Hikmah Ya Kuteremshwa Qur-aan Kidogo Kidogo Wakati Mbali Mbali

 

Hikmah Ya Kuteremshwa Qur-aan Kidogo Kidogo Wakati Mbali Mbali

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Qur-aan ni kitabu cha mwisho kilichoteremshwa na Allaah (سبحانه وتعالى), ni Mwongozo   kamili kwa walimwengu wote duniani,  kwa hiyo Qur-aan ni tofauti na vitabu vinginevyo ambavyo viliteremshwa kwa kaumu fulani au mataifa fulani kama mfano Tawraat imeteremshwa kwa Nabiy Muwsaa na watu wake Bani Israaiyl na Injiyl kwa Nabiy 'Iysaa na wafuasi wake.

 

 

Tofauti nyingine baina ya vitabu hivyo na Qur-aan ni kwamba Vitabu vilotangulia, vimeteremshwa kwa mteremsho mmoja. Ama Qur-aan haikuteremshwa mara moja ikawa kamilifu, bali imeteremshwa kidogo kidogo kwa wakati mbali mbali ima bila ya kutokea tukio au kwa kutokea matukio. Imeteremshwa kama ni Wahy (ufunuo) katika moyo wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Hikma za kuteremshwa Qur-aan ni nyingi miongoni mwazo ni zifuatazo:

 

 

Hikma Ya Kwanza: Kuwasahilishia Swahaba Hukmu Za Makatazo Ya Maasi Waliyokuwa Nayo Katika Ujaahiliyyah:

 

 

Moja ya hikma ni kwamba kwa sababu ya kuwavutia watu kuingia katika Dini kwa kufuata maamrisho yake na makatazo yake polepole, na hii ni njia itumikayo na yenye matunda katika da'wah.  Kwani ingelikuwa ni kufuata makatazo yote na kufuata maamrisho yote kwa pamoja, basi ingelikuwa ni vigumu sana watu kufuata, na ndio maana kwa muda wa miaka kumi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipokuwa Makkah hakukuwa na zaidi ya kuwaita watu kuingia katika Dini, neno la ‘Laa ilaah illa Allaah’, ndilo lililokuwa lengo, hakukuwa na amri za fardhi yoyote wala hukmu zozote.

 

Mfano, makatazo ya ulevi, kwa vile ulevi ulikuwa ni moja ya maasi makuu na hata baada ya kuja Uislamu, baadhi ya Swahaba walikuwa bado wakilewa. Hii ni kwa sababu ilikuwa ni ada na desturi zao walizozirithi katika ujaahiliyyah kama zilivyo desturi nyinginezo walizokuwanazo mfano kuwaua watoto wa kike, kuwanyima urithi wanawake n.k. Ukaja Uislamu na kuondosha dhulma zote hizo.  Hivyo jambo kama ulevi lilihitajika hikma ya kuukataza kwa polepole na ndio maana tunaona kwamba kuna Aayah tatu zinazohusiana na makatazo ya ulevi ilianza kwanza kwa kutaja madhara yake na manufaa yake, kisha polepole hadi kukataza kabisa.

 

Hadiyth ifuatayo imethibiti hayo:

 

حَدَّثَنَا إِبْرَاهِيمُ بْنُ مُوسَى، أَخْبَرَنَا هِشَامُ بْنُ يُوسُفَ، أَنَّ ابْنَ جُرَيْجٍ، أَخْبَرَهُمْ قَالَ وَأَخْبَرَنِي يُوسُفُ بْنُ مَاهَكَ، قَالَ إِنِّي عِنْدَ عَائِشَةَ أُمِّ الْمُؤْمِنِينَ ـ رضى الله عنها ـ إِذْ جَاءَهَا عِرَاقِيٌّ فَقَالَ أَىُّ الْكَفَنِ خَيْرٌ قَالَتْ وَيْحَكَ وَمَا يَضُرُّكَ قَالَ يَا أُمَّ الْمُؤْمِنِينَ أَرِينِي مُصْحَفَكِ‏.‏ قَالَتْ لِمَ قَالَ لَعَلِّي أُوَلِّفُ الْقُرْآنَ عَلَيْهِ فَإِنَّهُ يُقْرَأُ غَيْرَ مُؤَلَّفٍ‏.‏ قَالَتْ وَمَا يَضُرُّكَ أَيَّهُ قَرَأْتَ قَبْلُ، إِنَّمَا نَزَلَ أَوَّلَ مَا نَزَلَ مِنْهُ سُورَةٌ مِنَ الْمُفَصَّلِ فِيهَا ذِكْرُ الْجَنَّةِ وَالنَّارِ حَتَّى إِذَا ثَابَ النَّاسُ إِلَى الإِسْلاَمِ نَزَلَ الْحَلاَلُ وَالْحَرَامُ، وَلَوْ نَزَلَ أَوَّلَ شَىْءٍ لاَ تَشْرَبُوا الْخَمْرَ‏.‏ لَقَالُوا لاَ نَدَعُ الْخَمْرَ أَبَدًا‏.‏ وَلَوْ نَزَلَ‏.‏ لاَ تَزْنُوا‏.‏ لَقَالُوا لاَ نَدَعُ الزِّنَا أَبَدًا‏.‏

