Skip to main content

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

الطَّلَاقُ المُنَجَّزُ والمُضَافُ والمُعَلَّقُ

Talaka Inayopita Hapo Hapo Inapotolewa, Talaka Inayofungamanishwa Na Wakati, Na Talaka Inayofungamanishwa Na Jambo Fulani 

Alhidaaya.com 

03: Talaka Inayofungamanishwa Na Jambo Fulani (Au Tukio): 

Ni mume kufungamanisha talaka yake na kufanyika jambo fulani, ni sawa lifanywe na mume mwenyewe au lifanywe na mke wake, au lifanywe na mtu mwingine wa kando. 

Na kwa mujibu wa Jumhuwr ya ‘Ulamaa, jambo hilo likifanywa na mume, au mke, au mtu wa kando, basi litazingatiwa kama yamini (kiapo) kimajazi, yaani kwa maana ya mfano badala ya maana halisi.  Kwa sababu kiapo kinakuja kwa ajili ya kusisitizia na kutilia nguvu azima ya mwapaji au azima ya mwingine juu ya kutekeleza jambo fulani au kutolitekeleza.

Ni kama kumwambia mkewe:  "Ukitoka nyumbani, basi umeachika".  Au:  "Mimi nikisafiri, basi umeachika".  Au:  "Fulani akikutembelea, basi umeachika". 

Hukmu Yake:

Ikiwa mume atafungamanisha talaka yake kwa mkewe na jambo fulani, kisha jambo lenyewe likafanyika, kama kumwambia: "Ukitoka, basi umeachika", naye akatoka kweli, basi je, talaka inapita?

Jibu:  Hali ya mtu huyu haikosi moja ya mambo mawili: 

Jambo La Kwanza: 

Awe amekusudia talaka kweli ikiwa sharti aliloweka litafanyika.  Kwa huyu, ikiwa litafanyika jambo hilo aliloliwekea sharti, basi talaka yake itapita bila shaka.  Hii ni rai ya Jumhuwr ya 'Ulamaa. 

Lakini Ibn Hazm amekwenda kinyume na rai hii akisema kwamba talaka haipiti kwa hali yoyote, ni sawa litokee lililoshurutishwa au lisitokee kwa mujibu wa qaida yake maarufu aliyojiwekea kwamba hakuna talaka isipokuwa kwa namna ambayo Allaah 'Azza wa Jalla Ameamuru, na hakuna yamini isipokuwa kama vile Alivyoamuru Allaah Ta'aalaa.  Na Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"مَنْ كَانَ حَالِفًا فَلْيَحْلِفْ بِاللَّهِ أَوْ لِيَصْمُتْ ‏"‏‏

"Mwenye kuapa, basi na aape kwa Jina la Allaah au anyamaze (asiapie kwa kingine)".  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (6646) na Muslim (1646)]

Ninasema:  "Rai ya Jumhuwr ya 'Ulamaa ndiyo yenye nguvu zaidi, bali Sheikh wa Uislamu amesema: "Na kwa hakika, Wanachuoni kadhaa wameelezea kukubaliana kwao wote juu ya kupita talaka hii ya kushurutishiwa jambo, na hatukusikia mvutano wowote kuhusiana nayo tangu enzi na enzi". 

Jambo La Pili: 

Awe amekusudia kwayo kumshinikiza mke kufanya jambo au kutolifanya, na hakuwa na niya ya kweli ya talaka kama jambo litafanyika au halitofanyika.

'Ulamaa wana kauli mbili kuhusiana na hali hii:

Kauli Ya Kwanza: 

Talaka itapita kama jambo lililoshurutishiwa litafanyika.  Ni madhehebu ya Jumhuwr ya 'Ulamaa wakiwemo Maimamu wanne.  Dalili zao ni:

1-  Yaliyoelezewa na Al-Bukhaariy toka kwa Naafi'u aliyesema: 

"طَلَّقَ رَجُلٌ امْرَأَتَهُ الْبَتَةً إِنْ خَرَجَتْ، فَقَالَ ابْنُ عُمَر رَضِيَ اللهُ عَنْهُ:  إِنْ خَرَجَتْ فَقَدْ بُنَّتْ مِنْهُ، وَإِنْ لَمْ تَخْرُجْ فَلَيْسَ بِشَيءٍ"

“Mtu mmoja alimwambia mkewe: “Ukitoka (nyumbani), basi nitakuwa nimekuacha talaka tatu mpigo”.  Ibn 'Umar akasema:  Ikiwa atatoka, basi atakuwa ameachika talaka ya mwachano mkubwa.  Na kama hakutoka, basi hakuna kitu".  [Imechakatwa na Al-Bukhaariy (9-300)]

