Madhara Ya Kufuata Matamanio

 

Madhara Ya Kufuata Matamanio

 

Alhidaaya.com

 

 

Shukurani zote Anastahiki Allaah, Rabb wa ulimwengu wote. Rehma na amani zimshukie Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake na Swahaba wake.

 

Enyi Waislamu muogopeni Allaah kwa kadri Anavyopaswa kuogopewa.

Allaah Amesema,

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ

Enyi walioamini! Mcheni Allaah kama ipasavyo kumcha na wala msife isipokuwa nyinyi (mmeshakuwa) ni Waislamu. [Aal-'Imraan: 102]

 

Ucha Allaah ni dalili ya Iymaan. Kwani kwa ucha Allaah ndipo mtu anaweza kudumu katika njia iliyonyooka (iliyo sawa). Jueni kuwa muongozo sahihi ni muongozo wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Ubaya wa mambo yote ni uzushi, na kila uzushi ni uovu, na kila ovu linampeleka mtu motoni.

 

Enyi Waislamu! Allaah Amewaumba viume ili wamuabudu na wafungamane na Amri Zake na makatazo Yake. Allaah Anasema,

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

Na Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu. [Adh-Dhaariyaat :56]
 

Allaah pia Anasema,

 يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

Enyi watu! Mwabuduni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Al-Baqarah: 21]

 

Rusuli (‘Alayhim-salaam) hawakutumwa, wala Vitabu havikuteremshwa, wala Jannah na Moto havikuumbwa ila kwa ukweli huu mtukufu, wa kuwatoa watu kutoka kuabudu matamanio yao na kuwaleta katika kumuabudu Rabb wao Peke Yake. Wametakiwa kuamini upwekwe Wake, kutekeleza amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake katika vipengele vyote vya maisha. Wameamrishwa pia kurejea katika sharia Zake katika mambo yote na kujisalimisha katika maamuzi Yake katika hali zote. Vitabu vya Allaah na Sunnah za Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa pamoja vinakusudia lengo hili, ili mtu aweze kufanya matendo yale tu yanayomridhia Allaah. Iwapo mtu atakwenda kinyume na lengo hili, anatahadharishwa na adhabu hapa duniani na kesho Akhera. Allaah Anasema, 

 

أَلَا إِنَّ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ قَدْ يَعْلَمُ مَا أَنتُمْ عَلَيْهِ وَيَوْمَ يُرْجَعُونَ إِلَيْهِ فَيُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا ۗ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

Tanabahi! Hakika ni vya Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na ardhi. Kwa yakini (Allaah) Anajua mliyo nayo; na Siku watakayorejeshwa Kwake, Atawajulisha yale yote waliyoyatenda. Na Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi. [An-Nuwr :64]

 

Ndugu katika iymaan! Msingi wa kumuasi Allaah ni kufuata matamanio na kujisalimisha na matamanio ya kupita na starehe za muda. Allaah Anahesabu kufuata matamanio kuwa ni kinyume cha uongofu. Anasema,

 

أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ الْمُتَّقِينَ كَالْفُجَّارِ

Je, Tuwajaalie wale walioamini na wakatenda mema kama mafisadi katika ardhi? Au Tuwajaalie wenye taqwa kama waovu? [Swaad: 28]
 

Na Akasema, 

 

فَأَمَّا مَن طَغَىٰ ﴿٣٧﴾ وَآثَرَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿٣٨﴾ فَإِنَّ الْجَحِيمَ هِيَ الْمَأْوَىٰ ﴿٣٩﴾ وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ

 

عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٤٠﴾ فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَىٰ

Basi yule aliyepindukia mipaka kuasi. Na akahiari uhai wa dunia. Basi hakika moto uwakao vikali mno ndio makaazi yake. Ama yule aliyekhofu kisimamo mbele ya Rabb wake, na akaikataza nafsi yake na hawaa. Basi hakika Jannah ndio makaazi yake. [An-Naazi’aat: 37-41]

 

Allaah pia Anasema kuhusu Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),

 

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٣﴾ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

Na wala hatamki kwa hawaa. Hayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa. [An-Najm:3-4]

 

Inajulikana kutokana na uzoefu na ushahidi wa maandishi kuwa faida za dunia hii na zile za Akhera haziwezi kupatikana kwa kufuata matamanio na kujisalimisha na shauku bila kizuizi chochote. Kufanya hivyo kunapelekea machafuko (Shari’ah mkononi), mauaji, vita na maangamizi.

