Skip to main content

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

الطَّلَاقُ المُنَجَّزُ والمُضَافُ والمُعَلَّقُ

Talaka Inayopita Hapo Hapo Inapotolewa, Talaka Inayofungamanishwa Na Wakati, Na Talaka Inayofungamanishwa Na Jambo Fulani 

Alhidaaya.com 

06:  Kumtaliki Mke Kwa Kusema “In Shaa Allaah” (Akipenda Allaah):

“In Shaa Allaah” kisharia, ni kufungamanisha jambo lolote na Matakwa au Mapendeleo ya Allaah Ta’aalaa.  Basi je, talaka itapita mume akimwambia mkewe: “Nimekuacha In Shaa Allaah (Akipenda Allaah)”?

‘Ulamaa wana mielekeo miwili katika suala hili:  [Ibn ‘Aabidiyn (3/366), Al-Qawaaniynul Fiqhiyyah (243), Mughnil Muhtaaj (3/302), Ar-Rawdhwat (8/96), Al-Mughniy (7/402) na Al-Fataawaa (35/284)]

Mwelekeo Wa Kwanza: 

Talaka haipiti.  Ni Madhehebu ya Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy na Ibn Hazm.  Dalili zao ni:

1-  “In Shaa Allaah” katika talaka inaingia ndani ya ujumuishi wa kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

"مَنْ حَلَفَ عَلَى يَمِينٍ فَقَالَ: إِنْ شَاءَ اللَّهُ، فَلَا حِنْثَ عَلَيْهِ" 

“Atakayesema In Shaa Allaah wakati anaapia kiapo, basi hawajibikiwi na kafara asipokitekeleza”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (6639) na Muslim (1654)]

Dalili yao hii imejibiwa kwa kuambiwa kwamba mwenye kumwambia mkewe: “Nimekuacha In Shaa Allaah”, inakuwa si kiapo, hivyo Hadiyth isibebeshwe isilohusika nalo.

2-  Yaliyosimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas ikiwa Marfuw’u, amesema:

"مَنْ قَالَ لامْرَأَتِهِ: أَنْتِ طَالِقٌ إِنْ شَاءَ الله، أَوْ غُلَامِهِ حُرٌّ إِنْ شَاءَ الله، أَوْ عَلَيْهِ المَشْيُ إِلَى بَيْتِ الله إِنْ شَاءَ الله، فَلَا شَيْىء عَلَيْه"

“Atakayemwambia mkewe:  “Nimekuacha Akipenda Allaah, au mtumwa wake uko huru Akipenda Allaah, au nitatembea kwa miguu kwenda Nyumba ya Allaah Akipenda Allaah, basi hawajibikiwi na chochote”.  [Imechakatwa na Ibn 'Uday katika 'Al-Kaamil" (1/338), na Al-Bayhaqiy kutoka kwake (7/361).  Angalia "Al-Irwaa (7/154)]

3- Allaah Ta'alaa Amesema: 

"وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ" 

"Na hamtotaka isipokuwa Atake Allaah Rabb wa walimwengu".  [At-Takwiyr: 29]

Ibn Hazm amesema:  "Sisi tunajua kwamba lau Allaah Ta'aalaa Angetaka kuipitisha talaka hii, basi Angeirahisisha itoke bila ya tamko la "In Shaa Allaah".  Hivyo basi ni sahihi kwamba Allaah Hakupenda itokee, na kwa ajili hiyo, Amemrahisishia msemaji kushurutishia talaka yake na Matakwa Yake Allaah”. 

4-  Imepokewa toka kwa Ath-Thawriy kuhusu mtu aliyemwambia mkewe: "Nimekuacha In Shaa Allaah Ta'aalaa", na Twaawuws na Hammaad wakajibu kwamba talaka haipiti.  [Imechakatwa na 'Abdulrazzaaq katika "Al-Muswannaf" (11326)]

Mwelekeo Wa Pili:

Talaka inapita, na kusema “In Shaa Allaah” hakuathiri chochote.  Ni madhehebu ya Maalik, Ahmad, Al-Layth, Al-Awzaaiy na Abu 'Ubayd.  Ni chaguo pia la Sheikh wa Uislamu.  Dalili zao ni:

1-  Yaliyosimuliwa toka kwa Ibn 'Abbaas kwamba amesema: 

"إذَا قَالَ الرَّجُلُ لامْرَأَتِهِ: أَنْتِ طَالِقٌ إِنْ شَاءَ اللهُ، فَهِيَ طَالِقٌ"

"Mtu akimwambia mkewe nimekuacha In Shaa Allaah, basi ameachika".  [Al-Albaaniy amesema kwenye "Al-Irwaa" (2071): "Sikuiona ikiwa imepokewa toka kwa Ibn 'Abbaas, bali imechakatwa na Ibn Abiy Shaybah toka kwa Hasan Al-Baswriy, na Isnaad yake ni Swahihy"] 

2-  Yaliyosimuliwa toka kwa Ibn 'Umar na Abu Sa'iyd ambao walisema: 

"كُنَّا مَعَاشِرَ أَصْحَابِ رَسُولِ اللهِ نَرَى الإِسْتِثْنَاءَ جَائِزًا فِي كُلِّ شَيْىءٍ إِلاّ العِتَاقَ والطَّلَاقِ"

"Tulikuwa sisi kundi la Maswahaba wa Rasuli wa Allaah tunaona kwamba kusema In Shaa Allaah kunajuzu katika kila jambo isipokuwa katika kuacha huru mtumwa au kumtaliki mke".  [Ibn Qudaamah ameitaja katika "Al-Mughniy"]

Ibn Qudaamah amesema:  “Hii ni nukuu ya ‘Ijmaa.  Na hata kama itakadiriwa kwamba ni kauli ya baadhi yao na hakujulikana mwingine yeyote aliyekhalifiana nao, basi itakuwa ni ‘Ijmaa”.