Ametuhadithia Ibraahiym bin Muwsaa, ametujulisha Hishaam bin Yuwsuf, kwamba Ibn Jurayj amewajulisha amesema: Amesema au amenijulisha Yuwsuf bin Maahak kuwa alipokuwa pamoja na ‘Aaishah Mama wa Waumini  (رضي الله عنها), mara akaja kwake mtu kutoka Iraaq, akamuuliza: Ni kafani (sanda) gani iliyo bora zaidi? Akasema (رضي الله عنها): Allaah Akurehemu! Itakusaidia nini kujua hilo (ukiwa maiti sanda yoyote utakafiniwa nayo)?! Akasema: Ee Mama wa Waumini, nionyeshe Mswahafu wako. Akasema (رضي الله عنها): Kwa nini? Akasema: Huenda nikaukusanya na kuipanga Qur-aan kulingana nayo, kwani watu wanaisoma pamoja na Suwrah zake sio kwa mpangilio wa sawasawa. Akasema (رضي الله عنها): Haijalishi ni sehemu gani unayosoma mwanzo. (Fahamu kuwa) kitu cha kwanza kuteremshwa kwayo ni Suwrah za al-Mufaswswal (fupi fupi) ambazo kumetajwa ndani yake Jannah na Moto. Na watu wanapokuwa wamekomaa na nafsi zao kutulia juu ya hilo, Aayah kuhusiana na halali na haramu ziliteremshwa. Na lau ingeteremshwa mwanzo (kwa mfano): “Msinywe pombe (mvinyo)”, watu wangesema: “Hatutaacha kunywa (pombe)”. Na lau kungeteremshwa: “Msizini”, watu wangesema: “Hatutaacha kuzini”.  [Al-Bukhaariy]

 

'Umar ibn Al-Khatwtwaab (رضي الله عنه) ambaye alikuwa mmoja wa Swahaba aliyekuwa akilewa, aliomba hukmu kuhusu pombe alisema: “Ee Allaah tubainishie kuhusu pombe bainisho la kuridhisha.”  Ikateremshwa:

 

 سْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا ۗ  

Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: “Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na (baadhi ya) manufaa kwa watu. Na dhambi yake viwili hivyo ni kubwa kuliko manufaa yake.” [Al-Baqarah: 219]

 

Wakaendelea kunywa pombe hadi siku moja katika Swalaah, Swahaba mmoja alikosea kusoma Suwratul-Kaafiruwn basi hapo ikateremshwa Aayah:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُونَ  

Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa mpaka mjue mnayoyasema, [An-Nisaa: 43]

 

Wakaacha kulewa nyakati za Swalaah na wakaendelea nyakati nyingine hadi kukatokea maovu mengine ndipo 'Umar (رضي الله عنه) akasema tena: “Ee Allaah! Tupe Aayah iliyo wazi kabisa kuhusu Al-Khamr (pombe). Ndipo Aayah ya mwisho kuhusu makatazo ya ulevi ikateremshwa [Tafsiyr ibn Kathiyr] ambayo ni:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٩٠﴾ إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُوقِعَ بَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَعَنِ الصَّلَاةِ ۖ فَهَلْ أَنتُم مُّنتَهُونَ ﴿٩١﴾

Enyi walioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli; ni najisi na chukizo kutokana na kitendo cha shaytwaan; basi jiepusheni navyo, mpate kufaulu. Hakika shaytwaan anataka kukutilieni baina yenu uadui na bughudha katika pombe na kamari na akuzuieni na kumdhukuru Allaah na (akuzuieni pia) Swalaah; basi je mtakoma? [Al-Maaidah: 90 – 91]

 

Basi ‘Umar (رضي الله عنه) akasema: “Tumekoma.”

