04-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Al-Huduwd (Adhabu): Mlango Wa Adhabu Ya Mnywaji Pombe Na Kubainisha Kileo (Ni Nini)

 

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلْحُدُودِ

Kitabu Cha Haddi (Adhabu)

 

بَابُ حَدِّ اَلشَّارِبِ وَبَيَانِ اَلْمُسْكِرِ

04-Mlango Wa Adhabu Ya Mnywaji Pombe Na Kubainisha Kileo (Ni Nini)

 

 

 

 

1063.

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ ‏ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ ‏ {أَنَّ اَلنَّبِيَّ ‏ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ ‏أَتَى بِرَجُلٍ قَدْ شَرِبَ اَلْخَمْرَ، فَجَلَدَهُ بِجَرِيدَتَيْنِ نَحْوَ أَرْبَعِينَ.‏ قَالَ: وَفَعَلَهُ أَبُو بَكْرٍ، فَلَمَّا كَانَ عُمَرُ اِسْتَشَارَ اَلنَّاسَ، فَقَالَ عَبْدُ اَلرَّحْمَنِ بْنُ عَوْفٍ: أَخَفَّ اَلْحُدُودِ ثَمَانُونَ، فَأَمَرَ بِهِ عُمَرُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

وَلِمُسْلِمٍ: عَنْ عَلِيٍّ ‏ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ ‏ ‏فِي قِصَّةِ اَلْوَلِيدِ بْنِ عَقَبَةَ‏ {جَلَدَ اَلنَّبِيُّ ‏ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ ‏أَرْبَعِينَ، وَأَبُو بَكْرٍ أَرْبَعِينَ، وَعُمَرُ ثَمَانِينَ، وَكُلٌّ سُنَّةٌ، وَهَذَا أَحَبُّ إِلَيَّ}

 وَفِي هَذَا اَلْحَدِيثِ: {أَنَّ رَجُلًا شَهِدَ عَلَيْهِ أَنَّهُ رَآهُ يَتَقَيَّأْ اَلْخَمْرَ، فَقَالَ عُثْمَانُ: إِنَّهُ لَمْ يَتَقَيَّأْهَا حَتَّى شَرِبَهَا}

Kutoka kwa Anas bin Maalik (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Mtu mmoja aliletwa kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akiwa amekunywa khamr[1] (pombe), akamtandika kwa matawi mawili ya mtende mara arubaini hivi. Na Abuu Bakr naye alifanya hivyo. Ulipokuwa wakati wa ‘Umar aliwashauri watu. ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf amesema: ‘Adhabu hafifu zaidi ni mijeledi themanini.’ ‘Umar akaamuru iwe hivyo.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

Katika Riwaayah ya Muslim kutoka kwa ‘Aliy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) katika kisa cha Al-Waliyd bin ‘Uqbah[2]: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipiga mijeledi arubaini, Abuu Bakr alipiga mijeledi arubaini, ‘Umar alipiga mijeledi thamanini. Yote hayo ni Sunnah na hii yapendeza mno kwangu.”

Na katika hadiyth hii: “Mtu mmoja alimshuhudia (Al-Waliyd) akitapika pombe. ‘Uthmaan akasema: ‘Yeye hakutapika pombe ila baada ya kuwa amekunywa.’

 

 

 

1064.

وَعَنْ مُعَاوِيَةَ ‏ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ ‏ عَنْ اَلنَّبِيِّ ‏ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ ‏أَنَّهُ قَالَ فِي شَارِبِ اَلْخَمْرِ: {إِذَا شَرِبَ فَاجْلِدُوهُ، ثُمَّ إِذَا شَرِبَ اَلثَّانِيَةِ فَاجْلِدُوهُ، ثُمَّ إِذَا شَرِبَ اَلثَّالِثَةِ فَاجْلِدُوهُ، ثُمَّ إِذَا شَرِبَ اَلرَّابِعَةِ فَاضْرِبُوا عُنُقَهُ} أَخْرَجَهُ أَحْمَدُ وَهَذَا لَفْظُهُ، وَالْأَرْبَعَةُ

وَذَكَرَ اَلتِّرْمِذِيُّ مَا يَدُلُّ عَلَى أَنَّهُ مَنْسُوخٌ، وَأَخْرَجَ ذَلِكَ أَبُو دَاوُدَ صَرِيحًا عَنْ اَلزُّهْرِيِّ

Kutoka kwa Mu’aawiyah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alisema kuhusu mnywaji pombe: “Atakapokunywa (mara ya kwanza) mtandikeni, kisha atakapokunywa mara ya pili mtandikeni, kisha atapokunywa mara ya tatu mtandikeni, kisha atakapokunywa mara ya nne mkateni shingo yake.” [Imetolewa na Ahmad, matini hii ni ya Maimaam wane (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah). At-Tirmidhiy amesema kuwa ni mansuwkh.[3] Abuu Daawuwd pia amepokea kwa uwazi kutoka kwa Az-Zuhriyy]

 

 

 

1065.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ‏ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ ‏ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ ‏{" إِذَا ضَرَبَ أَحَدُكُمْ فَلْيَتَّقِ اَلْوَجْهَ"} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Atakapopiga mmoja wenu aepuke kupiga uso.”[4] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

1066.

وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ ‏{" لَا تُقَامُ اَلْحُدُودُ فِي اَلْمَسَاجِدِ"} رَوَاهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَالْحَاكِم

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Haddi (adhabu) hazitekelezwi ndani ya Msikiti.”[5] [Imetolewa na At-Tirmidhiy na Al-Haakim]

 

 

 

1067.

وَعَنْ أَنَسٍ ‏ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ ‏ قَالَ: {لَقَدْ أَنْزَلَ اَللَّهُ تَحْرِيمَ اَلْخَمْرِ، وَمَا بِالْمَدِينَةِ شَرَابٌ يَشْرَبُ إِلَّا مِنْ تَمْرٍ} أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Allaah Ameteremsha kuharamisha pombe na Madiynah hakuna pombe inayonywewa ila pombe ya tende.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

1068.

وَعَنْ عُمَرَ ‏ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ ‏ قَالَ: {نَزَلَ تَحْرِيمُ اَلْخَمْرِ، وَهِيَ مِنْ خَمْسَةِ: مِنْ اَلْعِنَبِ، وَالتَّمْرِ، وَالْعَسَلِ، وَالْحِنْطَةِ، وَالشَّعِيرِ.‏ وَالْخَمْرُ: مَا خَامَرَ اَلْعَقْلَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Imeteremka amri ya kuharamisha pombe, inayotokana na vitu vitano: Zabibu, tende, asali, ngano na shayiri.[6] Pombe ni kila kinachofunika akili.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

1069.

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، عَنْ اَلنَّبِيِّ ‏ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ ‏قَالَ: {" كُلُّ مُسْكِرٍ خَمْرٌ، وَكُلُّ مُسْكِرٍ حَرَامٌ"} أَخْرَجَهُ مُسْلِمُ.‏

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Kila kileo ni pombe na kila kileo ni haraam.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

1070.

وَعَنْ جَابِرٍ ‏ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ ‏ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ ‏ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ ‏قَالَ: {" مَا أَسْكَرَ كَثِيرُهُ، فَقَلِيلُهُ حَرَامٌ"} أَخْرَجَهُ أَحْمَدُ، وَالْأَرْبَعَةُ ‏ وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Chochote kinacholewesha kwa wingi, uchache wake[7] ni haraam.” [Imetolewa na Ahmad na Al-Arba’ah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah) na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

 

 

1071.

وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ ‏يُنْبَذُ لَهُ اَلزَّبِيبُ فِي اَلسِّقَاءِ، فَيَشْرَبُهُ يَوْمَهُ، وَالْغَدَ، وَبَعْدَ اَلْغَدِ، فَإِذَا كَانَ مَسَاءُ اَلثَّالِثَةِ شَرِبَهُ وَسَقَاهُ، فَإِنْ فَضَلَ شَيْءٌ أَهْرَاقَهُ} أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akitengenezewa kinywaji cha (kurowekwa) zabibu na akitiliwa katika chombo akinywa siku ile, siku inayofwatia na siku baada yake. Inapofika jioni ya siku ya tatu alikuwa akinywa na akimpa mtu mwingine anywe kinapobakia kitu anamwaga.”[8] [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

1072.

وَعَنْ أُمِّ سَلَمَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا، عَنْ اَلنَّبِيِّ ‏ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ ‏قَالَ: {" إِنَّ اَللَّهَ لَمْ يَجْعَلْ شِفَاءَكُمْ فِيمَا حَرَّمَ عَلَيْكُمْ"} أَخْرَجَهُ اَلْبَيْهَقِيُّ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ

Kutoka kwa Ummu Salamah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakika Allaah Hakujaalia ponyo lenu katika Alivyoharamisha.”[9] [Imetolewa na Al-Bayhaqiyy na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

 

 

1073.

وَعَنْ وَائِلٍ اَلْحَضْرَمِيِّ، أَنَّ طَارِقَ بْنَ سُوَيْدٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا {سَأَلَ اَلنَّبِيَّ ‏ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ ‏عَنْ اَلْخَمْرِ يَصْنَعُهَا لِلدَّوَاءِ ؟ فَقَالَ: " إِنَّهَا لَيْسَتْ بِدَوَاءٍ، وَلَكِنَّهَا دَاءٌ"} أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ.‏ وَأَبُو دَاوُدَ وَغَيْرُهُمَ

Kutoka kwa Waa-il Al-Hadhwramiyy amesema kuwa Twaariqa bin Suwayd[10] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا): Alimuuliza Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kuhusu pombe inayotengenezwa kwa ajili ya dawa? Akasema: “Hiyo (pombe) sio dawa lakini ni ugonjwa.” [Imetolewa na Muslim na Abuu Daawuwd na wengineo]

