Skip to main content

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

الطَّلَاقُ المُنَجَّزُ والمُضَافُ والمُعَلَّقُ

Talaka Inayopita Hapo Hapo Inapotolewa, Talaka Inayofungamanishwa Na Wakati, Na Talaka Inayofungamanishwa Na Jambo Fulani 

Alhidaaya.com 

05: Akishurutisha Talaka Na Kufunga Ndoa Na Mwingine:

Mume akimwambia mkewe:  “Nikimwoa fulani, basi wewe umeachika”, kisha kweli akamwoa, basi talaka hiyo haipiti kwa mujibu wa rai ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad bin Hanbali na Sheikh wa Uislamu. [Rawdhwat At-Twaalibiyna (8/68), Muntahaa Al-Iraadaat (2/280) na Majmuw’ul Fataawaa (33/233)]

Kwa sababu Allaah Ta’aalaa Amesema:

"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ  "

“Enyi walioamini!  Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki”. [Al-Ahzaab: 49] 

Hapa Allaah Ta’alaaa Ametaja ndoa kwanza kabla ya talaka, kwa maana, ni lazima amwoe huyo fulani aliyemkusudia kwanza, kisha ndio amtaliki mkewe kwa sharti jingine atakalomwekea au bila sharti. 

Ibn ‘Abbaas aliulizwa kuhusu mtu anayesema:  “Nikimwoa fulani, basi yeye ameachika”, akasema:

"لَيْسَ بِشَيءٍ إِنَّمَا الطَّلَاقُ لِمَنْ مَلَكَ"

“Hakuna kitu, kwani talaka ni kwa aliyemiliki tu”.  [Imechakatwa na Al-Bayhaqiy katika “As-Sunan Al-Kubraa” (7/320)]

Toka kwa ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake, amesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"لَا نَذْرَ لِابْنِ آدَمَ فِيمَا لَا يَمْلِكُ، وَلَا عِتْقَ فِيمَا لَا يَمْلِكُ، وَلَا طَلَاقَ فِيمَا لَا يَمْلِكُ"

“Mwanadamu hawezi kukiwekea nadhiri kisicho milki yake, wala kumwacha huru mtumwa asiye wake, wala kumtaliki mwanamke ambaye si mkewe”.  Hadiyth Swahiyh Bituruqih.  [Imechakatwa na At-Tirmidhiy (1181), Abu Daawuwd (2190), Ibn Maajah (2047) na wengineo.  Ina Hadiyth wenza nyingi]