Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
الطَّلَاقُ
Talaka
08: Talaka Ya Mgonjwa (Ya Kuepa Mke Asirithi)
Mgonjwa yuko katika maradhi ya kifo (matumaini ya kupona hayapo kabisa), kisha akamtaliki mkewe aliyekwishamuingilia bila mke kuomba talaka, na wakati mke akiwa bado kwenye eda, mume huyu akafariki, je, talaka yake itazingatiwa imepita au la?
Si katika Qur-aan wala katika Hadiyth za Rasuli suala kama hili limegusiwa. Na kwa muktadha huo, 'Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na hukmu yake. Jumhuwr ya 'Ulamaa wanasema kwamba talaka hii itazingatiwa ni ya kuepa ili kumzuia mwanamke asirithi. Hivyo basi, mwanamke atarithi ingawa talaka imeshatolewa. Na hii ni kwa ajili ya kumlinda mwanamke na kuziba mwanya wa kunyimwa sehemu yake ya urithi!! 'Ulamaa hawa wameridhishwa na Fatwa ya 'Umar na 'Uthmaan (Radhwiya Allaah 'anhumaa) waliosema kuwa anarithi.
Halafu, 'Ulamaa hawa hawa wamegawanyika katika makundi matatu:
1- Kundi la kwanza: Wanasema: "Atarithi madhali yuko ndani ya eda".
Kwa sababu eda kwa upande wao inaingia ndani ya sehemu ya ndoa. Wamemfananisha na aliyeachwa talaka rejea. Na hii ni kauli ya Abu Haniyfah na Ath-Thawriy.
2- Kundi la pili: Wanasema: "Atarithi madhali bado hajaolewa na mtu mwingine".
Inawezekana hawa wameiona 'Ijmaa ya Waislamu ya kwamba mwanamke mmoja harithi wanaume wawili.
3- Kundi la tatu: Wanasema: "Atamrithi kwa hali yoyote, ni sawa akiwa kwenye eda au la, ameolewa na mwingine au hajaolewa".
Ni madhehebu ya Maalik na Al-Layth.
Hawa wote wametoa dalili ya kumrithisha kwa haya yafuatayo:
(a) Kwamba 'Uthmaan bin 'Affaan:
"وّرَّثَ امْرَأَةَ عَبْدِ الرَّحمَنِ بن عَوْفِ بَعْدَ انْقِضَاء العدَّةِ وكَانَ طَلَّقَهَا مَرِيْضًا"
"Alimrithisha mke wa 'Abdulrahmaan bin 'Awf baada ya eda yake kumalizika. Alikuwa amemtaliki akiwa mgonjwa". [Isnaad yake ni swahiyh. Imechakatwa na 'Abdulrazzaaq (12191, 12195)]
(b) Toka kwa Ibn Abiy Maliykah:
"Kwamba yeye alimuuliza Ibn Az-Zubayr kuhusiana na mtu anayemtaliki mkewe talaka tatu, kisha anakufa ilhali mke bado yuko kwenye eda". Ibn Az-Zubayr akasema:
"طَلَّقَ عَبْدُ الرَّحمنِ بن عُوْفِ ابْنَةَ الإِصْبع الكِلْبِي فَبَتَّهَ ثُمَّ مَاتَ وهِيَ فِي عِدَّتِهَا فَوَرَّثَهَا عُثْمَانُ، قَالَ بنُ الزُّبَيْرِ: وَأَمَّا أنا فَلَا أَرَى أَنْ تَرِثَ المَبْتُوتَة"
"'Abdulrahmaan bin 'Awf alimtaliki binti ya Al-'Iswbagh Al-Kilbiy talaka tatu mpigo, kisha akafa nailhali mke bado yuko kwenye eda yake, na 'Uthmaan akamrithisha. Ibn Az-Zubayr akasema: Ama kuhusiana na mimi, sioni mwanamke aliyeachwa talaka tatu anaweza kurithi". [Isnaad yake ni swahiyh. Imechakatwa na 'Abdulrazzaaq (12192)na Ibn Abiy Shaybah (5/217]
(c) Toka kwa Ibn 'Umar, amesema:
"طَلَّقَ غِيْلَانُ بن سَلَمَة الثَّقَفِي نِسَاءَه وَقَسَّمَ أَمْوَالَهُ بين بَنِيْهِ في خِلَافَةِ عُمَرُ، فَبَلَغَ ذلِكَ عُمَرُ ، فقَالَ: طَلَّقْتَ نِسَاءَكَ وَقَسَّمْتَ مَالَكَ بين بَنِيْك؟ قالَ: نَعَمْ، قَالَ: إِنِّيٍ لأَرَى الشَّيْطَانَ فِيْمَا يَسْرِقُ من السَّمْعِ سَمِعَ بِمَوْتِكَ فَأَلْقَاهُ في نَفْسِكَ، فَلَعَلَّكَ أَنْ لا تَمْكُثَ إِلاَّ قَلِيْلاً، وَأَيْمُ اللهٍ لَئِنْ لَمْ تُرَاجِعْ نِسَاءَكَ وتَرْجِعْ في أَمْوَالِك لأُوَرِّثَهُنَّ مِنْكَ إذَا مُتَّ، ثُمَّ لآمُرَنَّ بِقَبْرِكَ فَلَيُرْجَمَنَّ كَمَا رُجِمَ قَبْرُ أَبِي رِغَال"
