Skip to main content

11B-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume: Talaka Rejea04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume: Talaka Rejea: Kumrejea Mke Ni Haki Thabiti Iliyo Kwenye Mamlaka Ya Mume

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

طَلَاقٌ رَجْعِي

Talaka Rejea 

Alhidaaya.com

20-Kumrejea Mke Ni Haki Thabiti Iliyo Kwenye Mamlaka Ya Mume:

Ni haki kwa mume kumrejelea mkewe madhali bado yuko kwenye eda, ni sawa mke aridhie kurejelewa au akatae.  Ni kwa Neno Lake Ta'aalaa:

"وَبُعُولَتُهُنَّ أَحَقُّ بِرَدِّهِنَّ فِي ذَٰلِكَ إِنْ أَرَادُوا إِصْلَاحًا"

"Na waume zao wana haki kuwarejea katika muda huo ikiwa watataka suluhu".  [Al-Baqarah: 228]

Haki hii mume amewekewa na Sharia ya Allaah, hivyo haruhusiwi kuidondosha au kuiachia.  Na kama mume atasema:  "Nimekuacha na sitokurejea", au:  "Nimeidondosha haki yangu ya kukurejea", basi haki yake hiyo haidondoki bali itabakia pale pale, kwa kuwa kuidondosha ni sawa na kubadilisha Sharia ya Allaah.  Hakuna yeyote mwenye mamlaka ya kubadilisha Sharia ya Allaah Ambaye Amempa mume haki ya kumrejea mkewe ndani ya wigo wa talaka mbili tu Aliposema: 

"الطَّلَاقُ مَرَّتَانِ ۖ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ"

"Talaka ni mara mbili tu. Hivyo kuzuia kwa mujibu wa shariy’ah au kuachia kwa ihsaan".  [Al-Baqarah: 229]

Hivyo basi, mume anatakiwa aitumie haki hii ya kumrejea mkewe akipenda kumrejea, na kama hana nia ya kumrejea, basi asubiri eda imalizike na mkewe huyo awe ameachika talaka mtengano "طَلَاقٌ بَائِنٌ" kama Alivyosema Allaah Ta'aalaa: 

"فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ فَارِقُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ"

"Basi wazuieni kwa wema, au farikianeni nao kwa wema." [At-Twalaaq: 02]

Na Aliposema tena:

"الطَّلَاقُ مَرَّتَانِ ۖ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ"

"Talaka ni mara mbili. Hivyo kuzuia kwa mujibu wa shariy’ah au kuachia kwa ihsaan".  [Al-Baqarah: 229]

Mume kumrejea mke kunaweza kuwa ni waajib, ikiwa alimtaliki talaka rejea wakati akiwa kwenye hedhi.  Suala hili litachambuliwa wakati wa kuzungumzia talaka ya kibid-'ah "طَلَاقٌ بِدْعِيٌّ" (iliyo kinyume na shari'ah).