Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
الطَّلَاقُ السُّنِّيُّ والبِدعِيُّ
Talaka Ya Kisunnah Na Kibid'ah
04: Talaka Ya Kibid'ah: Hukmu Yake:
Hii ni ile inayokwenda kinyume na talaka ya Kisunnah, ni sawa iwe wakati wa kuitoa, au kwa idadi ya talaka anazozitoa mume.
Ikiwa atamtaliki mkewe akiwa kwenye hedhi, au akiwa twahara lakini akawa amemuingilia, au akamtaliki talaka tatu akiwa katika hali ya twahara, basi hii inakuwa ni talaka ya kibid'ah, nayo ni haramu, na mume mwenye kufanya haya anapata madhambi kwa mujibu wa kauli ya 'Ulamaa wote.
Hukmu Yake:
Je, Talaka Hii Inapita Mwanamke Akiwa Hedhini? Na Je, Inahesabiwa Talaka Moja?
'Ulamaa wote wamekubaliana kwamba talaka hii ni haramu na anayeitoa anapata madhambi, lakini wamekhitilafiana kuhusiana na kupita talaka hii au kutokupita wakati mke yuko hedhini katika kauli mbili:
Kauli Ya Kwanza: Talaka Inapita Na Inahesabiwa:
Ni kauli ya 'Ulamaa wote. Na hizi ndizo dalili walizozitoa:
1- Hadiyth ya Ibn ‘Umar iliyotangulia ya kumtaliki mkewe akiwa kwenye hedhi na Rasuli akamwamuru amrejee mkewe kupitia kwa baba yake:
"مُرْهُ فَلْيُرَاجِعْهَا"
“Mwamuru amrejeshe”. [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma mara kadhaa]
Walio kinyume na rai hii wamejibu wakisema: “Kuamuriwa Ibn ‘Umar amrejeshe mkewe hakuna maana kwamba talaka imepita, bali yeye kwa dhana yake alijua imepita, na hapo Rasuli akamwamuru amrejeshe mkewe kwenye hali ya kawaida iliyokuwepo”.
2- Toka kwa Anas bin Siyriyn, amesema: “Nilimsikia Ibn ‘Umar akisema:
"طَلَّقَ ابْنُ عُمَرَ امْرَأَتَهُ وَهِىَ حَائِضٌ، فَذَكَرَ عُمَرُ لِلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: لِيُرَاجِعْهَا. قُلْتُ تُحْتَسَبُ؟ قَالَ: فَمَهْ" .
“Ibn ‘Umar alimtaliki mkewe akiwa hedhini, na ‘Umar akaliulizia hilo kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye akamwambia: Mwamuru amrejeshe. Nikamuuliza (Anas kwa Ibn ‘Umar):: Je (talaka) imehesabika? Akajibu: Bila shaka, na kama haikuhesabika, itakuwa ni nini basi?!” [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5252) na Muslim (1471)]
3- Toka kwa Yuwnus bin Jubayr, amesema:
"سَأَلْتُ ابْنَ عُمَرَ عَنْ رَجُلٍ طَلَّقَ امْرَأَتَهُ وَهِيَ حَائِضٌ فَقَالَ: هَلْ تَعْرِفُ عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عُمَرَ؟ فَإِنَّهُ طَلَّقَ امْرَأَتَهُ وَهِيَ حَائِضٌ، فَسَأَلَ عُمَرُ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَأَمَرَهُ أَنْ يُرَاجِعَهَا ثُمَّ يَسْتَقْبِلَ عِدَّتَهَا . فَقُلْتُ لَهُ: فَيَعْتَدُّ بِتِلْكَ التَّطْلِيقَةِ؟ فَقَالَ: مَهْ أَرَأَيْتَ إِنْ عَجَزَ وَاسْتَحْمَقَ "
“Nilimuuliza Ibn ‘Umar kuhusiana na mtu ambaye amemtaliki mkewe akiwa kwenye hedhi. Akaniuliza: Je, unamjua ‘Abdullaah bin ‘Umar? Yeye alimtaliki mkewe akiwa kwenye hedhi, na ‘Umar akamuuliza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na hukmu ya hilo, naye (Rasuli) akamwambia amuamuru (mwanaye) amrejeshe mkewe, kisha asubiri wakati mwafaka. Nikamuuliza: Je, talaka hiyo imehesabiwa? Akajibu: Ndio, inahesabika! Hata kama alilemewa au akafanya upumbavu”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5258) na Muslim (1471)]
4- Hadiyth ya Ibn ‘Umar iliyo wazi zaidi kuliko zilizotangulia ambapo mwenyewe alisema (kuhusiana na yeye kumwacha mkewe akiwa hedhini):
"حُسِبَتْ عَلَىَّ بِتَطْلِيقَةٍ"
“(Kumtaliki mke wangu akiwa kwenye hedhi) kulihesabiwa talaka moja dhidi yangu”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5253)]
Na katika riwaayah nyingine, Ibn ‘Umar amesema:
.
