Skip to main content

11B-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume: Talaka Rejea08-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume: Talaka Rejea: Namna Ya Kumrejea Mkewe

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

طَلَاقٌ رَجْعِي

Talaka Rejea 

Alhidaaya.com

24: Namna Ya Kumrejea Mkewe:

1- Kumrejea Kwa Kutamka Kauli:

Inaswihi mume kumrejea mkewe kwa kauli inayofahamisha hilo, na hili halina makhitilafiano yoyote kati ya 'Ulamaa.  Ni kama kumwambia akiwa bado ndani ya eda:  "Nimekurejea", au "Nimekurejesha kwenye hifadhi yangu", au neno jingine lolote lenye maana hii.  Au anaweza kusema hilo kwa nafsi ya mtu wa tatu:  "Nimemrejea mke wangu" au mfano wa hivyo.

Katika matamshi haya ya mume kumrejea mke, kuna ambayo yako wazi na yasiyo wazi (ya kimafumbo).

Yaliyo wazi ni yale ambayo hayafahamishi jingine lolote zaidi ya kumrejea mke.  Ni mithili ya hayo yaliyotajwa punde.  Haya yakitamkwa, basi hakuhitajiki niya kutoka kwa mume ya kumrejea mke.

Ama ya kimafumbo, haya ni yale ambayo yanafahamisha kumrejea mke pamoja na kubeba maana nyingine.  Ni kama kumwambia:  "Wewe kwangu ni kama ulivyokuwa", au "Wewe ni mwanamke wangu", au "Nimekurudisha", au "Nimekukamata" na mfano wa hayo. Ikiwa atakusudia kwa matamko kama haya kumrejea mkewe, basi itakuwa amemrejea, na kama hakukusudia, basi atakuwa hakurejeleka. 

2- Kumrejea Kwa Vitendo:

'Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na vitendo vya kuhisika ambavyo mume anaweza kuvifanya kwa mkewe ili awe amemrejea katika kauli nne: 

Kauli Ya Kwanza: 

Kumrejea kunapatikana kwa kumjimai na vitangulizi vyake kama kumpapasa papasa, au kumbusu kwa matamanio, ni sawa awe amekusudia kumrejea au kutomrejea. Pia kumwangalia kwenye utupu wake tu bila kuangalia sehemu nyingine yoyote zaidi ya hiyo.  Haya ni madhehebu ya 'Ulamaa wa Kihanafiy, na dalili zao ni: 

1- Kumrejea ni kwa lengo la kuendeleza ndoa iliyoko, si kwa kauli tu, bali kwa njia yoyote ile.  Hivyo basi, kitendo kinaweza kufanyika kikionyesha dhamira ya hilo. 

2- Kitendo kinachohisisha lengo hilo la kuendeleza ndoa iliyoko, ni lazima kihusishwe na ndoa tu, haijuzu kwa jambo jingine lolote.  Ni kama kumjimai, kumbusu, kumgusa kwa matamanio au kumwangalia kwenye utupu kwa matamanio. 

Na kama hiyo haitoshi, 'Ulamaa hawa wanasema pia kwamba ikiwa mke atamfanyia haya mumewe kama kumbusu au kumpapasa papasa kwa matamanio, basi mume atahukumiwa kuwa amemrejea kama hakumzuia kufanya hayo.   

Kauli Ya Pili: 

Kumrejea kunapatikana kwa kumjimai pamoja na vitangulizi vyake, lakini kwa sharti mume akusudie kumrejea kwa kufanya hayo. 

Ni madhehebu ya 'Ulamaa wa Kimaalik.  Na huenda dalili yao ni ujumuishi wa kauli ya Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam):

"إِنَّمَا الأَعْمَالُ بالنِّيَّاتِ"

"Hakika si vinginevyo, matendo yanategemea niya".  [Al-Bukhaariy na Muslim]

Kauli Ya Tatu: 

Kumrejea kunapatikana kwa kule kumuingilia tu, ni sawa amekusudia kwa hilo kumrejea au la. 

Ni madhehebu ya Mahanbali, ni kauli ya Ibn Al-Musayyib, Al-Hasan, Ibn Syriyn, 'Atwaa, Twaawuws, Az-Zuhriy, Ath-Thawriy na Al-Awzaa'iy.

