Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
طَلَاقٌ رَجْعِي
Talaka Rejea
32: Wakati Ambapo Talaka Inakuwa Ni Mtengano, Utengano Mkubwa "بَائِنٌ بَيْنُونَةٌ كُبْرَى"
Aina hii ya talaka inatokea ikiwa ni ya tatu kutokana na Kauli Yake Ta'aalaa:
"الطَّلَاقُ مَرَّتَانِ ۖ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ"
"Talaka ni mara mbili. Hivyo kuzuia kwa mujibu wa shariy’ah au kuachia kwa ihsaan". [Al-Baqarah: 229]
Na Kauli Yake:
"فَإِن طَلَّقَهَا فَلَا تَحِلُّ لَهُ مِن بَعْدُ حَتَّىٰ تَنكِحَ زَوْجًا غَيْرَهُ"
"Na akimtaliki (mara ya tatu), basi hatokuwa halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwengine". [Al-Baqarah: 230]
Hii ni itifaki ya 'Ulamaa.
Je, Talaka Inakuwa Mtengano, Utengano Mkubwa "بَائِنٌ بَيْنُونَةٌ كُبْرَى" Kama Mume Atatoa Talaka Tatu Kwa Mpigo?
Ni kama mume kumwambia mkewe: "Nimekuacha talaka tatu", au "Nimekuacha, nimekuacha, nimekuacha".
Suala hili ni mashuhuri, na 'Ulamaa wamekhitilafiana kwalo kwenye kauli tatu mashuhuri ambazo tutajaribu kuzitaja pamoja na dalili zilizotolewa na kila kundi na kuzihakiki kiasi tuwezavyo kutokana na umuhimu wa kadhia hii.
Kauli Ya Kwanza:
Ni talaka halali inayoruhusiwa na zinahesabiwa tatu. Ni kauli ya Ash-Shaafi'iy, na riwaayah ya kale toka kwa Ahmad na Ibn Hazm.
Kauli Ya Pili:
Ni talaka haramu, lakini zinahesabiwa tatu. Ni kauli ya Abu Haniyfah, Maalik, na riwaayah iliyokuja baadaye toka kwa Ahmad. Ni kauli pia iliyonukuliwa toka kwa Masalafi wa Kiswahaba na Taabi'iyna.
Makundi haya mawili yamelingana katika kuzingatia kwamba talaka zinakuwa ni tatu. Dalili zao ni:
1- Kauli Yake Ta'alaa:
"فَإِن طَلَّقَهَا فَلَا تَحِلُّ لَهُ مِن بَعْدُ حَتَّىٰ تَنكِحَ زَوْجًا غَيْرَهُ"
"Na akimtaliki (mara ya tatu), basi hatokuwa halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwengine". [Al-Baqarah: 230]
Wamesema: "Kwa muktadha wa aayah, talaka zikitolewa tatu kwa mpigo zinapita na hakuna njia ya kuzigawa".
Wanajibiwa: "Aayah hii Tukufu haina mahusiano ya kuhalalisha talaka tatu kwa mpigo au kwa kuzitenganisha. Inabainisha tu kwamba mwanamke aliyeachwa talaka tatu anaharamika kwa mume aliyemtaliki mpaka mwanamke aolewe na mtu mwingine".
2- Kauli Yake Ta'aalaa:
"الطَّلَاقُ مَرَّتَانِ"
"Talaka ni mara mbili". [Al-Baqarah: 229]
Wamesema: "Tumejua kwa mujibu wa muktadha wa aayah, kwamba talaka mbili zimekusanywa ndani ya mara moja ya mbili".
Wamejibiwa: "Kwamba makusudio si kuhesabu talaka zote ndani ya mara mbili, bali makusudio ni talaka ambayo mume anaimiliki ili aweze kumrejea mkewe kama walivyofasiri hivyo Jumhuwr ya 'Ulamaa".
