Inafaa Mwanamke Kuvaa ‘Abayah Zenye Vito Na Marembo Japokuwa Amejifunika Vizuri?

 

Inafaa Mwanamke Kuvaa ‘Abayah Zenye Vito Na Marembo Japokuwa Amejifunika Vizuri?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalamy Aleikum

 

Kwanza nawashkuru kwa ku2elimisha allaah subhana wa taala) atawalipa mimi nilikuwa naomba munifafanulie kuhusu vazi analotakiwa kuvaa mwanamke wakiislam je haya mabaibui 2nayoyavaa yanafaa je kati ya jilbab na haya mabaibui ambayo yana vito vinavyowaka pamoja mitandio mifupi naomba u2eleweshe mana vaz la baibui sasa limekuwa kama ni fashen nategemea majibu mazuri yatakayo2fundisha inshaalla

  

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Vazi la mwanamke Muislamu kuwa ni la sawa ni lazima litimize masharti kadhaa. Ikiwa vazi hilo litatimiza basi litakuwa la Kiislamu la, sivyo basi itakuwa mwanamke huyo amevaa nguo lakini si ya Kiislamu. Kabla ya kuingilia masharti, hebu tutazame Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anavyosema:

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾

Ee Nabiy! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Ahzaab 33: 59].

 

 

Tufahamu kuwa vazi hilo ni amri kutoka kwa Allaah Aliyetukuka, hivyo hatuwezi kuvaa tunavyotaka.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)  Anasema tena:

 

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ ...

Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao, na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au... [An-Nuwr: 31].

 

Ama kuhusu masharti kwa vazi la kike kuitwa la Kiislamu ni kama yafuatayo:

 

1.  Vazi la mwanamke wa Kiislamu ni lazima lisitiri mwili mzima: Wanachuoni wametofautiana kuhusu viganja vya mkono na uso kwa kauli mbili – wapo wanaosema ni lazima vifunikwe na wanaokubali kuwa vinafaa viachwe. Wengine wameunganisha kauli hizo kwa kusema hadi ya chini ni kuacha vitanga vya mkono na uso kuwa lakini vikifunikwa ni bora zaidi. Kuhusu kusitiri tayari tumenukuu aayah mbili – Suwrah Al-Nuwr Aayah ya 31 na Suwrah Al-Ahzaab Aayah ya 59.

 

2.     Vazi lenyewe lisiwe ni pambo: Hii ni kwa kauli ya Aliyetukuka: "wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika."  [An-Nuwr: 31). Na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Watu aina tatu hata usiwaulize: … Na mwanamke ambaye mumewe hayupo lakini amemtosheleza na mahitaji yake yote ya kidunia, naye akafanya Tabarruj" [Ahmad na al-Haakim]. Tabarruj ina maana mwanamke kuonyesha pambo lake na uzuri wake ambao unatakiwa usitiriwe, ambavyo vinamfanya mwanamme awe na matamanio. Na kusudio ya amri ya kuvaa Jilbaab ni kusitiri pambo la mwanamke, hivyo haingii akilini iwe Jilbaab lenyewe liwe ni pambo.

 

3.     Vazi liwe zito, kisionekane kilicho ndani yake: Hii ni kwa kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Watu aina mbili wa Ummah ni wa Motoni nami sijawaona… na wanawake waliovaa nguo lakini wapo uchi. Hao hawatoingia Peponi wala hawatopata harufu yake japokuwa harufu yake inafika masafa kadhaa na kadhaa” [Muslim]. Lengo ni kwa wale wanawake wanaovaa nguo hafifu ambayo inatoa sifa kamili na wala haisitiri. Hao kwa jina wamevaa lakini kwa uhakika wako uchi.

 

4.     Vazi liwe pana, sio la kubana: Kwani vazi likimbana mwanamke itamtoa umbile lake lote hivyo kumfanya kama kwamba hajajisitiri. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwambia Usaamah bin Zayd (Radhwiya Allaahu ‘anhuma): “Muamuru mkeo ajaalie Ghulaalah (shuka inayovaliwa chini ya nguo), kwani nakhofia isije ikasifu ukubwa wa mifupa yake” [Ahmad na Abu Daawuud].

 

5.     Vazi lisitiwe manukato: Hii ni kutokana na kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwanamke yeyote anayejitia manukato, akawapita mbele ya watu ili wapate harufu yake, basi yeye ni mzinifu” [Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy].

 

6.     Vazi lisifanane na vazi la Kiume: Huku ni kwa kule kulaaniwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wanaume wanaoshabihiana na wanawake na wanawake wenye kujifananisha na wanaume [al-Bukhaariy, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah]. Na pia amesema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelaaniwa mwanamme mwenye kuvaa nguo za kike, na mwanamke mwenye kuvaa nguo za kiume [Ahmad na Abu Daawuud].

 

7.     Vazi lisifanane na vazi la kikafiri: Shari’ah imekariri kutojuzu kwa Waislamu wanaume kwa wanawake kujifananisha na makafiri sawa katika ‘Ibaadah, au sherehe, au katika mavazi yao na kadhalika. Ama kuhusiana na kivazi, ni ile Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Amru (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) aliyesema: Alimuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amevaa nguo mbili za njano, akamwambia: “Hakika hizi nguo ni za makafiri kwa hivyo usivae” [Ahmad, Muslim na an-Nasaa’iy].

 

8.     Vazi lisiwe ni la kujionyesha: Hii ni kwa kauli yake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Mwenye kuvaa nguo ya umaarufu na kujionyesha hapa duniani, Allaah Atamvisha nguo ya udhalili Siku ya Qiyaamah, kisha Atamuingiza Motoni" [Abu Daawuud na Ibn Maajah].

 

 

Haya ndio masharti ambayo yanafaa yawepo katika vazi la mwanamke ili lijulikane kuwa ni la Kiislamu. Ikikosekana sharti hata moja basi litakuwa basi lenyewe ni la Kiislamu. Kwa ajili hiyo, ma ‘Abaaya mengi hayatimizi masharti haya wala yale mabaibui ya fesheni. Nasaha kwa dada zetu waepukane na hayo.

 

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Mwanamke Anavaa Hijaab Lakini Anavaa Suruwali Ya Kubana Anaposwali, Inakubaliwa Swalah Yake?

 

Kuvaa Niqaab Ni Fardhi? Nini Hukmu Ya Mwanamke Kuvaa Suruwali?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share