Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
طَلَاقٌ رَجْعِي
Talaka Rejea
26: Mume Na Mke Wakivutana Katika Suala La Kurejeana:
1- Ikiwa wawili watakhitilafiana kama kurejeana kumefanyika au la; mume akadai kwamba amemrejea jana kwa mfano na mke akakanusha, hapa mume atakubaliwa dai lake ikiwa mke bado yuko ndani ya eda. Hii ni kwa vile mume hapa ameeleza jambo ambalo bado analimiliki na ana mamlaka ya kulisema tena upya. Hivyo hawezi kukadhibishwa madai yake.
2- Ikiwa mume atadai baada ya eda kumalizika kwamba alimrejea mkewe wakati bado yuko ndani ya eda, na mke akakanusha, hapa hali itakuwa hivi:
(a) Ikiwa mume atathibitisha kwa dalili, basi ataruhusiwa kumrejea.
(b) Akishindwa kuleta dalili, basi mke ndiye atakayesikilizwa, kwa kuwa dai la mume la kumrejea limekuja katika wakati ambapo hawezi tena kumrejea.
3- Mume akimwambia mke aliye ndani ya eda: "Nimekurejea", na mke akamwambia: "Eda yangu ishamalizika", hapa hali itakuwa hivi:
(a) Ukiwa muda baina ya talaka na wakati ambapo mke anadai kumalizika eda unatosha kumalizika eda, basi kauli yake itakubaliwa, na kurejeana hakutawezekana.
(b) Lakini ikiwa muda huu hautoshi kumalizika eda, kwa kuwa ni mdogo kuliko muda wa eda kisharia, basi madai haya ya mke hayakubaliwi, na mume ataruhusiwa kumrejea baada ya kuthibitika uongo wake.
Ninasema: "Kwa muktadha wa yote haya, tunaona umuhimu wa kuhudhurisha mashahidi pamoja na kuthibitisha rasmi zoezi la talaka na kurejeana. Haitakikani kuyapuuza mambo haya, na hususan katika zama zetu za leo zilizojaa ujanja mwingi. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi".