Skip to main content

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

الطَّلَاقُ المُنَجَّزُ والمُضَافُ والمُعَلَّقُ

Talaka Inayopita Hapo Hapo Inapotolewa, Talaka Inayofungamanishwa Na Wakati, Na Talaka Inayofungamanishwa Na Jambo Fulani 

Alhidaaya.com 

04: Faida Kadhaa (Kuhusiana Na Kupita Kwa Talaka Iliyofungamanishwa Na Sharti):

1- Mume akimwambia mkewe kwamba atakuwa ameachika kama atafanya jambo fulani, kisha mkewe akalifanya jambo hilo kwa kusahau au kwa kulazimishwa, basi talaka itapita kwa mujibu wa rai ya Jumhuwr ya ‘Ulamaa. 

Lakini Ash-Shaafi'iy amesema kwamba haipiti.

2- Mume akifungamanisha talaka na sharti, mkewe atabakia ni halali kwake kwa tendo la ndoa wakati wowote autakao madhali lililoshurutishiwa halikutendwa.  Hii ni rai ya Jumhuwr ya ‘Ulamaa, lakini Maalik amesema si halali. 

3- Mume akifungamanisha talaka na sharti, na jambo lililoshurutishwa likatendwa, basi talaka itahesabiwa moja tu. Na kama mke atafanya tendo hilo hilo tena akiwa katika eda, basi hakuna talaka nyingine itakayohesabiwa, itakayohesabika ni ile ile tu ya mwanzo lakini kwa sharti tu kwamba mume asiwe alisema: “Kila ukirudia kufanya, basi itakuwa ni talaka”.   

Na hapa itakuwa ni vizuri kueleza kwamba ikiwa kitu kilichofungamanishwa sharti kitaharibika, au kutekekea au kuondoka,, basi kiapo kitavunjika, hakitozingatiwa tena.  Ni kama kumwambia:  “Ukiingia nyumba ya fulani, basi umeachika”, halafu nyumba hiyo ikabomoka, hapo yamini inakuwa haihesabiki tena hata kama atakuja kuingia nyumba hiyo baada ya kujengwa tena upya.