Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
الطَّلَاقُ
Talaka
12: Masharti Ya Talaka: Masharti Ya Tamko La Talaka
Asili ya talaka ni kuitamka kwa maneno, lakini katika baadhi ya nyakati mahala pa tamko panaweza kuwakilishwa na maandishi au ishara.
(a) Talaka Kwa Matamshi:
Tamko la talaka linaweza kuwa wazi la kufahamika au la kimafumbo.
1- Tamko wazi la kufahamika:
Hili ni lile ambalo likitamkwa linamaanisha talaka moja kwa moja bila kubeba maana nyingine, kwa kuwa halitumiki ila katika talaka tu, kilugha au kimazoea. Ni kama mtu kusema: "Nimekutaliki, au nimekuacha ". أَنْتِ طَالِقُ/طَلَّقْتُكِ/أَنْتِ مُطَلَّقَةُ]]
Tamko hili limetumika kwenye Qur-aan Tukufu kama Alivyosema Allaah Ta'aalaa:
"يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا الْعِدَّةَ"
"Ee Nabiy! Mtakapowataliki wanawake, basi watalikini katika wakati wa eda (twahaarah) zao, na hesabuni barabara eda". [At-Twalaaq: 01]
Na Neno Lake Ta'aalaa:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ"
"Enyi walioamini! Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kujimai nao". [Al-Ahzaab: 49]
Vile vile,
"وَلِلْمُطَلَّقَاتِ مَتَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُتَّقِينَ"
"Na wanawake waliotalikiwa wapewe kiliwazo (kitoka nyumba) kwa mujibu wa shariy’ah, ni haki juu ya wenye taqwa". [Al-Baqarah: 241]
Kwa upande wa 'Ulamaa wa Kishaafi'iy, Kihanbali na Kidhwaahiriyyah, wao wanayazingatia matamshi ya "Kufarikiana" "الفِرَاقُ"na "Kuachia" "السَّرَاحُ"kama matamshi wazi yenye maana ya talaka. "Kufarikiana" liko kwenye Kauli Zake Ta'aalaa:
"فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ فَارِقُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ"
"Basi wazuieni kwa wema, au farikianeni nao kwa wema." [At-Twalaaq: 02]
Na
"وَإِن يَتَفَرَّقَا يُغْنِ اللَّـهُ كُلًّا مِّن سَعَتِه"
"Na kama watafarikiana, basi Allaah Atamtosheleza kila mmoja kwa Wasaa Wake". [An Nisaa: 130]
Ama "Kuachia", hili liko kwenye Kauli Zake Ta'alaa:
"فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ"
"Hivyo kuzuia kwa mujibu wa shariy’ah au kuachia kwa ihsaan" [Al-Baqarah: 229]
Na pia,
"وَأُسَرِّحْكُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا"
"Na nikuacheni huru, mwachano mzuri". [Al-Ahzaab: 28]
Ninasema: "Kauli ninayoiona yenye nguvu ni ya 'Ulamaa wa Kimaalik na Kihanafiy kwamba matamshi ya "kufarikiana" na "kuachana" si ya wazi kwa talaka, bali ni mafumbo, kwa kuwa yanabeba pia maana nyingine zisizo talaka. Ni kama Kauli Zake Ta'aalaa:
"وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا"
"Na shikamaneni kwa Kamba ya Allaah nyote pamoja, wala msifarikiane". [Aal 'Imraan: 103]
Na Kauli Yake:
"وَمَا تَفَرَّقَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ إِلَّا مِن بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَةُ"
"Na hawakufarikiana wale waliopewa kitabu isipokuwa baada ya kuwajia hoja bayana". [Al-Bayyinah: 04]
Maneno haya mawili hapa "msifarikiane" na "hawakufarikiana" hayana uhusiano kabisa na talaka ya ndoa kama tunavyoona.
Sambamba na hayo, ni vyema ijulikane hapa kwamba kugawa matamko kwenye matamko wazi na matamko fumbo, ingawa jambo hili ni sahihi katika uasili wa hali, lakini ugawaji huu unatofautiana kwa mujibu wa utofauti wa watu, nyakati na mahala. Si hukumu thabiti kwa tamko lenyewe. Tamko wazi kwa watu fulani linaweza kuwa fumbo, au likawa wazi katika zama fulani au mahala fulani kisha likabadilika kuwa fumbo katika zama nyingine au mahala. Na uhalisia wa hali uko wazi. Kuna tamko hili "السَّرَّاحُ" ambalo kwa sasa hakuna anayelitumia tena, si kwa talaka ya tamko wazi wala la fumbo, limeshakufa kimatumizi. Haiwezekani kwa mtu anatayelitamka aambiwe kwamba amemtaliki mkewe, ni sawa akiwa amenuwia au hajanuwia.