"Ghiylaan bin Salamah Ath-Thaqafiy aliwataliki wakeze, kisha akagawa mali zake kati ya watoto wake wakati wa Ukhalifa wa 'Umar. Habari ikamfikia 'Umar (akamuita) na kumuuliza: Ni kweli umewataliki wakezo na kugawa mali zako kwa watoto wako? Akamjibu naam. Akamwambia: Wa-Allaah, mimi kwa hakika ninamwona shaytwaan katika udukuzi wake wa habari kuwa amesikia kwamba utakufa, kisha akaitupia habari hiyo kwenye nafsi yako, na huenda wewe usiishi ila muda mchache. Basi naapa kwa Allaah, kama hujawarejesha wakezo na ukarejesha mali zote (ulizozigawa), mimi nitawarithisha ukifa, kisha nitaamuru kaburi lako lipigwe mawe kama lilivyopigwa kaburi la Abu Righaal". [[Isnaad yake ni swahiyh. Imechakatwa na 'Abdulrazzaaq (12216)]
Wamesema: "Hili lilifanyika wakati Maswahaba wako hai, na wala hawajalipinga, na kwa hivyo limekuwa ni 'Ijmaa".
Ama kwa upande wa Ash-Shaafi'iy katika madhehebu yake mapya pamoja na Ibn Hazm, wao wanaona kwamba talaka ya mgonjwa wa umauti inapita, na mwanamke hamrithi, ni sawa mume kafa mke akiwa kwenye eda au baada ya eda. Na hii ni kutokana na haya yafuatayo:
1- Mume katoa talaka akiwa baleghe na mwenye akili zake timamu. Hivyo basi, talaka yake inapita sawa na mtu mwenye afya kamili.
2- Akimpa talaka tatu, hapo uhusiano wa ndoa unakatika kabisa, na haijuzu kumrithisha, si kwa sababu wala kwa nasaba.
3- Fatwa ya 'Umar na 'Uthmaan (Radhwiya Allaah 'anhumaa) inapingwa na fatwa ya Ibn Zubayr. Lakini hoja hii inapingwa kwa kusemwa kwamba Ibn Az-Zubayr hakuwa wakati huo ni katika Fuqahaa, na wala hakujulikana kwa fatwa yoyote wala umashuhuri kwenye Nyanja ya Fiqh.
4- Kutoa sababu ya talaka kutokupita kwa kujenga dhana kwamba mgonjwa anataka kumdhulumu mkewe kwa kukimbia asimrithi, dhana hii haitakikani kubatilishwa kwayo hukumu za kisharia. Isitoshe, dhana hii hii pia inaweza kuwepo katika hali ya uzima wake, afya yake na nguvu zake.
Kauli Yenye Nguvu:
Tukilichukulia kiuhakiki, tunakuta kwamba suala hili halikosi moja ya mambo mawili:
Kwanza: Talaka ipite, ndoa ivunjike na kurithiana kati yao kusiwepo.
Pili: Talaka isipite na isizingatiwe katika ugonjwa wa umauti, ndoa ibakie na kurithiana kati yao kubakie.
Kwa muktadha huu, mwenye kukubaliana na fatwaa ya 'Uthmaan na 'Umar (Radhwiya Allaah 'anhumaa), basi atazingatia kwamba talaka haipiti, na lazima mwanamke apewe fungu lake la mirathi.
Ama ambaye hakuifanya fatwaa hiyo kuwa hoja au dalili (ya kutokupita talaka na mwanamke kurithi), huyu atakuwa juu ya msingi wa asili, nao ni talaka ya mgonjwa wa umauti kuzingatiwa imepita, na mirathi kwa mke kufutwa. Hili ndilo lililo karibu zaidi. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
Faida:
Ya kwanza: Mume akimtaliki mkewe talaka rejea halafu akafariki katika hali ya ugonjwa au katika hali nyingine, au mwanamke akafariki, basi wote watarithiana kwa itifaki ya 'Ulamaa.
Ya pili: Ikiwa mke mwenyewe atadai talaka, au mume akamwambia: "Chagua mwenyewe, ubaki nami au nikupe talaka", naye akachagua talaka, au akadai khuluu, hapa 'Ulamaa wengi wamesema kwamba mwanamke atarithi. Ni Imaam Abu Haniyfah pekee aliyesema kwamba harithi.