Skip to main content

11A-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha كتاب الفرق بين الزوجين - Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Talaka Kutengana Mke Na Mume: Talaka Ya Aliyekosea

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

الطَّلَاقُ

Talaka

Alhidaaya.com 

05:  Talaka Ya Aliyekosea:

Huyu ni yule ambaye hajakusudia kabisa kuitamka talaka bali alikusudia neno jingine ulimi ukamponyoka, akaitamka talaka bila kukusudia.  Ni kama mtu aliyetaka kumwambia mkewe: "أَنْتِ طَاهِرٌ" (Wewe umetwaharika) akakosea na kujikuta akimwambia: "أَنْتِ طَالِقٌ" (Nimekuacha) bila ya kuwa anafanya mzaha, bali kwa kuteleza ulimi.  Mwenye kufanya mzaha, talaka yake ya kimzaha inapita na inakuwa ni sahihi, ni sawa amekusudia au hajakusudia kama itakavyokuja kubainishwa mbeleni. 

'Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na kupita talaka ya mtu huyu aliyekosea tamshi. Jumhuwr wanasema kwamba talaka haipiti, ni sawa kwa upande wa kimahakama au kidini (yaani kati yake na Allaah), lakini ikiwa kukosea kwake kutathibitika kwa dalili.  Ikiwa hakujathibitika, basi talaka itapita kwa upande wa mahakama tu, na si kidini.  Ni kwa Hadiyth ya Ibn 'Abbaas kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"إِنَّ اللهَ وَضَعَ عَنْ أُمَّتِيْ الخَطَأَ والنِّسْيَانِ وما اسْتُكْرِهُوا عَلَيْهِ"

"Hakika Allaah Anausamehe umma wangu wanapokosea, wanaposahau au wanapolazimishwa jambo ".  [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh.  Abu Haatim ameitia kasoro katika Al-'Ilal (1/431)]

Mwenye kukosea hawekwi mizani moja na mwenye kufanyia mzaha talaka.  Mfanya mzaha huyu anakuwa amekusudia wazi tamko la talaka.  Hivyo basi, atastahiki adhabu ya kuzingatiwa mzaha wake kuwa talaka kweli kinyume na aliyekosea.

Ama kwa 'Ulamaa wa Kihanafiy, talaka ya aliyekosea inapita kwa upande wa kimahakama, ni sawa kosa lithibiti au lisithibiti, lakini kidini haipiti.