Qur-aan Na Uimamu Wa Mashia

 

 

Mada hii inachunguza utumikaji wa neno “Imaam” ndani ya Qur-aan ili tuweze kuona kama inaunga mkono hoja ya Mashia inayohusiana na Uimamu. Ndani yake tunaonyesha kwanza uimamu kama unavyofahamika na Mashia na wafuasi wake na halafu tunatazama kwa makini kabisa kila mahali ndani ya Qur-aan tukufu ambapo neno “Imaam” (Imamu) au wingi wake “A-immah”(Maimamu) lilivyotumiwa na Allaah Ta’ala.

 

Hapatakuwa na upinzani tukisema tofauti zilizopo baina ya Ahlus-Sunnah na Mashia ya kuwa Uimamu ndio uliobeba sehemu kubwa ya mfarakano baina yetu. Hivyo ni sawa kabisa kujenga hoja au kutumia mantiki kwa kiasi fulani ya kuwa suala la Uimamu ndio chimbuko la tofauti kati ya Sunni na Shia; tofauti zote zitakazokuja baadae tukizichunguza kwa makini utaona tofauti hizo zinalenga kwenye chimbuko hilo (la Uimamu).

 

Hivyo basi, hakuna mtu yeyote au kundi lolote linalotaka kuwaleta Mashia na Masunni karibu linaweza kumudu kutoangalia nadharia ya Imaamah (Uimam). Juhudi zote za kuondosha vikwazo vinavyowatenganisha Ahlu Sunnah na Mashia ni lazima zianzie katika nukta hii. Kuanzia popote pale kwengine, itakuwa ni sawa na kutibu dalili za ugonjwa na sio kutibu chanzo chake. Kwa muda dalili za ugonjwa zitafifia, hadi hapo siku za baadae zitazihirishwa tena na chanzo cha ugonjwa wenyewe. Kadhalika kujaribu kutatua tofauti kati ya Ahlu Sunnah na Mashia kutokana mtazamo usiotokana na chimbuko hilo la Uimamu, utaweza kwa muda mfupi kutengeneza fikra ya kuondosha kikwazo cha kupatikana umoja wa Kiislamu. Ukweli halisi ni kwamba vikwazo hivyo hivyo vitarudi pale tu ambapo wingi wa furaha ya umoja huo utakapoanza kufifia.

 

Kama Waislamu tunalazimika tuzirudishe tofauti baina yetu kwa Allaah na Mtume Wake. Katika makala haya tunarudisha nadharia ya Uimamu kwenye Qur-aan, na lengo la kuhakikisha ya kuwa nadharia hii kama vile inavyofahamika na kuaminika na Shia Ithna ‘Ashari (au Ja’fari) imethibitishwa na wahyi au la.

 

 

Nadharia Ya Uimamu

Kabla hatujaenda mbali itakuwa ni jambo la busara, kwa manufaa ya wale ambao hawajui Uimamu unamaanisha nini kwa Mashia, kuwaelezea kwa undani kuhusu jambo hili. Pindi msomaji atakapokuwa na maana ya sawa sawa kuhusu maana ya Uimamu kwa Mashia na una hadhi gani katika muundo wa imani ya Kishia, tutaendelea na maelezo kuhusu nadharia hii kwa mtazamo wa Qur-aan tukufu.

 

Kimsingi, Uimamu ni uongozi wa Ummah baada ya kuondoka Mtume Wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mashia wanaamini kama vile Allaah Alivyomchagua Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa mjumbe Wake kwa wanaadamu, ndivyo vivo hivyo Alivyowachagua watu kumi na mbili wawe ni viongozi wa Ummah baada yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mambo ya kiibada na kidunia. Kiongozi wa kwanza au Imamu kama wanavyoitwa, alikuwa ‘Aliy ibn Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu). Kisha akafuatiwa na kijana wake mkubwa Al-Hasan (Radhiya Allaahu ‘anhu) naye akafuatiwa na Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhu). Baada ya Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhu) Uimamu uliendelea kwenye kizazi chake mpaka mwaka wa 260AH, ambapo Imamu wa kumi na mbili akiwa mtoto wa umri wa miaka mitano alipotoweka na kughibu. Kutokana na watu kumi na mbili hawa wanaotokana na katika kizazi cha Mtume Wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) peke yao ndio kunawastahiki uongozi wa Ummah. Kuna sura mbili za Uimamu zinazohitaji mtazamo wa makini. La kwanza ni namna ya wanavyoteuliwa na la pili ni namna ya uongozi wao.

