Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
طَلَاقٌ رَجْعِي
Talaka Rejea
23: Je, Aliyetalikiwa Talaka Rejea Anaweza Kupata Talaka Nyingine Akiwa Bado Yuko Kwenye Eda?
Mwanamke huyu anakuwa bado yuko ndani ya fungamano la ndoa. Na kwa ajili hiyo, Jumhuwr ya 'Ulamaa wanasema kwamba talaka nyingine ya mume inampata akiwa ndani ya eda kama inavyompata "Dhwihaar "ظِهَارٌ", au "Li'aan" "لِعَانُ" au "Iylaa" "إِيْلاءٌ". Ibn Qudaamah amenukulu 'Ijmaa kuhusiana na hili!
-
["Dhwihaar "ظِهَارٌ", ni mume kumfananisha mkewe na mtu ambaye ni maharimu wake wa milele kama mama yake au dada yake kwa kumwambia kwa mfano: “Wewe nakuona kama mama yangu tu”.]
-
["Li'aan" "لِعَانُ", ni hatua ya kisharia inayofanyika kati ya mke na mume wakati mume anapomtuhumu mkewe kwamba amezini bila kuwa na mashahidi, au kudai mtoto si wake. Wataapishwa wote wawili ili kila mmoja wao akane au athibitishe tuhuma]
-
["Iylaa" "إِيْلاءٌ" ni mume kuapa kwamba hatomuingilia mkewe kwa muda wa miezi minne].
Lakini kwa upande wake, Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah anaona kwamba mwanamke hapatwi na talaka nyingine hata kama bado yuko ndani ya eda. Dalili aliyoitoa ni Neno Lake Ta'aalaa:
"يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا الْعِدَّةَ"
"Ee Nabiy! Mtakapowataliki wanawake, basi watalikini katika wakati wa eda (twahaarah) zao, na hesabuni barabara eda". [At-Twalaaq: 01]
Anasema kwamba Kauli hii inaonyesha kwamba haijuzu kuandamiza talaka juu ya talaka nyingine mpaka eda imalizike, au amrejee.
Na pia Kauli Yake Ta'alaa:
"فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ فَارِقُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ"
"Na watakapokaribia kufikia muda wao, basi wazuieni kwa wema, au farikianeni nao kwa wema ". [At-Twalaaq: 02]
Anasema, hapa mume amekhiyarishwa kati ya kumrejea, au kumwacha amalize muda wake wa eda na afarikiane naye kwa wema. Na ikiwa atampa talaka nyingine kabla ya eda kumalizika, basi atakuwa hakumzuia kwa wema, wala hakufarikiana naye kwa ihsaan.
Ninasema: "Inaelekea kwamba mvutano katika suala hili, unarejea kwenye makhitilafiano yaliyopo kati ya Ibn Taymiyah na Jumhuwr ya 'Ulamaa katika suala la: Je, talaka tatu kwa mpigo zinahesabiwa tatu au inahesabiwa moja tu? Hili litafafanuliwa kwenye milango ya mbele In Shaa Allaah".