Skip to main content

11B-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume: Talaka Rejea06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume: Talaka Rejea: Je, Mke Aliyetalikiwa Talaka Rejea Anajipamba Kwa Mumewe? Nini Mume Anaruhusiwa Kukiona Kwake?

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

طَلَاقٌ رَجْعِي

Talaka Rejea 

Alhidaaya.com

22-Je, Mke Aliyetalikiwa Talaka Rejea Anajipamba Kwa Mumewe?  Nini Mume Anaruhusiwa Kukiona Kwake?

'Ulamaa wa Kishaafi'iy na Kimaalik –kwa jinsi ilivyo mashuhuri kwao- wanasema kwamba haijuzu mke aliyepewa talaka rejea kujipamba kwa mumewe, na mume hana ruhusa ya kustarehe na chochote kwa mke huyo, kwa sababu amekuwa ni mtu wa kando (ajnabiyya) kwake.  Pia, ndoa inamhalalishia kustarehe na mkewe apendavyo, lakini talaka inamharamishia yote, kwa kuwa ni kinyume na ndoa. 

Mwono wao huu umepokelewa kwa njia sahihi toka kwa 'Atwaa.  Toka kwa Ibn Jurayj amesema: "Nilimuuliza 'Atwaa:

"مَا يَحِلُّ لِلرَّجُلِ مِنِ امْرَأَتِهِ يُطَلِّقُهَا فَلَا يَبِتُّهَا؟ قَالَ: لا يَحِلُّ لَهَا منْ شَيْء مَا لَمْ يُرَاجِعْهَا" ‏

“Ni jambo gani lililo halali kwa mume aliyemtaliki mkewe talaka rejea?  Akajibu: "Si halali kwake chochote madhali bado hajamrejea". [Isnaad yake ni swahiyh. Imechakatwa na 'Abdulrazzaaq katika Al-Muswannaf (11030-11032)]

Ama 'Ulamaa wa Kihanafi, Kihanbali na Kidhwaahiriyyah, wao wanasema kwamba aliyetalikiwa talaka rejea atajipamba kwa mumewe kwa mapambo na mavazi tofauti kama anavyojipamba mke kwa mumewe.  Na hii ni kwa ajili ya kumtia mume chachu na hamu ya kumrejea ambapo huenda akamwona alivyojipamba, na hapo akajikuta analainika, akajuta kwa kumtaliki, na kuamua kumrejea.  Na mume anaruhusiwa kuangalia chochote akitakacho kwa mkewe. 

Dalili yao wanasema kwamba mwanamke aliyeachwa talaka rejea  anazingatiwa kuwa bado ni mke, na ndoa bado iko, kwa kuwa yuko ndani ya eda.  Na hii ni kutokana na Neno Lake Ta'aalaa: 

"وَبُعُولَتُهُنَّ أَحَقُّ بِرَدِّهِنَّ فِي ذَٰلِكَ إِنْ أَرَادُوا إِصْلَاحًا"

"Na waume zao wana haki kuwarejea katika muda huo ikiwa watataka suluhu".  [Al-Baqarah: 228]

Na hapa kwenye aayah hii, Allaah bado Anawataja kama ni waume. 

Ninasema:  "Kauli hii ndiyo yenye nguvu zaidi kutokana na aayah hii, lakini pia hakuna dalili nyingine yoyote inayomzuia mume kumwangalia mkewe au kumwekea mipaka ya uangaliaji huo (katika kipindi cha eda). 

Lakini pamoja na hivyo, baadhi ya 'Ulamaa waliobobea fani ya Fiqh wanasema kwamba mume anatakikana ambishie hodi kabla ya kuingia chumbani kwake kama hana nia ya kumrejea.  Na sababu ya hilo ni kwamba anaweza kumkuta hajavaa kitu, halafu jicho lake likaangukia kwenye utupu, na akawa kwa tukio hilo amemrejea mkewe kwa mujibu wa 'Ulamaa wanaolizingatia hilo kama ni sababu ya mume kumrejea mkewe.  Hili litafafanuliwa mbeleni In Shaa Allaah. 

Ama ikiwa ana nia ya kumrejea, basi hakuna ubaya kuingia bila kumbishia, kwa kuwa nia yake ni kumrejea, na kwa hivyo anakuwa ni mkewe na hususan pakizingatiwa kwamba kumrejea mke hakuhitaji aridhie. 

Imepokewa kwa njia sahihi toka kwa Ibn 'Umar kwamba:

"أنَّهُ طَلَّقَ امرأتَهُ صَفِيَّةَ بنتَ أَبِيْ عُبَيْد تَطْلِيْقَةً أَوْ تَطْلِيْقَتَيْنِ فَكَانَ لَا يَدْخُلُ عَلَيْهَا إِلاّ بِإِذْنٍ، فَلَمَّا رَاجَعَهَا أَشْهَدَ علَى رَجْعَتِهَا وَدَخَلَ عَلَيْهَا"

“Alimtaliki mkewe Swafiyyah bint Abiy 'Ubayd talaka moja au mbili, na akawa haingii kwake ila kwa kubisha hodi.  Na alipomrejelea, alishuhudisha kumrejelea kwake, na akamuingilia. [Isnaad yake ni swahiyh. Imechakatwa na Al-Bayhaqiy (7/373)