"فَرَاجَعْتُهَا وَحَسَبْتُ لَهَا التَّطْلِيقَةَ الَّتِي طَلَّقْتُهَا"
“Nikamrejesha, na nikaihesabu talaka niliyoitoa kwake kuwa ni talaka moja (halali)”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Muslim (1471) na An-Nasaaiy (3391)]
Waliopinga kauli hii wamesema: “Hakuna kinachoeleza kwamba suala hilo liliwasilishwa kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Sasa je, ni nani alipitisha neno lake: “Ilihesabiwa talaka moja dhidi yangu”? Je, ni Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au (baba yake) ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa)? Au ni yeye mwenyewe Ibn ‘Umar aliyehesabu hivyo?” [Tahdhiybus Sunan (3/101-102)]
Al-Haafidh amejaribu kujibu pingamizi hili akisema: Uwezekano uko mbali sana wa kuhesabiwa hayo aliyoyasema Ibn ‘Umar na mtu mwingine asiye Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Inaingia vipi akilini Ibn ‘Umar kusema jambo (la kisharia) kwa rai yake, wakati yeye mwenyewe anaeleza kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichukizwa na kitendo chake (cha kumtaliki mkewe akiwa hedhini)? Na vipi asimshauri kuhusiana na hayo aliyoyafanya katika kisa chake alichokieleza?! [Fat-hul Baariy (9/266)]
Ninasema: Haya aliyoyaeleza Haafidh yanatiliwa nguvu na Hadiyth ifuatayo:
5- Toka kwa Naafi'u, toka kwa Ibn ‘Umar ambaye yeye:
"طَلَّقَ امْرَأَتَهُ وَهِىَ حَائِضٌ فَأَتَى عُمَرُ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَذَكَرَ ذلِكَ لَهُ فَجَعَلَهَا وَاحِدَةً"
“Alimtaliki mkewe akiwa kwenye hedhi, kisha ‘Umar akalieleza hilo kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Rasuli akaifanya talaka moja”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na At-Twayaalisiy (68), Ad-Daaraqutwniy (4/9) na Al-Bayhaqiy (7/326)]
Halafu yote haya yanatiliwa nguvu na fatwa ya Ibn ‘Umar katika Hadiyth hii ifuatayo:
6- "Ibn 'Umar alikuwa anapoulizwa na mtu aliyemtaliki mkewe akiwa hedhini humwambia:
"أَمَّا أَنْتَ طَلَّقْتَهَا طَلْقَةً وَاحِدَةً أَوِ اثْنَتَيْنِ، فَإِنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَمَرَهُ أَنْ يُرَاجِعَهَا ثُمَّ يُمْهِلَهَا حَتَّى تَحِيضَ حَيْضَةً أُخْرَى، ثُمَّ يُمْهِلَهَا حَتَّى تَطْهُرَ، ثُمَّ يُطَلِّقَهَا قَبْلَ أَنْ يَمَسَّهَا، وَأَمَّا أَنْتَ طَلَّقْتَهَا ثَلاثًا فَقَدْ عَصَيْتَ رَبَّكَ فِيمَا أَمَرَكَ بِهِ مِنْ طَلاقِ امْرَأَتِكَ، وَبَانَتْ مِنْكَ"
Ikiwa umempa talaka moja au mbili, basi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru (yeye Ibn ‘Umar) amrejeshe, kisha amsubirie mpaka apate hedhi nyingine, halafu angoje mpaka awe twahara, halafu amtaliki kabla hajamuingilia. Na ikiwa wewe umempa talaka tatu, basi utakuwa umemwasi Mola wako katika yale Aliyokuamrisha kuhusiana na kumtaliki mkeo ambaye ameshakuwa haramu kwako". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Muslim (1471) na An-Nasaaiy (6/213)]
Kauli Ya Pili: Talaka Katika Hedhi Haipiti Na Haihesabiwi:
Ni kauli ya Twaawuws, 'Ikrimah, Khallaas bin 'Amri, Muhammad bin Is-Haaq na Daawuwd bin Hazm. Pia ni madhehebu ya Ibn Taymiyah na mwanafunzi wake Ibn Al-Qayyim. Dalili walizozitoa ni:
1- Hadiyth ya Abu Az Zubayr kwamba alimsikia 'Abdulrahmaan bin Ayman mwachwa huru wa 'Urwah akimuuliza Ibn 'Umar:
"كَيْفَ تَرَى فِي رَجُلٍ طَلَّقَ امْرَأَتَهُ حَائِضًا؟ فَقَالَ: طَلَّقَ ابْنُ عُمَرَ امْرَأَتَهُ وَهِىَ حَائِضٌ عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، فَسَأَلَ عُمَرُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: إِنَّ عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عُمَرَ طَلَّقَ امْرَأَتَهُ وَهِىَ حَائِضٌ . فَقَالَ لَهُ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ " لِيُرَاجِعْهَا " . فَرَدَّهَا وَقَالَ " إِذَا طَهَرَتْ فَلْيُطَلِّقْ أَوْ لِيُمْسِكْ " .
