Skip to main content

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume 

الطَّلَاقُ

Talaka

Alhidaaya.com 

13: Mtu Akimwambia Mkewe: “Wewe Ni Haramu Kwangu” Je Itazingatiwa Ni Talaka?

Hakuna ndani ya Qur-aan Tukufu wala katika Hadiyth za Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) aayah au matini yoyote iliyo wazi, iliyo sahihi au inayotegemewa kuhusiana na hukumu ya suala hili.  Na kwa ajili hiyo, 'Ulamaa wamevutana sana na wakakhitilafiana kwa kauli nyingi.  Ibn Hazm amezitaja kauli 12 kati ya hizo huku Ibn Al-Qayyim akitaja madhehebu 13 asili ambayo yalijigawa na kufikia hadi 23.  Lakini, kauli zilizo karibu zaidi kuzingatiwa ni hizi nne: 

Kauli Ya Kwanza: 

Akikusudia kwa tamko lake hilo talaka, basi talaka inapita, na kama hakukusudia, basi itakuwa ni kiapo (yamini ya kuharamisha halali ambayo ni lazima itolewe kafara kama ilivyotajwa kwenye Qur-aan).    

Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, na Maalik (kwa mwanamke aliyeingiliwa), Ash-Shaafi-'iy na riwaayah toka kwa Ahmad.  Na hoja yao wanasema tamko la talaka linaweza kufumbiwa, lakini kwa wale tu walioshurutisha niya ili talaka ipite kama ilivyotangulia nyuma.  Na kama hakuna niya ya talaka, basi (tamko hili la mume kumwambia mkewe kwamba ni haramu kwake) litakuwa ni kiapo (yamini) kutokana na Neno Lake Ta'aalaa:

"يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ لِمَ تُحَرِّمُ مَا أَحَلَّ اللَّـهُ لَكَ ۖ تَبْتَغِي مَرْضَاتَ أَزْوَاجِكَ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ قَدْ فَرَضَ اللَّـهُ لَكُمْ تَحِلَّةَ أَيْمَانِكُمْ ۚ وَاللَّـهُ مَوْلَاكُمْ ۖ وَهُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ"

"Ee Nabiy!   Kwa nini unaharamisha kile Alichokuhalalishia Allaah?  Unataka kuwaridhisha wake zako!   Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu • Allaah hakika Amekuwekeeni shariy’ah ya ukomboaji wa viapo vyenu, na Allaah Ni Mola wenu,  Naye Ndiye Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote ".  [At-Tahriym: 1-2]

Al-Qurtubiy amesema:  "Kukomboa kiapo ni kwa kutoa kafara".

Kauli Ya Pili: 

Tamko hili litazingatiwa kuwa ni "Dhwihaar  "ظِهَارٌ"ni sawa akikusudia 

“Dhwihaar” au asiikusudie, na ni juu yake mume atoe kafara ya “Dhwihaar”.   

["Dhwihaar  "ظِهَارٌ"ni mume kumfananisha mkewe na mtu ambaye ni maharimu wake wa milele kama mama yake au dada yake kwa kumwambia kwa mfano:  “Wewe nakuona kama mama yangu tu”]

Ni madhehebu ya Ahmad na kauli ya Ash-Shaafi'iy, lakini pia imepokewa kwa njia sahihi toka kwa Ibn 'Abbaas.

Hoja ya kauli hii ni kwamba Allaah Ta'aalaa Amekufanya mtu kumfananishia mkewe na mtu aliye haramu kwake milele kuwa ni "Dhwihaar".  Ibn Al-Qayyim akiiandamizia hoja hii amesema:”

“Hii ndiyo kauli iliyonyooka zaidi kuliko zingine. Inazatitiwa pale tunapoona kwamba Allaah Mtukufu Hakumruhusu mtu yeyote kuhalalisha au kuharamisha jambo lolote, bali jukumu hilo ni Lake Yeye tu.  Mtu akisema kumwambia mkewe: “Wewe nakuona kama mgongo wa mama yangu”, au “Wewe ni haramu kwangu”, basi atakuwa ametamka kauli mbaya, ya uzushi na ya kumwongopea Allaah Ta’aalaa.  Kwani Allaah Hakumharamishia mtu mkewe, au kumfanya kuwa kama mgongo wa mama yake.  Na kwa ajili hiyo, Amewajibisha kafara nzito ya "Dhwihaar  "ظِهَارٌ"kutokana na kauli hii mbaya ya uzushi”. 

Kauli Ya Tatu: 

Ni kiapo (yamini) ambacho kinafutwa na kafara ya kiapo, ni sawa akiwa alikusudia talaka au hakukusudia.