 

Maelezo ya Hadiyth kama ilivyothibiti:

 

عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ، قَالَ لَمَّا نَزَلَ تَحْرِيمُ الْخَمْرِ قَالَ عُمَرُ: اللَّهُمَّ بَيِّنْ لَنَا فِي الْخَمْرِ بَيَانًا شِفَاءً ، فَنَزَلَتِ الآيَةُ الَّتِي فِي الْبَقَرَةِ: ((‏يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ)) الآيَةَ قَالَ: فَدُعِيَ عُمَرُ فَقُرِئَتْ عَلَيْهِ، قَالَ: اللَّهُمَّ بَيِّنْ لَنَا فِي الْخَمْرِ بَيَانًا شِفَاءً، فَنَزَلَتِ الآيَةُ الَّتِي فِي النِّسَاءِ: ((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لاَ تَقْرَبُوا الصَّلاَةَ وَأَنْتُمْ سُكَارَى))‏ فَكَانَ مُنَادِي رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم إِذَا أُقِيمَتِ الصَّلاَةُ يُنَادِي: أَلاَ لاَ يَقْرَبَنَّ الصَّلاَةَ سَكْرَانُ، فَدُعِيَ عُمَرُ فَقُرِئَتْ عَلَيْهِ  فَقَالَ: اللَّهُمَّ بَيِّنْ لَنَا فِي الْخَمْرِ بَيَانًا شِفَاءً فَنَزَلَتْ هَذِهِ الآيَةُ: ((‏فَهَلْ أَنْتُمْ مُنْتَهُونَ))‏ قَالَ عُمَرُ: انْتَهَيْنَا.‏

Imepokelewa kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه) kwamba ilipoharamishwa pombe alisema ‘Umar: Ee Allaah tubainishie kuhusu pombe bainisho la kuridhisha.” Hapo ikateremshwa Aayah katika Suwratul-Baqarah:

 ‏يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ

Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: “Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa.    

 

[Al-Baqarah 2: 219] Akaitwa ‘Umar akasomewa. Kisha akasema: “Ee Allaah tubainishie kuhusu pombe bainisho la kuridhisha.” Kisha ikateremshwa Aayah katika Suwratun-Nisaa:

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لاَ تَقْرَبُوا الصَّلاَةَ وَأَنْتُمْ سُكَارَى

“Enyi waloamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa...” [An-Nisaa 4: 43]

 

Kisha muitaji wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akitangaza pale inapokimiwa Swalaah: “Tahadharini! Aliyelewa asikaribie Swalaah!” ‘Umar akaitwa tena na akasomewa akasema: “Ee Allaah tubainishie kuhusu pombe bainisho la kuridhisha.” Ikateremka Aayah:

‏فَهَلْ أَنْتُمْ مُنْتَهُونَ

“...basi je, mtakoma?” [Al-Maaidah 5: 90-91] ‘Umar akasema: “Tumekoma.” [Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd (3670)]

 

 

 

Hikma Ya Pili: Kuthibitisha Qur-aan Katika Kifua Cha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

Hikma nyingine ya kuteremshwa kidogokidogo ni kwa sababu ya kuithibisha Qur-aan katika kifua cha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwani ingelikuwa vigumu kwake kuipokea yote mara moja. Hii ni kwa sababu Qur-aan ni maneno mazito ya Allaah (عز وجل) kama Anavyosema Mwenyewe Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا﴿٤﴾ إِنَّا سَنُلْقِي عَلَيْكَ قَوْلًا ثَقِيلًا﴿٥﴾

Na soma Qur-aan kwa kisomo cha utaratibu upasao, kuitamka vizuri na kutaamali. Hakika Sisi Tutakuteremshia juu yako kauli nzito. [Al-Muzzammil: 4 – 5]

 

 

Na pia, kumwezesha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhifadhi na kuifahamu kwani alikuwa ana pupa na hamu kubwa ya kuipokea, kuisoma, kuihifadhi na kuifahamu, Allaah (سبحانه وتعالى) Akamwambia:

 

وَلَا تَعْجَلْ بِالْقُرْآنِ مِن قَبْلِ أَن يُقْضَىٰ إِلَيْكَ وَحْيُهُ ۖ وَقُل رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا ﴿١١٤﴾

wala usiiharakize Qur-aan (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kabla haikumalizwa kufunuliwa Wahy kwako. Na sema: Rabb wangu! Nizidishie elimu. [Twaahaa: 114]

 

 Allaah (سبحانه وتعالى) Akamtuliza na kumthibitishia kuisoma kwake, kuhifadhi na kuifahamu kwa kumwambia:

 

لَا تُحَرِّكْ بِهِ لِسَانَكَ لِتَعْجَلَ بِهِ﴿١٦﴾ إِنَّ عَلَيْنَا جَمْعَهُ وَقُرْآنَهُ﴿١٧﴾ فَإِذَا قَرَأْنَاهُ فَاتَّبِعْ قُرْآنَهُ﴿١٨﴾ ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا بَيَانَهُ﴿١٩﴾

 

Usiutikisie (huu Wahy) ulimi wako ili kuiharakiza (Qur-aan ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Hakika ni juu Yetu kuikusanya na kukuwezesha kuisoma kwake. Basi Tunapoisoma (kupitia Jibriyl), fuata kusomwa kwake. Kisha ni juu Yetu kuibainisha (kwako). [Al-Qiyaamah: 16 – 19]

 

