Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
الطَّلَاقُ
Talaka
04: Talaka Ya Mlevi:
Ama mlevi aliyefikia kiwango cha uchakari na hajui asemacho, na anaporudi katika hali yake ya kawaida hatambui nini alisema wakati yuko chakari, huyu anaweza kuwa katika moja ya hali mbili:
Ya Kwanza: Awe Alilewa Kwa Kutokusudia:
Ni kama kulewa kwa kulazimika, au kulazimishwa kwa nguvu, au kutumia dawa kwa matibabu ya lazima aliyoandikiwa na daktari wa Kiislamu anayeaminika, au kupigwa sindano ya ganzi, au kutumia mada ambayo hakujua kama inalewesha na mfano wa hayo, huyu talaka yake haizingatiwi kwa 'Ijmaa ya 'Ulamaa.
Ya Pili: Awe Alilewa Kwa Kukusudia:
Ni kama kunywa pombe kwa hiari yake mwenyewe huku akijua madhara yake, au kubwia mihadarati na mfano wake. Huyu 'Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na talaka yake kupita katika kauli mbili:
Kauli Ya Kwanza:
Talaka yake inapita anapokuwa chakari. Ni kauli ya Jumhuwr ya 'Ulamaa akiwemo Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi'iy na Ahmad. Ni kauli pia ya Ibn Al-Musayyib, Al-Hasan, Ash-Sha'abiy, 'Atwaa, Al-Awzaaiy, Ath-Thawriy na kundi la Masalaf. Dalili zao ni:
Ya Kwanza: Ni kwamba hukumu ya uwajibishwaji inatekelezwa juu yake, na kwa hivyo anaadhibiwa kwa kosa alilolifanya. Na dalili ya hili ni Kauli Yake Ta'aalaa:
"لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُون"
"Msikaribie Swalaah na hali mmelewa mpaka mjue mnayoyasema". [An-Nisaa: 43]
Wanajibiwa: "Hoja hii ni dhaifu, kwa sababu asiye na akili wala kufahamu anachoambiwa wala kujua akisemacho, basi huyo si mwajibishwaji kisharia (mukallaf). Na kwa Itifaki ya 'Ulamaa, mukallaf sharti awe na akili.
Ama aayah tukufu, aayah hii inawakataza kulewa hadi kufikia hali ya wao kutoweza kuelewa wakifanyacho au wakisomacho, au inawakataza kunywa katika wakati ulio karibu na swalaah, au inamkataza yule ambaye nishai imeanza kumpanda. Ama mtu aliyelewa, huyo huwezi kumwambia lolote akakufahamu".
Ya Pili: Kupita kwa talaka ni adhabu kwake.
Wanajibiwa: "Kwamba sharia haijamwadhibu yeyote kwa aina hii ya kupita talaka au kutokupita, bali adhabu yake ya kupigwa viboko inamtosha, lakini pia anaweza kupata Radhi za Allaah kutokana na adhabu hii ya kisharia, mbali na kwamba kumwadhibu mtu kwa adhabu nyingine ni kubadili mipaka ya sharia. Isitoshe, katika hili kuna madhara kwa mkewe ambaye hana makosa".
Ya Tatu: Maswahaba wamemzingatia mlevi sawa na mtu mwenye akili zake timamu katika kutekelezewa adhabu ya kisharia (hadd). Adhabu ya kulewa wameifanya sawa na adhabu ya kusingizia zinaa (mijeledi 80). Maswahaba hawa wamesema:
"إِذَا شَرِبَ سَكَرَ، وإِذَا سَكَرَ هَذَى، وَإِذا هَذَى افْتَرَى، وحَدُّ المُفْتَرِيْ ثَمَانُونَ"
"Anapokunywa hulewa, anapolewa hubwabwaja maneno, na anapobwabwaja huzusha, na adhabu ya kisharia ya mzushi ni fimbo 80". Lakini hii ni Hadiyth Dhwa'iyf. [Imechakatwa na Maalik (1533), Ash-Shaafi'iy (293), 'Abdul Razzaaq (7/378), Ad-Daaraqutwniy (3/157, 166), Al-Haakim (4/417), na Al-Bayhaqiy (8/320)]
Imejibiwa: "Kuzusha hapa ni dhana tu, si hakika. Haijulikani atazusha nini, atazusha wakati gani, na nani atamzushia? Ni sawa na aliyelala ambaye anaweza kuponyokwa na upepo, na asiweze kujua kama ulimtoka au la".
