Skip to main content

11A-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha كتاب الفرق بين الزوجين - Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume10-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Talaka Kutengana Mke Na Mume: Talaka Ya Anayefanya Mzaha

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

الطَّلَاقُ

Talaka

Alhidaaya.com 

10:  Talaka Ya Anayefanya Mzaha

(a)  Jumhuwr ya'Ulamaa wanasema kwamba mwenye kutamka tamko wazi la talaka hata kwa utani au kwa mchezo tu, na akawa amebaleghe na mwenye akili timamu, basi talaka yake inapita.  Haitomsaidia kudai na kusema:  "Nilikuwa ninacheza au natania tu, au sikukusudia talaka, au mfano wa hayo". Dalili zao ni:

1- Kauli Yake Ta'aalaa: 

"وَلَا تَتَّخِذُوا آيَاتِ اللَّـهِ هُزُوًا"

"Na wala msizifanyie mzaha Aayaat (na Shariy’ah) za Allaah".  [Al-Baqarah: 231]

2-  Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"ثَلَاثٌ جَدُّهُنَّ جَدٌّ وَهَزْلُهُنَّ جَدٌّ: النِّكَاحُ والطَّلَاقُ والرَّجْعَةُ" 

"Mambo matatu kweli yake ni kweli na utani wake ni kweli:  Ndoa, talaka na kumrejelea mke".  [Hadiyth Dhwa'iyf.  Imechakatwa na Abu Daawuwd (2194), At-Tirmidhiy (1184) na Ibn Maajah (2039) kwa Sanad Dhwa'iyf. Ina Hadiyth wenza Dhwa'iyf pia ambazo 'Ulamaa wa Hadiyth wamekhitilafiana kuhusu kuzitumia ili kuifanya Hadiyth hii kuwa Hasan.  Lakini pamoja na hivyo, Al-Albaaniy ameihasinisha katika Al-Irwaa (6/224)]

Wamesema:  "Lau kama hili litaachiwa kwa watu, basi hukmu ya kisharia haitofanya kazi, na wala mwenye kutaliki, au mwenye kuoa au mwenye kuacha huru asingesita kusema:  "Nilikuwa nasema kwa kutania tu", na kwa muktadha huu, sharia za Allaah zitakuwa ni zenye kutenguliwa, na hili bila shaka halifai.  Hivyo basi, yeyote atakayetamka lolote katika yaliyomo ndani ya Hadiyth hii, basi litapita, na hatokubaliwa kudai kinyume chake".  [Ma'aalimus Sunan cha Al-Khattwaabiy]

(b) Ama Maalik na wengineo, wao wanasema kwamba ili tamko wazi la talaka liweze kupita kisharia, ni lazima iwepo niya, mhusika ajue maana ya tamshi lenyewe na atake mwenyewe kwa hiari yake. Dalili zao ni hizi zifuatazo:

1- Kauli Yake Ta'aalaa:

"وَإِنْ عَزَمُوا الطَّلَاقَ فَإِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ"

"Na wakiazimia talaka, basi hakika Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote".  [Al-Baqarah:  227]

Wamesema:  "Aayah imesisitizia kuazimia, na mwenye kutania anakuwa hajaazimia alilolisema". 

Lakini wamejibiwa kwa kuambiwa kwamba kutolea dalili kwa aayah hii kimsingi si sahihi, kwa sababu aayah hii ilishuka kuhusiana na mtu aliyefanya "Iylaa" "إِيْلاءُ"(aliyemwapia mkewe kwamba hatomuingilia kwa muda wa miezi minne".

2-  Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam):

"إِنَّمَا الأَعْمَالُ بالنِّيَّاتِ..."

"Hakika si vinginevyo, matendo ni kwa mujibu wa niya".  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (1) na Muslim]