Kumuombea Du'aa Mgonjwa Kwa Mkusanyiko Inafaa?

 

Kumuombea Du'aa Mgonjwa Kwa Mkusanyiko Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam Alaykum,

 

Mie nilikuwa naomba kuelimishwa kuhusu suali hili, ikiwa mwenzetu amefikwa na shida au maradhi tukakutana ndugu au jamaa lakini wanawake peke yao au wanaume peke yao tukamuombe dua jambo hili linafaa? na kama linafaa naomba utaratibu wake vipi iwe na kama haifai naomba tufahamishwe nini tunatakiwa tufanye kwa mujibu kwa sheria ya dini yetu na mafundisho ya Nabiy wetu (s.a.w). nimesahau kwa kufahamisha zaidi nakusudia kwa mfano mgonjwa yupo mbali yaani nchi nyengine sie ndugu hatuwezi kuenda kumuona.

Jazaka llahulkheir.

 

Allaah (s.w.t) awajaze kheri na afya njema na elimu bora zaid ili tuzidi kunufaika na sie amin.

 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Ugonjwa unaomfika yeyote inakuwa ni mtihani kwake na jamaa zake na hivyo awali ya yote inafaa asisitiziwe mgonjwa awe na subira pamoja na jamaa zake pia wawe katika hali hiyo. Pia ifahamike kuwa mponeshaji mkubwa ni Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), ndipo Qur-aan ikatufahamisha yafuatayo:

وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ ﴿٨٠﴾

Na ninapokuwa mgonjwa, basi Yeye Ananiponyesha. [Ash-Shu'araa: 80].

 

 

Zipo Du’aa nyingi ambazo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha tunapomtembelea mgonjwa kwa mfano: “La ba-as Twahuur In shaa Allaah – Hakuna neno, ugonjwa ni kusafishwa dhambi akipenda Allaah” [al-Bukhaariy].

 

 

Pia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hapana mja yeyote Muislamu anayemtembelea mgonjwa ambaye wakati wake wa kufa bado haujafika na akamuombea mara saba, hivi: "As-alu Llahal ‘Adhiym Rabbal ‘Arshil ‘Adhiym ay-yashfiyaka – Namuomba Allaah Mtukufu, Rabb Mlezi wa Arshi tukufu akuponyeshe" Isipokuwa Allaah humponyesha mgonjwa huyo" [Abu Daawuud na at-Tirmidhiy].

 

 

Hakujapatikana katika Siyrah ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala Swahaba zake kuwa wamekusanyikana ili wamuombee mgonjwa Du’aa. Hivyo, ni vyema nyinyi kama jamaa mulio mbali na mgonjwa wenu kumuombea katika kila nyakati hasa zile nyakati ambazo Du’aa hujibiwa kama mtu anapofungua akiwa amefunga, baina ya Adhaan na Iqaamah, baada ya Swalah, akiwa katika sijdah, akiwa safarini, kuinuka usiku watu wakiwa wamelala na wakati mwingine wowote.

 

 

Du'aa zifuatazo zimethibiti katika Sunnah kuwa ni za kumuombea mgonjwa:

 

 

Duaa za Kumtembelea Mgonjwa 

 

 

Pia soma kitabu hichi muhimu cha Du’aa ujue Du’aa mbalimbali katika matukio tofauti:

 

 

HISWN AL MUSLIM

 

 

Na hapa pia tungependa kutoa nasaha kuwa mgonjwa huyo apatiwe matibabu kwa kupelekwa kwa madaktari waliobobea katika fani ya ugonjwa wake. Huko ni kufuata Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyotuagizia katika Hadiyth zake sahihi.

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amuafu na Ampatie shifaa.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share