06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Zakaa Ya Madeni

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah

 

06-Zakaah Ya Madeni

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Na juu ya vipengee hivi vitatu, ‘Ulamaa wamekhitalifiana katika Zakaah ya deni. Je itamlazimu mwenye kudai kutoa kwa kuwa ndiye mmiliki halisi wa mali ambayo ni deni? Au itamlazimu mdaiwa kutoa kwa kuwa ndiye mwenye kuisarifu mali na mwenye kunufaika nayo? Au wote wawili husameheka kwa kuwa milki ya kila mmoja wao si milki kamili?

 

Kauli yenye uwiano mzuri zaidi kuhusu Zakaah ya deni, ni kusema deni ni la aina mbili:

 

1- Deni lenye matumaini ya kulipwa. Hili ni deni lililo mkononi mwa mwenye uwezo anayekiri kudaiwa deni hilo. Huyu ataiwahisha Zakaah yake pamoja na mali yake anayoimiliki kila mwaka.

 

Kauli hii imesimuliwa na Abu ‘Ubayda katika Kitabu cha Al-Amwaal (uk. 432) toka kwa ‘Umar, ‘Uthmaan na Ibn ‘Umar ambao ni katika Swahaba na wengineo katika Taabi’iyna.

2- Deni lisilo na matumaini ya kulipwa kutokana na hali ngumu ya mdaiwa isiyotarajika kupata faraja, au deni lililo kwa mtu anayelikanusha na hakuna uthibitisho. 

 

(Hapa ‘Ulamaa wamekhitalifiana). Kuna wanaosema litatolewa Zakaah kwa miaka yote iliyolipitia deni hilo. Haya ni madhehebu ya ‘Aliy. [Isnaad yake ni Swahiyh. Amesimulia kutoka kwake Abu ‘Ubayd katika Al-Amwaal (431/1220), na Al-Bayhaqiy (4/150) kwa Sanad Swahiyh)]

 

Pia Ibn ‘Abbaas. Isnaad yake ni Dhwa’iyf. Imesimuliwa na Abu ‘Ubayd katika Al-Amwaal, na Al-Albaaniy kasema ni Dhwa’iyf katika Al-Irwaa (786).

Wengine wamesema atalitolea Zakaah ya mwaka mmoja anapolipokea. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah.

 

Wengine wa mwisho wamesema hapaswi kutoa Zakaah kwa deni lililopitiwa na miaka na hata kwa mwaka aliolipwa. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah.

 

Sheikh wa Uislamu amesema (52/84): “Kauli iliyo karibu zaidi ni kauli ya wale wasiowajibisha chochote wakati ule ule anapopokea deni mpaka upite mwaka, au wale wenye kuwajibisha Zakaah ya mwaka mmoja tu anapolipokea deni. Kauli hii ina picha yake, na ile ina picha yake”.

 

Imepokelewa kwa njia swahiyh toka kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan kuwa amesema:

 

((هَذَا شَهْرُ زَكَاتِكُمْ، فَمَنْ كَانَ عَلَيْهِ دَيْنٌ فَلْيُؤَدِّ دَيْنَهُ، حَتَّى تَحْصُلَ أَمْوَالُكُمْ، فَتُؤَدُّونَ مِنْهَا الزَّكَاةَ))

((Huu ni mwezi wa Zakaah yenu. Basi anayedaiwa alipe deni lake, ili mali zenu zipate [kiwango] mzitolee Zakaah toka humo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Maalik (591), na kutoka kwake Ash-Shaafi’iy (1/237) na Al-Bayhaqiy (4/148). Ni Swahiyh kama ilivyo kwenye Al-Irwaa (789)]

 

‘Aaishah amesema: ((Hakuna Zakaah katika deni [mpaka alipokee])). [Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (4/32) kwa njia mbili ambayo kila moja ni dhwa’iyf. Al-Albaaniy kasema ni Hasan katika Al-Irwaa (784)]

 

Faida

 

Mtu mwenye mali mkononi ambayo imewajibikiwa Zakaah na wakati huo huo anadaiwa, na deni hilo likamomonyoa kiwango chake cha kutolewa Zakaah au likapunguza mali isifikie kiwango, basi haina Zakaah.

 

Na likiwa deni linapunguza mali lakini kiwango cha kutolewa Zakaah kikazidi, basi atalipa deni lake kamili na ataitolea Zakaah mali iliyobakia. Kwa mfano, ikiwa mali yake ni dinari 30, na anadaiwa dinari tano, ataitolea Zakaah dinari 25.

 

4- Mali ipitiwe na mwaka kamili wa Hijria (ikiwa mkononi mwa mmiliki).

 

Hili limeshurutishwa katika Zakaah ya dhahabu, fedha (silva) na mifugo. Ama mazao na matunda, sharti hili halipo. Mwaka wa mazao na matunda ni pale yanapokomaa vizuri na kuiva. Hili limekubaliwa na Fuqahaaul Amswaar. [Bidaayatul Mujtahid (2/261-262) na Majmuw’u Al-Fataawaa (14/25)]

Na hapa linakuja swali:

 

Nini  hukmu ya mali inayotumika ndani ya mwaka?

 

Mali inayopatiwa manufaa ndani ya mwaka ina vigawanyo vitatu: [Al-Mughniy (2/626), (3/32), Fat-hul Qadiyr cha Ibn Al-Hamaam (1/510) na Al-Mawsuw’at Al-Fiqhiyyah (23/244)]

1- Ikiwa mali inayopatiwa manufaa imetokana na faida ya mali aliyonayo (ambayo haikuchanganyika na nyingine) kama faida ya mali ya biashara na zao la mifugo, basi mali hii (faida) ni lazima ijumuishwe kwenye asili yake (mtaji wa asili), na mwaka wake utahesabiwa sambamba na mwaka wa mali ya asili. Ibn Qudaamah amesema: “Hatujui mvutano wowote kwenye hili”. [Inaonyesha Ibn Hazm hakukubaliana na hili. Angalia Al-Muhallaa (6/82 na kurasa zinazofuatia]

 

2- Ikiwa mali inayopatiwa manufaa haitokani na aina ya mali aliyonayo kama mali yake kuwa ni ngamia, kisha akapata faida kutokana na dhahabu ya urithi au mfano wake, basi faida hii ya dhahabu itahesabiwa mwaka wake tokea siku alipoanza kuipatia manufaa kama itafikia kiwango (cha kutolewa Zakaah). Haitofungamanishwa na mwaka wa mali yake ya asili (ya ngamia).

 

3- Ikiwa mali inayopatiwa manufaa inatokana na mali ile ile aliyonayo -ambayo imefikia kiwango– lakini mali hii inayopatiwa manufaa haitokani na faida ya mali ya asili, na mfano wake ni kama mtu kuwa na mbuzi au kondoo arobaini waliopitiwa na sehemu ya mwaka, kisha akanunua wengine 100 au akapewa bure, basi hapa kuna madhehebu mawili:

 

La kwanza: Ataichanganya mali ya pili kwenye mali ya asili katika kiwango tu na si kwa mwaka, na kila moja ataitolea Zakaah yake kwa mwaka wake maalum. Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Hanbali.

 

Ya pili: Ataichanganya mali ya pili kwenye mali ya asili –atazitolea zote mbili Zakaah– ukitimia mwaka wa mali ya kwanza. Ni madhehebu ya Hanafiy.

 

Share