Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
الطَّلَاقُ
Talaka
06: Talaka Ya Aliyelazimishwa:
Jumhuwr ya 'Ulamaa wakiwemo Maalik, Ash-Shaafi'iy, Ahmad, Al-Awzaa'iy, Is-Haaq, Abu Thawr, Abu 'Ubayd na kundi la Masalaf, ikiwa pia ni kauli iliyosimuliwa toka kwa 'Umar, 'Aliy, Ibn 'Abbaas, Ibn 'Umar na Ibn Zubayr, wote hawa wanasema kwamba talaka ya mwenye kulazimishwa haipiti. Ni chaguo pia la Sheikh wa Uislamu. Dalili zao ni:
1- Kauli Yake Ta'aalaa:
"مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ"
"Atakayemkufuru Allaah baada ya iymaan yake, isipokuwa yule aliyekirihishwa (kukanusha) na huku moyo wake umetua juu ya iymaan, lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao juu yao ni ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kuu". [An-Nahl: 106]
Hapa Allaah Ta'aalaa Ameiondosha hukmu ya ukafiri kwa aliyelazimishwa ukafiri. Na ikiwa Ameiondosha kwa jambo kubwa kama hili, basi kwa madogo mengine ndiyo kabisa.
2- Hadiyth iliyotangulia nyuma kuhusiana na talaka ya aliyekosea isemayo:
"إِنَّ اللهَ وَضَعَ عَنْ أُمَّتِيْ الخَطَأَ والنِّسْيَانِ وما اسْتُكْرِهُوا عَلَيْهِ"
"Hakika Allaah Anausamehe umma wangu wanapokosea, wanaposahau au wanapolazimishwa jambo". [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Abu Haatim ameitia kasoro katika Al-'Ilal (1/431)]
3- Hadiyth Dhwa'iyf ya Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam):
"لاَ طَلَاقَ، ولا عتَاقَ في إِغْلَاقِ"
"Talaka na kuacha huru mtumwa hakupiti kwa kulazimishwa". [Hadiyth Dhwa'iyf. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2193), Ahmad (6/276) na Al-Haakim (2/198). Angalia Jaamiu' Ahkaamin Nisaa (4/115)]
4- Imepokelewa toka kwa Thaabit bin Al Ahnaf akisema:
"أّنَّ عَبْدَ الرَّحمن بن زَيْدٍ تُوُفِّيَ وَترَكَ أُمَّهَاتِ أَوْلادِهِ، قَالَ: فَخَطَبْتُ إِحْدَاهُنَّ إِلَى أُسَيْدِ بْنِ عَبْدِ الرَّحمن، وَهُو أَصْغَرُ مِنْ عَبْدِ الله بن عَبْدِ الرَّحمن فَأَنْكَحَنِيْ، فَلَمَّا بَلَغَ ذلِكَ عَبْدَ الله بَعَثَ إِلَيَّ، فَاحْتَمَلْتُ إِلَيْهِ فَإِذَا حَدِيْدٌ وسِيَاطٌ فَقَالَ: طَلِّقْهَا وإِلَّا ضَرَبْتُكَ بِهذِهِ السِّيَاطِ، وإِلَّا أَوْثَقْتُكَ بِهَذا الحَدِيْد، قَالَ: فَلَمَّا رَأَيْتُ ذلِكَ طَلَّقْتُهَا ثَلَاثًا، أَوْ قَالَ: بِتْتُّهَا، فَسَأَلْتُ كُلَّ فَقِيْهٍ بِالمَدِيْنَةِ فَقَالُوا: لَيْسَ بِشَيْء، فَسَأَلْتُ ابنَ عُمَرَ فَقَالَ: ائْتِ ابْنِ الزُّبَيْرِ، قَالَ: فَاجْتَمَعْتُ أَنا وابنُ عُمَرُ عند ابن الزُّبَيْرِ بِمَكَّةَ، فقَصَصْتُ عَلَيْهِمَا فَرَدَّاهَ عليَّ"
"Kwamba 'Abdulrahmaan bin Zayd alifariki na kuacha wake na watoto, nami nikamposa mmoja wao. Shauri langu nilimpelekea Usayd bin 'Abdulrahmaan ambaye ni mdogo kuliko 'Abdullah bin 'Abdulrahmaan, naye akaniozesha. Habari ilipomfikia 'Abdullah, alituma mtu kuniita nimwendee. Nikaenda nikiwa na wasiwasi, na nilipofika tahamaki naona vyuma na mijeledi. Akaniambia: Mtaliki, la sivyo nitakutandika mijeledi hii, au nikufunge vyuma hivi. Nilipoona mambo hivi, nilimtaliki talaka tatu. Nikawauliza Fuqahaa wote wa Madina (kuhusiana na hilo) nao wakaniambia kwamba hakuna kitu (talaka haikupita). Halafu nikamuuliza Ibn 'Umar, naye akanitaka nimlete Ibn Az Zubayr. Tukakusanyika mimi na Ibn 'Umar nyumbani kwa Ibn Az Zubayr mjini Makkah. Nikawaelezea mkasa ulivyo, na wao wakanirejeshea mke wangu". [Isnaad yake ni Swahiyh. Imechakatwa na 'Abdulrazzaaq (11410). Hadiyth mfano wake iko kwa Maalik (2/587) na Al-Bayhaqiy (7/358) kwa matini ndefu]
5- Mtu anayelazimishwa anakuwa hana uhuru wa kujiamualia lolote isipokuwa kutii tu. Kwa hali hiyo, anakuwa daraja moja na mwendawazimu na aliyelala.
Faida:
Ibn Qudaamah ameeleza masharti matatu ambayo ni lazima yawepo ili talaka ya aliyelazimishwa isipite:
1- Anayemlazimisha awe na uwezo wa kumdhuru kwa madaraka aliyonayo, au mtu aliyemzidi nguvu na kumdhibiti na kadhalika.
2- Awe na uhakika usio na shaka kwamba anayemlazimisha anaweza kutekeleza vitisho vyake kwake.
3- Madhara yanayoweza kumpata yawe ni makubwa kama kuuawa, kupata kipigo kikali, kushikiliwa muda mrefu na kadhalika. Ama ikiwa tishio ni matusi tu au maneno machafu, au kuchukuliwa pesa kidogo, hili halihesabiki.
Ninasema: "Rai ya Jumhuwr ya 'Ulamaa ndio yenye nguvu zaidi kutokana na uimara wa dalili zao, na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi".
Hapa ni muhimu tuzingatie kwamba kulazimishwa huko ni lazima kuwe kwa njia ya dhulma. Lakini ikiwa atalazimishwa kutoa talaka kwa haki, kama kwa aliyefanya "Iylaa" "إِيْلاءُ" nako ni mume kumwapia mkewe kwamba hatomuingilia kwa muda wa miezi minne, kisha muda huo ukamalizika na asimrejee mkewe, kisha kadhi akamlazimisha kutoa talaka, naye akaitoa, basi talaka hii inapita kwa 'Ijmaa.
["Iylaa" "إِيْلاءُ", ni kitendo cha mume kumwapia mkewe kwamba hatomuingilia kwa muda wa miezi minne]