“Unasemaje kuhusu mume aliyemtaliki mkewe akiwa hedhini? Akasema: Ibn 'Umar alimtaliki mkewe akiwa hedhini enzi za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam), na ‘Umar akamuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akimwambia: ‘Abdullaah bin ‘Umar amemtaliki mkewe akiwa hedhini (basi nini hukmu yake?). Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambie anieleze nimrejeshe mke, naye akamrejesha kwangu, na Rasuli akamwambia: Akitwaharika, ampe talaka, au abaki naye kwenye ndoa”. [Imechakatwa na Abu Daawuwd (2185) na wengineo. Sheikh wetu amezikusanya sanadi zake na kubainisha kasoro zake katika Jaami’u Ahkaamin Nisaa (4/42)]
2- Ibn Hazm amesimulia toka kwa Naafi'u toka kwa Ibn 'Umar kwamba alisema kuhusiana na mtu aliyemtaliki mkewe akiwa kwenye hedhi:
"لا يُعْتَدُّ بِذلِكَ"
"Kwa njia hiyo talaka haihesabiki". [Isnaad yake ni layyin. Imechakatwa na Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (10/163)]
3- Imepokewa toka kwa Twaawuws kwamba amesema:
"وَجْهُ الطَّلّاقِ أَنْ يُطَلِّقَهَا طَاهِرًا مِنْ غَيْرِ جِمَاعٍ وإِذَا اسْتَبَانَ حَمْلُهَا"
"Talaka sahihi ni mume kumtaliki mkewe akiwa twahara bila kumuingilia, au pale mimba inapothibiti". [Isnaad yake ni dhwa'iyf. Imechakatwa na 'Abdulrazzaaq katika Al-Muswannaf (10923)]
4- Imepokewa toka kwa Khullaas bin ‘Amri kwamba amesema kuhusiana na mtu ambaye amemtaliki mkewe akiwa hedhini:
"لا يُعْتَدُّ بِهَا"
"Talaka yake haihesabiki". [Isnaad yake ni dhwa'iyf. Imechakatwa na Ibn Hazm (10923)]
Kauli Yenye Nguvu Zaidi:
Kwa mujibu wa dalili zilizotolewa na makundi mawili, mwono wa Jumhuwr (Salaf na Khalaf) kwamba talaka inapita kwa mwanamke aliye kwenye hedhi, ndio mwono wenye nguvu zaidi. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
Na kwa muktadha huu, mwanamke akipewa talaka akiwa hedhini, ni lazima abaki katika hedhi yake mpaka atwaharike.
Je, Aliyetoa Talaka Ya Kibid'ah Ni Lazima Amrejeshe Mkewe?
Nyuma ishaelezwa kwamba Ibn 'Umar alipomtaliki mkewe akiwa hedhini, na kisha baba yake akaenda kumuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na hukmu ya hilo, Rasuli alimwambia:
"مُرْهُ فَلْيُرَاجِعْهَا"
"Mwamuru amrejeshe (mkewe)".
Amri hii au agizo hili kwa mujibu wa Abu Haniyfah, Ash-Shaafi'iy, Al-Awzaaiy na Ahmad, wao wameichukulia kama ni jambo linalopendeza tu kulifanya, na si wajibu.
Ama Maalik na wenye kumuunga mkono, wao wanasema ni amri ya lazima kwa mume ikiwa hedhi bado inaendelea. Ni kauli iliyoungwa mkono pia na 'Ulamaa wa Kihanafiy na Daawuwd Adh-Dhwaahiriy. Na kauli hii ndiyo inayowafikiana zaidi na uhalisia wa mambo, ndiyo inayohafifisha kosa kwa kuondosha athari ambayo ni eda, na kuondosha madhara ya kurefusha eda.