Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
الطَّلَاقُ
Talaka
15: Kuhudhurisha Mashahidi Wa Talaka
Jumhuwr ya 'Ulamaa na Maimamu wengineo, wanaona kwamba inapendeza mtu kuhudhurisha mashahidi kwa talaka yake ili kulinda haki na kuzuia migogoro kati yake na mtalaka wake. Allaah Ta'aalaa Anasema:
"فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ فَارِقُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ وَأَشْهِدُوا ذَوَيْ عَدْلٍ مِّنكُمْ وَأَقِيمُوا الشَّهَادَةَ لِلَّـهِ"
"Na watakapokaribia kufikia muda wao, basi wazuieni kwa wema, au farikianeni nao kwa wema, na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu, na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Allaah". [At-Twalaaq: 02]
'Ulamaa hawa wameipa amri ya kushuhudishia talaka mashahidi wawili daraja ya kuwa jambo lenye kupendeza tu lakini si waajib. Hili linatiliwa nguvu na:
1- Hadiyth ya Ibn 'Umar:
"أنَّهُ طَلَّقَ امرأتَهُ وهيَ حائضٌ عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ، فَسَأَل عُمَرُ بن الخَطَّابِ رَسُولَ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنْ ذلِكَ، فقال رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: مُرْهُ فليُراجِعْهَا ثم ليُطلِّقْها طاهرًا أو حاملًا"
"Ni kwamba alimtaliki mkewe akiwa kwenye hedhi enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na 'Umar bin Al-Khattwwaab akamuuliza Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na kitendo hicho, na Rasuli akamwambia: Mwamuru amrejelee mkewe, kisha amtaliki akiwa twahara, au mjamzito". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5251) na Muslim (1471)]
Hapa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuamuru wawepo mashahidi wa kutaliki wala wa kumrejelea mke.
2- Toka kwa Ibn 'Umar, kwamba:
"أنَّهُ طَلَّقَ امرأتَهُ صَفِيَّةَ بنتَ أَبِيْ عُبَيْد تَطْلِيْقَةً أَوْ تَطْلِيْقَتَيْنِ فَكَانَ لَا يَدْخُلُ عَلَيْهَا إِلاّ بِإِذْنٍ، فَلَمَّا رَاجَعَهَا أَشْهَدَ علَى رَجْعَتِهَا وَدَخَلَ عَلَيْهَا"
“Alimtaliki mkewe Swafiyyah bint Abiy 'Ubayd talaka moja au mbili, na akawa haingii kwake ila kwa kuomba ruksa. Na alipomrejelea, alishuhudisha kumrejelea kwake, na akamuingilia. [Isnaad yake ni swahiyh. Imechakatwa na Al-Bayhaqiy (7/373)]
3- Kwenye aayah mbalimbali na hata kwenye Hadiyth za Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam), talaka imetajwa bila kufungamanishwa na uwepo wa mashahidi.
4- Talaka ni katika haki za mume, hivyo hahitajii ushahidi ili kuitumia haki yake.
5- Ni kama ushuhudiliaji mwingine wowote.
'Ulamaa wengi tu wamenukuu kwa sauti moja kwamba ushuhudishaji wa talaka ni jambo linalopendeza lakini si wajibu. Lakini pamoja na hivyo, mwelekeo wao huu hauwezi kuwa ndio uamuzi wa mwisho, kwani kuna kauli nyingine inayoashiria juu ya uwajibu wa kushuhudishia, ambayo imesimuliwa toka kwa 'Aliy bin Abiy Twaalib, 'Imraan bin Huswayn, 'Atwaa, Ibn Jurayj na Ibn Siyriyn. Ni kauli ya kale pia ya Ash-Shaafi'iy, kisha mwelekeo wake ukatua kuwa ni jambo linalopendeza. Isitoshe, ni madhehebu ya Ahlul Bayt. Dalili zao ni:
1- Uwazi wa agizo katika Kauli Yake Ta'aalaa:
"وَأَشْهِدُوا ذَوَيْ عَدْلٍ مِّنكُمْ وَأَقِيمُوا الشَّهَادَةَ لِلَّـهِ"
"Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu, na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Allaah". [At-Twalaaq: 02]
Agizo hili linahukumia uwajibu wa hilo.
2- Allaah Amejumuisha kwa pamoja ndani ya aayah mume kumrejea mke, talaka na kushuhudishia. Hivyo basi, haijuzu kutenganisha kila kimoja peke yake. Na kwa muktadha huo, mwenye kumtaliki au kumrejea mkewe bila kuwashuhudishia watu wawili waadilifu, basi atakuwa amepetuka Mipaka ya Allaah.
[Na Aayah yenyewe inasema:
"فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ فَارِقُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ وَأَشْهِدُوا ذَوَيْ عَدْلٍ مِّنكُمْ وَأَقِيمُوا الشَّهَادَةَ لِلَّـهِ"
"Na watakapokaribia kufikia muda wao, basi wazuieni kwa wema, au farikianeni nao kwa wema, na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu, na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Allaah". [At-Twalaaq: 02]
3- Toka mwa Mutwarrif bin 'Abdullaah:
"أَنَّ عِمْرَانَ بْنَ حُصَيْنٍ، سُئِلَ عَنِ الرَّجُلِ يُطَلِّقُ امْرَأَتَهُ ثُمَّ يَقَعُ بِهَا وَلَمْ يُشْهِدْ عَلَى طَلاَقِهَا وَلاَ عَلَى رَجْعَتِهَا، فَقَالَ: طَلَّقْتَ لِغَيْرِ سُنَّةٍ، وَرَاجَعْتَ لِغَيْرِ سُنَّةٍ، أَشْهِدْ عَلَى طَلاَقِهَا وَعَلَى رَجْعَتِهَا وَلاَ تَعُدْ"
“Kwamba 'Imraan bin Huswayn aliulizwa kuhusu mtu ambaye anamtaliki mkewe kisha anamuingilia bila kuwa mashahidi wawili wakati wa kumtaliki wala wakati wa kumrejea. Akasema (kumwambia mtu huyo): "Umemtaliki mkeo kinyume na Sharia, na umemrejea kinyume na Sharia. Lete mashahidi wakati unamtaliki mkeo na wakati unamrejea, na wala usifanye tena ulivyofanya". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2186)]
Hadiyth hii inaonyesha kwamba sunnah ni kushuhudishia, lakini, ni wazi kwa kila mtu kwamba haiashirii wajibu wa kuweko mashahidi.
Ninasema: "Lau ingesemwa kwamba uwepo mashahidi kwa talaka na hilo kuthibitishwa rasmi na vyombo vya kisharia ni waajib, basi bila shaka ingelikuwa ni bora zaidi iwe hivyo na hususan katika zama zetu za leo ambapo imani zimeharibika na dini kuendelea kupuuzwa. Tunaona watu wakifurika kwenye mahakama kutokana na migogoro ya kutothibitishwa talaka na kutokuwepo mashahidi. Kutokana na hali hiyo, tunaweza kusema kwamba ni waajib kufanya hivyo, na anayeacha anapata madhambi. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi".
Faida:
Mwanamke akidai kwamba mumewe amemtaliki na mume akakanusha, basi suala hili litachukua picha zifuatazo:
1- Kama mwanamke hana shahidi, madai yake hayatokubaliwa, na wala mume hatoapishwa kukanusha madai ya mkewe.
2- Akileta mashahidi wawili juu ya talaka hiyo, basi talaka itapita.
3- Akileta shahidi mmoja tu basi hatotosha, na wala kiapo chake pamoja na shahidi wake hakitozingatiwa, kwa kuwa shahidi na kiapo vinakuwa kwenye masuala ya mali tu.
Na Je, Mume Anaweza Kuapishwa?
Na’am, anaweza kuapishwa. Akiapa, atazingatiwa ni mkweli na madai ya mkewe yatatupiliwa mbali. Ni kauli ya Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi'iy na Ahmad.
Na Kama Mume Atagoma Kuapa, Na Mkewe Kaja Na Shahidi Mmoja, Je, Talaka Itahesabiwa Imepita?
Kwenye hili kuna riwaayah mbili toka kwa Maalik. Iliyo sahihi zaidi ni ile isemayo kwamba talaka itahukumiwa imepita kwa kuwepo shahidi mmoja (aliyeletwa na mwanamke) na mume kukataa kuapa.
Inatiliwa nguvu na Hadiyth ya 'Amri bin Shu'ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake toka kwa Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema:
"إِذَا ادَّعَتِ الْمَرْأَةُ طَلاَقَ زَوْجِهَا فَجَاءَتْ عَلَى ذَلِكَ بِشَاهِدٍ عَدْلٍ اسْتُحْلِفَ زَوْجُهَا فَإِنْ حَلَفَ بَطَلَتْ شَهَادَةُ الشَّاهِدِ وَإِنْ نَكَلَ فَنُكُولُهُ بِمَنْزِلَةِ شَاهِدٍ آخَرَ وَجَازَ طَلاَقُهُ "
"Mke akidai kwamba mumewe amemtaliki, na akamleta shahidi mmoja mwadilifu wa kuthibitisha madai hayo, basi mumewe ataapishwa. Mume akiapa, basi ushahidi wa shahidi utabatilika. Na kama atagoma, basi kugoma kwake ni sawa na shahidi mwingine (wa pili dhidi yake), na talaka yake itapitishwa". [Imechakatwa na Ibn Maajah (2038)]
Hadiyth inaonyesha kwamba kugoma ni sawa na ushahidi wa ukweli wa madai ya mke. Mwanamke anapoleta shahidi mmoja –ambaye ni nusu ya ushahidi- basi kugoma kwa mume kuapa kumekuwa ni kikamilisho cha nusu nyingine. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.