Skip to main content

11A-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha كتاب الفرق بين الزوجين - Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume11-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Talaka Kutengana Mke Na Mume: Masharti Ya Talaka: Masharti Ya Mwanamke Anayetalikiwa

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

الطَّلَاقُ

Talaka

Alhidaaya.com 

11: Masharti Ya Talaka: Masharti Ya Mwanamke Anayetalikiwa

Ili talaka ipite kwa mwanamke anayetalikiwa, ni lazima yawepo masharti haya yafuatayo:

1-  Ndoa iwe bado ipo kati yake na mumewe kiuhalisia au kihukumu.  Ni kama mtalikiwa kuwa bado ni mke, au awe yuko kwenye eda ya talaka rejea"طَلَاقٌ رَجْعِيْ" .  Ikiwa yuko eda kutokana na talaka mtengano, utengano mdogo "بَائِنٌ بَيْنُونَةٌ صُغْرَى", au talaka ya ndoa iliyovunjwa kwa amri ya mahakama (iliyofusakhiwa), hapa Jumhuwr wanasema kwamba talaka haitopita kwa kuwa ndoa haitokuwepo tena kutokana na hali hizi mbili. 

Na ikiwa mwanamke atatalikiwa kabla ya mume kumuingilia au kukaa naye faragha, basi mwanamke huyo hana eda.  Na hii ni kutokana na Kauli Yake Ta'aalaa: 

"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا ۖ فَمَتِّعُوهُنَّ وَسَرِّحُوهُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا"

"Enyi walioamini!  Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kujimai nao, basi hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu.  Basi wapeni kitoka nyumba na waacheni huru, kwa mwachano mzuri".  [Al-Ahzaab: 49]

Na hii ya kabla ya kumuingilia mke inakuwa ni talaka mtengano, utengano mdogo "بَائِنٌ بَيْنُونَةٌ صُغْرَى", na hivyo basi, hakuna talaka nyingine baada ya hapo kwa mujibu wa 'Ulamaa wa Kihanafiy na Kishaafi'iy.  Ikiwa mtu atamwambia mkewe ambaye hajawahi kumuingilia au kukaa naye faragha:  "Nimekuacha, nimekuacha, nimekuacha", basi haipiti hapo ila talaka moja tu, kwa kuwa kwa talaka ya kwanza tu, mke anakuwa hawezi tena kurejea kwa mume, na anakuwa mtu wa kando naye (ajnabiyya), na pia anakuwa hana tena talaka nyingine baada ya hapo. 

Lakini 'Ulamaa wa Kimaalik na Kihanbali wamesema kwamba kwa matamshi haya matatu mtawalia, talaka tatu zinapita, kwa kuwa matamshi yamepangana, hayajatengana.  Na kwa hivyo basi, mume anakuwa ashazitoa talaka tatu moja kwa moja kwa mke. 

2-  Mume amuainishe anayemtaliki kwa kuashiria, au kwa sifa au kwa kumkusudia.  Ikiwa amemuainisha anayemtaliki kwa ishara, kwa sifa na kwa niya, basi talaka itapita kwa itifaki ya 'Ulamaa.  Ni kama kumwambia mkewe Zaynab akimwelekea na kumkusudia:  "Ewe Zaynab, nimekuacha". 

Vile vile, akimwashiria mmoja kati ya wake zake bila kumuainisha kwa sifa yoyote wala kumkusudia mwingine, basi talaka itapita kwa itifaki ya 'Ulamaa. 

Na ikiwa atasema:  "Nimemtaliki mke wangu mmoja", akamkusudia mmoja wao bila kumwashiria yeyote kati yao, basi aliyemkusudia ndiye atakayeachika, na waliobaki watakuwa wamepona.

Na ikiwa amemwashiria mmoja lakini akamwelezea mwingine kama vile kumwambia mkewe Salmaa:  "Wewe, ewe Zaynab, nimekuacha", na Zaynab huyo pia ni katika wake zake, basi atakayeachika ni Salmaa aliyemwashiria, na si Salmaa ambaye hakumkusudia.

Pia, akimwashiria lakini akamwelezea kwa sifa asiyokuwa nayo, talaka inapita kwa mwashiriwa.