01-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Kutaja Jina La Allaah Mwanzoni na Kumaliza Kwa Kumshukuru

 

Riyaadhw Asw-Swaalihiyn

 

باب التسمية في أوله والحمد في آخره

01-Mlango Wa Kutaja Jina La Allaah Mwanzoni na Kumaliza Kwa Kumshukuru

 

Alhidaaya.com

 

 

Hadiyth – 1

وعن عُمَرَ بنِ أبي سَلمة رضي الله عنهما ، قَالَ : قَالَ لي رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((  سَمِّ اللهَ ، وَكُلْ بِيَمِينكَ ، وكُلْ مِمَّا يَليكَ )) متفقٌ عَلَيْهِ .

Imepokewa kutoka kwa 'Umar bin Abu Salamah (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) ambaye amesema: Aliniambia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Mtaje Allaah, na kula kwa mkono wa kuume (kulia) na kula kilicho mbele yako." [Al-Bukhaariy, Muslim, Maalik, Abu Daawuwd na At-Tirmidhiy]

 

 

Hadiyth – 2

وعن عائشة رضي الله عنها ، قالت : قَالَ رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( إِذَا أكَلَ أحَدُكُمْ فَلْيَذْكُرِ اسْمَ اللهِ تَعَالَى، فإنْ نَسِيَ أنْ يَذْكُرَ اسْمَ اللهِ تَعَالَى في أوَّلِهِ، فَلْيَقُلْ: بسم اللهِ أوَّلَهُ وَآخِرَهُ )) رواه أَبُو داود والترمذي، وقال: (( حديث حسن صحيح )).

Imepokewa kutoka kwa 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Anapokula mmoja wenu na alitaje jina la Allaah Ta'aalaa, lakini anaposahau kulitaja jina la Allaah Ta'aalaa mwanzoni, aseme: 'Bismi Llaahi Awwalahu wa Aakhirahu - Kwa jina la Allaah mwanzoni na mwishoni." [Abu Daawuwd na At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

 

Hadiyth – 3

وعن جابرٍ رضي الله عنه ، قَالَ : سَمِعْتُ رسول الله صلى الله عليه وسلم ، يقولُ : ((  إِذَا دَخَلَ الرَّجُلُ بَيْتَهُ ، فَذَكَرَ اللهَ تَعَالَى عِنْدَ دُخُولِهِ ، وَعِنْدَ طَعَامِهِ ، قَالَ الشَّيْطَانُ لأَصْحَابِهِ : لاَ مَبِيتَ لَكُمْ وَلاَ عَشَاءَ ، وَإِذَا دَخَلَ فَلَمْ يَذْكُرِ اللهَ تَعَالَى عِنْدَ دُخُولِهِ ، قَالَ الشَّيْطَانُ : أدْرَكْتُمُ المَبِيتَ ؛ وَإِذَا لَمْ يَذْكُرِ اللهَ تَعَالَى عِنْدَ طَعَامِهِ ، قَالَ : أدْرَكْتُم المَبيتَ وَالعَشَاءَ )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Anapoingia mtu nyumbani kwake, na akamtaja Allaah Ta'aalaa pale anapoingia na anapokula, shetani anamwambia sahibu yake: 'Hakuna malazi (sehemu ya kulala) wala chakula kwako leo.' Na anapoingia, na asimtaje Allaah Ta'aalaa wakati anapoingia (nyumbani kwake), shetani anasema: 'Kwa uchache tumepata malazi.' Na asipomtaja Allaah Ta'aalaa wakati anapokula, shetani anasema: 'Umepata malazi na chakula cha usiku'." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 4

وعن حُذَيْفَةَ رضي الله عنه ، قَالَ : كُنَّا إِذَا حَضَرْنَا مَعَ رَسُولِ اللهِ صلى الله عليه وسلم طَعَاماً ، لَمْ نَضَعْ أيدِينَا حَتَّى يَبْدَأَ رَسُولُ الله صلى الله عليه وسلم فَيَضَعَ يَدَهُ ، وَإنَّا حَضَرْنَا مَعَهُ مَرَّةً طَعَاماً ، فَجَاءتْ جَارِيَةٌ كَأنَّهَا تُدْفَعُ ، فَذَهَبَتْ لِتَضَعَ يَدَهَا في الطَّعَامِ ، فَأَخَذَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم بِيَدِهَا ، ثُمَّ جَاءَ أَعْرَابِيّ كأنَّمَا يُدْفَعُ ، فَأخَذَ بِيَدهِ ، فَقَالَ رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم : (( إنَّ الشَّيْطَانَ يَسْتَحِلُّ الطَّعَامَ أنْ لا يُذْكَرَ اسمُ اللهِ تَعَالَى عَلَيْهِ ، وَإنَّهُ جَاءَ بهذِهِ الجارية لِيَسْتَحِلَّ بِهَا ، فأَخَذْتُ بِيَدِهَا ، فَجَاءَ بهذا الأعرَابيّ لِيَسْتَحِلَّ بِهِ ، فَأخذْتُ بِيَدِهِ ، والَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ ، إنَّ يَدَهُ في يَدِي مَعَ يَدَيْهِمَا )) ثُمَّ ذَكَرَ اسْمَ اللهِ تَعَالَى وَأكَلَ. رواه مسلم .