Na pia, kuthibitisha moyo wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kukariri kumteremshia Wahyi kidogokidogo kwani hivyo ilimsaidia Nabiy kuihifadhi kwa wepesi na kufahamu hukmu na shariy’ah zake na hivi ndivyo ilivyowezekana kuthibitisha moyo wake na kuimarisha azimio lake.  Allaah (سبحانه وتعالى) Akamwambia:

 

وَكُلًّا نَّقُصُّ عَلَيْكَ مِنْ أَنبَاءِ الرُّسُلِ مَا نُثَبِّتُ بِهِ فُؤَادَكَ ۚ وَجَاءَكَ فِي هَـٰذِهِ الْحَقُّ وَمَوْعِظَةٌ وَذِكْرَىٰ لِلْمُؤْمِنِينَ﴿١٢٠﴾

Na yote Tunayokusimulia katika khabari muhimuu za Rusuli, Tunathibitisha kwazo moyo wako. Na imekujia katika hii haki na mawaidha na ukumbusho kwa Waumini. [Huwd: 120]

 

 

 

Hikma Ya Tatu:  Kuithibitisha Qur-aan Kwa Swahaba Katika Kujifunza Kuisoma Na Kuifanyia Kazi.

 

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى)

 

  وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا﴿٤﴾

Na soma Qur-aan kwa kisomo cha utaratibu upasao, kuitamka vizuri na kutaamali. [Al-Muzzammil: 4]

 

Kwa Tartiyl (Usomaji wa taratibu wa kutaamali) hiyo, Allaah (سبحانه وتعالى) Akamfundisha Nabiy Muhammad    (صلى الله عليه وآله وسلم) polepole na kidogokidogo naye awasomee Waumini hivyo hivyo. Ingelikuwa  Qur-aan imeteremshwa kwa mteremsho mmoja, asingeweza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuisoma hivyo kwa Tartiyl na kuwafundisha Swahaba, jambo ambalo nao wasingeweza kuwafikishia Ummah wakaweza kuisioma na kuihifdhai kiwepesi. 

 

Ndio maana Anasema Allaah (سبحانه وتعالى

 

وَقُرْآنًا فَرَقْنَاهُ لِتَقْرَأَهُ عَلَى النَّاسِ عَلَىٰ مُكْثٍ وَنَزَّلْنَاهُ تَنزِيلًا ﴿١٠٦﴾

Na Qur-aan Tumeigawanya sehemu mbali mbali ili uwasomee watu kwa vipindi mbali mbali; na Tumeiteremsha mteremsho wa kidogokidogo. [Al-Israa:106]

 

Basi Aayah zilipokuwa zinateremshwa, Swahaba walikuwa wakizisoma na kuzihifadhi na kuzifanyia kazi. Hawakuwa wakihifadhi Aayah nyingine hadi wahakikishe wamezifahamu vizuri hizo chache, na kutekeleza maamrisho na makatazo yake. Imaam Atw-Twabariy (رحمه الله) amesema katika Tafsiyr yake: [Atw-Twabariy (1/80)]

 

Abu ‘Abdirrahmaan As-Salamiy amesema "Wametuhadithia wale ambao walikuwa wakitusomea Qur-aan, kwamba walikuwa wakitafuta kujifunza kuisoma Qur-aan kutoka kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), wakawa wanajifunza Aayah kumi kisha hawaendelei mpaka wazifanyie kazi, basi na hivyo hivyo nasi tukajifunza Qur-aan na kuifanyia kazi pamoja kwa wakati mmoja.”  [Tafsiyr Atw-Twabariy (1/80)]  

 

Lakini makafiri katika kejeli na ukaidi wao wa kukanusha Qur-aan walileta swali hili, "Kwa nini Qur-aan isiteremshwe mara moja?” Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akawajibu kwamba Ameteremsha kwa kutaka kuthibitisha Quraan katika kifua cha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم): 

 

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا نُزِّلَ عَلَيْهِ الْقُرْآنُ جُمْلَةً وَاحِدَةً ۚ كَذَٰلِكَ لِنُثَبِّتَ بِهِ فُؤَادَكَ ۖ وَرَتَّلْنَاهُ تَرْتِيلًا ﴿٣٢﴾

Na wakasema wale waliokufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur-aan kwa ujumla mara moja tu? Hivyo hivyo, ili Tukithibitishe kifua chako; na Tumeifunulia Wahyi punde kwa punde kwa kuratibu. [Al-Furqaan:32]

 

Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) katika Tafsiyr yake amesema kuhusu Kauli hiyo ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا نُزِّلَ عَلَيْهِ الْقُرْآنُ جُمْلَةً وَاحِدَةً كَذَلِكَ لِنُثَبِّتَ بِهِ فُؤَادَكَ

 

“Kwa sababu kila alipoteremshiwa Qur-aan (صلى الله عليه وآله وسلم), alizidishiwa utulivu na thabaat (kuthibitika moyoni), khaswa wakati kulikuwa na sababu ya khofu, wasiwasi na dhiki, kwani Qur-aan ilipoteremshwa wakati wa sababu ya tukio fulani (Sabab Nuzuwl), basi huwa ina hadhi kubwa na uthibitisho wake ni wa nguvu na mkubwa zaidi kuliko kama ingeteremshwa kabla ya hapo. Na hivyo hukumbukwa zaidi inapotatuliwa jambo la tukio  (kwa sababu ya kuteremshwa Qur-aan).”

