09-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Zakaah Katika Pesa Za Noti (Bank Note)

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah

 

09-Zakaah Katika Pesa Za Noti (Bank Note)

 

Alhidaaya.com

 

 

Uoanisho (uendanishaji) wake wa Kifiqhi

 

Kutokana na uchache wa kuamiliana watu katika wakati wetu wa leo na dhahabu na fedha na badala yake kutumia zaidi sarafu za noti almaarufu kama (banknotes), Fuqahaa wamekumbana na changamoto ya “Uoanishaji wa Kifiqhi kwa sarafu za noti”, na ‘Ulamaa wa sharia wamepigana kufa na kupona ili kutohoa hukmu kwa aina hii mpya ya pesa kwa mujibu wa walivyoendanisha na kuiainisha nguvu ya pesa hii.

 

Katika suala hili, nimeziangalia kwa utaamuli kauli tano za ‘Ulamaa: [An-Nuquwd.. Wadhwaaifuhaa Al-Asaasiyya Waahkaamuhaa Ash-Shar-’iyyah cha ‘Alaaud Diyn Za’atariy (uk. 329 na zinazofuatia). Ni utafiti wenye faida kubwa sana]

 

1- Ni kuwa pesa hizi ni dhamana za madeni (debt securities) juu ya upande ulizozitoa

 

Wamekubali na kupitisha kuwa hii ndiyo hali yake halisi kwa mujibu wa muktadha wa tamko la kukiri deni lililosajiliwa katika kila noti ya sarafu. Na kwa ajili hiyo, wametumia juu yake hukmu za kuamiliana na dhamana za madeni. [Kati ya waliosema hili ni Baraza Kuu la ‘Ulamaa wa Al-Azhar na Al-‘Allaamah Ash-Shanqiytwiy katika Adhwaaul Bayaan (1/257)]

 

Kati ya tija hasi za uoanishaji huu ni kuwa pesa hizi zitaingia kwenye duara la mvutano tulioutaja nyuma kati ya ‘Ulamaa kuhusiana na Zakaah ya deni. Hivyo basi, ambaye haoni ulazima wa kutoa Zakaah ya deni, atazuia pia kuitoa katika pesa hizi.

 

Kadhalika, kama pesa hizi ni dhamana za madeni, basi haijuzu kuziuzia kama deni kutokana na Ijma’a isemayo kuwa haijuzu kuuza deni kwa deni. Ukiongezea na hilo, ikiwa dhamana za madeni zimechovywa dhahabu na fedha, basi haijuzu kamwe kununuliwa kwazo dhahabu na fedha, kwa kuwa sharti lililopo hapa ni kukabidhishana mkono kwa mkono, nalo halipo.

 

2- Ni kuwa pesa hizi ni mali kati ya mali ya biashara na bidhaa kati ya bidhaa [Kati ya waliosema hili ni As-Sa’adiyy (Rahimahul Laah) kama ilivyo katika kitabu cha Al-Fataawaa As-Sa’adiyyah (uk 338-339). Lakini mwanafunzi wake Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahul Laah) hakukubaliana naye]

 

Wamekubali kuielezea kama ni mali itiwayo thamani ambapo matashi hutofautiana kwayo, na huingia ndani ya kanuni ya ugavi na mahitaji (supply and demand). Hivyo basi, wamejaribu kutumia hukmu za kifiqhi zinazohusiana na mali za biashara katika sarafu hizi.

 

Kati ya tija hasi za uoanishaji huu ni kuwa unafungua mlango wa riba, kwani kuzizingatia pesa hizi kama mali za biashara, itajuzu kuziuza zenyewe kwa zenyewe kwa kuzidiana ubora hata kama ni za aina moja! Na hii ni haramu halisi.

 

Kadhalika, hazitowajibikiwa na Zakaah kwa kuwa ni mali za biashara ikiwa hazikutayarishwa kwa ajili ya biashara na kuzalishwa!

 

 

3- Ni kuwa pesa hizi zinafanana na “coins” zilizofuliwa kutokana na madini nyinginezo zisizo dhahabu au fedha kama shaba au nikeli

 

[Kati ya waliosema hili ni Mustwafaa Az Zarqaa kama Ibn Maniy’i alivyomnukuu katika kitabu cha Al-Waraq An-Naqdiy (uk 147)]

 

Wamesema: “Ni kama pesa zilizotengenezwa kwa karatasi, na thamani ya fedha hizi inategemea desturi na mazoea ya watu, na si thamani ya mada iliyotengenezewa”.

