Masharti Ya Talaka: Masharti Ya Mtoa Talaka:

Ili talaka iwe sahihi, ni lazima pawepo masharti yanayohusu pande zake tatu ambazo ni mume (mtoa talaka), mke (mpewa talaka) na tamko la talaka.

Masharti Ya Mume:

1-  Awe ni mume halali:

Ni lazima pawepo kati yake na mke anayemtaliki fungamano sahihi la ndoa.  Ikiwa atasema kwa mfano kabla ya kumwoa mwanamke:  “Nikimwoa fulani, nitakuwa nimemtaliki”, basi hilo halitozingatiwa.  Na hii ni kwa Hadiyth ya 'Amri bin Shu'ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake, amesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"لا نَذَرَ لابن آدَمَ فِيْمَا لا يَمْلِكُ، ولا عِتْقَ لَهُ فِيْمَا لا يَمْلِكُ، ولا طَلَاقَ لَه فِيْمَا لا يَمْلِكُ"

"Mwanadamu hawezi kuweka nadhiri kwa asichokimiliki, wala kuacha huru kwa asichokimiliki, wala kutoa talaka kwa asichokimiliki".  [Hadiyth Swahihy Lighayrihi.  At-Tirmidhiy (1181), Abu Daawuwd (2190) na Ibn Maajah (2047).  Ina Hadiyth nyingi wenza]

Hivyo basi, mwanaume hamiliki talaka isipokuwa baada ya kuwa mume wa mtu.  Na hii ni kwa Kauli Yake Ta'aalaa:

"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ

"Enyi walioamini!  Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki".  [Al-Ahzaab: 49]

2-  Awe amebaleghe:

Jumhuwr ya 'Ulamaa wanasema kwamba talaka ya mtoto mdogo haipiti, ni sawa akiwa ni mpambanuzi au la, kwa kuwa talaka ni jambo zito ambalo mtoto mdogo haruhusiwi kulibeba, na hata walii wake pia.  Na hii nii kwa Hadiyth ya 'Aaishah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"رُفِعَ اَلْقَلَمُ عَنْ ثَلَاثَةٍ: عَنِ اَلنَّائِمِ حَتَّى يَسْتَيْقِظَ، وَعَنِ المُبْتَلَى حَتّى يَبْرَأَ، وَعَنِ الصَّبِيِّ اَلصَّغِيرِ حَتَّى يَكْبُرَ"

"Kalamu imenyanyuliwa kwa watu watatu:  Kwa aliyelala mpaka azindukane, kwa mgonjwa wa akili mpaka arejee hali yake ya kawaida, na kwa mtoto mdogo mpaka abaleghe".  [Swahiyh Lighayrih:  Imechakatwa na Abu Daawuwd (4398) na Ibn Maajah (2041).  Ina Hadiyth wenza kwa Abu Daawuwd (4401) na Ahmad (1/116) kwa Sanad Swahiyh Mawquwf, lakini haifai kuwa Marfuw'u]  

Kwa muktadha huu, mtoto kwa vile hajawa mwajibishwa kisharia (mukallaf), talaka yake haikubaliki.

Lakini kwa upande wao, 'Ulamaa wa Kihanbali wanasema kwamba ikiwa mtoto ni mtambuzi, basi talaka yake inapita wakitegemea Hadiyth Marfuw'u isemayo:

"كُلُّ طَلَاقٍ جَائزٌ، إِلا طَلَاق المعْتُوهُ المغْلُوبُ على عَقْلِهِ"

"Talaka zote zinapita, ila talaka ya mlemavu wa akili aliyevurugikwa". [Swahiyh Mawquwf.  Imechakatwa kwa mfano wake na 'Abdulrazzaaq (7/78), Sa'iyd bin Mansuwr (1113) na Al-Bayhaqiy (7/359)]

Vile vile, yaliyosimuliwa toka kwa 'Aliy kwamba amesema: 

"اكْتُمُوا الصِّبْيَانَ النِّكَاحَ"

"Msizitangaze talaka za vijana wadogo".  [Isnaad yake ni dhwa'iyf.  Imechakatwa na Ibnu Abiy Shaybah (4/74)] 

Hadiyth hii inafahamisha kwamba watoto hao wanatakiwa wasiwataliki wake zao, na wanapowataliki, basi habari zifichwe ili kuzuia kukithiri talaka za vijana hao wadogo.  Maneno kama haya yamesemwa na Ibn Al-Musayyib, 'Atwaa, Al-Hasan, Ash-Sha'abiy na Is-Haaq.  Pia Sheikh wa Uislamu ameunga mkono kwa kauli yake isemayo:  "Lakini mtoto mpambanuzi, au mwendawazimu ambaye wakati mwingine anajitambua, kauli yake inazingatiwa wakati anapokuwa anajitambua".  [Majmuw'u Al-Fataawaa (33/108).  Angalia Al-Mughniy (7/116), Fat-hul Baariy (9/393), na Jaami'u Ahkaamin Nisaa (4/102-103)]

3- Awe na akili timamu:

Talaka ya mwendawazimu au taahira haipiti.  Chochote wanachokifanya hawa hakitambuliwi wala hakizingatiwi.  Na hili linaashiriwa na Hadiyth iliyotangulia ya 'Aaishah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"رُفِعَ اَلْقَلَمُ عَنْ ثَلَاثَةٍ: عَنِ اَلنَّائِمِ حَتَّى يَسْتَيْقِظَ، وَعَنِ اَلصَّغِيرِ حَتَّى يَكْبُرَ، وَعَنِ اَلْمَجْنُونِ حَتَّى يَعْقِلَ أَوْ يَفِيقَ"

"Kalamu imenyanyuliwa kwa watu watatu:  Kwa aliyelala mpaka aamke, kwa mtoto hadi abaleghe, na kwa mwendawazimu mpaka akili zikae sawa ".  

Na pia kwa Hadiyth ya Maa'iz wakati alipokiri mbele ya Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba amezini.  Rasuli alimuuliza:

"أَبِكَ جُنُوْنٌ"

"Je, uko sawa wewe?"  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Muslim (1695) na wengineo kutoka kwa Buraydah, na mfano wake kwa Al-Bukhaariy (5270), toka kwa Jaabir bila kutaja jina la mpokezi].    

Hadiyth inaonyesha kwamba linalotamkwa na mwendawazimu halizingatiwi wala matendo yake wala kauli zake.  Ni kama alivyosema nyuma kidogo 'Aliy bin Abiy Twaalib:

"كُلُّ طَلَاقٍ جَائزٌ، إِلا طَلَاق المعْتُوهُ المغْلُوبُ على عَقْلِهِ"

"Talaka zote zinapita, ila talaka ya mlemavu wa akili aliyevurugikwa". [Swahiyh Mawquwf.  Imechakatwa kwa mfano wake na 'Abdulrazzaaq (7/78), Sa'iyd bin Mansuwr (1113) na Al-Bayhaqiy (7/359)]

Mtoto, mwendawazimu na mlevi, wote hawa wako kundi moja na mlemavu huyu wa akili.

Mwendawazimu mkusudiwa hapa ni yule mwenye hali ya kudumu.  Ama yule ambaye hali inamjia muda, kisha inaondoka, halafu inarudi tena na kadhalika, huyu ikiwa atatoa talaka wakati hali yake haiko sawa, basi talaka haipiti, na akiitoa wakati hali iko sawa, basi itapita. 

'Ulamaa wamewaweka aliyelala, aliyepoteza fahamu, na aliyepatwa na mfazaiko kundi moja na mwendawazimu.