3- Hadiyth ya Sahl bin Sa'ad kuhusiana na kisa cha kuapizana laana (kufanya "Li'aan" "لِعَانُ") kati ya 'Uwaymar Al-'Ajlaaniy na mkewe mbele ya Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam). Sehemu ya kisa inasema:
"فَلَمَّا فَرَغَا قَالَ عُوَيْمِرٌ: كَذَبْتُ عَلَيْهَا يَا رَسُولَ اللَّهِ، إِنْ أَمْسَكْتُهَا، فَطَلَّقَهَا ثَلاَثًا قَبْلَ أَنْ يَأْمُرَهُ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ".
"Walipomaliza (kuapizana laana), 'Uwaymar alisema: Ikiwa nitabaki naye, basi sitomtendea haki ewe Rasuli wa Allaah. Kisha akamtaliki hapo hapo talaka tatu kabla Rasuli hajamwamuru kufanya hivyo". [Imechakatwa na Abu 'Awaanah (3/200) na At-Twabaraany katika "Al-Kabiyr" (6/117). Kuna ulaini katika Sanad yake]
Wamesema: "Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakumkatalia kutoa talaka tatu kwa mpigo. Na kama ingekuwa haifai, basi asingemkubalia kufanya hivyo".
Wamejibiwa: "Madai haya hayana hoja ndanimwe. Kwa sababu mke baada ya kuapizana laana, anaharamika kwa mumewe milele. Na talaka hizi tatu hazikuongezea uharamu huo isipokuwa usisitizo na nguvu tu. Isitoshe, talaka hii imetolewa kwa mtu wa kando (ajnabiyya) ambaye ameshatengana na mumewe kwa sababu ya kuapizana".
Haya yanatiliwa nguvu na kauli ya Sahl katika riwaayah nyingine isemayo:
"فَطَلَّقَهَا ثَلاَثَ تَطْلِيقَاتٍ عِنْدَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَأَنْفَذَهُ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ "
"Akamtaliki talaka tatu, na Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akazipitisha". [Imechakatwa na Abu 'Awaanah (3/200), na At-Twabaraaniy katika Al Kabiyr (6/117)]
Inaonyesha kwamba alihitajia Rasuli apitishe hilo (ili apate kutulia roho).
4- Hadiyth ya Faatwimah bint Qays kwamba:
"أَنَّ زَوْجَهَا أَبَا حَفْصِ بْنَ الْمُغِيرَةِ الْمَخْزُومِيَّ طَلَّقَهَا ثَلاَثًا ثُمَّ انْطَلَقَ إِلَى الْيَمَنِ، فَانْطَلَقَ خَالِدُ بْنُ الْوَلِيدِ فِي نَفَرٍ، فَأَتَوْا رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي بَيْتِ مَيْمُونَةَ أُمِّ المُؤمنِيْنَ فَقَالُوا: إِنَّ أَبَا حَفْصٍ طَلَّقَ امْرَأَتَهُ ثَلاَثًا، فَهَلْ لَهَا مِنْ نَفَقَةٍ؟ فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: "لَيْسَتْ لَهَا نَفَقَةٌ وَعَلَيْهَا الْعِدَّةُ"
“Mumewe Abu Hafsw bin Al-Mughiyrah alimpa talaka tatu, kisha akasafiri kwenda Yemen. Na hapo hapo, Khalid bin Al-Waliyd akiwa na baadhi ya watu, alikwenda kwa Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa katika nyumba ya Mama wa Waumini Maymuwnah akamwambia: Hakika Abu Hafsw amemwacha mkewe talaka tatu. Basi je, anawajibikiwa kumpa matumizi? Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia: Hapana, mke hana tena matumizi ya kupewa, lakini ni wajibu wake kukaa eda". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Muslim (1480) na wengineo]
Na Hadiyth:
"أنَّ رَجُلاً طَلَّقَ امْرَأَتَهُ ثَلَاثًا، فَتَزَوَّجَت، فَطُلِّقَتْ، فَسَأَلَتْ رَسُولَ الله صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: أَتَحِلُّ للأَوَّلِ؟ قَالَ لا، حَتَّى يَذُوكَ عُسَيْلَتَهَا كَمَا ذَاقَ الأَوَّلُ"
"Kwamba mtu mmoja alimtaliki mkewe talaka tatu, na mke huyo akaolewa (na mtu mwingine), kisha akaachwa. Halafu mwanamke huyo akamuuliza Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama anaweza kuhalalika kwa mumewe wa awali, na Rasuli akamjibu kwamba haiwezekani mpaka (mume wa pili) aonje asali yake (amjimai kisawasawa) kama alivyoonja wa awali". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5261), Muslim (1433), An-Nasaaiy (6/148) na Abu Daawuwd (3209)]
Wamesema: "Katika Hadiyth mbili, Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakupinga wanaume kutoa talaka tatu".
