Nabiy 'Iysaa (عَلَيْهِ السَّلام) Alisulubiwa?

 

Nabiy 'Iysaa (عَلَيْهِ السَّلام) Alisulubiwa? 

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalam Aleykum

 

Swali langu naomba mnisaidie ni kwamba eti Isa Bin Maryam alisulubiwa kweli? Na tafadhali kama inawezekana naomba aya inayohakikisha swala hii. Allaah Azidi Kutuongoza

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Hili kwa hakika ni jambo ambalo lipo wazi kabisa katika Uislamu na halina utata wowote. Allaah Aliyetukuka Anatuelezea dhahiri shahiri kuwa ‘Iysaa bin Maryam (‘Alayhis-salaam) hakuuliwa na Mayahudi wala hawakumsulubu. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

وَقَوْلِهِمْ إِنَّا قَتَلْنَا الْمَسِيحَ عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ رَسُولَ اللَّـهِ وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَـٰكِن شُبِّهَ لَهُمْ ۚ وَإِنَّ الَّذِينَ اخْتَلَفُوا فِيهِ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ ۚ مَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِلَّا اتِّبَاعَ الظَّنِّ ۚ وَمَا قَتَلُوهُ يَقِينًا ﴿١٥٧﴾بَل رَّفَعَهُ اللَّـهُ إِلَيْهِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا ﴿١٥٨﴾

Na kauli yao: Hakika sisi tumemuua Al-Masiyh ‘Iysaa mwana wa Maryam, Rasuli wa Allaah. Na wala hawakumuua wala hawakumsulubu lakini walishabihishiwa tu. Na hakika wale waliokhitilafiana katika hayo, kwa hakika wamo katika shaka nalo. Hawana ujuzi nalo kabisa isipokuwa kufuata dhana tu. Na kwa yakini hawakumuua. Bali Allaah Alimnyanyua Kwake. Na Allaah daima ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [An-Nisaa: 157-158]

 

Waislamu inapasa tuthibitishe 'Aqiydah yetu Swahiyh baada ya kupata maelezo na uongofu katika Qur-aan, tusiwe kama wengine wasioamini baadhi ya kauli za Allaah kwa kuleta shubuhaat na kubadilisha maana za Aayah. Wasioamini kuwa Nabiy ‘Iysaa alinyanyuliwa na Allaah ni wapotofu ambao wameshindwa kutambua dalili kadhaa zinazohusiana na kupandishwa kwake mbinguni akiwa hai kama zifuatazo:

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokwenda safari ya Israa Wal-Mi'raaj alikutana na Rusuli katika kila mbingu hadi mbingu ya saba. Hivyo alikutana na Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-salaam) akiwa katika mbingu ya pili akiwa pamoja na Nabiy Yahya bin Zakariyyah ('Alayhimas-salaam) akiwa ni binamu yake. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Nilikutana na ‘Iysaa bin Maryam. Alikuwa na umbo la wastani na uso wake ni mwekundu kama vile katoka kuoga…" [Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 4 Namba 647] Jibriyl alisema,  “Hawa ni Yahya bin Zakariyyah na ‘Iysaa  ('Alayhimus-salaam) wasalimie”, na Nabiy aliwasalimu na wote wawili walijibu salamu zake na wakamwambia, “Unakaribishwa Ee ndugu yetu Nabiy Mtukufu” na kisha wakamwombea du’aa njema.

 

Vile vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametuthibitishia kutokufa kwake hapo mwanzo hadi karibu na Qiyaamah ndipo atakapofariki:

 

وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا ﴿١٥٩﴾

Na hakuna yeyote katika Ahlil-Kitaabi ila atamwamini kabla ya kufa kwake. Na Siku ya Qiyaamah atakuwa shahidi juu yao. [An-Nisaa: 159]

 

Hii ni kwa maana atateremka kutoka mbinguni na kuja ardhini kubakika miaka arubaini atekeleze mas-ala mbali mbali. Matukio haya ni katika matukio makuu ya kusimama Qiyaamah. Kuteremka kwake Nabiy ‘Iysaa imeelezewa katika Hadiyth mbali mbali, tunanukuu hapa baadhi:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَة قَالَ : قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ   ((يَنْزِل عِيسَى اِبْن مَرْيَم فَيَقْتُل الْخِنْزِير وَيَمْحُو الصَّلِيب وَتُجْمَع لَهُ الصَّلَاة وَيُعْطِي الْمَال حَتَّى لَا يُقْبَل وَيَضَع الْخَرَاج وَيَنْزِل الرَّوْحَاء فَيَحُجّ مِنْهَا أَوْ يَعْتَمِر أَوْ يَجْمَعهُمَا))  أحمد

Kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesema: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((‘Iysaa mwana wa Maryam atateremka na kuua nguruwe, atavunja misalaba, ataimamisha watu katika Swalah ya Jama’ah, na kutoa mali hadi hakuna atakayetaka kupokea tena. Ataondosha jizya (kodi) na atakwenda Ar-Rawhaa ambako ataelekea kutekeleza Hajj, ‘Umrah au zote mbili)) [Ahmad]  

 

عن أبي هُرَيْرَة قَالَ : قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  ((كَيْف بِكُمْ إِذَا نَزَلَ فِيكُمْ الْمَسِيح اِبْن مَرْيَم وَإِمَامكُمْ مِنْكُمْ)) البخاري

Kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesema: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtakuwaje atakapoteremka Al-Masiyh, mwana wa Maryam (‘Iysaa) akiwa Imaam wenu ni miongoni mwenu wenyewe?)) [Al-Bukhaariy] 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَة أَنَّ النَّبِيّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ   ((الْأَنْبِيَاء إِخْوَة لِعَلَّات أُمَّهَاتهمْ شَتَّى وَدِينهمْ وَاحِد وَإِنِّي أَوْلَى النَّاس بِعِيسَى اِبْن مَرْيَم لِأَنَّهُ لَمْ يَكُنْ نَبِيّ بَيْنِي وَبَيْنه وَإِنَّهُ نَازِل فَإِذَا رَأَيْتُمُوهُ فَاعْرِفُوهُ رَجُل مَرْبُوع إِلَى الْحُمْرَة وَالْبَيَاض عَلَيْهِ ثَوْبَانِ مُمَصَّرَانِ كَأَنَّ رَأْسه يَقْطُر إِنْ لَمْ يُصِبْهُ بَلَل فَيَدُقّ الصَّلِيب وَيَقْتُل الْخِنْزِير وَيَضَع الْجِزْيَة وَيَدْعُو النَّاس إِلَى الْإِسْلَام وَيُهْلِك اللَّه فِي زَمَانه الْمِلَل كُلّهَا إِلَّا الْإِسْلَام وَيُهْلِك اللَّه فِي زَمَانه الْمَسِيح الدَّجَّال ثُمَّ تَقَع الْأَمَنَة عَلَى الْأَرْض حَتَّى تَرْتَع الْأُسُود مَعَ الْإِبِل وَالنِّمَار مَعَ الْبَقَر وَالذِّئَاب مَعَ الْغَنَم وَيَلْعَب الصِّبْيَان بِالْحَيَّاتِ لَا تَضُرّهُمْ فَيَمْكُث أَرْبَعِينَ سَنَة ثُمَّ يُتَوَفَّى وَيُصَلِّي عَلَيْهِ الْمُسْلِمُونَ))  أبو داود و أحمد

Kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesema: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Rusuli ni binamu, mama zao tofauti, lakini dini yao moja. Mimi ndiye mwenye haki zaidi kwa ‘Iysaa mwana wa Maryam kuliko yeyote mwengine, kwani hakukuwa na Nabiy baina yake na mimi. Atateremka na mtakapomuona mtamtambua. Ni mtu aliyeumbika vizuri, (rangi ya ngozi yake) baina nyekundu na nyeupe. Atateremka akiwa amevaa nguo mbili ndefu, rangi ya njano isiyokoza. Kichwa chake kitakuwa kina michirizi ya matone ya maji, japokuwa umande haukugusa. Atavunja misalaba, ataua nguruwe, ataondosha jizyah na atawaita watu katika Uislamu. Wakati huu, Allaah Ataangamiza dini zote isipokuwa Uislamu na Allaah Atamuangamiza Masiyh-Dajjaal. Usalama utajaa ardhini, hadi kwamba simba watachanganyika na ngamia, chui na ng'ombe, fisi na kondoo, watoto watacheza na nyoka na hawatowadhuru. ‘Iysaa atabakia muda wa miaka arubaini kisha atafariki, na Waislamu watamswalia Swaalah ya janaazah". [Abu Daawuud, Ahmad]

 

Dalili hizo pekee zinatutosheleza kukinaika kuamini kuwa Nabiy ‘Iysaa yu hai mbinguni na atarudi kuishi ardhini kisha ndio atafariki kama viumbe vinginevyo.

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share