Skip to main content

11B-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume: Talaka Rejea03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume: Talaka Rejea: Masharti Ya Kuweza Kumrejea Mke

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

طَلَاقٌ رَجْعِي

Talaka Rejea 

Alhidaaya.com

19-Masharti Ya Kuweza Kumrejea Mke: 

1- Kuwe ni baada ya talaka ya kwanza au ya pili, ni sawa iwe imetoka kwa mume au kwa qadhi.  Ni hatua ya kuanza tena upya maisha ya ndoa baada ya kukatishwa na talaka.

2- Mke mtalikiwa awe ameingiliwa na mume. Ikiwa mume amemtaliki kabla ya kumuingilia, kisha akataka kumrejea, basi hilo haruhusiwi kwa itifaki ya 'Ulamaa (ila kwa ndoa mpya na mahari mapya).  Ni kutokana na Kauli Yake Ta'aalaa: 

"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا"

"Enyi walioamini!  Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kujimai nao, basi hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu".  [Al-Ahzaab: 49]   

3- Mume amrejee mkewe katika kipindi cha eda.  Eda ikimalizika, basi hawezi kumrejea kwa itifaki ya 'Ulamaa (ila kwa ndoa mpya na mahari mapya). Ni kwa Neno Lake Ta'aalaa:

"وَالْمُطَلَّقَاتُ يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ ثَلَاثَةَ قُرُوءٍ"

"Na wanawake waliotalikiwa wabakie kungojea zipite hedhi (na twahara) tatu".  [Al-Baqarah: 228] 

Kisha Akasema kwenye aayah hii hii:

"وَبُعُولَتُهُنَّ أَحَقُّ بِرَدِّهِنَّ فِي ذَٰلِكَ"

"Na waume zao wana haki kuwarejea katika muda huo".  [Al-Baqarah: 228] 

4- Wasiwe waliachana kutokana na ndoa kuvunjwa (na kadhi au mahakama) kabla ya kumrejea. 

5- Kuachana kusiwe kulitokana na malipo ya fidia (khulu).  Ikiwa walitengana kwa mke kulipa fidia ya mali ili aachane na mumewe, basi haijuzu kumrejea, kwa kuwa kwa malipo hayo, mke anakuwa ameshafungika. 

6- Kumrejea kusifungamanishwe na masharti yoyote au kwa wakati ujao.  Jumhuwr ya 'Ulamaa wamesema:  Kwa sababu kumrejea mke lengo lake ni kuendeleza na kurejesha upya safari ya mkataba wa ndoa, na ndoa haikubali kufungamanishwa na chochote.