Wamejibiwa: "Kwamba talaka tatu zilizotajwa kwenye Hadiyth, hazikuwa kwa mpigo, bali zilitolewa mbili za awali, kisha ikamaliziwa ya tatu kama ilivyotajwa katika baadhi ya riwaayah za Hadiyth zilizo kwa Muslim ambapo riwaayah moja inasema:
"فَأَرْسَلَ إِلَى امْرَأَتِهِ فَاطِمَةَ بنت قَيْسٍ بِتَطْلِيْقَةٍ كَانَتْ بَقِيَتْ مِنْ طَلَاقِهَا.."
"Akatuma kwa mkewe Faatwimah bint Qays talaka ya mwisho iliyokuwa imesalia". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5261), Muslim (1433), An-Nasaaiy (6/148) na Abu Daawuwd (2309)]
5- Yaliyosimuliwa:
"أنَّ رُكَانةَ بنَ عبدِ يزيدِ طَلَّقَ امرأتَهُ ألبتةَ، فأَخْبَر النبيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بذلكَ فقال: واللهِ ما أردتُ إلا واحدةً، فقال رسولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : واللهِ ما أردتَ إلا واحدةً؟ فقال رُكَانةُ: واللهِ ما أردتُ إلا واحدةً، فردَّها إليهِ رسولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ، فطَلَّقَهَا الثَّانيةَ في زمانِ عُمَرَ بنِ الخَطَّابِ والثَّالِثةَ في زَمَانِ عُثْمَانَ بنِ عَفَّانِ"
"Kwamba Rukaanah bin 'Abdu Yaziyd alimtaliki mkewe talaka tatu kwa mpigo, kisha akamweleza Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya hilo akimwambia: Naapa kwa Allaah, sikukusudia isipokuwa talaka moja tu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamkaririsha kiapo chake na kauli yake. (Rukaanah) akakariri tena: Naapa kwa Allaah, sikukusudia isipokuwa talaka moja tu. Hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamrejeshea mkewe. Halafu baadaye (Rukaanah) akaja kumtaliki talaka ya pili enzi za (Ukhalifa wa) 'Umar bin Al-Khattwaab, na ya tatu enzi za 'Uthmaan". [Hadiyth Dhwa'iyf Mudh-twarib. Ina mlolongo wa wapokezi wengi tofauti kwa Abu Daawuwd (2196-2206), At-Tirmidhiy (1177), Ahmad (1/265), 'Abdulrazzaaq (11334-11335), Al-Haakim (2/491), Al-Bayhaqiy (2/491) na wengineo]
Wamesema: "Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwapisha athibitishe kwamba alikusudia talaka moja badala ya tatu alizozitoa. Hivyo inaonyesha kwamba lau angekusudia talaka zaidi ya moja, basi zingepita".
Wamejibiwa: "Kwamba Hadiyth hii ni "Mudh-twarib", haifai. Imekosolewa na Maimamu kama Ahmad, Al-Bukhaariy na wengineo. Isitoshe, kwenye baadhi ya Asaaniyd zake pameelezwa kwamba:
"أَنَّهُ طَلَّقَهَا ثَلَاثًا فِيْ مَجْلِسٍ واحِدٍ، فَقَالَ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : فِيْ مَجْلِسٍ واحِدٍ؟ قَالَ: نَعَمْ: فَالَ: فَإِنَّمَا تِلْكَ وَاحِدَةٌ، فَأَرْجِعْهَا إِنْ شِئْتَ"
“Kwamba yeye alimtaliki talaka tatu kwa mpigo, na Rasuli akamuuliza: Kwa mpigo? Akajibu: Na'am. Akamwambia: Basi zote hizo zinahesabiwa talaka moja tu, hivyo unaweza kumrejesha ukipenda”. Na hii pia ni dhwa'iyf".
