Skip to main content

11C-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume: الطَّلَاقُ السُّنِّيُّ والبِدعِيُّ Talaka Ya Kisunnah Na Kibid'ah02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume: Talaka Ya Kisunnah Na Kibid'ah: Talaka Ya Kisunnah: Wakati Wa Kutolewa Kwake

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

الطَّلَاقُ السُّنِّيُّ والبِدعِيُّ

Talaka Ya Kisunnah Na Kibid'ah

Alhidaaya.com 

02: Talaka Ya Kisunnah: Wakati Wa Kutolewa Kwake:

Kama ilivyotaarifiwa, talaka ya kisunnah ni ile inayokwenda sambamba na Amri ya Allaah Ta'aalaa na amri ya Rasuli Wake (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam), na ikatolewa kwa njia iliyoruhusika kisharia.  Njia hii inahusiana na mambo mawili, nayo ni wakati wa kutolewa kwake na idadi ya talaka. Tutaanaza na wakati wa kutolewa kwake.

Kwanza: 

Kuhusiana Na Mwanamke Ambaye Ameingiliwa Na Mumewe Na Ni Katika Wanaopata Hedhi:

Ili talaka iwe ya kisunnah kwa mwanamke huyu, ni lazima pawepo masharti matatu:

La Kwanza:   Atalikiwe akiwa twahara, si wakati wa hedhi au nifasi.

La Pili:  Mume asiwe amemuingilia wakati akiwa twahara kabla ya kumpa talaka.

Allaah Ta'alaa Amesema:

"يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا الْعِدَّةَ"

"Ee Nabiy!  Mtakapowataliki wanawake, basi watalikini katika wakati wa eda (twahara) zao, na hesabuni barabara eda".  [At-Twalaaq: 01]

Makusudio ya aayah hii ni kwamba mume anatakiwa amtaliki mkewe akiwa katika hali ya utwahara bila ya kuwa amemuingilia.  Hili limesemwa pia na Ibn Mas-'uwd na Ibn 'Abbaas.

Toka kwa Naafi'u, Saalim na 'Abdullaah bin Diynaar toka kwa Ibn 'Umar (Radhwiya Allaah 'anhu):

"أَنَّهُ طَلَّقَ امْرَأَتَهُ وَهِىَ حَائِضٌ عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، فَسَأَلَ عُمَرُ بْنُ الْخَطَّابِ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنْ ذَلِكَ، فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: مُرْهُ فَلْيُرَاجِعْهَا، ثُمَّ لِيُمْسِكْهَا حَتَّى تَطْهُرَ ثُمَّ تَحِيضَ، ثُمَّ تَطْهُرَ، ثُمَّ إِنْ شَاءَ أَمْسَكَ بَعْدُ وَإِنْ شَاءَ طَلَّقَ قَبْلَ أَنْ يَمَسَّ، فَتِلْكَ الْعِدَّةُ الَّتِي أَمَرَ اللَّهُ أَنْ تُطَلَّقَ لَهَا النِّسَاءُ ‏"‏‏.‏

Kwamba yeye alimtaliki mkewe akiwa hedhini enzi ya Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kisha 'Umar bin Al-Khattwaab akamuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na hukmu ya kitendo hicho.  Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  “Mwamuru (mwanao) amrejeshe mkewe (katika ndoa) na akae naye mpaka atwaharike, halafu asubiri apate hedhi nyingine mpaka atwaharike. Kisha hapo, akitaka atabaki naye (kwenye ndoa yao), na akitaka atamtaliki kabla hajamuingilia.  Hiyo ndiyo eda ambayo Allaah Ameamuru kwayo wanawake waachwe”. [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5251-7160) na Muslim (1471)]. 

Hadith hii inafahamisha kwamba mume anatakiwa asubiri mpaka mke amalize hedhi nyingine baada ya hedhi ile ya awali ambayo alimpia talaka ndanimwe ili aruhusike kumtaliki. 

