16-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Zakaah Ya Ghanam (Mbuzi Na Kondoo)

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah

 

16-Zakaah Ya Ghanam (Mbuzi Na Kondoo)

 

Alhidaaya.com

 

 

Viwango Vya Mbuzi Na Kondoo Na Kiasi Cha Wajibu Wake

 

‘Ulamaa kwa kauli moja wamekubaliana kuwa ni waajib kutoa Zakaah ya mbuzi na kondoo kwa mujibu wa Hadiyth ya Anas katika barua ya Abu Bakr iliyotangulia. Pia wamekubaliana kwa sauti moja kuwa “ghanam” ni mbuzi na kondoo, nao hujumuishwa kwa pamoja, kwa kuwa ni aina mbili za wanyama wa jamii moja. [Angalia Al-Majmuw’u (5/417) na Majmuw’u Al-Fataawaa (25/30-35)]

 

Na kwa mujibu wa Hadiyth ya Anas, Zakaah ya mbuzi na kondoo huchukuliwa kufuatana na jedwali ifuatayo:

 

Idadi ya mbuzi na kondoo

 

Kiasi kilicho wajibu kutolewa

Kuanzia

Hadi

1

39

Hakuna Zakaah

40

120

Mbuzi mmoja

121

200

Mbuzi wawili

201

339

Mbuzi watatu

400

499

Mbuzi wanne

500

599

Mbuzi watano

 

 

Na hivi hivi waliozidi 300, katika kila mbuzi 100, mbuzi mmoja kwa mujibu wa Jumhuri ya ‘Ulamaa.

 

Faida

 

Kondoo au mbuzi, jike au dume, anatosheleza kwa Zakaah. Ni kauli ya Hanafiy, Maalik na Ibn Hazm ambayo ndiyo yenye mwelekeo sawa zaidi. [Angalia Al-Muhallaa (5/268), Al-Majmuw’u (5/422) na Haashiyat ibn ‘Aabidiyna (2/19)]

 

Masuala jumla kuhusu Zakaah ya mifugo

 

Je, mifugo wadogo (wachanga) hutolewa Zakaah?

 

Wanachuoni wamekhitalifiana kuhusu Zakaah ya ngamia wachanga au ndama, au mbuzi na kondoo wachanga. [Badaai-‘u As-Swaanaai (2/31), Fat-hul Qadiyr  (1/504), Ad-Durru Al-Mukhtaar (2/26), Al-Mughniy (2/602) na vinginevyo]

 

1- Baadhi yao wamesema: “Wanyama wachanga (vitoto) huhesabiwa sehemu ya kiwango cha Zakaat, na ni lazima wajumuishwe ndani ya Zakaah hata kama ni wachanga, na atamtoa mmoja kati yao”.

Wengine wamesema: “Atalazimika kununua mwenye umri wa wajibu kutoka kwengine”.

 

2- Wengine wamesema: “Wanyama wachanga huhesabiwa sehemu ya kiwango, na si lazima wajumuishwe ndani ya Zakaah isipokuwa kama wako na mama zao, ni sawa mama zao wakifikia kiwango peke yao au wasifikie”.

 

Makundi haya mawili yametolea dalili aliyoyasema ‘Umar kumwambia mkusanyaji Zakaah wake Sufyaan bin ‘Abdullaah Ath-Thaqafiy: ((Wajumlishe hesabuni kondoo na mbuzi wachanga…….)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Maalik (600) Ash-Shaafi’iy katika Al-Musnad (651) na Ibn Hazm kwa Sanad Hasan]

 

3- Wengine wamesema: “Mama wakifikia kiwango, basi vichanga vilivyozidi kiwango huhesabiwa”. Ni madhehebu ya Jumhuri. [Amenukulu haya kutoka kwao Sheikh wa Uislamu katika Al-Fataawaa (25/38)]

 

4- Ibn Hazm kasema: “Kichanga ambacho hakiwezi kuitwa mbuzi au kondoo, hakifai kuchukuliwa katika Zakaah ya wajibu, wala hakihesabiwi katika wanyama wanaochukuliwa Zakaah mpaka kitimize mwaka. Kikitimiza kitahesabiwa, na Zakaah yake itachukulika”. [Al-Muhallaa (5/274)]

 

Wengine wametolea dalili Hadiyth ya Suwayd bin Ghafalah aliyesema: ((Alitujia mkusanyaji Zakaah wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), nikakaa kumsikiliza, nikamsikia akisema: Hakika katika niliyoyachukulia ahadi ni kuwa tusimchukue anayenyonya maziwa)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1579), An Nasaaiy (5/28) na Ahmad (4/315). Sanad yake ni Hasan].

 

Jumhuri wamechukulia muradi wa Hadiyth hii kuwa hachukuliwi, yaani mwenye kunyonya katika Zakaah, na hakuna kizuizi kuingizwa katika idadi ya kiwango.

 

Ibn Hazm ameihoji kauli yao akisema: “Ikiwa (Suwayd) anakusudia kuwa mwenye kunyonya asichukuliwe katika Zakaah angesema: Tusimchukue mwenye kunyonya maziwa, lakini alipozuia mwenye kunyonya maziwa asichukuliwe kwa Zakaah –na mwenye kunyonya maziwa ni nomino jumla (common noun)– imeruhusika kwa hilo wasihesabiwe wenye kunyonya katika wanyama wenye kuchukuliwa katika Zakaah”. [Al-Muhalla (5/278-279].

 

Sifa zinazochungwa kwa mnyama anayechukuliwa katika Zakaah ya mifugo

 

Mnyama anayechukuliwa katika Zakaah ya mifugo anatakiwa awe wa wastani, na hili linahitajia mambo mawili. La kwanza ni kwa mkusanyaji Zakaah ambaye ni mtumishi maalum aliyeteuliwa na mtawala kwa kazi hiyo, na la pili ni kwa mmiliki wa mifugo.

 

1- Mkusanyaji anatakiwa ajiepushe kuchukua mali ya thamani kubwa ya mtoaji Zakaah kama mwenyewe hakuitoa kwa roho safi. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia Mu’aadh wakati alipomwamuru kuchukua Zakaah kwa watu wa Yemen:   

 

((إياك وكرائمَ أموالهم، واتقِ دعوة المظلوم؛ فإنه ليس بينها وبين الله حجابٌ))

((Chunga usije kuchukua mali za watu za thamani kubwa, na ogopa sana du’aa ya aliyedhulumiwa, kwani haina kizuizi kati yake na kati ya Allaah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1496) na Muslim (19).

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akisema: ((Kondoo na mbuzi wa Zakaah walipitishwa kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab. Akaona kati yao mbuzi aliyenona na vilembwe (chuchu) vimejaa maziwa. Akasema: Huyu mbuzi ni wa nini? Wakasema: Ni mbuzi wa Zakaah. Akasema: Watu wake hawakumtoa wakiwa wameridhika, msiwafitini watu (wakachukia Amri za Allaah), msichukue mali za thamani kubwa za Waislamu, waachieni cha kuwapa chakula)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa ikhraaj na Maalik (602), na kutoka kwake Ash-Shaafi’iy katika Musnadi wake (654) na Sanadi yake ni Swahiyh].

 

2- Mmiliki asitoe mali mbovu. Kama kumtoa mnyama mwenye kasoro, au mwenye maradhi, au aliyevunjika, au kikongwe ambaye hana tena meno, au mwenye ila yenye kupunguza manufaa yake na thamani yake. Allaah Ta’alaa Amesema:

 

((وَلَا تَيَمَّمُوا الْخَبِيثَ مِنْهُ تُنفِقُونَ))

((Na wala msikusudie vibaya kutoka humo mkavitoa)). [Al-Baqarah 2:267]

 

 

Na Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Mu’aawiyah inasema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam amesema:

 

((ثلاث من فعلهن طعم طعم الايمان:...وأعطى زكاة ماله طيبة بها نفسه، راقدة عليه كل عام، ولا يعطي الهرمة ولا الدرنة، ولا المريضة، ولا الشرط اللئيمةـ ولكن من وسط أموالكم، فإن الله لم يسألكم خيره، ولم يأمركم بشره))

((Matatu mtu akiyafanya, ataonja ladha ya iymaan: …na akatoa Zakaah ya mali yake roho yake ikiwa safi, yenye kumsaidia kwa kipato kila mwaka, na asitoe mzee, wala mwenye pele, wala mgonjwa, wala asiyetamanika asiye na maziwa, bali toeni mali zenu za thamani ya wastani, kwani Allaah Hajawatakeni bora ya mali, wala Hakuwaamuruni mbovu yake)). [Abu Daawuud (1582), na wapokezi wake ni waaminifu]

 

Je, Zakaah ni waajib kwa mali yenyewe husika au kwa dhima ya mtoaji?

 

‘Ulamaa wana rai mbili katika suala hili:

 

Ya kwanza: Zakaah ni waajib kwa mali yenyewe husika. Hii ni kauli ya Jumhuri. Kati ya yanayozalikana na hili ni:

 

(a) Kuwa mali ikiharibika (ikiteketea) baada ya kuwajibikiwa na Zakaah, basi Zakaah itapomoka kwa kuteketea huko.

 

(b) Kuwa mwenye mbuzi 40 kwa mfano, atatoa mbuzi mmoja. Na kama hakutoa Zakaah ya mwaka (uliomwajibikia) na akabakiwa na mbuzi hao hao 40 (bila kuongezeka idadi), ni lazima amtoe mbuzi huyo mmoja, lakini hatowajibika kumtoa kwa mwaka unaofuatia, kwa kuwa mbuzi hao 40 wako katika hukumu ya mbuzi 39.