6- Yaliyosimuliwa toka kwa Ibraahiym bin 'Ubaydullaah bin 'Ubaadah bin As-Swaamit toka kwa Daawuwd bin 'Ubaadah toka kwa baba yake toka kwa babu yake, amesema:
"طَلَّقَ جَدِّي امرَأَةً لَه أَلْفَ تَطْلِيْقَةً، فَانْطَلَقَ أَبِيْ إِلَى رسول الله صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَذَكَرَ لَهُ ذلِكَ، فَقَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : ماتَّقَى اللهَ جَدُّكَ، أَمَّا ثَلَاثٌ فَلَهُ، وَأَمَّا تِسْعُمِائَة وَسَبْعَةٌ وَتِسْعُونَ فَعُدْوَانٌ وَظُلْمٌ، إِنْ شَاءَ اللهُ عَذَّبَهُ وإِنْ شَاءَ غَفَرَ لَهُ"
"Babu yangu alimtaliki mkewe talaka 1000, kisha baba yangu akaenda kwa Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumuuliza kuhusu kitendo hicho. Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Babu yako hakumcha Allaah. Ama talaka tatu, hizo ni haki yake. Ama 997, basi hizo ni uadui na dhulma. Allaah Akipenda Atamwadhibu, na Akitaka Atamsamehe". [Hadiyth Baatwil. Imechakatwa na 'Abdulrazzaaq (11339) na Ad-Daaruqutwniy (4/12)]
Wamejibiwa: "Hadiyth ni Baatwil, hivyo haifai kama hoja au dalili".
7- Yaliyosimuliwa toka kwa Mu'aadh:
"سَمِعْتُ رَسُولَ الله صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُوْلُ: يَا مُعَاذ، مَنْ طَلَّقَ لِلْبِدْعَةِ وَاحِدَةً أَوِ اثْنَتَيْنِ أَوْ ثَلَاثًا أَلْزَمْنَاهُ بِدْعَتَهُ"
"Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: Ewe Mu'aadh! Mwenye kutaliki kinyume na Sunnah (Sharia) talaka moja, au mbili, au tatu, basi tutamwajibishia ukiukaji wake". [Hadiyth Munkar. Imechakatwa na Ad-Daaraqutwniy (4/20)]
Wamejibiwa: "Hadiyth hii ni Baatwil, haifai kuwa dalili au hoja".
8- Toka kwa Mujaahid kwamba Ibn 'Abbaas aliulizwa kuhusiana na mtu ambaye amemtaliki mkewe talaka 100, akajibu (kumwambia mtu huyo):
"عَصَيْتَ رَبَّكَ وَفَارَقْتَ امْرَأَتَكَ"
“Umemwasi Mola wako, na mkewe umemwacha". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Ad-Daaraqutwniy (4/13-20), At-Twahaawiy (2/33), na Al-Bayhaqiy (7/337). Angalia Al-Irwaa (2056)]
Na katika tamshi jingine:
"يَكْفِيْكَ مِنْ ذلِكَ ثَلَاثٌ"
"Zinakutosha katika hizo (100) tatu tu".
Wamesema: "Fatwaa ya Ibn 'Abbaas inaonyesha kwamba mwenye kumtaliki mkewe talaka tatu kwa mpigo, basi mke anakuwa ameachika talaka mtengano, utengano mkubwa بَائِنٌ بَيْنُونَةٌ كُبْرَى"
Wamejibiwa: "Kwamba hii ni fatwa yake na rai yake. Lakini kwa upande wa pili, kumesimuliwa kwamba wakati wa enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam), talaka tatu zilikuwa zikihesabiwa kuwa moja. Hoja inayozingatiwa ni kwa kile alichokisimulia kikiwa Marfuw'u, na si rai yake binafsi wala fatwa zake kama ilivyobainishwa katika taaluma ya Usuwl"
9- Katika enzi ya 'Umar, 'Ijmaa ilikubaliana kuwa talaka tatu zinapita, na haikupata kuripotiwa kwamba kuna yeyote aliyekhalifu hilo wakati huo!!