Na amesema Hudhayfah (Radhwiya Allaahu 'anhu): Tulikuwa tunapohudhuria chakula pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hatuanzi kula (kwa kutia mikono yetu) mpaka aanze kutia mkono wake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na kwa hakika tulihudhuria chakula siku moja pamoja naye, akaja haraka haraka kijakazi kama kwamba ana njaa sana na akataka kuingiza mkono wake (ili apate kula) lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaushika mkono wake. Kisha akaja bedui haraka kama kwamba ana njaa mno na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaushika mkono wake. Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Hakika shetani anakihalalisha kwake chakula ambacho jina la Allaah halikutajwa juu yake. Na hakika amekuja na huyu kijakazi ili akihalalishe chakula, hivyo nikaushika mkono wake. Akaja na huyu bedui ili akihalalishe kwayo, nami nikamshika mkono wake. Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake! Hakika mkono wake (shetani) upo katika mkono wangu pamoja na mikono yao." Kisha akataja jina la Allaah Ta'aalaa na akala chakula hicho." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 5

وعن أُمَيَّةَ بن مَخْشِيٍّ الصحابيِّ رضي الله عنه ، قَالَ : كَانَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم جَالِسَاً، وَرَجُلٌ يَأكُلُ، فَلَمْ يُسَمِّ اللهَ حَتَّى لَمْ يَبْقَ مِنْ طَعَامِهِ إِلاَّ لُقْمَةٌ ، فَلَمَّا رَفَعَهَا إِلَى فِيهِ ، قَالَ : بِسْمِ اللهِ أوَّلَهُ وَآخِرَهُ ، فَضَحِكَ النَّبيّ صلى الله عليه وسلم ، ثُمَّ قَالَ : ((  مَا زَالَ الشَّيْطَانُ يَأكُلُ مَعَهُ ، فَلَمَّا ذَكَرَ اسمَ اللهِ اسْتَقَاءَ مَا فِي بَطْنِهِ )) رواه أَبُو داود والنسائي .

Imepokewa kutoka kwa Umayyah bin Makhshiyy, ambaye ni Swahaaba (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba amesema: Alikuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameketi chini na yupo mtu aliyekuwa akila chakula bila ya kutaja jina la Allaah na akaendelea mpaka likabaki tonge moja tu. Alipolinyanyua tonge hilo mdomoni mwake alisema: "Bismi Llaahi Awwalahu wa Aakhirahu (Kwa  jina la Allaah mwanzoni na mwishoni)." Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitabasamu, kisha akasema: "Shetani aliendelea kula naye lakini aliporaja jina la Allaah, shetani alitapika chakula chote kilichokuwa tumboni mwake." [Abu Daawuwd na An-Nasaaiy]

 

 

Hadiyth – 6

وعن عائشة رضي الله عنها ، قالت : كَانَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم يَأكُلُ طَعَاماً في سِتَّةٍ مِنْ أصْحَابِهِ ، فَجَاءَ أعْرَابِيٌّ ، فَأكَلَهُ بلُقْمَتَيْنِ . فَقَالَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم : ((  أما إنَّهُ لَوْ سَمَّى لَكَفَاكُمْ )) رواه الترمذي ، وقال : (( حديث حسن صحيح )) .

Na amesema 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akila chakula pamoja na Swahaaba zake sita, alikuja bedui akawa ni mwenye kula kwa matonge mawili. Hapo akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Ama kwa hakika lau angetaja jina la Allaah basi chakula hicho kingewatosha." [At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

 

Hadiyth – 7

وعن أَبي أُمَامَة رضي الله عنه: أنَّ النبيَّ صلى الله عليه وسلم كَانَ إِذَا رَفَعَ مَائِدَتَهُ، قَالَ: (( الْحَمْدُ للهِ حَمداً كَثِيراً طَيِّباً مُبَاركَاً فِيهِ، غَيْرَ مَكْفِيٍّ ، وَلاَ مُوَدَّعٍ ، وَلاَ مُسْتَغْنَىً عَنْهُ رَبَّنَا )) رواه البخاري .

Imepokewa kutoka kwa Abu Umamah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimaliza kula na kitambara cha chakula kunyanyuliwa, akisema: "Alhamdullillaah Kathiyran Twayyban Mubaarakan Fihi Ghayra Makfiyyi walaa muwadda'in walaa Mustaghnan 'anhu Rabbana "Sifa zote njema, nyingi zilizo nzuri anastahiki Allaah na iliyojaa baraka ndani yake isiyoepikika (kwa kuwa Ndiye Mwenye kulisha na wala Yeye halishwi na yeyote) na wala hamuachi mwenye kumuomba wala hatuwezi kuwa na ukwasi nayo, ee Rabb." [Al-Bukhaariy]

 

 

Hadiyth – 8

وعن معاذِ بن أنسٍ رضي الله عنه ، قَالَ : قَالَ رسولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم : ((  مَنْ أكَلَ طَعَامَاً، فَقال : الحَمْدُ للهِ الَّذِي أطْعَمَنِي هَذَا، وَرَزَقنِيهِ مِنْ غَيْرِ حَوْلٍ مِنِّي وَلاَ قُوَّةٍ ، غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ )) رواه أَبُو داود والترمذي ، وقال : (( حديث حسن )) .

Imepokewa kutoka kwa Mu'aadh bin Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Yeyote anayekula chakula kisha akasema: "Alhamdullillaahil Ladhiy Atw'amaniy hadhaa wa Razaqaniyhi min ghayri Hawli minniy walaa Quwwah - Sifa zote njema Anastahiki Allaah ambaye kwamba Amenilisha mimi hichi (chakula) na Akaniruzuku mimi bila ya hila au juhudi na nguvu kutoka kwangu. Huyo atakuwa ni mwenye kusamehewa madhambi yake yaliyotangulia." [Abu Daawuwd na At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan]

 

 

 

Share