 

Enyi Waislam! Hakuwezi kuwa na Uislam wa kweli iwapo akili hazitojisalimisha na kukubali kikamilifu matakwa ya Allaah. Na Allaah Anasema,

 

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ

Sema: Hakika Swalaah yangu, na kuchinja kafaara na ‘ibaadah zangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu. Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza.  [Al-An'aam: 162-163]

 

Asili ya Uislam ni kujisalimisha kwa Allaah kwa utii, ina maana kusiwe na mashaka yoyote na kukubali kwa kuridhia maamuzi Yake na amri Zake katika vipengele vyote vya maisha. Huu ndio msingi wa Uislam. Yeyote atakaepinga sharia za Allaah kwa maoni yake hakujisalimisha kwa Allaah. Yeye ni mtumwa tu wa matamanio yake, na yeye ndie yule aliyetajwa kwa maneno ya Allaah,

 

أَفَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَـٰهَهُ هَوَاهُ وَأَضَلَّهُ اللَّـهُ عَلَىٰ عِلْمٍ وَخَتَمَ عَلَىٰ سَمْعِهِ وَقَلْبِهِ وَجَعَلَ عَلَىٰ بَصَرِهِ غِشَاوَةً فَمَن يَهْدِيهِ مِن بَعْدِ

 

اللَّـهِ ۚ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ

Je, umemuona yule aliyejichukulia hawaa zake kuwa ndio mwabudiwa wake, na Allaah Akampotoa juu ya kuwa na elimu na Akapiga mhuri juu ya masikio yake na moyo wake; na Akaweka kifuniko juu ya macho yake? Basi nani atamuongoa baada ya Allaah? Je, basi hamkumbuki? [Al-Jaathiyah: 23]

 

Allaah pia Anasema,

 

فَإِن لَّمْ يَسْتَجِيبُوا لَكَ فَاعْلَمْ أَنَّمَا يَتَّبِعُونَ أَهْوَاءَهُمْ ۚ وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّنِ اتَّبَعَ هَوَاهُ بِغَيْرِ هُدًى مِّنَ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ

 

الظَّالِمِينَ 

Na wasipokuitikia basi juwa kwamba hakika wanafuata hawaa zao. Na nani mpotofu zaidi kuliko yule aliyefuata hawaa zake bila ya Mwongozo kutoka kwa Allaah? Hakika Allaah Haongoi watu madhalimu. [Al-Qasas: 50]

 

Kujisalimisha katika matakwa ya Allaah katika mambo yote si msingi tu wa Uislam; bali pia ni sharti la iymaan ya kweli. Allaah Anasema,

 

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

Basi Naapa kwa Rabb wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao karaha katika yale uliyohukumu na wajisalimishe, kwa kujisalimisha kikamilifu. [An-Nisaa: 65]

 

Katika Hadiyth, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema, “Hatoamini mmoja wenu hadi yawe matamanio yake ni yale niliyokuja nayo”        

 

Enyi Waislam! Ingawa sharia za Kiislam na kanuni zake zinawafikiana na mahitaji ya binaadamu, shari'ah hizi hazitegemei shauku na matamanio ya binaadamu. Allaah anasema,

 

وَلَوِ اتَّبَعَ الْحَقُّ أَهْوَاءَهُمْ لَفَسَدَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ ۚ بَلْ أَتَيْنَاهُم بِذِكْرِهِمْ فَهُمْ عَن ذِكْرِهِم مُّعْرِضُونَ

Na lau kama haki ingelifuata hawaa zao; basi zingelifisidika mbingu na ardhi na waliokuwemo humo. Bali Tumewaletea ukumbusho wao lakini wao ni wenye kupuuza ukumbusho wao. [Al-Muuminuwn :71]

 

Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah anasema,

 

“Ni Kitabu tu kutoka mbinguni kinachoweza kutatua matatizo ya watu. Lau kama watu wangeachwa kufuata rai zao, basi kila mmoja kati yao bila shaka angekuwa na rai”

 

Ndugu wapenzi! Muislamu anaweza kuwa dhaifu, akampa shetani fursa ya kumlazimisha kufanya madhambi. Iwapo atatubia kutokana na madhambi hayo, Allaah Atamkubalia toba yake; lakini iwapo atakufa kabla ya kutubia Allaah Anaweza Akampa adhabu Akitaka au Akamsamehe Akitaka. Hii ni hali ya watu karibu wote. Wana Adam wote ni wafanya madhambi na waliobora katika wafanya madhambi ni wale wenye kutubia.

 

Mtu wa kulaumiwa anayestahiki tishio la adhabu ni yule mwenye majivuno, anayejadili kwa kukubaliana na madhambi na matamanio yake, anayepinga makatazo ya Allaah kwa maoni yake, anakusudia kuudhalilisha Uislam, anapiga vita akhlaaq zote zinazokwenda kinyume na matamanio yake na kukubaliana na mambo yote yanayopendzesha matamanio yake tu. Mtu huyu anafuata njia za wanafilosofia wa zamani kwa kukubaliana na anayoyataka na asiyoyataka tu katika matamanio yake mpaka akapotea katika giza la starehe na makosa, kama chombo kilichochanganyikiwahakitambui kipi kilicho kizuri au kukataa kilicho kibaya.

