Skip to main content

11A-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha كتاب الفرق بين الزوجين - Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume09-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Talaka Kutengana Mke Na Mume: Je, Talaka Ya Kafiri Inapita?

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

الطَّلَاقُ

Talaka

Alhidaaya.com 

09:  Je, Talaka Ya Kafiri Inapita?

Faida ya suala hili inajikita katika picha ya kama kafiri amemtaliki mkewe talaka mbili kisha akasilimu.  Sasa je, talaka hizi mbili zitahesabiwa na kubakia moja kwa mkewe?  Au hazihesabiwi bali zitabaki tatu za asili?  'Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na hili katika kauli mbili:

Kauli Ya kwanza: 

Talaka ya mshirikina (mpagani) inapita na inahesabiwa.  Ni madhehebu ya Jumhuwr ya 'Ulamaa, na dalili zao ni:

1- Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliithibitisha ndoa ya mshirikina na akapitisha uhalali wake katika Uislamu.  Na hali kadhalika talaka, kwa kuwa talaka inathibiti kwa kuthibiti ndoa, na inadondoka kwa kudondoka ndoa. 

2-  Vipengele vya sharia vinamhusu kafiri.

Kauli Ya Pili: 

Talaka ya mshirikina haipiti na haihesabiwi.  Ni madhehebu ya Maalik, Daawuwd na Ibn Hazm.  Ni kauli pia ya Hasan, Qataadah na Rabiy-'ah.  Dalili walizotoa ni:

1-  Kauli Yake Ta'aalaa:

"قُل لِّلَّذِينَ كَفَرُوا إِن يَنتَهُوا يُغْفَرْ لَهُم مَّا قَدْ سَلَفَ وَإِن يَعُودُوا فَقَدْ مَضَتْ سُنَّتُ الْأَوَّلِينَ"

"Waambie waliokufuru kwamba wakikoma wataghufuriwa yaliyopita, lakini wakirudia, basi imekwishapita desturi ya watu wa awali".  [Al-Anfaal: 38]

2- Hadiyth ya 'Amri bin Al-'Aaswiy ya kwamba Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: 

"الإِسْلَامُ يَهْدُمُ مَا قَبْلَهُ"

"Uislamu unafutilia mbali yote (madhambi na maasi) yaliyofanywa nyuma (kabla ya mtu kusilimu)".  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Muslim na wengineo]

3- Wanaume walikuwa wanasilimu kwa Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam), na hakuwa akiwauliza idadi ya talaka walizozitoa kwa wake zao  kabla ya kusilimu. 

Ninasema:  "Hoja hizi ndizo zilizo karibu zaidi na usahihi.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi".