Skip to main content

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

طَلَاقٌ رَجْعِي

Talaka Rejea 

Alhidaaya.com 

28:  Talaka Mtengano "طَلَاقٌ بَائِنٌ":

Hii ni talaka ambayo mume anakuwa hana tena haki ya kumrejea mtalaka wake, nayo ni ya aina mbili: 

1- Talaka Mtengano, Utengano Mdogo "طَلَاقٌ بَائِنٌ بَيْنُونَةٌ صُغْرَى"

2- Talaka Mtengano, Utengano Mkubwa "طَلَاقٌ بَائِنٌ بَيْنُونَةٌ كُبْرَى"

(a) Talaka Mtengano, Utengano Mdogo "طَلَاقٌ بَائِنٌ بَيْنُونَةٌ صُغْرَى"

Hii ni talaka ambayo mume anakuwa hana tena haki ya kumrejea mtalaka wake isipokuwa kwa kufunga naye ndoa nyingine mpya kwa mahari mapya.  Talaka hii inabeba athari zifuatazo: 

1- Mafungamano ya kindoa yanakatika, na mwanamke mtalikiwa anakuwa ni mtu wa mbali (ajnabiyya) kwa mumewe. Kadhalika, haki anazopaswa kila mmoja juu ya mwenzake zitaondoka isipokuwa fedha za matumizi kwa mwanamke ikiwa ni mja mzito, ni lazima mume ampatie. 

Ikiwa mume atataka kumrejea mtalaka wake huyu, itabidi afunge naye ndoa upya kwa mahari mengine mapya. 

2- Mume hana tena haki ya kumrejea katika kipindi cha eda.  Lakini anaweza kufunga naye ndoa mpya kwa mahari mapya ikiwa mwenyewe ataridhia, ni sawa akiwa bado yuko kwenye eda au baada ya kumalizika eda. 

3- Ni lazima mume alipe sehemu ya mahari iliyobakia ambayo alikuwa hajailipa. 

4-  Masuala yafuatayo yanakuwa hayapo tena: 

Kurithiana kati yao, mume kufanya "Dhwihaar”  "ظِهَارٌ" (kumfananisha mkewe na mtu ambaye ni maharimu wake wa milele), au kufanya “Iylaa" "إِيْلاءُ" (kumwapia mkewe kwamba hatomuingilia kwa muda wa miezi minne),  au kuwepo "Li'aan" "لِعَانُ" (hatua ya kisharia inayofanyika kati ya mke na mume wakati mume anapomtuhumu mkewe kwamba amezini bila kuwa na mashahidi, au kudai mtoto si wake). 

5-  Talaka hii inapunguza idadi ya talaka anazomiliki mume.   Ikiwa mume atamrejea kwa ndoa mpya kabla hajaolewa na mume mwingine baada ya talaka moja mtengano "بَائِنٌ", basi atarudi kwenye ndoa na mume atabakiwa na talaka mbili tu mkononi.  Hukumu inakuwa hivyo hivyo ikiwa atamrejea kwa ndoa mpya baada ya mtalaka kuolewa na mwanaume mwingine kisha akamwacha, au akafa kabla hajamuingilia.  Hili halina mvutano kati ya 'Ulamaa. 

Ama hali nyinginezo tofauti na hizi, kuna makhitilafiano kati ya 'Ulamaa katika kuhesabu idadi ya talaka.  Makhitilafiano haya tutayaona katika suala lifuatalo la "Kufutika Talaka".