4- Kuondoka akili yake hakujulikani ila kwa kupimwa maneno yake. Lakini kiujumla anakuwa ni faasiq kwa kunywa pombe.
5- Ni Hadiyth Dhwa'iyf iliyosimuliwa nyuma isemayo:
"كُلُّ طَلَاقٍ جَائزٌ، إِلا طَلَاق المعْتُوهُ المغْلُوبُ على عَقْلِهِ"
"Talaka zote zinapita, ila talaka ya mlemavu wa akili aliyevurugikwa".
Kauli Ya Pili (Kuhusu Kupita Talaka Ya Mlevi Au La):
Talaka ya mlevi haipiti kabisa. Hii ni kauli ya kale ya Ash-Shaafi'iy iliyoungwa mkono na Al-Mazniy, At-Twahaawiy na Ahmad. Ni kauli pia ya 'Umar bin 'Abdul 'Aziyz, Al-Layth, Is-Haaq na Abu Thawr. Aidha, ni chaguo la Sheikh wa Uislamu, lakini pia imesimuliwa toka kwa 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhwiya Allaah 'anhu). Dalili kuhusiana na kauli hii ni:
1- Kauli Yake Ta'aalaa:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُونَ وَلَا جُنُبًا إِلَّا عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىٰ تَغْتَسِلُوا"
"Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa mpaka mjue mnayoyasema, na wala mkiwa mna janaba isipokuwa mmo safarini mpaka muoge josho". [An-Nisaa: 43]
Wamesema: "Allaah hapa Ameyafanya maneno ya mlevi si yenye kuzingatiwa, kwa kuwa mlevi huyu hajui anachokisema, na kwa hivyo basi, swalaah yake inakuwa batili, kwa kuwa akili hazimo. Kwa muktadha huo, mkataba wake wa ndoa hauvunjiki, kwani anakuwa ndani ya wigo mmoja na mtu aliyelala, mwendawazimu na mfano wa wawili hawa".
2- Ni neno lake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam):
"إِنَّمَا الأعْمَالُ بالنِّيَّاتِ"
"Hakika si vinginevyo, matendo ni kwa mujibu wa niya". [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (1) na Muslim]
Aliyelewa hana nia wala kusudio. Hivyo basi, ni sharti liwepo kusudio lake katika kutekeleza au kuvunja mikataba inayomuhusu au matendo yake mengineyo yote.
3- Hadiyth ya Buraydah kuhusiana na kisa cha Maa'iz ambaye alikiri kwamba amezini na Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza:
"أَشَرِبَ خَمْرًا؟ فَقَامَ رَجُلٌ فَاسْتَنْكَهَهُ فَلَمْ يَجِدْ مِنْهُ رِيْحَ خَمْرٍ"
"Je, amekunywa pombe? Na hapo mtu mmoja akasimama na kumnusa mdomo kama una harufu, lakini hakumsikia akinuka pombe". [Hadiyth Swahiyh. Muslim (1695), Al-Bayhaqiy (2535) na An-Nasaaiy (7125)]
Hapa Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameuweka ulevi daraja moja na wendawazimu katika kufuta adhabu ya kisharia.
Inajibiwa: "Kwamba hili linahusiana na mlango wa adhabu za kisharia, na si talaka".
4- Hadiyth ya 'Aliy kuhusiana na kulewa Hamzah bin 'Abdul Muttwalib na Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaingia nyumbani kwa Hamzah (na kumkuta chakari). Kipande cha Hadiyth kinaeleza:
"فَإِذَا هُمْ شرب، فَطَفِقَ رَسُولُ الله صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَلُومُ حَمْزَةَ فيْمَا فَعَلَ، فَإِذَ حَمْزَة قَدْ ثَمُلَ مُحمرةً عَيْنَاه، فَنَظَرَ حَمْزَةُ إلى رَسُولِ الله صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ...ثُمَّ قَالَ: هَلْ أَنْتُمْ إِلا عَبِيْدٌ لأَبِيْ، فَعَرِفَ رَسُولُ الله صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنَّهُ قَدْ ثَمُلَ، فَنَكَصَ رَسُولُ الله صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ على عَقِبَيْهِ القَهْقَرِيّ وخَرَجْنَا مَعَه"
"….na akashtukizwa kuwakuta wanakunywa, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaanza kumlaumu Hamza kwa alichokifanya, na Hamza mwenyewe yuko chakari macho yamemwiva kwa wekundu. Hamza akamwangalia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia: Hivi kwani nyinyi si watumwa tu wa baba yangu!! Na hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akagundua kwamba Hamzah yuko chakari, akarudi kinyume nyume na tukatoka nje pamoja". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (3091)]
Ibn Hazm (10/211) amesema: "Hapa tunamwona Hamzah (Radhwiya Allaah 'anhu) anasema maneno ambayo lau angeliyasema akiwa hajalewa, basi angekufuru. Na kwa hakika Allaah Alimlinda na hilo. Na kwa muktadha huu, tunaelewa kwamba mlevi hachukuliwi kwa anayoyasema au kuyafanya".