 

Na kuhusu Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى)

 

وَرَتَّلْنَاهُ تَرْتِيلًا  
  

Yaani, Tuliichelewesha polepole na tukakuambatanisha nayo, na yote haya yanaonyesha utunzaji wa Allaah (سبحانه وتعالى) juu ya Kitabu Chake na Rasuli Wake Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) kwani Alifanya kuteremshwa Kitabu Chake kwa mtiririko wa polepole  kulingana na hali ya Rasuli na masilahi yake ya Dini.

 

Na kuhusu kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقُرْآنًا فَرَقْنَاهُ لِتَقْرَأَهُ عَلَى النَّاسِ عَلَىٰ مُكْثٍ وَنَزَّلْنَاهُ تَنزِيلًا ﴿١٠٦﴾

Na Qur-aan Tumeigawanya sehemu mbali mbali ili uwasomee watu kwa vipindi mbali mbali; na Tumeiteremsha mteremsho wa kidogokidogo. [Al-Israa:106]

 

 عَلَى مُكْثٍ

kwa vipindi mbali mbali

 

Yaani: Polepole ili waizingatie na watafakari maana zake na watoe humo maarifa kuhusu Sayansi yake.

 

 وَنَزَّلْنَاهُ تَنْزيلاً

na Tumeiteremsha mteremsho wa kidogokidogo:

 

Yaani: Kidogokidogo kwa kutengwa katika miaka ishirini na tatu.  

 

 

 

Hikma Ya Nne: Baadhi ya maswali aliyokuwa akiulizwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) yalihitaji asubiri ateremshiwe Wahyi:

 

 

Changamoto pindi makafiri walipokuwa wakimjaribu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  kwa kumuuliza maswali ya kimiujiza. Ikawa ni ngumu kwake kuwajibu bila ya kuweko tayari Wahyi. Mfano kama vile kumuuliza juu ya Saa (Qiyaamah kitatokea lini), na wakati wowote washirikina walipomuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) swali kama hilo, Allaah (سبحانه وتعالى) Aliteremsha Qur-aan kujibu swali lao, juu ya kuwa Wahyi uliteremshwa kidogokidogo kwa wakati tofauti na mbalimbali, lakini hawakuweza wao kuleta kitu kama Qur-aan juu ya kuwa walijaribu kutunga maneno yao yakawa batili, Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

قُل لَّئِنِ اجْتَمَعَتِ الْإِنسُ وَالْجِنُّ عَلَىٰ أَن يَأْتُوا بِمِثْلِ هَـٰذَا الْقُرْآنِ لَا يَأْتُونَ بِمِثْلِهِ وَلَوْ كَانَ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ ظَهِيرًا ﴿٨٨﴾

  Sema: Ikiwa watajumuika wana Aadam na majini ili walete mfano wa hii Qur-aan; hawatoweza kuleta mfano wake na japokuwa watasaidiana wao kwa wao. [Al-Israa: 88]

 

 

Qur-aan ikaendelea kuteremshwa katika hali za kuhitajika kwa dharura pia kama kuhusu swali la washirikina kuungana na Mayahudi kutaka kumjaribu Unabii wake Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) wakamuuliza kuhusu roho, Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha:

 

 وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ ۖ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٥﴾

Na wanakuuliza kuhusu roho. Sema: Roho ni katika amri ya Rabb wangu. Na hamkupewa ujuzi isipokuwa kidogo tu. [Al-Israa: 85]

 

 

Au kuhusu swali la Waumini waliomuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu hukmu ya pombe, na kuhusu kutoa mali zao, na kuhusu Yatima, Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha Aayah mbili zinazofuatana kujibu yote hayo:

 

 

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا ۗ وَيَسْأَلُونَكَ مَاذَا يُنفِقُونَ قُلِ الْعَفْوَ ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَتَفَكَّرُونَ ﴿٢١٩﴾ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۗ وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْيَتَامَىٰ ۖ قُلْ إِصْلَاحٌ لَّهُمْ خَيْرٌ ۖ وَإِن تُخَالِطُوهُمْ فَإِخْوَانُكُمْ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ الْمُفْسِدَ مِنَ الْمُصْلِحِ ۚ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَأَعْنَتَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٢٢٠﴾

 

Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na (baadhi ya) manufaa kwa watu. Na dhambi yake viwili hivyo ni kubwa kuliko manufaa yake. Na wanakuuliza nini watoe. Sema: Yaliyokuzidieni. Hivyo ndivyo Allaah Anavyokubainishieni Aayaat (na shariy’ah) ili mpate kutafakari. Katika dunia na Aakhirah. Na wanakuuliza kuhusu mayatima. Sema: Kuwatengeneza ni khayr. Na mkichanganya mambo yenu na yao basi hao ni ndugu zenu. Na Allaah Anamjua fisadi na mtengenezaji. Na lau Angetaka Allaah Angelikutieni katika shida. Hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [Al-Baqarah: 219 – 220]

 

 

Na maswali mengi mengineyo alikuwa akiulizwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ima na washirikina au Waumini na akawa anasubiri Wahyi uteremshwe kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) ili awajibu. Na hii ndio hikma mojawapo iliyohitajika kuteremshwa Qur-aan kidogokidogo kwa sababu ilithibitisha zaidi Unabii wake kwa kuwa alitegemea na kusubiri Wahyi uteremshwe kutoka kwa Rabb wake.  

 

 

 

Hikma Ya Tano: Kuteremshwa Kutokana Na Matukio Mbalimbali Kipindi Tofauti.

 

Kwa vile baadhi ya Aayah za Qur-aan zilikuwa zikiteremshwa kutokana na sababu ya matukio mbali mbali mfano; Kisa cha Watu watatu waliokhalifu katika vita vya Tabuk au kisa cha Ifk (kusingiziwa kashfah Mama Wa Waumini) n.k. hivyo kulihitaji kuweko na hukmu zake, ndio maana Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ﴿٨٩﴾

Na Tumekuteremshia Kitabu kikiwa ni kielezo bayana cha kila kitu na ni mwongozo na rahmah na bishara kwa Waislamu. [An-Nahl: 89]

 

Matukio mengine yalimhitaji Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) asubiri Wahy kutoka kwa Allaah, mfano mmoja mzuri kabisa ni kisa cha Swahaabiyyah Khawlah bint Khuwaylid pindi mumewe alipomtajia idhwhaar (tamko la talaka la zama za kijaahiliyyah) basi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alishindwa  kumpa hukmu. Baada ya muda si mrefu Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha hukmu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

قَدْ سَمِعَ اللَّـهُ قَوْلَ الَّتِي تُجَادِلُكَ فِي زَوْجِهَا وَتَشْتَكِي إِلَى اللَّـهِ وَاللَّـهُ يَسْمَعُ تَحَاوُرَكُمَا ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ﴿١﴾ الَّذِينَ يُظَاهِرُونَ مِنكُم مِّن نِّسَائِهِم مَّا هُنَّ أُمَّهَاتِهِمْ ۖ إِنْ أُمَّهَاتُهُمْ إِلَّا اللَّائِي وَلَدْنَهُمْ ۚ وَإِنَّهُمْ لَيَقُولُونَ مُنكَرًا مِّنَ الْقَوْلِ وَزُورًا ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ لَعَفُوٌّ غَفُورٌ﴿٢﴾ وَالَّذِينَ يُظَاهِرُونَ مِن نِّسَائِهِمْ ثُمَّ يَعُودُونَ لِمَا قَالُوا فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مِّن قَبْلِ أَن يَتَمَاسَّا ۚ ذَٰلِكُمْ تُوعَظُونَ بِهِ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ﴿٣﴾ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ شَهْرَيْنِ مُتَتَابِعَيْنِ مِن قَبْلِ أَن يَتَمَاسَّا ۖ فَمَن لَّمْ يَسْتَطِعْ فَإِطْعَامُ سِتِّينَ مِسْكِينًا ۚ ذَٰلِكَ لِتُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ۚ وَتِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ ۗ وَلِلْكَافِرِينَ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٤﴾

 

Allaah Amekwishasikia kauli ya yule mwanamke anayejadiliana nawe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu mumewe, na anamshitakia Allaah; na Allaah Anayasikia majibizano yenu. Hakika Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. Wale miongoni mwenu wanaowatamkia wake zao dhwihaar: Nyinyi kwetu kama migongo ya mama zetu.  Hao wake zao si mama zao. Hawakuwa mama zao isipokuwa wale waliowazaa. Na hakika wao bila shaka wanasema yasiyokubalika na kauli ya kuchukiza na uongo. Na hakika Allaah bila shaka ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kughufuria. Na wale wanaowatamkia wake zao dhwihaar, kisha wakarudi katika waliyoyasema (kuitengua dhwihaar), basi ni kuacha huru mtumwa kabla ya kugusana. Hayo mnawaidhiwa kwayo. Na Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. Na yule asiyepata uwezo, basi afunge Swiyaam miezi miwili mfululuzo kabla ya kugusana. Na yule asiyeweza, basi alishe chakula masikini sitini. Hivyo ili mumuamini Allaah na Rasuli Wake. Na hiyo ni mipaka ya Allaah. Na makafiri watapata adhabu iumizayo.  [Al-Mujaadalah: 1- 4]. 

