Kutoa Mimba Isiyotimia Mwezi, Yaani Kabla Haijapuliziwa Roho, Atakabiliwa Na Hukumu Ya Kuua? Na Ataweza Kusamehewa?

SWALI:

Asalam aleykum ndugu zangu waislamu natanguliza samahni kama kutakuepo usumbufu flani katika mpangilio wakuuliza swali

Mimi ni dada wa kiislam nataka kujua je mtoa mimba anasamehewa sababu niliwahi kusikia kama kuna hukmu yakuuwa kama kiumbe hakija fikisha mwezi yaani wiki tatu hapo kina kua hakija puliziwa pumzi je mtu akitoa uja uzito huo wawiki tatu tiari anakua na hukmu ya kuua au vipi nombeni mwanga zaidi.


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kutoa mimba.

Hakika ni kuwa Allaah Aliyetukuka Amekataza kutoa mimba au kuua kiumbe kwa hofu ya rizki. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuhimiza tuoane ili tupate kuzaana na kuwa wengi kwani kwa hilo atajifakharisha siku ya Qiyaamah.

Ni hakika isiyopingika kuwa mtoto anapokuwa tumboni kwa mama yake kwa muda wa siku arubaini, akiwa katika hali ya mbegu, baadaye tone la damu kwa muda kama huo, tena huwa ni kipande cha nyama kwa muda kama huo, tena hupelekwa  Malaika anayempulizia pumzi za uhai. Hivyo, roho inatiwa katika mwezi wa nne.

Hii haimanishi Uislamu umekubali kiumbe kitolewe kwenye tumbo la mama yake akiwa hajafika mwezi wa nne.

Hata kikiwa kiumbe kina siku moja tumboni, hairuhusiwi kabisa kukiua. Na mtu akifanya hivyo atapata madhambi makubwa ya kuua.

Kuna hali ambazo zimeruhusika kukitoa kiumbe tumboni kwa mama yake kikiwa amepuliziwa roho au bado kupuliziwa roho. Hali hiyo ni kikiwa kukua kwake kunakhatarisha maisha ya mama mzazi.

Ikiwa ulifanya kosa hilo inabidi urudi kwa Allaah Aliyetukuka uombe msamaha, uweke azma ya kutorudia kosa hilo, usilifanye tena kosa hilo na ujute katika kulifanya kosa hilo. Baada ya hapo ufanye mema mengi ili Allaah Aliyetukuka Akutazame kwa jicho la huruma na Akusamehe madhambi yako.

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo na manufaa zaidi:

Kutoa Mimba - Hukmu Na Kafara Yake

Kutoa Mimba Ikiwa Ikiachwa, Mtoto Atakuwa Mgonjwa Au Kufariki Baadaye

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share