Wamejibiwa: "Katika suala hili hakuna 'Ijmaa. Mvutano katika hili ni wa kale, na kauli kwamba talaka tatu zinazingatiwa kuwa moja, ilikuwa ni maarufu katika enzi za Abu Bakr na mwanzoni mwa enzi ya ukhalifa wa 'Umar”.
10- Allaah Ta'aalaa Amemmilikisha mume talaka tatu na Akampa pia mamlaka ya kuzitoa. Ikiwa atazitoa tatu kwa mpigo juu ya muktadha wa kwamba hilo linajuzu, basi atakuwa amefanya jambo lililoruhusiwa kwake. Na kama tutasema hilo ni haramu, basi sharia imempa mamlaka ya kuzitenganisha talaka kwa ajili ya kumpa nafasi. Hivyo basi, ikiwa atazitoa kwa mpigo, atakuwa amekusanya kile ambacho amepewa nafasi katika kukitenganisha, na kwa hivyo, hukmu yake itamlazimu kama vile ambavyo angezitenganisha.
Kauli Ya Tatu:
Ni talaka haramu, lakini zinahesabiwa kuwa moja tu rejea.
Imenukuliwa toka kwa kundi la Maswahaba wakiwemo Az-Zubayr bin Al-'Awwaam, 'Abdulrahmaan bin 'Awf, 'Aliy bin Mas-'uwd na Ibn 'Abbaas. Kadhalika, ni kauli ya Mataabi'iyna wengi na waliokuja baada yao wakiwemo Twaawuws na Muhammad bin Is-Haaq. Vile vile, kalisema hili Daawuwd Adh-Dhwaahiriy pamoja na baadhi ya wafuasi wa Abu Haniyfah, Maalik na Ahmad. Isitoshe, Shaykhul Islaam ameiunga mkono kauli hii pamoja na mwanafunzi wake Ibn Al-Qayyim. Dalili zao ni:
1- Kauli Yake Ta'aalaa:
"الطَّلَاقُ مَرَّتَانِ"
"Talaka ni mara mbili ". [Al-Baqarah: 229]
Aayah hapa inabainisha kwamba talaka rejea ambayo mume anakuwa ndanimwe ana haki ya kumrejea mkewe, ni mara mbili; talaka ya kwanza kisha ya pili.
Ni kama kumwambia mtu kwa mfano afanye tasbiyh mara mia. Mtu huyu ni lazima aseme: Subhaanal Laah, Subhaanal Laah, mpaka aikamilishe idadi anayotakiwa ya 100. Na lau atasema: Subhaanal Laah mara 100, basi atakuwa hajasabbih isipokuwa mara moja tu.
Hivyo basi, atakayemwambia mkewe: "Nimekuacha talaka mbili au tatu, au kumi au elfu, basi anakuwa hajamtaliki isipokuwa talaka moja tu.
Ama Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwambia Mama wa Waumini Juwayriyah:
"لَقَدْ قُلْتُ بَعْدَكِ أَرْبَعَ كَلِمَاتٍ لَوْ وُزِنَتْ بِمَا قُلْتِهِ لَوَزَنَتْهُنَّ: سُبْحَانَ الله وَبِحَمْدِهِ عَدَدَ خَلْقِهِ، وَرِضَا نَفْسِهِ، وَزِنَةَ عَرْشِهِ، وَمِدَادَ كَلِمَاتِهِ"
"Hakika nimesema baada ya kukuacha (hapo ulipokaa) maneno manne, lau kama yatapimwa kulinganisha na hayo uliyoyasema (muda wote uliokaa), basi yatayazidi kupindukia: Subhaanal Laah wabihamdihi, 'adada Khalqihi, wa Ridhwaa Nafsihi, wazinata 'Arshihi, wa midaada Kalimaatihi. [Ametakasika Allaah na Himdi zote njema ni Zake, kwa idadi ya Viumbe Vyake, kwa kiasi kinachokuwa sababu ya Yeye Kuridhia, kwa uzito wa 'Arshi Yake, na kwa wino wa Maneno Yake"]
Maana yake ni kwamba Yeye Subhaanahu, Anastahiki kusabihiwa kwa idadi ya vitu hivyo vyote, na si kwamba Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) amemsabbih kwa idadi hiyo.
