Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
الطَّلَاقُ
Talaka
07: Talaka Ya Mwenye Ghadhabu Kali Na Talaka Ya Safihi:
Hasira (ghadhabu), ni hali ya mchemko wa neva inayopelekea kutokuwiana kwa akili. Hali hii humpata mwanadamu wakati mwenzake anapomjeruhi kwa maneno au kwa jinginelo. Hasira hii au ghadhabu ina vigawanyo vitatu:
Cha kwanza: Ni hasira inayompata mtu akabaki katika hali yake ya kawaida bila akili yake wala hisia zake kubadilika, akawa anajua ayasemayo au ayakusudiayo. Mume akitoa talaka katika hali hii, basi talaka yake itapita, na hususan ikiwa ataitoa baada ya kukaa akapanga na kupangua mambo.
Cha pili: Ni hasira inayofikia ukomo ambapo akili inakuwa imefunga, mtu hajielewi tena na hajui asemacho. Mume akitoa talaka katika hali hii, basi talaka yake haipiti. Na hili halina makhitilafiano kati ya 'Ulamaa.
Ninasema: "Hasira hii inabeba maana ya Hadiyth isemayo:
"لاَ طَلَاقَ، ولا عتَاقَ في إِغْلَاقِ"
"Talaka na kuacha huru mtumwa hakupiti kwa kulazimishwa". [Hadiyth Dhwa'iyf. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2193), Ahmad (6/276) na Al-Haakim (2/198). Angalia Jaamiu' Ahkaamin Nisaa (4/115)]
Akiandamiza Hadiyth hii ambayo ni Dhwa'iyf, Abu Daawuwd amesema katika Sunanih: "Ninadhani maana ya "الإغلاق" hapa ni ghadhabu".
Cha tatu: Ni hasira ya kati na kati (wastani) iliyo baina ya hali mbili zilizotangulia. Ni ile iliyovuka mpaka wa ukali, lakini haijafikia ukomo wa juu kabisa wa mchemko. 'Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu hasira ya namna hii kati ya kupita talaka au kutokupita.
Ninasema: "Katika hali hii, hasira inamfikisha mtu kwenye ngazi ya kuchanganyikiwa kimaneno na kivitendo, lakini pia anashindwa kujidhibiti na kutamakani ingawa akili yake inakuwa haijaondoka yote. Madhehebu ya Maimamu wanne yanasema kwamba talaka ya mwenye hasira ya namna hii inapita. Lakini wengine wanasema kwamba haipiti katika hali hii, nalo ndilo chaguo la Sheikh wa Uislamu na mwanafunzi wake Ibn Al-Qayyim ambaye amesema: "Dalili za kisharia zinaonyesha kwamba talaka yake haipiti, wala kuacha huru mtumwa wala kuvunja au kupitisha mikataba inayomuhusu".
Talaka Ya Safihi:
Safihi ni mtu mwenye akili tepetepe ambaye kwa kawaida hutumia mali zake bila busara au kwa misingi ya kisharia. Talaka ya mtu huyu kwa mujibu wa 'Ulamaa walio wengi inapita, kwa kuwa talaka anaimiliki, na pia ni mwajibishwa kisharia (mukallaf).