Lakini kwa upande mwingine, kuna wasimulizi wengi waliopokea toka kwa Ibn ‘Umar kwamba mume atasubiri mpaka mke atwaharike na hedhi aliyompia talaka, kisha hapo anaweza kumpa talaka.  Kati ya masimulizi hayo, ni yale yaliyopokewa toka kwa Yuwnus bin Jubayr toka kwa Ibn ‘Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

"أَمَرَهُ أَنْ يُرَاجِعَهَا فَإِذَا طَهُرَتْ فَأَرَادَ أَنْ يُطَلِّقَهَا فَلِيُطَلِّقَهَا"

“Alimwamuru amrejeshe mkewe, na mara hedhi inapokatika naye akataka kumtaliki, basi na amtaliki”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5258) na Muslim (1471)]

Kwa muktadha huu, ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na kusubiri hadi hedhi nyingine ya pili. 

Maalik na ‘Ulamaa wa Kihanbali wanaona kwamba ni lazima mume asubiri hadi hedhi nyingine ya pili ndio ampe talaka, na kama ataipitisha talaka kwenye hedhi hiyo ya awali, basi atakuwa amefanya jambo la haramu.  Sheikh wa Uislamu amekubaliana na rai hii.

Dalili yao wameitoa toka Hadiyth ya kwanza ya Naafi'u, Saalim na 'Abdullaah bin Diynaar toka kwa Ibn 'Umar ambayo ni:

"مُرْهُ فَلْيُرَاجِعْهَا، ثُمَّ لِيُمْسِكْهَا حَتَّى تَطْهُرَ ثُمَّ تَحِيضَ، ثُمَّ تَطْهُرَ، ثُمَّ إِنْ شَاءَ أَمْسَكَ بَعْدُ وَإِنْ شَاءَ طَلَّقَ قَبْلَ أَنْ يَمَسَّ، فَتِلْكَ الْعِدَّةُ الَّتِي أَمَرَ اللَّهُ أَنْ تُطَلَّقَ لَهَا النِّسَاءُ‏"

“Mwamuru (mwanao) amrejeshe mkewe (katika ndoa) na akae naye mpaka atwaharike, halafu asubiri apate hedhi nyingine hadi pale atakapotwaharika.  Kisha hapo, akitaka atabaki naye (kwenye ndoa yao), au atamtaliki kabla hajamuingilia. Hiyo ndiyo eda ambayo Allaah Ameamuru kwayo wanawake waachwe”.

Lakini kwa upande wa pili, Ahmad katika riwaayah ambayo As-Swan’aaniy ameinasibisha kwa Abu Haniyfah anaona kwamba kusubiri atwaharike na hedhi ya pili ni jambo linalopendeza (mustahabbu), na si lazima. Dalili yao wameitoa toka Hadiyth ya pili ya Yuwnus bin Jubayr toka kwa Ibn ‘Umar ambayo ni:

"أَمَرَهُ أَنْ يُرَاجِعَهَا فَإِذَا طَهُرَتْ فَأَرَادَ أَنْ يُطَلِّقَهَا فَلِيُطَلِّقَهَا"

“Alimwamuru amrejeshe mkewe, na mara hedhi inapokatika naye akataka kumtaliki, basi na amtaliki”. 

Ninasema:  “Hadiyth ya kwanza imesimuliwa na watu wanaoaminika zaidi toka kwa Ibn ‘Umar, wakati ya pili imesimuliwa na watu wengi zaidi.  Hivyo basi, inakuwa ni vigumu kuipa moja uzito zaidi kuliko nyingine.  Na kwa ajili hiyo, lililo bora itakuwa ni kuoanishwa kati yake kwa yale aliyoyaelezea Ibn Qudaamah katika “Al-Mughniy” akisema:

“Ikiwa atamrejesha, basi ni lazima amzuie mpaka amalize eda (atwaharike).  Na itakuwa ni vyema zaidi amzuie mpaka apate hedhi nyingine hadi ikatike”.  Maneno haya ya Ibn Qudaamah yanatiliwa nguvu na Hadiyth ya Ibn ‘Umar isemayo:

" مُرْهُ فَلْيُرَاجِعْهَا، ثُمَّ لْيُطَلِّقْهَا طَاهِرًا أَوْ حَامِلًا "

“Mwamuru amrejeshe, kisha amtaliki akiwa ametwaharika, au akiwa mja mzito”.  [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Muslim (1471), Abu Daawuwd (2181), An-Nasaaiy (6/141) na Ibn Maajah (2023)]