Ni madhehebu ya Al-Awzaa'iy na Abu Thawr, lakini pia ni kauli ya Abu Bakr, 'Umar, Ibn 'Abbaas, 'Aaishah, Zayd bin Thaabit, Ibn Mas-'uwd na wengineo.  Hoja ya kauli hii ni:

1-  Kauli Yake Ta'aalaa:

"يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ لِمَ تُحَرِّمُ مَا أَحَلَّ اللَّـهُ لَكَ ۖ تَبْتَغِي مَرْضَاتَ أَزْوَاجِكَ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ قَدْ فَرَضَ اللَّـهُ لَكُمْ تَحِلَّةَ أَيْمَانِكُمْ ۚ وَاللَّـهُ مَوْلَاكُمْ ۖ وَهُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ"

"Ee Nabiy!   Kwa nini unaharamisha kile Alichokuhalalishia Allaah?  Unataka kuwaridhisha wake zako!  Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu • Allaah hakika Amekuwekeeni shariy’ah ya ukomboaji  wa viapo vyenu, na Allaah Ni Mola wenu,  Naye Ndiye Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote ".  [At-Tahriym: 1-2]

Na sababu ya kushuka aayah hii ni pale Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipojiharamishia mwenyewe kukaa muda mrefu kwa baadhi ya wakeze na kunywa asali.

Toka kwa 'Aaishah (Radhwiya Allaah anhaa): 

"كَانَ رسولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَشْربُ عَسَلًا عِنْدَ زَينبَ بنتِ جِحْشٍ وَيمْكُثُ عِنْدَهَا، فتواطَأْتُ أنا وَحَفْصَةُ أنْ أيَّتَنا دَخَلَ عليها النَّبيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فلتقُلْ إنِّي أجدُ مِنْكَ رِيْحَ مَغَافِيرَ! أَكَلْتَ مَغَافِيْرَ؟! فَدَخَلَ عَلى إِحْدَانَا، فَقَالَتْ لَهُ ذلِكَ فَقَالَ: لا! ولكنِّيْ كُنْتُ أَشْرَبُ عَسَلًا عِنْدَ زينبَ بِنْتِ جَحْشٍ فَلَنْ أَعُوْدَ، وقَدْ حَلَفْتُ، لا تُخْبِرِيْ بِذلِكَ أَحَدًا"

“Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anakaa kwa Zaynab bint Jahsh na kunywa asali.  Nikakubaliana kwa siri mimi na Hafswah kwamba yeyote kati yetu sisi wawili ambaye Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) ataingia kwake, basi amwambie kwamba anamsikia kunuka harufu ya "maghaafiyr" (gundi ya mti yenye harufu mbaya) na amuulize:  Je, umekula maghaafiyr?!  Na Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoingia kwa mmoja wetu alimwambia maneno hayo, naye akasema:  Hapana, sijala, bali nilikuwa kwa Zaynab bint Jahsh nikinywa asali, basi sitokunywa tena.  Nami nimeshaapa (kwamba sitokunywa), usimweleze yeyote hilo".  [Hadiyth Swahiyh.  Al-Bukhaariy (4912) na Muslim]

Katika tamko la Al-Bukhaariy ipo ziada isemayo:  “Na hapo ikateremka:

"يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ لِمَ تُحَرِّمُ مَا أَحَلَّ اللَّـهُ لَكَ"

"Ee Nabiy!  Kwa nini unaharamisha kile Alichokuhalalishia Allaah?”

2-  Toka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaah 'anhu), amesema: 

"إِذَا حَرَّمَ الرَّجُلُ امرَأَتَهُ، فَهِيَ يَمِيْنٌ يُكَفِّرُهَا، وَقَالَ:"لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ"

"Mtu akimwambia mkewe:  Wewe kwangu ni haramu, basi inakuwa ni kiapo cha kutolewa kafara (si talaka), na akasoma:  Kwa yakini mna kigezo kizuri kwa Rasuli wa Allaah".  Al-Ahzaab: 21 [Hadiyth Swahiyh.  Muslim ameichakata kwa tamko hili (1473)] 

Kauli Ya Nne: 

Ni upuuzi na batili, na hakuna lolote la kuzingatiwa, si talaka wala yamini. 

Ni kauli ya wafuasi wa madhehebu ya Adh-Dhwaahiriyyah na Aswhaabul Hadiyth ('Ulamaa wenye kutohoa hukumu za kisharia toka kwenye Qur-aan na Sunnah, hawazingatii rai na qiyaas), moja ya kauli mbili za 'Ulamaa wa Kimaalik, na pia ni kauli iliyopokelewa toka kwa Ibn 'Abbaas.  Hoja yao ni haya yafuatayo:

1- Hadiyth iliyopita ya 'Aaishah:  Al-Haafidh amesema:   

“Al-Qurtubiy na wengineo wametolea dalili kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Nami nimeshaapa (kwamba sitokunywa)”, kwamba kafara hapa inakuwa ni kwa ajili ya yamini (kiapo) na si kuharamisha tu.  Na hii ni dalili yenye nguvu kwa wenye kauli isemayo kwamba kuharamisha ni upuuzi usiokuwa na kafara”. 