 

Pesa hizi zinaangaliwa kwa mazingatio mawili: (Kwanza), zingatio la asili yake ambayo ni (mali). Kwa kuwa asili ya shaba, nikeli na mfano wake, ni katika mali ambazo huuzwa na kununuliwa. (Pili), zingatio la maishilio yake ya kuwa kitu kingine ambacho ni (thamani).

 

Mwenye kuangalia asili yake, ataona kuna tija hasi zilizoelezewa katika mali za biashara. Na mwenye kuangalia mgeuko wake wa kuwa kitu kingine ambacho ni thamani, basi atabakiwa na mushkeli, nao ni kutofautiana pesa na sarafu hizi za karatasi kwa njia mbalimbali jambo linalozuia kuziweka pamoja sarafu za karatasi na pesa ambazo ziko chini yake kihadhi na kifanisi. [Angalia katika An-Nuquwd cha Az-Za-’atariy (uk. 346 na zinazofuatia)]

 

4- Ni kuwa pesa hizi zinachipukia kutoka kwenye dhahabu na fedha [Kati ya waliosema hili, ni Sheikh ‘Abdul Razzaaq ‘Afiyfiy (Rahimahul Laah) ambaye alikuwa mjumbe wa Bodi ya ‘Ulamaa Wakuu wa Saudia]

 

Wamesema: “Noti ni badala ya viwili hivi (dhahabu na fedha), na wakapitisha kuwa kutolesha noti kunahitajia kuichovya kwa dhahabu au fedha. Na kama mchovyo wa sarafu ni dhahabu, basi hukmu yake ni hukmu ya dhahabu, na kama ni fedha, basi hukmu yake ni fedha”.

 

Na kati ya tija hasi za uoanishaji huu ni kuwa kwa sasa hakuna ulimwenguni sarafu mbili zilizo sawa kithamani pamoja na kuwa zimetokana na tawi moja la dhahabu. Hivyo, kutokana na sababu hii, inalazimu kutojuzu kuzidiana wakati wa kubadili dinari ya Kuwait kwa dinari ya Libya –kwa mfano- bali ni lazima ziwe sawa –kwa msingi kwamba jinsi yao ni moja- huku tofauti kati yao ni kubwa!

 

Halafu kuftaridhi (assume) kuwepo mchovyo kamili wa dhahabu au fedha  kwenye sarafu ya noti, kunatenguliwa na hukmu ya uhalisia wa hali unaothibitisha kwamba pesa zinategemea zaidi nguvu ya dola (nchi) na ushawishi wa mamlaka yake.

 

5- Ni kwamba noti ni sarafu inayojitegemea yenyewe

 

[Hili limesemwa na Bodi ya ‘Ulamaa Wakuu wa Saudia (azimio namba 10) lililopitishwa tarehe 17/4/1393 Hijria, Dk. Al-Qaradhwaawiy na wengineo]

 

Wamesema: “Kwa kuwa kila mali yenye kubeba thamani ambayo watu huitegemea katika kufanya kazi za sarafu, basi huchukua sifa ya uthamani. Na hivyo basi, inafaa kuwa sarafu na hususan pakizingatiwa kuwa katika sharia hakuna kinachoashiria kuwa ni dhahabu na fedha tu ndivyo vyenye thamani”.

 

Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyyah alidokeza kuwa ikiwa watu watakubaliana kukifanya kitu thamani, basi kitachukua hukmu ya thamani. Akasema: “Pesa zikiwa ni thamani na zikawa na jina, basi thamani haiuzwi kwa thamani kwa malipo ya mbeleni”. [Majmuw’u Al-Fataawaa (30/472)]

 

Akasisitiza kuwa uthamani hauishilii tu kwenye dhahabu na fedha (silver), bali marejeo katika hili ni mazoea na desturi ya watu na wanavyokubaliana wenyewe. Akasema: “Äma dirham na dinari, hakuna mpaka wa kikawaida au wa kisharia unaojulikana kuhusiana na sarafu hizi, bali marejeo yake ni kwa mazoea ya watu na wanavyokubaliana. Na hii ni kwa vile, kiasli, kuzikusudia hakufungamani nazo, bali lengo ni kuwa kipimo cha watu kuamiliana nacho..”[Majmuw’u Al-Fataawaa (19/251)]

 

Ninasema: “Huenda kauli hii ya mwisho inayosema kuwa sarafu za noti ni thamani ambayo hubeba hukmu za vitu vya thamani, ndiyo kauli sahihi.  Kwayo, miamala tofauti ya kimali huratibiwa”.

 

 

 

Share