 

[1] Khamr kwa Kiarabu maana yake ni kuficha, kufinika. Mtu anapolewa kile kilevi hufunika akili yake na hii ndio maana ya Khamr. Katika istwilaah ya Shariy’ah kila kilevi ni haraam. Na kila kinachopelekea katika kilevi ni haraam. Kuna makubaliano ya ‘Ulamaa kwa athari ya kilevi na adhabu ya mtu anayopewa. Hata hivyo, kuna rai tofauti kwa mnywaji pombe. Wakati wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) na Abuu Bakr, adhabu kwa mnywaji pombe ilikuwa ni mijeledi arubaini. ‘Umar aliongeza kufikia themanini na ndio uliyokuwa msimamo uliokuja chukuliwa. Kwa hivyo basi baadhi ya Maimaam wametoa hukumu zao adhabu ya mijeledi themanini. Kwa kuwa adhabu ya mijeledi themanini haikuwepo wakati wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), baadhi ya ‘Ulamaa wanaona kuwa adhabu ni mijeledi arubaini tu. Nukta nyingine ya tafaruku baina ya ‘Ulamaa kulingana na adhabu ni je, suala la adhabu ni lazima kutumia mijeledi au kopo au kiatu kinatosheleza. Kulingana na muono wa ‘Ulamaa wengi, ni sawa kutumia chombo chochote (mjeledi, kiatu, kopo na kadhalika) wakati wa kumuadhibu mtu mwenyewe.

 

[2] Al-Waliyd bin ‘Uqbah bin Abiy Mu’ait Al-Qurayshiy alikuwa ni ndugu wa ‘Uthmaan bin ‘Affaan upande wa mama. Alisilimu siku ya Fat-h Makkah. Alikuwa miongoni mwa ma-Quraysh wacheshi, mvumilivu, jasiri na mshairi. ‘Uthmaan alimfanya gavana wa mji wa Kufa nchini ‘Iraaq kisha akamuuzulu kwa tuhuma za kunywa pombe. Alijzuia kuingia katika fitnah baada ya kuuwawa kwa ‘Uthmaan, aliishi Ruqa na alifia huko na kuzikwa kwa maeneo ya Bulaykh.

[3] Imam Shaafi’iy anaripoti makubaliano ya ‘Ulamaa (isipokuwa madhehebu ya Zuhri na Imaam Ibn Hazm) kuwa mnywa pombe kwa hali yoyote hawezi kuuwawa, bila kujali amekunywa mara ngapi. Vivyo hivyo, kila atakapokamatwa akinywa pombe hukumu mpya itatolewa dhidi yake, bila kujali kama aliadhibiwa kabla ya hapo na hukumu hiyo hiyo. Kuna makubaliano ya hukumu hii kwa ‘Ulamaa.

 

[4] Muda wowote pindi mtu anapopigwa kwa adhabu yoyote iliyotolewa dhidi yake, mtu huyo anayetekeleza hukumu ile asipige usoni kwa yeyote atakayeadhibiwa.

 

[5] Hii ni kwa sababu Misikiti imesimamishwa kwa lengo maalum la kumuabudu Allaah. Hivyo basi, inatakiwa iwe safi muda wote kwa ajili ya jukumu lile la kumuabudu Allaah. Damu ya mtu aliyeadhibiwa (aliyehukumiwa) haitakiwi kutapakaa maeneo ya Msikiti. Maeneo haya ni matukufu na sehemu ya kusubiri Rahmah za Allaah, wakati adhabu iliyotolewa ni kulipa kisasi cha Allaah.

[6] Lengo la kutaja Hadiyth hii ni kuelezea kuwa sio tu kwamba pombe inayotokana na mzabibu ndio iliyoharamishwa bali zote zinazolewesha ni haraam.

[7] Ina maana chochote kinacholewesha kwa kunywa kwa wingi wake basi ni haraam  kukichukuwa kwa uchache wake. Hata kama kichache chake hakilevi.

[8] Huenda kile kilichobaki kikawa kilevi baada ya muda. Kinywaji kile kinapoanza kubadilika ni lazima kimwagwe. Haswa ikiwa ni zaidi ya siku tatu, kinywaji kile kisitumike kikianza kuonekana kimeharibika hata kama ni siku ya pili.

[9] Hii inamaanisha kuwa ni haraam kutumia vitu vilivyoharamishwa, hata kwa ajili ya tiba. Vitu hivi ni kama vile pombe, bangi, madawa ya kulevya na mfano wake.

 

[10] Huyu ni Swahaba aliyekuwa akijulikana kwa jina la Twaariqa bin Suwayd. Alikuwa mhadharami na inasemekana alikuwa Ju’fi. Ana Hadiyth moja ambayo watu wa mji wa Kufa walikuwa wakipokea kutoka kwake.

Share