Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
طَلَاقٌ رَجْعِي
Talaka Rejea
25: Kuhudhurisha Mashahidi Wakati Wa Kumrejea Mke:
Allaah Ta'aalaa Amesema:
"فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ فَارِقُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ وَأَشْهِدُوا ذَوَيْ عَدْلٍ مِّنكُمْ"
"Na watakapokaribia kufikia muda wao, basi wazuieni kwa wema, au farikianeni nao kwa wema, na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu". [At-Twalaaq: 02]
Makusudio ya "Wazuieni kwa wema" hapa ni kumrejea mke.
'Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu hukmu ya kushuhudisha mashahidi wawili wakati mume anapomrejea mkewe katika kauli mbili:
Kauli Ya Kwanza:
Ni lazima kushuhudisha mashahidi. Haya ni madhehebu ya zamani ya Ash-Shaafi-'iy, riwaayah ya pili toka kwa Ahmad, Abu Muhammad bin Hazm, na ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. Dalili zao ni:
1- Neno Lake Ta'aalaa:
وَأَشْهِدُوا ذَوَيْ عَدْلٍ مِّنكُمْ"
"Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu". [At-Twalaaq: 02]
Wanasema ilivyo dhahiri hapa ni kuwa agizo hili ni la lazima, na maana hii ndio alioifahamu 'Imraan bin Huswayn. 'Imraan bin Huswayn huyu aliulizwa kuhusu mtu aliyemtaliki mkewe talaka rejea kisha akamrejea bila mashahidi, naye akamjibu mtu yule akimwambia:
"طَلَّقْتَ لِغَيْرِ سُنَّةٍ، وَرَاجَعْتَ لِغَيْرِ سُنَّةٍ، أَشْهِدْ عَلَى ذلِكَ وَلاَ تَعُدْ "
“Umemtaliki kinyume na Sharia, na umemrejea kinyume na Sharia. Lete mashahidi washuhudilie hilo, na wala usirudie tena kufanya hivyo”. [Isnaad yake ni swahiyh]
2- Kumrejea mke ni kuhalalisha jimai. Hivyo basi, haiswihi kumrejea bila uwepo wa mashahidi kama ilivyo katika kufunga nikaah.
3- Allaah Ta'aalaa Ameunganisha katika aayah iliyotangulia kati ya kumrejea mke, kumtaliki na kushuhudishia. Hivyo basi, haifai kuchukua baadhi ya vipengele na kuviacha vingine. Na Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنْ عَمِلَ عَمَلًا لَيْسَ عَلَيْهِ أَمْرُنَا فَهُوَ رَدٌّ"
"Mwenye kufanya amali yoyote ambayo haiko kwenye jambo letu, basi inarejeshwa (haikubaliwi)". [Hadiyth Swahiyh]
Kauli Ya Pili:
Ni jambo linalopendeza kuhudhurisha mashahidi, lakini si wajibu. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Maalik na Ash-Shaafi'iy (madhehebu mapya), na moja ya riwaayah mbili toka kwa Ahmad. Dalili zao ni:
1- Uwepo wa mashahidi ni lazima wakati wa kufunga ndoa tu kwa ajili ya uthibitisho. Na mume kumrejea mke ni uendelezo wa ndoa, na si mwanzo wake, hivyo basi hakuna ulazima wa kulishuhudishia hilo.
2- Kumrejea mke ni haki ya mume, hahitajii mke akubali wala walii wake, hivyo ushuhudishiaji si lazima.
3- Amri ya kushuhudishia katika aayah tukufu, inachukulika kama ni ya jambo zuri linalopendeza, lakini si la lazima. Na hii ni kwa haya yafuatayo:
(a) Amri hii inafanana na amri iliyoko kwenye aayah 282 ya Suwrat Al-Baqarah Aliposema Allaah Ta'aalaa:
"وَأَشْهِدُوا إِذَا تَبَايَعْتُمْ"
"Na shuhudisheni mnapouziana".
Jumhuwr ya 'Ulamaa wanasema kwamba kuuziana kunaswihi bila uwepo wa mashahidi.
(b) Kushuhudisha ni kwa ajili tu ya kuepusha mke kuja kukanusha, na pia kuziba mwanya wa mgogoro. Hivyo kushuhudisha ni sawa na dhamana ya kinga.
(c) Aayah imempa mume haki ya ima kumzuia mkewe (kumrejea) au kufarikiana naye, kisha ikataja ushuhudisho wa mashahidi wawili. Kwa muktadha huo, tunapata kujua kwamba kumrejea mke kunapatikana kabla ya kushuhudisha, na kushuhudisha huku si sharti ya hilo. Na aayah ndiyo hii:
"فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ فَارِقُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ وَأَشْهِدُوا ذَوَيْ عَدْلٍ مِّنكُمْ وَأَقِيمُوا الشَّهَادَةَ لِلَّـهِ"
"Na watakapokaribia kufikia muda wao, basi wazuieni kwa wema, au farikianeni nao kwa wema, na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu, na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Allaah". [At-Twalaaq: 02]
(d) Ikiwa kufarikiana na mke ni haki ya mume, na hilo linafaa bila kushuhudisha, basi hata kumrejea pia ni haki yake halali bila kuwepo mashahidi.
Kauli Yenye Nguvu:
"Kauli ambayo ninaona ina nguvu ni ile inayosema kwamba ni wajibu mume kushuhudisha wakati wa kumrejea mkewe kutokana na agizo wazi lililopo kwenye aayah tukufu pamoja na dalili imara walizozitoa wenye kauli hii. Kadhalika, wajibu huu unamzuia mume kukanusha lolote na baadaye kuja kuingia katika haramu. Pia, mke atakosa njia ya kukanusha kurejelewa ili aolewe na mtu mwingine baada ya eda kumalizika (kwa madai kwamba mumewe hajamrejea)".