2-  Yaliyosimuliwa toka kwa 'Urwaa bin Az-Zubayr ambaye amesema: "Az-Zubayr alimpiga (mkewe) Asmaa bint Abiy Bakr, na Asmaa akapiga kelele ya kuomba msaada kwa (mwanaye) 'Abdullaah bin Az-Zubayr.  Na (Az-Zubayr) alipomwona 'Abdullaah alimwambia:  Ukiingia, basi mama yako atakuwa ameachika.  'Abdullaah akamwambia:  Unamfanya mama yangu kuwa ndio kinga ya kiapo chako!!  Akamvaa na kumnasua mama yake, na hapo akawa ameachika”. [Isnaad yake ni Dhwa'iyf.  Imechakatwa na At-Twabaraaniy katika "Al-Kabiyr" (1/121), na Adh-Dhahabiy katika "As-Siyar".  Angalia "Al-Miyzaan" (4/178)]

Ushahidi wa dalili hapa ni neno lake:  “Na hapo akawa ameachika”, lakini Hadiyth hii ni Dhwa'iyf.

3-  Ibn Mas-'uwd alipoulizwa kuhusiana na mtu aliyemwambia mkewe kwamba akifanya jambo fulani atakuwa ameachika na mkewe huyo akalifanya, alijibu:

"هِيَ وَاحِدَةٌ، وَهُوَ أَحَقُّ بِهَا"

"Hiyo ni talaka moja, na yeye bado ana haki ya kumrejea”.  [Ni Dhwa’iyfIsnaad yake imekatika.  Imechakatwa na Al-Bayhaqiy (7/356).  Imekatika kati ya Ibraahiym na Ibn Mas-'uwd]

4- Ujumuishi wa neno la Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam):

"المُسْلِمُونَ عِنْدَ شُرُوطِهِمْ، إِلَّا شَرْطًا حَرَّمَ حَلَالًا أَوْ أَحَلَّ حَرَامًا"

"Waislamu ni lazima wachunge masharti waliyowekeana, isipokuwa sharti linaloharamisha halali, au linalohalalisha haramu”.   [Hadiyth Swahiyh]

Kauli Ya Pili: 

Talaka haipiti.  Ni kauli ya 'Ikrimah, Twaawuws na Ibn Hazm.  Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah na baadhi ya 'Ulamaa wa Kishaafi'iy wameunga mkono kauli hii.  Dalili zao ni:

1-  Kauli Yake Ta'alaa: 

"قَدْ فَرَضَ اللَّـهُ لَكُمْ تَحِلَّةَ أَيْمَانِكُمْ" 

"Allaah hakika Amekuwekeeni shariy’ah ya ukomboaji wa viapo vyenu".  [At-Tahriym: 02]

Na Kauli Yake:

"ذَٰلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَانِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ"

"Hiyo ndio kafara ya viapo vyenu mnapoapa". [Al-Maaidah: 89]

Sheikh wa Uislamu amesema:  "Kiapo cha talaka, ni miongoni mwa viapo vya Waislamu vyenye kutolewa kafara, nacho kinaingia ndani ya jumla ya viapo vilivyotajwa kwenye aayah”.

2- Neno la Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam: 

"‏ مَنْ حَلَفَ عَلَى يَمِينٍ فَرَأَى غَيْرَهَا خَيْرًا مِنْهَا فَلْيُكَفِّرْ عَنْ يَمِينِهِ وَلْيَفْعَلْ ‏"‏ ‏

"Mwenye kuapia jambo, halafu akaona jingine kuwa ni la kheri zaidi kuliko hilo, basi atoe kafara kwa kiapo chake, kisha alifanye lile aliloliona kuwa la kheri zaidi".  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Muslim (1650) na wengineo]

3- Kauli ya Maswahaba saba waliosema kwamba mtumwa haachwi huru kwa kiapo.  Na kwa kipimo hicho hicho, pia talaka haipiti kwa kiapo.  Limeelezwa hili na Ibn Taymiyah.   

Maswahaba hao ni Ibn ‘Umar, Ibn ‘Abbaas, Abu Hurayrah, ‘Aaishah, Ummu Salamah, Hafswah na Zaynab binti Abiy Salamah. 

Kauli Yenye Nguvu:

“Nimeona kwamba katika suala hili hakuna matini ya wazi toka kwenye Qur-aan au Hadiyth za Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala hata 'Ijmaa iliyotua.  Ninaloliona ni kuwa, lililo karibu zaidi na kiini cha shariy'ah na makusudio yake ni kwamba talaka iliyofunganishiwa sharti haipiti kama mwapaji hakusudii kwayo isipokuwa kutishia tu, au kuhimizia jambo, au kuzuia jambo lisifanyike.  Kipengele hiki ndicho kinatumiwa kwa sasa na mahakama za Misri katika mada ya pili ya sheria nambari 25 ya mwaka 1929 inayosema:

"Talaka isiyo ya hapo kwa hapo "المُنَجَّزُ" haipiti ikiwa mume atakusudia kwayo kuhimizia jambo lifanyike au lisifanyike na si vinginevyo". 

Kama atakusudia talaka kikweli ikiwa sharti aliloliweka litafanywa, basi talaka yake itapita.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.