Na Al-Haafidh amesema: "Na hii ni moja kati ya dalili zenye nguvu zaidi kwa kundi lisilochukulia yanayofanywa na mlevi wakati yuko chakari ikiwa ni pamoja na talaka na mengineyo".
5- Yaliyopokelewa toka kwa 'Uthmaan (Radhwiya Allaah 'anhu), amesema:
"كُلُّ الطَلاَقٍ جَائِزٌ إِلاَّ طَلاَقَ النَّشْوَان والْمَجْنُونُ"
"Talaka zote zinapita isipokuwa talaka ya mlevi na mwendawazimu". [Isnaad yake ni swahiyh. Imechakatwa na Sa'iyd bin Mansour (1112), 'Abdulrazzaaq (12308), Ibn Abiy Shaybah (5/39) na Al-Bayhaqiy (7/359)]
6- Imepokelewa toka kwa 'Umar bin 'Abdul 'Aziyz kwamba:
"أَنَه أُتِيَ بِرَجُلً طَلَّقَ امرَأَتَهُ وَهُوَ سَكْرَانٌ، فاسْتَحْلَفَهُ بالله الذِيْ لا إِلَهَ إِلاَ هُوَ أَنَّهُ طَلَّقَ ومَا يَعْقِلُ، فَحَلَفَ، فَرَدَّ عليْهٍ امرَأَتَهُ وَضَرَبَهُ الحدَّ"
"Aliletewa mtu ambaye alimtaliki mkewe akiwa amelewa. Akamtaka mtu yule aape kwa Allaah Ambaye hakuna mola mwingine ila Yeye kwamba amemtaliki mkewe akili zikiwa hazimo. Akaapa, akamrejeshea mkewe, lakini alimchapa viboko kama adhabu ya kisharia (ya kulewa)". [Isnaad yake ni Swahiyh. Imechakatwa na Sa'iyd bin Mansuwr (1110) na Ibn Abiy Shaybah (5/39)]
7- Mwenye kulewa kwa kunywa kilichoharamishwa, bila shaka anapata madhambi na anastahiki adhabu ya duniani na aakhirah (kama alikusudia akijua madhara yake na uharamu wake). Na sharia haijamweka mlevi daraja moja na mtu mzima mwenye akili timamu. Hivyo basi, anachostahiki mlevi ni adhabu ya kisharia tu, lakini talaka yake haihusiki.
Ninasema: "Kauli inayosema talaka ya mlevi haipiti kwa hali yoyote, ndiyo yenye nguvu zaidi na ndiyo yenye kunasibiana hasa na makusudio ya sharia na misingi yake. Halafu, kiuhakika, hakuna tofauti kati ya kuondoka akili ya mtu kwa kutumia kilichoharamishwa au kwa kinginecho. Mwanamke mjamzito akijipiga kwa makusudi tumbo lake damu ya nifasi ikamtoka, basi faradhi ya swalah inamwondokea. Kauli hii ndiyo inayofanyiwa kazi kwenye mahakama za Misri. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi".
Kuitamka Talaka Kwa Lengo Jingine:
Linalokusudiwa hapa ni mtu kuitamka talaka kwa khiyari yake mwenyewe kwa ajili ya kubainisha kwa watu umbo la tamko la talaka linavyokuwa. Ni kama mwalimu au shekhe anapowafundisha wanafunzi wake neno la talaka lilivyo akalitamka. Pia, kwa mtu anayejisemesha mwenyewe au anamsemesha mwingine kuhusiana na neno hilo. Hawa hawazingatiwi, kwa kuwa hawajakusudia talaka, bali ni kwa lengo la kufundisha au kujizungumzia tu. Kadhalika, talaka ya mtu asiyefahamu Kiarabu haipiti ikiwa atafundishwa tamko bila yeye kufahamu maana yake. Hili limekubaliwa kwa itifaki ya wote.