Mahanbali wametoa dalili zifuatazo kuwa kumuingilia tu mke inakuwa mume ashamrejea. 

1- Kipindi cha eda ni muda ambao mke aliyetalikiwa anakwenda kufungika asiweze kurejelewa na mumewe.  Ikiwa muda huu utamalizika, basi kumrejea huzuilika (ila kwa ndoa mpya na mahari mapya).  Hivyo basi, akimuingilia kabla ya muda kumalizika, atarudi kwake kama ilivyo kwenye “Iylaa” "إِيْلَاءٌ"

2- Talaka ni sababu ya kuondoka umiliki wa mume kwa mkewe.  Na mume ana khiyari ya kuuhifadhi umiliki huu au kuuwachia.  Hivyo basi, ikiwa atamuingilia mkewe, atakuwa amezuia umiliki wake kuondoka. 

Sambamba na hayo, wametoa dalili za kuonyesha kwamba vitendo vya kabla ya jimai, havitoshi kujuzisha kumrejea mke isipokuwa jimai tu.  Dalili hizo ni:

1- Vitendo hivi na mfano wake haviko katika maana ya jimai.  Jimai inakuwa ni dalili ya wazi ya nia kamili ya kumrejea.

2- Kuangalia sehemu ya utupu au kuigusa kunaweza kufanyika kutoka kwa mtu mwingine asiye mume kwa dharura (kama daktari).

Kauli Ya Nne:  Kumrejea hakupatikani isipokuwa kwa kauli, na si kwa kujimai au kwa jinginelo lolote. 

Ni madhehebu ya 'Ulamaa wa Kishaafi'iy na Muhammad bin Hazm.  Dalili zao ni:

1- Kumrejea ni kuhalalisha jimai kwa kutamka, haiswihi kwa kitendo. 

2- Mwanamke katika talaka rejea anazingatiwa kuwa mtu wa mbali (ajnabiyya) kwa mumewe –na hii ni kwa Mashaafi'iy tu-, hivyo si halali kwake kumuingilia.  Isitoshe, kumrejea ni sawa na kufunga tena ndoa upya ambayo haiswihi isipokuwa kwa matamshi yenye kuashiria hilo, na ndivyo hali ilivyo kwenye kumrejea!!

3- Haikuelezwa si katika Qur-aan wala katika Sunnah kwamba kujimai ndio njia mojawapo ya kumrejea mke.  Pia, hakuna makhitilafiano yoyote kwamba kumrejea mke kwa matamshi ndio kumrejea kiuhalisia. 

4- Kumrejea kwa wema kulikoamuriwa, hakuwezi kujulikana ila kwa maneno.

Kauli Yenye Nguvu:

Ninasema:  "Kauli ya mwisho siioni kama ina mwelekeo mzuri, kwa sababu Neno Lake Ta'aalaa:

وَبُعُولَتُهُنَّ أَحَقُّ بِرَدِّهِنَّ فِي ذَٰلِكَ إِنْ أَرَادُوا إِصْلَاحًا"

"Na waume zao wana haki kuwarejea katika muda huo ikiwa watataka suluhu", na neno lake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwambia 'Umar amwamuru mwanawe amrejee mkewe, maneno haya, hayajumuishi kauli tu, bali na mengineyo zaidi ya hapo.  Hivyo basi, haijuzu kuhusisha mtu kumrejea mkewe kwa kauli tu bila kitendo isipokuwa kwa dalili, na dalili yenyewe haipo.

Kisha lile ambalo linaonekana ni kwamba kauli iliyo adilifu zaidi ya kuwezekana mume kumrejea mke kwa kujimai, ni kama atafanya hilo akiwa na niya ya kumrejea kama alivyosema Maalik, Ahmad na Is-Haaq ambalo pia ni chaguo la Sheikh wa Uislamu.

Ama kuwezekana kumrejea kwa vitangulizi vya jimai, ikiwa patasemwa kwamba kunawezekana kwa sharti ya uwepo wa nia toka kwa mume, basi haliko mbali hili, na kama si hivyo, basi kumrejea hakufanyiki.