 

Shaykhul-Islaam ibn Taymiyyah amesema,

 

“Kufuata matamanio katika masuala ya dini ni kubaya zaidi kuliko kufuata mambo mengine ya starehe Hiyo ya mwanzo ilikuwa ndio hali ya wasioamini miongoni mwa washirikina. Hawa ndio wale waliokusudiwa na maneno ya Nabiy katika hadiyth iliyosimuliwa na Hudhayfah, “Kutakuwa na watu katika milango ya moto watakaowaita watu kuingia humo. Atakayeitikia wito wao, basi watamtupa kwenye moto. Nikasema, “Ee Rasuli wa Allaah, tujulishe kuhusu watu hao. Akasema: Sawa. Hao ni watu katika sisi na wanaozungumza lugha yetu.”

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia amesema, “Watu watazuka kutoka katika umma wangu ambao watakuwa wamejaa matamanio kama ugonjwa wa kuambukizwa na mnyama unavyozagaa mwili mzima na kuathiri mishipa na viungo vyote” [Abu Dawuud]

 

Ash-Shaatwibiy amesema,

 

“Kile wanachofanya ni kuwa wanafuata hukumu za akili zao tu na kushirikisha hayo na Shari’ah za Allaah katika kukubaliana au kutokubaliana na jambo. Iwapo wangesita hapo, mambo yangekuwa ni mepesi zaidi bali wamekiuka mipaka yote mpaka wakatangaza vita dhidi ya Allaah na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kukipinga kitabu cha Allaah na Sunnah za Nabiy Wake.”

 

Enyi Waislamu! Hakuna nafasi kwa akili ya mtu binafsi mbele ya ushahidi wa maandiko, na kunatakiwa kusiangaliwe mawazo ya yeyote mbele ya maamuzi ya Allaah na yale ya Nabiy Wake. Allaah anasema,

 

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ

 

ضَلَالًا مُّبِينًا 

Na haiwi kwa Muumini mwanamume na wala kwa Muumini mwanamke, Anapohukumu Allaah na Rasuli Wake jambo lolote, iwe wana hiari katika jambo lao.  Na anayemuasi Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amepotoka upotofu bayana. [Al-Ahzaab :36]

 

Kuonyesha kuchukizwa na Shari’ah ya Allaah na kutafuta Shari’ah nyingine kinyume na Zake kunafisidi amali. Allaah Anasema,

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَرِهُوا مَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ

Hivyo kwa sababu wao wamekirihika ambayo Ameteremsha Allaah, basi Amezibatilisha ‘amali zao. [Muhammad: 9]

 

Ibn Rajab anasema,

 

“Madhambi yanafanywa kwa sababu ya kupendelea matamanio zaidi kuliko mapenzi ya Allaah na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Uzushi katika dini ni matokeo ya kupendelea matamanio zaidi kuliko Shari’ah za Allaah, na hii ni hatari zaidi. Iwapo akili imeshazoeshwa matamanio, kuitoa akili hiyo nje ya matamanio ni kugumu"

 

Ndugu katika Iymaan! Allaah Ameumba mipaka katika  uwezo wa akili ya binaadamu. Haiwezekani kwa akili ya binaandamu kufahamu kila kitu kwa usahihi wake. Ujuzi wa kila kitu ni sifa maalumu  ya Allaah Peke Yake. Ufahamu wa binaadamu una kasoro na (binaadam) hawawezi kukubaliana na nadharia yoyote. Ndio sababu ukawaona wanaanza kufuata mawazo/rai fulani leo na wanaachana nayo kesho na kufuata mtazamo mwengine, na kesho kutwa wanahamia katika rai nyingine tofauti. Iwapo kila maamuzi yanayochukuliwa kwa akili za binaadamu ni sahihi kungekuwa na uhakika wa kutosha wa maisha mazuri ya watu wote katika dunia yao na Akhera yao, kusingekuwa na haja ya kutumwa Manabii na kusingekuwa na haja ya ujumbe mtukufu.

 

Imekuwa kwa hivyo ni lazima kwa Muislam kuwa macho katika kufuata njia ya hatari yenye makosa  ya kukataa sehemu yoyote ya maamrisho ya Allaah na kuchukizwa nayo au kupendelea zaidi matamanio na kujadili juu ya Shari’ah (Ya Allaah). Wafuasi wa Sunnah wamekubaliana ya kuwa yeyote anayefanya mambo yaliyokatazwa ambayo yako chini ya ushirikina, basi mtu huyo atachukuliwa kuwa hakuamini; na yeyote ataeyachukulia mambo yaliyokatazwa kuwa yanafaa – hata kama hayafanyi- mtu huyo hakuamini, iwapo mambo hayo yanaangukia katika mambo ambayo ni lazima yajulikane katika dini.

Waache wale wanaotafuta uongofu wasome maneno ya Allaah kwamba,

 

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa. [Al-An'aam: 153]

 

Enyi Waislamu! Mazingatio yamesifiwa kwa binaadamu. Kama si hivyo, kusingekuwa ni wajibu ulioamrishwa maalum juu ya binaadam. Allaah Ameelezea mazingatio ya binaadamu katika aya nyingi katika Kitabu Chake. Amemuamrisha binaadamu kufikiri na kufahamu. Yeye pia amefahamisha sababu mbali mbali katika Amri Zake nyingi Anamalizia kwa Kusema, “kwayo mpate kuwa na taqwa”.

      

Ingawa ni Allaah Mwenyewe Aliyeumba ufahamu kwa binaadamu, Amewafanya tofauti baina mmoja na mwengine. Ameumba hisia na matamanio ya kimaumbile ya binaadamu lakini Akaifanya Sharia iwe ni hakimu wa yote hayo, Yeye (Allaah) Anaweza kumuweka mtu katika mtihani. Yule atakayejisalimisha kwa Allaah peke yake ndie Muislam wa kweli ambaye anamtii Allaah na kwa hivyo, anastahiki Jannah. Lakini yule anayejivuna na akatumia akili na kuasi amri za Allaah, yeye ameahidiwa adhabu.

 

Wanachuoni wametaja tabia za watu wa matamanio na wale waliopendelea zaidi maoni yao juu ya Shari’ah sahihi za Kiislam na amri zake. Kuwa tabia hizi zilikuwepo kwa watu wa matamanio wa umma za mwamzo, na vile vile zipo kwa ummah wa mwisho.  Moja ya tabia hizi ni kufuata aya zisizo wazi (mutashaabihaatikatika Qur’aan. Allaah Anasema,

 

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا

 

تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ ۗ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا ۗ وَمَا

 

يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ

Yeye Ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu humo mna Aayaat zenye maana wazi, hizo ndio msingi wa Kitabu, na nyinginezo zisizokuwa wazi maana zake. Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu hufuata zile zisizokuwa wazi maana zake kutafuta fitnah (upotofu) na kutafuta maana zake zilofichika, na hakuna ajuae maana zake isipokuwa Allaah. Na wenye msingi madhubuti katika elimu husema: Tumeziamini,zote ni kutoka kwa Rabb wetu. Na hawakumbuki ila wenye akili. [Aal-‘Imraan: 7]

 

Tabia nyingine ya watu hawa ni kuwa wanawatukana Waislam wa mwanzo, kama Swahaba ambao wanajulikana (ni maarufu) kwa elimu yao na ucha Allaah wao na wameigwa na wale waliokuja baada yao. Watu wa matamanio wanasifu wale wanaokubaliana na shauku zao kama wanafalsafa.

 

Watu wa matamanio pia wanajulikana kwa kudharau amri za Uislam na kutojali kwao katika kuzipinga. Baadhi yao hata wamefikia kiwango cha kuzifanyia mzaha amri hizi na kuwafanyia mzaha wale waliofungamana na amri hizo na kuwatoa makosa na kuwalaumu.

 

Tabia nyingine ya watu wa matamanio ni kuwa wao hawafuati Sunnah katika matendo yao ya ibada, desturi zao na hali zao. Pamoja na hayo, utamuona mmoja wao akijifananisha na wanachuoni watukufu/maarufu wa Sunnah. Wao ni kama wale Allaah Aliowaeleza katika Qur’aan kama,

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يُجَادِلُ فِي اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَلَا هُدًى وَلَا كِتَابٍ مُّنِيرٍ ﴿٨﴾ ثَانِيَ عِطْفِهِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ لَهُ فِي الدُّنْيَا

 

خِزْيٌ ۖ وَنُذِيقُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَذَابَ الْحَرِيقِ ﴿٩﴾ ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ يَدَاكَ وَأَنَّ اللَّـهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ

Na miongoni mwa watu wako wanaobishana kuhusu Allaah bila ya elimu, wala mwongozo na wala Kitabu chenye Nuru. Mwenye kugeuza shingo yake kwa kibri ili apoteze (watu) njia ya Allaah. Atapata duniani hizaya, na Tutamuonjesha Siku ya Qiyaamah adhabu ya kuungua. (Ataambiwa): Hivyo ni kwa sababu ya yale yaliyotanguliza mikono yako; na kwamba Allaah si Mwenye kudhulumu waja. [Al-Hajj: 8-10]

                                                                                     

 

Ya Allaah! Zithibitishe nyoyo zetu katika dini na uwaongoze wale Waislamu waliokwenda upande.

 

Share