 

Tukio kama hili na mengineyo, ni hikma ya kuteremshwa Qur-aan kidogokidogo pamoja na hukumu yake ili watu wafahamu pia hizo hukmu zake polepole. Mfano pia tukio lilosababisha kuteremshwa Aayah za Tayammu kama ifuatavyo:

 

عَنْ عَائِشَةَ، زَوْجِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَتْ خَرَجْنَا مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فِي بَعْضِ أَسْفَارِهِ، حَتَّى إِذَا كُنَّا بِالْبَيْدَاءِ ـ أَوْ بِذَاتِ الْجَيْشِ ـ انْقَطَعَ عِقْدٌ لِي، فَأَقَامَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم عَلَى الْتِمَاسِهِ، وَأَقَامَ النَّاسُ مَعَهُ، وَلَيْسُوا عَلَى مَاءٍ، فَأَتَى النَّاسُ إِلَى أَبِي بَكْرٍ الصِّدِّيقِ فَقَالُوا أَلاَ تَرَى مَا صَنَعَتْ عَائِشَةُ أَقَامَتْ بِرَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم وَالنَّاسِ، وَلَيْسُوا عَلَى مَاءٍ، وَلَيْسَ مَعَهُمْ مَاءٌ‏.‏ فَجَاءَ أَبُو بَكْرٍ وَرَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم وَاضِعٌ رَأْسَهُ عَلَى فَخِذِي قَدْ نَامَ فَقَالَ حَبَسْتِ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم وَالنَّاسَ، وَلَيْسُوا عَلَى مَاءٍ، وَلَيْسَ مَعَهُمْ مَاءٌ‏.‏ فَقَالَتْ عَائِشَةُ فَعَاتَبَنِي أَبُو بَكْرٍ، وَقَالَ مَا شَاءَ اللَّهُ أَنْ يَقُولَ، وَجَعَلَ يَطْعُنُنِي بِيَدِهِ فِي خَاصِرَتِي، فَلاَ يَمْنَعُنِي مِنَ التَّحَرُّكِ إِلاَّ مَكَانُ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم عَلَى فَخِذِي، فَقَامَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم حِينَ أَصْبَحَ عَلَى غَيْرِ مَاءٍ، فَأَنْزَلَ اللَّهُ آيَةَ التَّيَمُّمِ فَتَيَمَّمُوا‏.‏ فَقَالَ أُسَيْدُ بْنُ الْحُضَيْرِ مَا هِيَ بِأَوَّلِ بَرَكَتِكُمْ يَا آلَ أَبِي بَكْرٍ‏.‏ قَالَتْ فَبَعَثْنَا الْبَعِيرَ الَّذِي كُنْتُ عَلَيْهِ، فَأَصَبْنَا الْعِقْدَ تَحْتَهُ‏.‏

Mama wa ‘Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) amehadithia: “Tulikwenda katika moja ya safari tukafika Al-Baydaa au Dhaatul-Jaysh ambako kidani changu kilivunjika (na kikapotea). Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akawa anakitafuta, kisha pia watu wengineo wakainuka kukitafuta. Hapakuweko na maji sehemu hiyo, basi watu wakamwendea Abuu Bakr Asw-Swiddiyq na kusema: Huoni alivyofanya ‘Aaishah? Kamfanya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) pamoja na watu wakae sehemu ambayo hakuna maji! Abuu Bakr akaja wakati Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa amelaa akiwa amelaza kichwa chake mapajani mwangu. Akaniambia: Umemzuia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na watu sehemu ambako hakuna maji na wala hawana (akiba ya) maji. Basi akanigombesha na akasema Aliyomjaalia (Allaah) kusema kuhusu mimi na akanipiga ubavuni kwa mkono wake. Hakuna kilichonizuia kusogea (kutokana na maumivu) isipokuwa kwa vile Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alilala mapajani mwangu. Hapo Allaah Akateremsha Aayah ya tayammum, basi wakatayammam. ‘Usayd bin Al-Hudhwayr akasema: Ee ahli ya Abuu Bakr! Hii si baraka ya kwanza kwenu. Kisha akaendeshwa ngamia ambaye nilikuwa nimempanda na tukakipata kidani chini yake.” [Al-Bukhaariy].

 

Kadhaalika matukio mengineo ambayo pia yametokea kisha zikateremshwa Aayah pamoja na hukmu zake na ndipo ikawa wepesi Swahaba kuisoma, kuihifadhi na kuifanyia kazi maamrisho na makatazo yake yote.