Niya Si Sharti Ya Kupita Talaka Ya Tamko Wazi:
Mtu akitamka tamko wazi la talaka, na hata kama alikusudia vingine, basi talaka yake itapita kwa mujibu wa sheria za mahakama. Na hali ni hivyo hivyo, kama atatamka tamko hilo wazi kisha akasema "Sikukusudia kwalo lolote", basi talaka pia itapita. Na lau atasema: "Nimekusudia kinyume na talaka", basi haitopita kwa mujibu wa sharia za kimahakama, bali itapita kwa mujibu wa sharia za kidini, lakini kwa sharti kwamba tamko lisiwe limeambatana na vielelezo vinavyoashiria ukweli wa nia yake ya kukusudia jinginelo lisilo talaka. Ikiwa kitapatikana kielelezo kinachoashiria kutokukusudia talaka, basi atasadikishwa mahakamani pia, na ikithibitika kweli, basi talaka yake haitopita, na atahesabiwa kama aliyekosea au aliyelazimishwa kama ilivyoelezwa nyuma.
Na kwa muktadha huu, inashurutishwa kwa atakayetamka tamko wazi la talaka afahamu maana yake na alichague.
Ama tamko fumbo, nalo ni lile ambalo halitumiki maalumu kwa talaka bali pia linabeba maana tofauti, hili, ikiwa halijabeba maana ya talaka, basi haliwi ni fumbo, bali litakuwa ni upuuzi tu, na halitoleta madhara yoyote kwa ndoa.
Mfano wa matamshi fumbo ni kama mtu kusema: "سَرَّحْتُكِ" “Nimekuachilia”, "أَنْتِ مُسَرَّحَةٌ" “Umeachiliwa”, "فَارَقْتُكِ" “Nimefarikiana nawe”, "أَنْتِ مُفَارَقَةٌ" “Wewe umeachwa”.
Matamshi mengine kwa mujibu wa baadhi ya 'Ulamaa ni:
"اعْتَدِّيْ"“Kakae eda”, "اسْتَبْرَئِيْ رَحِمَكِ" “Kasubirie tumbo la uzazi lisafike”, "الْحَقِيْ بِأَهْلِكِ" “Nenda kwa jamaa zako”, "أَنْتِ خَلِيَّةٌ" “Huna lako jambo”, "أَنْتِ مُطْلَقَةٌ" “Uko huru” na mfano wa hayo.
Ni lazima iwepo niya ili talaka ya tamko fumbo ipite, kwa kuwa tamko linabeba maana ya talaka na maana nyinginezo. Hivyo basi, tamko haliwezi kupelekwa kwenye maana ya talaka ila kwa nia na makusudio ya mtu.
Faida: Je, Vielelezo Vya Hali Vinawakilisha Mahala Pa Niya Katika Kupita Talaka Fumbo?
Ikiwa mtu anagombana na mkewe na hasira kali zimempanda, akamwambia mkewe: "Nenda kwa jamaa zako", lakini hakukusudia kwa tamko hilo talaka, je talaka inapita?
1- 'Ulamaa wa Kihanafiy wanaona kwamba vielelezo vya hali vinawakilisha mahala pa niya katika talaka fumbo. Hivyo katika hali hii (ugomvi na hasira), talaka inapita hata kama hajaikusudia.
2- 'Ulamaa wa Kimaalik na Kishaafi'iy hawazingatii hapa vielelezo vya hali (ugomvi na hasira kali). Wanasema kwamba talaka hapa haipiti kwa tamshi hilo la fumbo ila tu kama mume atakusudia kwalo talaka.
Ninasema: "Kauli hii ndiyo yenye nguvu zaidi. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi".
Talaka Haipiti Mtu Akimtaliki Mkewe Moyoni Bila Kutamka:
Ni kwa Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) iliyopokelewa na Abu Hurayrah:
"إِنَّ اللهَ تَجَاوَزَ عَنْ أُمَّتِي مَا حَدَّثَتْ بهِ أَنْفُسُهَا مَا لَمْ تَعْمَلْ أَوْ تَتَكَلَّمْ"
"Hakika Allaah Ameusamehe ummati wangu yale ambayo nafsi zao zimewazungumzisha madhali hawakuyafanya au kuyazungumza". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5269) na Muslim (127)]
Hii ni kauli ya 'Ulamaa wote.