Hadiyth hii haijagusia mume asubiri hadi hedhi nyingine ya pili.  Halafu, uharamisho ulikuwa ni kutokana na mke kuwa hedhini, na anapotwaharika, basi uharamisho unakuwa haupo tena.  Hivyo basi, inaruhusika kumtaliki baada ya kutwaharika na hedhi hii ya kwanza, na hali kadhalika inayofuatia, na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

Faida:

Hekima ya kupendelewa kusubiri hedhi nyingine ya pili na kutwaharika nayo, ni kwamba muda wa kukaa naye utarefuka, na mume anaweza kumuingilia katika kipindi hicho na kujikuta anapoa na kusahau yaliyopelekea yeye kutoa talaka, na hivyo kuamua kuendelea kuishi na mkewe. 

La Tatu:  Asimtaliki -hedhi inapokata- ila baada ya mke kufanya ghusl  (kuoga josho la kujitwaharisha)

Katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar isemayo:

"مُرْ عَبْدَ اللَّهِ فَلْيُرَاجِعْهَا فَإِذَا اغْتَسَلَتْ فَلْيَتْرُكْهَا حَتَّى تَحِيضَ فَإِذَا اغْتَسَلَتْ مِنْ حَيْضَتِهَا الأُخْرَى فَلاَ يَمَسَّهَا حَتَّى يُطَلِّقَهَا فَإِنْ شَاءَ أَنْ يُمْسِكَهَا فَلْيُمْسِكْهَا فَإِنَّهَا الْعِدَّةُ الَّتِي أَمَرَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ أَنْ تُطَلَّقَ لَهَا النِّسَاءُ‏"

“Mwamuru ‘Abdullaah amrejeshe.  Na anapofanya ghusl, basi amwache mpaka apate hedhi nyingine.  Na anapofanya ghusl ya hedhi yake nyingine, basi asimguse mpaka atakapomtaliki.  Na kama atataka kuendelea kubaki naye, basi abaki naye, kwani huo ndio muda ambao Allaah ‘Azza wa Jalla Ameamuru mwanamke apewe talaka”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na An-Nasaaiy] 

Pili: 

Kuhusiana Na Mwanamke Ambaye Hakuingiliwa Na Mumewe:

Mtu akioa mwanamke na akawa hakumuingilia, ni sawa mwanamke akiwa ni mwenye kupata hedhi au asiyepata, basi anaruhusika kumtaliki wakati wowote anapotaka, akiwa twahara au akiwa kwenye hedhi.  Allaah Ta’alaa Amesema: 

"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا"

“Enyi walioamini!  Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kujimai nao, basi hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu”.  [Al-Ahzaab: 49] 

Tatu:

Kuhusiana Na Mwanamke Ambaye Hapati Hedhi Kutokana Na Umri Wake Mdogo Au Umri Mkubwa:

Mwanamke kama huyu, mumewe anaweza kumtaliki wakati wowote atakao, ni sawa akiwa amemuingilia au hakumuingilia, kwani mwanamke kama huyu eda yake inakuwa ni miezi mitatu, nayo inaanza kuhesabika wakati wowote atakaomtaliki, kwa sababu huyu hahesabu eda kwa twahara wala kwa ujauzito.  Allaah Ta’aalaa Amesema:

"وَاللَّائِي يَئِسْنَ مِنَ الْمَحِيضِ مِن نِّسَائِكُمْ إِنِ ارْتَبْتُمْ فَعِدَّتُهُنَّ ثَلَاثَةُ أَشْهُرٍ وَاللَّائِي لَمْ يَحِضْنَ"

“Na wale wanawake wanaokoma hedhi miongoni mwa wanawake wenu, mkiwa mna shaka, basi eda yao ni miezi mitatu, pamoja na wale wanawake wasiopata hedhi”. [At-Twalaaq: 04]

Hapa aayah inaashiria kwamba hawa hawana eda ya kuhesabu kwa twahara, bali watahesabu miezi mitatu tokea siku ya kupewa talaka.

Ikiwa atamuingilia binti mdogo ambaye bado hajapata hedhi, au mwanamke mkubwa aliyekatikiwa hedhi, kwa hawa talaka inaruhusiwa wakati wowote, kwa kuwa sababu ya kuharamishwa kutoa talaka wakati wa twahara baada ya kufanya naye tendo la jimai (kwa wanawake wenye kupata hedhi), ni uwezekano wa kupata mimba, kisha mume akajuta.  Na hali hii haipo kwa aliyekatikiwa na hedhi au binti mdogo ambaye bado hajapata hedhi hata kama wataingiliwa. 