 

Ya pili: Zakaah ni waajib kwa dhima. Hii ni kauli ya Mahanbali na Ibn Hazm. Kauli yao inatotoa yafuatayo:

 

(a) Zakaah baada ya kuwa waajib, haiondoki kwa kuhiliki mali kwa kuwa imefungamana na dhima ya mwenye mali.

 

(b) Ambaye hakutoa Zakaah ya mbuzi 40 baada ya kupita mwaka wa kwanza, ni lazima atoe mbuzi wawili mwaka unaofuatia, kwa kuwa mbuzi wa kwanza amebakia katika dhima yake, na ni lazima amtoe mwingine kwa hao 40.

 

Ikiwa mifugo ni ya ushirika wa watu wawili, vipi Zakaah hutolewa?

 

Ushirika, -sawasawa ukiwa ni wa mifugo ya aina moja, au wa mifugo tofauti– unafanya mali mbili kuwa mali moja. Ni kwa Hadiyth:

 

((لا يجمع بين متفرق، ولا يفرق بين مجتمع، خشية الصدقة [وما كان من خليطين، فإنهما يتراجعان بينهما بالسوية]))

((Hawachanganywi kati ya waliotenganishwa, na wala hawatenganishwi kati ya waliochanganyishwa kwa kuogopa Zakaah [Na kwa wanyama wa washirika wawili, basi hao watarejesheana hesabu kati yao kwa usawa])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (145), Ibn Maajah (1801) bila nyongeza, nayo iko kwa An-Nasaaiy (2447), Abu Daawuwd (1567) na At-Tirmidhiy (621)]

 

Na Zakaah ni waajib kwa mali ya shirika kama ilivyo waajib kwa mali ya mtu mmoja kwa masharti yafuatayo: [Angalia Al-Fiqhu Al-Islaamiy wa adillatuhu)]

 

1- Washirika wawili wawe na masharti ya kuwajibikiwa na Zakaah (kama kuwa Muislamu, muungwana, kuwa na umiliki kamili wa mali n.k).

 

2- Mali iliyochanganywa ifikie kiwango.

 

3- Ushirika wao upitiwe na mwaka kamili, na kama si hivyo, kila mmoja atatoa kivyake kwa mujibu wa mwaka wake.

 

4- Mali ya mmoja wao isitenganike na ya mwenzake katika mambo sita: machungio, boma la kulala, manyweo ya maji, sehemu ya kukamwa maziwa, mafahali na mchungaji. [Hanafiy na Ibn Hazm katika Al-Muhalla (6/51 na kurasa zinazofuatia) wanasema kuwa ushirika hauna athari yoyote, na ushirika haufanyi mali mbili kuwa moja]

 

Ama maana ya Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

((لا يجمع بين مفترق، ولا يفرق بين مجتمع خشية الصدقة..))

((Hawachanganywi kati ya waliotenganishwa, wala hawatenganishwi kati ya waliochanganyishwa kwa kuogopa Zakaah)) ni kuwa:

 

1-Ushirika (unaozifanya mali mbili kuwa kama mali moja) unaweza kuwafaidisha washirika wawili kwa kuwapunguzia Zakaah. Ni kama kila mmoja wao kuwa na mbuzi 40 ambao wakichanganywa wanakuwa 80, na hapa watawajibika kutoa mbuzi mmoja tu, kinyume na kama si washirika, kila mmoja atatoa hapo mbuzi mmoja.

 

Na hapa ndipo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akakataza watu wawili kufanya hila, wakashirikiana kukwepa Zakaah na kuipunguza.

 

2- Ushirika unaweza kuongeza mzigo wa Zakaah kwa washirika wawili kama wote wawili kuwa na mbuzi 40. Hapa wote wawili ni lazima watoe mbuzi mmoja, kinyume na kama watatengana, hapo hawajibikiwi yeyote kati yao kutoa chochote. Na hapa washirika hawa wanakatazwa kutenganisha wanyama wao ili kukwepa Zakaah.

 

Je, ushirika una athari katika mali isiyo ya mifugo?

 

Madhehebu ya Hanbali yanasema kuwa hauathiri kwa mali nyinginezo zisizo wanyama wa kufugwa, kwa kuwa ushirika katika mifugo unakuwa na faida wakati fulani na hasara wakati mwingine. Ama mali isiyo mifugo, hiyo haidhaniwi jingine isipokuwa hasara tu kwa mwenye mali, kwa kuwa inampasa kuitolea Zakaah iliyozidi kiwango katika hesabu yake, na kuichanganya na mhisa wake hakusaidii kitu. Hivyo, ikiwa kila mmoja katika washirika wawili ana mali ambayo sio mifugo inayofikia nusu ya kiwango, basi hawawajibikiwi kutoa Zakaah. [Al-Inswaaf (3/83)]

 

Lakini madhehebu ya Ash-Shaafi’iy yanasema kuwa ushirika unaathiri katika mali isiyo ya mifugo vile vile kama mazao, matunda, dirhamu, dinari na mfano wake. [Mughnil Muhjtaaj (2/76)]

 

 

Share