Skip to main content

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

طَلَاقٌ رَجْعِي

Talaka Rejea 

Alhidaaya.com 

29: Kufutika Talaka:

Mtu akimtaliki mkewe mara moja au mbili, kisha akaolewa na mtu mwingine, na mtu huyu akamtaliki, kisha mume wa mwanzo akamwoa tena, je hapa, talaka alizompa mwanzo zitaendelea kuhesabika na mke atarejea na zile zilizobakia kati ya tatu?  Au kuolewa na mume mwingine kutakuwa kumefuta talaka za mwanzo, na mume ataanza tena upya na talaka tatu kamili mkononi?

'Ulamaa wamekhitilafiana katika kauli mbili kuhusiana na suala hili:

Kauli Ya Kwanza:

Talaka zilizotangulia zitahesabiwa.  Mke atarejea kwa mume wake wa awali na talaka zile tu zilizobakia.  Ikiwa alimpa talaka moja, basi mke atarudi zikiwa zimebakia mbili tu, na zikiwa mbili, basi itakuwa imebakia moja ya mwisho.

Hii ni kauli ya 'Umar bin Al-Khattwwaab, 'Aliy, 'Imraan bin Huswayn, Abu Hurayrah na Maswahaba wengineo (Radhwiya Allaah 'anhum).   Vile vile ni kauli ya Ibn Al-Musayyib, Al-Hasan, Ath-Thawriy, Muhammad bin Al-Hasan, Maalik, Ash-Shaafi'iy, Is-Haaq, Abu 'Ubayd, Abu Thawr na Ibn Al-Mundhir. Dalili zao ni:

1-  Fatwaa ya 'Umar kuhusiana na hili.  Toka kwa Abu Hurayrah, amesema:

سَأَلْتُ عُمَرَ بن الخَطَّابِ عَنْ رَجُلً مِنْ أَهْلِ البَحْرَيْنِ طَلَّقَ امْرَأَتَهُ تَطْلِيْقَةً أَوْ تَطْلِيْقَتَيْنِ ثُمَّ انْقَضَتْ عِدَّتُهَا، فَتَزَوَّجَهَا رَجُلٌ غَيْرُهُ ثُمَّ طلَّقَهَا أَوْ مَاتَ عَنْهَا، ثُمَّ تَزَوَّجَهَا زَوْجُهَا الأَوَّلُ، قَالَ: هي عِنْدَهُ على مَا بَقِيَ"

"Nilimuuliza 'Umar bin Al-Khattwaab kuhusiana na mtu kutoka Bahrain.  Mtu huyu alimtaliki mkewe talaka moja au mbili, kisha eda yake ikamalizika.  Halafu mwanamke huyu akaolewa na mtu mwingine, kisha mume huyu akamtaliki au alifariki, halafu mume wake wa awali akamwoa tena.  'Umar akasema: “Mume atabaki na talaka zilizosalia kwa mkewe".  Isnaad yake ni swahiyh.  [Imechakatwa na Ash-Shaafi'iy kama ilivyo kwenye Musnad yake (2/125)]

2-  Ndoa ya mume wa pili ndiyo inayofuta uharamu wa kuolewa tena mwanamke aliyeachwa talaka tatu na mume wake wa awali kutokana na Kauli Yake Ta'aalaa: 

 "فَإِن طَلَّقَهَا فَلَا تَحِلُّ لَهُ مِن بَعْدُ حَتَّىٰ تَنكِحَ زَوْجًا غَيْرَهُ"

"Na akimtaliki (mara ya tatu), basi hatokuwa halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwengine".  [Al-Baqarah: 230] 

Wanasema hivi kwa sababu mume akimpa mkewe talaka tatu, kisha akaolewa na mtu mwingine, halafu akaja kumwoa tena kwa ndoa mpya, hapo atakuwa na talaka zingine tatu mpya mkononi.  Na hii ni kwa mujibu wa itifaki ya ‘Ulamaa. 

Kauli Ya Pili:

Ndoa ya mume wa pili inafuta talaka zote za mwanzo. Mke atarejea kwa mume wake wa awali, na mume ataanza tena upya akiwa na  talaka tatu mkononi. 

Ni kauli ya Ibn 'Umar na Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaah 'anhumaa) pamoja na 'Atwaa, An-Nakh-'iy, Shurayh, Abu Haniyfah na Abu Yuwsuf.  Pia, ni riwaayah nyingine toka kwa Ahmad.  Dalili zao ni:

1-  Jimai ya mume wa pili inafungua uhalali wa kuolewa tena mwanamke na mume wake wa awali kwa aqdi mpya na mahari mapya. 

2-  Itifaki ya ‘Ulamaa wote imekita kwamba jimai ya mume wa pili, inafuta talaka zote tatu za mume wa awali.