Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
طَلَاقٌ رَجْعِي
Talaka Rejea
21-Ridhaa Ya Mke Si Sharti Ili Mume Aweze Kumrejea:
Ni kwa Kauli Yake Ta'aalaa:
"وَبُعُولَتُهُنَّ أَحَقُّ بِرَدِّهِنَّ فِي ذَٰلِكَ إِنْ أَرَادُوا إِصْلَاحًا"
"Na waume zao wana haki kuwarejea katika muda huo ikiwa watataka suluhu". [Al-Baqarah: 228]
Hapa, aayah inatujulisha kwamba wanaume ndio waliopewa haki ya kuwarejea wake zao.
Na Aliposema pia:
"فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ"
"Basi wazuieni kwa wema." [At-Twalaaq: 02]
Na hapa Allaah Anawazungumzisha waume Akiwapa agizo hilo, na wanawake Hajawapa chaguo lolote.
Kadhalika, si sharti uwepo wa walii wala kulipa mahari, kwa kuwa mwanamke anakuwa bado yuko ndani ya duara la ndoa, na kumrejea ni sawa na kumbakisha humo ndani na kuendeleza ndoa.
Mume Kumjulisha Mkewe Kwamba Amemrejea:
Jumhuwr ya Fuqahaa wanasema kwamba mume kumjuza mkewe kwamba amemrejea ni jambo linalopendeza, kwa kuwa kumjuza huko kunakata mzizi wa mgogoro ambao unaweza kuzuka kati yao kama hakumjuza. Mke kama hakujua kwamba mumewe amemrejea, anaweza kuolewa na mtu mwingine baada ya eda yake kumalizika akidhani kwamba mumewe hakumrejea. Ikiwa itatokea hivyo, na mume akathibitisha kwa dalili kwamba amemrejea, basi atabakia kwenye ndoa yake ya awali, na ndoa ya mume wa pili itavunjwa na ataikalia eda kama aliwahi kumuingilia, halafu atarudi kwa mumewe wa awali. Na hapa mke atakuwa ni mwenye makosa, kwa kuwa ilikuwa lazima amuulize mumewe kama amemrejea au la, kabla ya kuolewa na mume mwingine, na mume naye atakuwa pia na makosa kwa kuacha kumjulisha kwamba amemrejea.
Lakini pamoja na yote, hata kama mume hakumtaarifu kwamba amemrejea hakuna tatizo, kwani ni ukamilisho wa ndoa yao iliyopo na si ndoa mpya.
Nao kwa upande wao, Adh-Dhwaahiriyyah wanaona kwamba mume ni lazima amjulishe mkewe kwamba amemrejea, na kama hakumjulisha, basi kumrejea kwake hakutazingatiwa. Na hii ni kwa Kauli Yake Ta'aalaa:
"فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ فَارِقُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ"
"Basi wazuieni kwa wema, au farikianeni nao kwa wema." [At-Twalaaq: 02]
Wanasema kwamba kumrejea ndio kumzuia, na hakuwi kwa mujibu wa aayah hii ila kwa wema, na miongoni mwa wema, ni kumjulisha. Na kama hakumjulisha, basi anakuwa hakumzuia kwa wema, bali kwa munkari.
Kadhalika, Kauli Yake Ta'aalaa:
وَبُعُولَتُهُنَّ أَحَقُّ بِرَدِّهِنَّ فِي ذَٰلِكَ إِنْ أَرَادُوا إِصْلَاحًا"
"Na waume zao wana haki kuwarejea katika muda huo ikiwa watataka suluhu". [Al-Baqarah: 228]
Mume hapa ndiye mwenye haki zaidi ya kumrejea mkewe, ikiwa mume huyu anataka suluhu. Na ikiwa atamficha kwamba amemrejea, au akamjulisha kwa njia isiyoweza kumfikia, basi huyo bila shaka hana nia ya suluhu wala kumrejea mkewe, bali nia yake ni kuchafua.
Ninasema: "Ninavyoona mimi, ni kwamba rai hii ndiyo yenye nguvu zaidi, na ndiyo yenye kunasibiana zaidi na makusudio ya kisharia na misingi yake. Ni kauli pia ya 'Umar bin Al-Khattwwaab (Radhwiya Allaah 'anhu).
Ibn Hazm amesimulia kwamba 'Umar alisema kuhusiana na mwanamke ambaye mumewe alimtaliki na akamjulisha (kwamba amemtaliki), halafu akamrejea bila kumtaarifu (kwamba amemrejea) mpaka eda yake ikamalizika, alisema:
"قَدْ بَانَتْ مِنْهُ"
"Huyo ashakuwa haramu kwake".
Na kwa muktadha huu, ikiwa mume atamrejea mkewe bila kumjulisha, na mkewe naye akaolewa na mume mwingine baada ya eda yake kumalizika, basi hapo ndoa ya mume wa pili itakuwa ndiyo sahihi, kwa sababu kiuhalisia, anakuwa hakumrejea. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.