 

 

Hikma Ya Sita: Kuthibitisha Nyoyo Za Waumini Kwa Subira Katika Mitihani:

 

 

Waumini pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) walihitaji kuthibitishwa katika iymaan zao kwa sababu walisibiwa na mitihani mbali mbali kwa kuingia kwao katika Uislaam, ikawa ni jaribio la iymaan zao, Allaah (سبحانه وتعالى) Akawateremshia Kauli Zake mbali mbali zikiwemo:

 

 

أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لَا يُفْتَنُونَ ﴿٢﴾ وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۖ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّـهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ ﴿٣﴾

Je, wanadhani watu kwamba wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao ndio wasijaribiwe?  Kwa yakini Tuliwajaribu wale wa kabla yao, ili Allaah Awatambulishe wale walio wakweli na ili Awatambulishe walio waongo. [Al-‘Ankabuwt: 2 – 3]

 

Na pia,

 

أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ ﴿١٤٢﴾

Je, Mnadhani kwamba mtaingia Jannah na hali Allaah Hakudhihirisha wale waliofanya jihaad miongoni mwenu na Akadhihirisha wenye kusubiri? [Aal-‘Imraan: 142]

 

Na pia,

 

أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَأْتِكُم مَّثَلُ الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلِكُم ۖ مَّسَّتْهُمُ الْبَأْسَاءُ وَالضَّرَّاءُ وَزُلْزِلُوا حَتَّىٰ يَقُولَ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ مَتَىٰ نَصْرُ اللَّـهِ ۗ أَلَا إِنَّ نَصْرَ اللَّـهِ قَرِيبٌ ﴿٢١٤﴾

Je, mnadhani kwamba mtaingia Jannah na hali bado haijakufikieni (mitihani) kama ya wale waliopita kabla yenu? Iliwagusa dhiki za umasikini na maafa ya magonjwa na njaa na wakatetemeshwa mpaka Rasuli na wale walioamini pamoja naye wanasema: Lini itafika nusura ya Allaah? Tanabahi! Hakika nusura ya Allaah iko karibu. [Al-Baqarah: 214]

 

Kwa hiyo Allaah (سبحانه وتعالى) Alipowateremshiwa Kauli Zake, ziliwasaidia kuendeleza subira zao na kuwafunza kubakia katika subra.

 

 

Na pia Suwrah na Aayah mbali mbali ziliteremshwa kusimulia visa vya Manabii waliotangulia ili wapate funzo kuwa si pekee yao waliosibiwa na mitihani.

 

 

Na pia Waumini walipohajiri kutoka Makkah kwenda Madiynah wakaacha masikani zao, mali zao na hata familia zao, baada ya kudhikishwa na makafiri wa Makkah, Allaah (سبحانه وتعالى) Akawateremshia Aayah za kuwabashiria Nusra kutoka Kwake na kuwaahidi malipo mema ya Jannah kutokana na subira zao na kuthibitika kwao na kubakia katika taqwa zao. Allaah (سبحانه وتعالى) Akawabashiria:

 

أُذِنَ لِلَّذِينَ يُقَاتَلُونَ بِأَنَّهُمْ ظُلِمُوا ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ نَصْرِهِمْ لَقَدِيرٌ ﴿٣٩﴾ الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِم بِغَيْرِ حَقٍّ إِلَّا أَن يَقُولُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ۗ وَلَوْلَا دَفْعُ اللَّـهِ النَّاسَ بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لَّهُدِّمَتْ صَوَامِعُ وَبِيَعٌ وَصَلَوَاتٌ وَمَسَاجِدُ يُذْكَرُ فِيهَا اسْمُ اللَّـهِ كَثِيرًا ۗ وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٤٠﴾

 

Wameruhusiwa (kupigana) kwa wale wanaopigwa kwa kuwa wamedhulumiwa. Na kwamba Allaah bila shaka ni Muweza wa kuwanusuru. Ambao wametolewa majumbani mwao bila ya haki isipokuwa kwa kuwa wanasema: Rabb wetu ni Allaah. Na lau ingelikuwa Allaah Hawakingi watu baadhi yao kwa wengine, bila shaka yangelivunjwa mahekalu na makanisa, na masinagogi na Misikiti inayotajwa humo Jina la Allaah kwa wingi. Na bila shaka Allaah Atamnusuru yeyote yule anayenusuru Dini Yake. Hakika Allaah bila shaka ni Mwenye nguvu zote, Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika. [Al-Hajj: 39 – 40]

 

Hivyo ndio ikawa hikma mojawapo ya kuteremshwa Qur-aan kidogokidogo na kwa wakati mbalimbali khasa wakati wa matukio.

 

 

 

 .

 

 

Share