Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
الطَّلَاقُ
Talaka
14: Talaka Kwa Maandishi Na Ishara
Kwa mujibu wa rai ya Jumhuwr ya 'Ulamaa wakiwemo Maimamu wanne na wengineo, ikiwa mume yuko mbali, akamwandikia mkewe (barua au kwa njia yoyote) kwamba amemtaliki, basi talaka itapita kama ameikusudia. Dalili ya maneno haya ni:
1- Hadiyth ya Faatwimah bint Qays:
"أَنَّ أَبَا عَمْرو بن حَفْصِ طَلَّقَهَا أَلْبَتَة وَهُوَ غَائِبٌ، فَأَرْسَلَ إِلَيْهَا وَكِيْلَه بِشَعِيْرٍ فَسَخِطَتْهُ، فَقَالَ: والله مَالَكِ عَليْنَا مِنْ شَيءٍ، فَجَاءَتْ رَسُولَ الله فَذَكَرَتْ لَهُ، فَقَالَ: "لَيْسَ لَكِ علَيْهِ نَفَقَةٌ."
"Kwamba Abu 'Amri bin Hafsw alimtaliki talaka tatu mpigo akiwa safarini. Akamtuma mwakilishi wake ampelekee ngano (mtalaka wake), naye (Faatwimah) hakuridhishwa na hilo. (Mwakilishi) akamwambia: "Wa-Allaah, huna chochote juu yetu (si chakula wala makazi)". Akamwendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumshtakia, na Rasuli akamwambia: Si wajibu wake tena kukupa matumizi". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Muslim (1480) na Abu Daawuwd (2284)]
2- Toka kwa Az-Zuhriy, amesema: "Mume akimwandikia mkewe talaka, basi talaka itapita. Na kama mume atakanusha, basi atatakwa aape”. [Isnaad yake ni swahiyh. Imechakatwa na 'Abdulrazzaaq (11433)]
3- Toka kwa Al-Hasan Al-Baswriy kuhusiana na mtu aliyeandika barua ya kumtaliki mkewe kisha akaifuta kabla ya kuitamka, amesema: "Hakuna kitu, ila tu kama ataiacha kama ilivyo, au aitamke". [Isnaad yake ni swahiyh. Imechakatwa na Sa'iyd bin Mansouwr]
4- Toka kwa Ibraahiym An-Nakh-'iy, amesema: "Mtu akiandika kwa mkono wake talaka, basi itakuwa ni talaka". [Isnaad yake ni Swahiyh. Imechakatwa na Sa'iyd bin Mansuwr]
5- Kwa vile kuandika ni kwa herufi ambazo kwazo hufahamika makusudio. Ikiwa aliyoyaandika mume ni talaka kwa mkewe na yakafahamika hivyo, lakini pia akakusudia, basi talaka inapita sawa na iliyotamkwa kwa kinywa.
Lakini kwa upande mwingine, Abu Muhammad bin Hazm (Rahimahul Laah) anaona kwamba talaka haipiti ila kwa kutamkwa. Ama ya maandishi, yeye haikubali!!
Hadiyth ya Faatwimah bint Qays iliyotajwa ni hoja dhidi yake. Na lililo sahihi ni kwamba talaka ya maandishi inapita kama imeambatana na niya. Ikiwa hakunuwia talaka, basi haipiti kwa mujibu wa rai ya Jumhuwr, kwa kuwa kuandika kunaweza kubeba mambo kadhaa. Anaweza kuwa alikuwa anaijaribu kalamu, au anafanya zoezi la kuboresha mwandiko wake na kadhalika.
Na ili talaka ya maandishi iweze kupita, 'Fuqahaa wa Kihanafiy wameiwekea masharti mawili:
La kwanza: Iandikwe kwenye karatasi, au ukutani au popote pale kwa namna ya kuweza kusomeka na kufahamika.
La pili: Itumwe kwa jina la mke mkusudiwa.
Faida:
1- Akimtumia talaka hii ya maandishi kwa njia ya mitandao ya kisasa kama whatsup kwa mfano, na akawa ameiandika kwa mkono kwa hati zake maarufu, basi talaka itapita. Na kama ameandika kwa "keyboard", linaloonekana ni kwamba haipiti talaka mpaka mke ahakikishe kwamba mumewe ndiye aliyeandika ili asije akahadaiwa.
2- Baadhi ya 'Ulamaa wameshurutisha mashahidi wawili waadilifu washuhudilie kwamba barua inatoka kweli kwa mume.
Ibn Qudaamah (7/239) amenukuu toka kwa Ahmad kwamba mwanamke mmoja ilimjia barua ya talaka toka kwa mumewe kwa mwandiko wake na muhuri wake huku akimweleza kwamba asiolewe mpaka washuhudie mashahidi waadilifu (kwamba ameachika kupitia barua). Ahmad akaulizwa: Je, itatosha ushahidi wa aliyeleta barua? Akasema hapana, bali lazima wawe mashahidi wawili. Hakukubali kauli ya mleta barua tu, bali lazima na mwingine awe pamoja naye.
Talaka Kwa Ishara:
Mwenye uwezo wa kutamka na kusema, basi talaka yake ya maandishi haipiti kwa mujibu wa rai ya Jumhuwr ya 'Ulamaa kinyume na 'Ulamaa wa Kimaalik. Ama bubu, Jumhuwr wanasema kwamba talaka yake inapita kwa ishara. Lakini 'Ulamaa wa Kihanafiy wameweka sharti kwamba ni lazima bubu huyu awe hawezi kuandika, na kama anaweza kuandika, basi ishara haitokubaliwa, bali maandishi, kwani ndiyo yenye kubainisha zaidi makusudio.