Nne: 

Kuhusiana Na Mjamzito Ambaye Mimba Yake Imethibiti:

Huyu pia mumewe anaruhusiwa kumtaliki wakati wowote atakao kutokana na yafuatayo:

1-  Kauli Yake Ta'alaa:

"وَأُولَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ"

“Na wenye mimba muda wao (wa eda) watakapozaa mimba zao”.  [At-Twalaaq: 04]

Allaah Ta'alaa Amekufanya kuzaa kuwa ndiyo mwisho wa eda ya mjamzito, na muda wa kuzaa unakuwa haujulikani kutokana na kutofautiana kila mwanamke na mwingine, na hivyo basi imekuwa haiwezekani kuainisha wakati maalumu ambao mjamzito anaweza kutalikiwa.

2-  Hadiyth ya Ibn 'Umar ambaye alimtaliki mkewe akiwa kwenye hedhi, na baba yake (‘Umar) akamuuliza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya hukmu ya kitendo hicho, na Rasuli akamwambia: 

" مُرْهُ فَلْيُرَاجِعْهَا، ثُمَّ لْيُطَلِّقْهَا طَاهِرًا أَوْ حَامِلًا "

“Mwamuru amrejeshe, kisha amtaliki akiwa ametwaharika, au akiwa mja mzito”.  [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Muslim (1471), Abu Daawuwd (2181), An-Nasaaiy (6/141) na Ibn Maajah (2023)]

Al-Khattwaabiy amesema:  “Ndani ya Hadiyth hii kuna ubainisho kwamba mume akimtaliki mkewe akiwa mjamzito, basi anamtaliki Kisunnah, na mume anaruhusiwa kumtaliki wakati wowote wa ujauzito huo.  Na hii ndio kauli ya ‘Ulamaa wote”.  [Maalim As Sunan (6/163).  Chapisho la Maktabatul ‘Ilmiyyah]

3- Imehadithiwa (katika simulizi dhwa’iyf) toka kwa Ibn 'Abbaas kwamba amesema:

"الطَّلاقُ عَلَى أَرْبَعَةِ مَنَازِلَ : مَنْزِلانِ حَلالٌ ، ومَنْزِلانِ حَرَامٌ ، فَأَمَّا الْحَرَامُ فَأَنْ يُطَلِّقَهَا حِينَ يُجَامِعَهَا لا يَدْرِي أَيَشْتَمِلُ الرَّحِمُ عَلَى شَيْءٍ أَمْ لا ؟ وأَنْ يُطَلِّقَهَا وهِيَ حَائِضٌ ، وأَمَّا الْحَلالُ فَأَنْ يُطَلِّقَهَا لأَقْرَائِهَا طَاهِرًا عَنْ غَيْرِ جِمَاعٍ ، وأَنْ يُطَلِّقَهَا حَامِلا مُسْتَبِينًا حَمْلُهَا "

"Talaka ina ngazi nne:  Ngazi mbili halali, na ngazi mbili haramu.  Ama mbili zilizo haramu, ni mume kumtaliki mkewe baada ya kumjimai huku akiwa hajui kama mimba imeingia kwa jimai hiyo au la, na kumtaliki akiwa kwenye hedhi.  Ama mbili zilizo halali, ni kumtaliki akiwa twahara bila kumuingilia, na kumtaliki akiwa mjamzito mimba ikiwa imethibiti".  [Dhwa'iyf.  Imechakatwa na 'Abdulrazzaaq (6/303), Ad-Daaraqutwniy (4/5-37), na Al-Bayhaqiy (7/325), lakini maana yake ni sahihi] 

4- Mume anayemtaliki mkewe ambaye ujauzito wake umethibiti, anamtaliki huku akili yake ikiwa makini, imetulia.  Hahofii jambo ambalo linaweza kujitokeza na kujadisisha majuto ya kutoa talaka.  Kadhalika, mwanamke naye anakuwa hana shaka kwa upande wa eda yake kutokana na uhakika wa mimba yake.