Skip to main content

11B-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume: Talaka Rejea15-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume: Talaka Rejea: Talaka Ya Mtengano, Utengano Mkubwa

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

طَلَاقٌ رَجْعِي

Talaka Rejea 

Alhidaaya.com 

31: Talaka Ya Mtengano, Utengano Mkubwa "طَلَاقٌ بَائِنٌ بَيْنُونَةٌ كُبْرَى"

Hii ni ile ambayo mume hawezi kumrejea mtalaka wake, si katika kipindi cha eda wala baada ya kumalizika eda isipokuwa kwa ndoa mpya na kwa mahari mapya.  Lakini hii ni baada ya mtalaka wake kuolewa na mume mwingine, na mume huyo akamjimai kimwili, kisha mume huyo akamtaliki au akafariki na eda yake ikamalizika.

Masharti Ya Ndoa Ya Kumwezesha Mume Wa Awali Kuhalalikiwa Na Mkewe Baada Ya Talaka Mtengano, Utengano Mkubwa "طَلَاقٌ بَائِنٌ بَيْنُونَةٌ كُبْرَى"

1-  Ndoa ya mume wa pili iwe sahihi kidhahiri na kiundani:

Kuswihi kidhahiri ni kuwepo masharti yote ya kuwezesha ndoa kufungika.  Ndoa ikikosa masharti yake, basi itakuwa ni batili, na kwa hivyo mume hatopata uhalali wa kumwoa mtalaka wake, na hii ni kwa mujibu wa itifaki ya 'Ulamaa.

Ama kuswihi kiundani, ni kwamba huyo atakayemwoa awe na nia ya kweli na ya dhati ya kufanikisha malengo halisi ya ndoa kama vile kujenga naye familia, kupata watoto, na kuwa na kinga dhidi ya zinaa. Lakini kama atakusudia kumhalalishia mume wa awali, basi uhalalishaji huo ni batili. 

2-  Lazima mume wa pili amuingilie (amjimai):

Haitoshi tu kufunga naye ndoa sahihi bila kumjimai. Hii ni itifaki ya Jumhuwr ya Salaf na waliofuatia isipokuwa Ibn Al-Musayyib.  Na hivi ndivyo Sunnah inavyoeleza.

Toka kwa 'Aaishah (Radhwiya Allaah 'anhaa) kwamba:

نَّ امْرَأَةَ رِفَاعَةَ الْقُرَظِيِّ جَاءَتْ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَتْ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، إِنَّ رِفَاعَةَ طَلَّقَنِي فَبَتَّ طَلاَقِي، وَإِنِّي نَكَحْتُ بَعْدَهُ عَبْدَ الرَّحْمَنِ بْنَ الزَّبِيرِ الْقُرَظِيَّ، وَإِنَّمَا مَعَهُ مِثْلُ الْهُدْبَةِ‏.‏ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ‏لَعَلَّكِ تُرِيدِينَ أَنْ تَرْجِعِي إِلَى رِفَاعَةَ؟ لاَ، حَتَّى يَذُوقَ عُسَيْلَتَكِ وَتَذُوقِي عُسَيْلَتَهُ ‏"

“Mke wa Rifa-'at Al-Quradhwiy alikuja kwa Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Ewe Rasuli wa Allaah!  Hakika Rifa-'at ameniacha talaka tatu kwa mpigo, nami baada ya kuniacha, nimeolewa na 'Abdulrahmaan bin Az-Zubayr Al-Quradhwiy, naye ana mfano wa ncha ya nguo (dhakari yake imelegea, haisimami vizuri).  Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Inaonyesha unataka kurudi kwa Rifa-'at.  Hapana, huwezi kurudi, mpaka ('Abdulrahmaan) aonje asali yako (akuingilie kisawasawa) na wewe uonje asali yake (akufikishe kileleni)".  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (21639) na Muslim (1433)

Jumhuwr wanasema asali hapa ni utamu wa jimai unaopatikana kwa kuzamisha kichwa cha dhakari kwenye utupu hata bila ya kumwaga maji ya uzazi.

Jumhuwr ya 'Ulamaa wa Kihanbali wameshurutisha kwamba jimai ni lazima iwe wakati ufaao kisharia wa kuruhusika kufanya tendo.  Na lau atamuingilia akiwa hedhini, au kwenye nifasi, au akiwa amehirimia (hajji au 'umrah), basi haitoshelezi kumhalalisha mwanamke kwa mume wake wa awali.  Lakini lililo sawa ambalo Ibn Qudaamah amelikhitari, ni kwamba jimai kwenye hali kama hizo inatosha, kwa kuwa ladha ya jimai imepatikana, na inaingia kwenye ujumuishi wa Kauli Yake Ta'aalaa:

"حَتَّىٰ تَنكِحَ زَوْجًا غَيْرَهُ"

"Mpaka aolewe na mume mwengine".  [Al-Baqarah: 230]

[Yaani, aolewe ndoa sahihi kisharia na mume amuingilie jimai shibishi] 

Hukumu Na Athari Za Talaka Hii:

1- Ni athari zote zilizotajwa kwenye talaka mtengano, utengano mdogo "بَائِنٌ بَيْنُونَةٌ صُغْرَى"

2- Mwanamke hawi halali kwa mumewe wa awali mpaka aolewe na mume mwingine ndoa sahihi kama ilivyoelezwa, amuingilie jimai shibishi, kisha aachane naye kwa talaka au kifo, halafu akae eda na aimalize.

Faida:  Ndoa Ya Mume Wa Pili Inafuta Talaka Tatu:

Mwanamke akiolewa tena na mume wake wa awali baada ya kuachwa na mume wa pili na eda yake ikamalizika, basi mume huyu wa awali atamiliki mkononi talaka tatu mpya.  Hii ni itifaki ya 'Ulamaa.