2-  Allaah Ta'aalaa Amesema:

"لِمَ تُحَرِّمُ مَا أَحَلَّ اللَّـهُ لَكَ"

"Kwa nini unaharamisha kile Alichokuhalalishia Allaah?".  [At-Tahriym: 01]

Hapa Allaah Ta'alaa Anamshangaa Rasuli Wake kujiharamishia kile ambacho Yeye Amemhalalishia.  Na mke ni katika Alivyovihalalisha Allaah, na kumharamisha ni munkari, na munkari ni jambo linalokataliwa, nalo halina hukumu nyingine zaidi ya mtu kutubia na kuomba maghfira kwa Allaah.

3—Toka kwa Ibn 'Abbaas, amesema:  

"إِذَا حَرَّمَ الرَّجُلُ امرَأَتَهُ، فَهِيَ يَمِيْنٌ يُكَفِّرُهَا، وَقَالَ: "لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ"

"Mtu akimwambia mkewe:  Wewe kwangu ni haramu", basi neno hilo linakuwa ni yamini ambayo ni lazima aitolee kafara (na si talaka), na akasoma:  Kwa yakini mna kigezo kizuri kwa Rasuli wa Allaah".  [Hadiyth Swahiyh.  Muslim ameichakata kwa tamko hili (1473)] 

4- Allaah Ta'aalaa Amesema: 

"وَلَا تَقُولُوا لِمَا تَصِفُ أَلْسِنَتُكُمُ الْكَذِبَ هَـٰذَا حَلَالٌ وَهَـٰذَا حَرَامٌ لِّتَفْتَرُوا عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ لَا يُفْلِحُونَ"

"Na wala msiseme kwa ndimi zenu zinazopambia uongo:  Hii ni halali na hii ni haramu ili mumtungie Allaah uongo.  Hakika wale wanaomtungia Allaah uongo hawafaulu".  [An-Nahl: 116]

Hivyo basi, atakayemwambia mkewe ambaye ni halali kwake kwa Sharia ya Allaah kwamba ni haramu kwake, basi amesema uongo na amezua, na wala mkewe huyo hawi ni haramu kwake kwa tamko lake hilo, ila kwa namna ambayo Allaah Amemharamishia kwayo. 

5-  Neno lake Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam):

"مَنْ أَحْدَثَ فِي أَمْرِنَا هذا ما لَيْسَ مِنْهُ فَهُوَ رَدٌّ"  

"Atakayezusha katika jambo letu hili (dini yetu) lisilokuwemo, basi uzushi huo haukubaliwi". [Hadiyth Swahiyh] 

Kuhalalisha haramu si katika Maamrisho ya Allaah Ta'aalaa, na kwa hivyo hilo linakataliwa. 

Kauli Yenye Nguvu:

Ninaloliona kuwa ni lenye nguvu baada ya kuzitafiti kwa kina dalili zilizotolewa, ni kusema:

Anayemwambia mkewe:  "Wewe ni haramu kwangu", basi hakosi moja kati ya hali mbili:

Ya kwanza:  Awe hakukusudia talaka, kwa maana kwamba amekusudia kumharamisha mwanamke mwenyewe tu. Huyu kauli yake itazingatiwa ni upuuzi na batili, na hakuna chochote juu yake.   

Ya pili:  Awe amekusudia talaka.  Lililo dhahiri hapa ni kwamba hakuna kizuizi cha kuliunganisha tamko lake hili na matamko mengineyo ya kimafumbo ambayo kwayo talaka inapita inapokuwepo niya ya kuacha, tukijua kwamba matamko hayazingatiwi yenyewe kama yenyewe, bali kwa mujibu wa makusudio ya mtamkaji. 

Hivyo basi, ikiwa atatamka neno linaloashiria maana, na akakusudia kwa neno hilo maana hiyo, basi hukumu yake itapita.  Na kwa ajili hiyo, Allaah Ta'aalaa Ametaja talaka na wala Hakuainisha kwayo tamko maalum, bali Amewaachia hilo watu wenyewe watumie matamko yenye maana hiyo kwa mujibu wa ada na desturi.  Kwa mantiki hii, neno lolote lenye maana ya talaka kwao linapita na talaka inatuka sambamba na niya, na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

Ama ya kwamba talaka inapita kwa "Dhwihaar  "ظِهَارٌ", ikiwa hili ni sahihi, basi Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) angetoa kafara ya "Dhwihaar", na lau angelifanya hivyo, basi habari kuhusu hilo ingetangaa na kuwafikia watu.  Na kwa vile haijatangaa, basi ni wazi kabisa kwamba hakufanya. 

["Dhwihaar" ni mume kumfananisha mkewe na mtu ambaye ni maharimu wake wa milele kama mama yake au dada yake kwa kumwambia kwa mfano:  “Wewe nakuona kama mama yangu tu”]