Hivyo basi, mwenye kumtaliki mkewe akabadili umbo la kisharia kwa kuifanya talaka moja ndiyo sababu ya kutengana moja kwa moja kwa kuzikusanya tatu kwa pamoja, hawezi kuruhusiwa kufanya hivyo, kwa sababu, kufanya hivyo, ni kubadili Sharia ya Allaah na kuifuta baada ya kufariki kwa Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam). Hili halijuzu kabisa. Na kwa muktadha huu, talaka inakuwa ni moja tu; talaka rejea.
Wamejibiwa: "Ingawa kutoa talaka tatu kwa mpigo imekatazwa, lakini pamoja na hivyo, haizuii kupita kwake kama ilivyo "Dhwihaar "ظِهَارٌ" . Na Allaah Ameitaja "Dhwihaar "ظِهَارٌ"kwenye aayah tukufukama ni kauli isiyokubalika, ya kuchukiza na ya uongo, na hilo halikuzuia mkewe kuharamika kwake mpaka afanye kafara ambayo Allaah Amemwamuru.
Hivyo basi, haiwezekani talaka kuwekwa kipimo kimoja na "Dhwihaar" "ظِهَارٌ", kwani "Dhwihaar" yenyewe kiasili ni haramu na ni kosa ambalo sharia imeliwekea faini ambayo ni kafara kinyume na talaka.
["Dhwihaar "ظِهَارٌ" ni mume kumfananisha mkewe na mtu ambaye ni maharimu wake wa milele kama mama yake au dada yake kwa kumwambia kwa mfano: “Wewe nakuona kama mama yangu tu”]
2- Toka kwa Twaawuws toka kwa Ibn 'Abbaas, amesema:
"كَانَ الطَّلَاقُ عَلى عَهْدِ رَسُولِ الله صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَأَبِيْ بَكْرٍ وَسَنَتَيْنِ من خِلَافَةِ عُمَرِ، طَلَاقُ الثَّلَاثِ وَاحِدَةٌ، فَقَالَ عُمَرُ بن الخَطَّابِ: إِنَّ النَّاسَ قَدِ اسْتَعْجَلُوا في أَمْرٍ قَدْ كَانَتْ لَهُمْ فيْهِ أُنَاه فَلَوْ أَمْضَيْنَاهُ عَلَيْهِمْ، فَأَمْضَاهُ عَلَيْهِمْ"
"Katika enzi ya Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam), Ukhalifa wa Abu Bakr, na katika miaka miwili ya Ukhalifa wa 'Umar, talaka tatu zilikuwa zinahesabiwa moja. [Na watu walipozoea tabia mbaya ya kutumia tamko la talaka tatu], 'Umar bin Al-Khattwaab [aliwataka rai baadhi ya Maswahaba wakubwa kuhusiana na tabia hiyo] na kuwaambia: Watu wameliharakia jambo ambalo wamepewa nafasi ya kulifanya hatua kwa hatua, je, mnaonaje tulipitishe? (Wakakubaliana) naye akalipitisha". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Muslim (1472), Abu Daawuwd (2200) na An-Nasaaiy (6/145)]
Na katika tamko jingine lililopokelewa toka kwa Twaawuws ni kwamba Abu As-Swahbaa alimwambia Ibn 'Abbaas:
"هَاتِ من هَنَاتِكَ، أَلَمْ يَكُنِ الطَّلَاقُ الثَّلَاثُ عَلى عَهْدِ رَسُولِ الله صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَأَبِيْ بَكْرٍ وَاحِدَةٌ؟ فَقَالَ: قَدْ كَانَ ذلِكَ، فَلَمَّا كَانَ في عَهْدِ عُمَرِ تَتَابَعَ النَّاسُ في الطَّلَاقِ فَأَجَازَهُ عَلَيْهِمْ"
"Hebu tujuze tupate faida kutoka kwako. Hivi haikuwa enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Abu Bakr talaka tatu zinahesabiwa moja? Akasema: Naam, ilikuwa ni hivyo. Lakini katika enzi ya 'Umar, watu walianza tabia ya kujitamkia talaka ovyo ovyo, na yeye akapitisha amri ya kuhesabika talaka kama wanavyotamka". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Muslim (1472)]