 

 

Namna Ya Uteuzi Wa Maimamu Kumi Na Mbili

Kwa utaratibu wa kuhusu uteuzi wao wameafikiana Mashia wote ya kuwa haki ya Maimamu kumi na mbili kuiongoza Ummah ilitawazishwa na Allaah Aliyetukuka Mwenyewe. Na hapana tofauti kati ya uteuzi wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ule wa Maimamu kumi na mbili kama warithi wake. Na kusisitizia kipengele hiki muhimu cha Uimamu Mwanachuoni mkubwa wa Kishia Muhammad Husayn Kashif al-Ghita, ambaye alikuwa Mwanachuoni mashuhuri sana huko Najaf nchini Iraq katika miaka ya sabini, ameandika kwenye kitabu chake kiitwacho Asl ash-Shi‘ah wa-Usuluha:

“Uimamu ni cheo kitakatifu, kama vile Unabii. Kama vile ambavyo Allaah Anamchagua Amtakaye awe ni Nabii na Mjumbe Wake, vile vile, kwenye Uimamu, Humchagua yeyote Amtakaye.”1

 

Inatia shauku kufahamu kitabu ambacho jumla hii imenukuliwa kiliandikwa kwa madhumuni ya kusahihisha fikra potofu juu ya Mashia. Hivyo Uimamu katika utekelezaji wake unaendana samabamba na Unabii na Ujumbe, hivyo desturi inaashiria kuukataa Uimamu kutalazimisha adhabu ya yule anayekataa Unabii na Ujumbe. Kama ikiwa kuukataa Unabii wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuliwafanya kina Abu Jahl na Abu Lahab wawe nje ya Uislamu, kwa hiyo ni kimantiki kutarajia kuukataa Uimamu wa ‘Ali ibn Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) kutawafanya Abu Bakar, ‘Umar na waliobakia katika Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wawe wametoka nje ya Uislamu. Na kwa yule anayechukua rai ya tatizo hili kwa mtazamo huu hatoshangaa kuona ya kuwa Mashia wananukuu kutokana na Maimamu wao ya kuwa “Watu waliritadi baada ya kifo cha Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), isipokuwa watu watatu,”2 Hivyo fikra hiyo itakuwa inaendana sambamba na msimamo wao wa kuulinganisha Uimamu na Unabii kwa muono wao wa kuwa viwili hivi vimeteuliwa na Allaah Aliyetukuka.

 

La kustajibisha ni ile rai ya Mashia wa leo wanayoelezea kuhusu Ahlu Sunnah kwa ujumla. Mtu atategemea wao waseme juu yao kuwa ni makafiri, walitoka nje ya Uislamu. Hata hivyo, kuna wengi wasiokuwa Waislamu wanaamini upweke wa Allaah, lakini hawaamini Utume wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kwa hilo tunahesabu wote hao kuwa ni makafiri. Kama Uimamu ni “cheo kitakatifu,kama vile Unabii” Massuni ambao hawaamini Uimamu wa Maimamu kumi na mbili ni lazima wawe makafiri.

 

 Kumekuwepo maulamaa wa Kishia wa zamani ambao wameonyesha msimamo usiotetereka ya kuwa yeyote asiyeukubali Uimamu wa Maimamu kumi na mbili – Kama vile Ahlu Sunnah - kuwa ni makafiri. Mfano Ibn Babawayh al-Qummi (aliyefariki 381AH), mwandishi wa moja kati ya vitabu vinne vikuu vilivyokusanya hadithi zinazotegemewa na Mashia Man La Yahdhuruhu al-Faqih, anasema katika maandiko yake kueelezea imani ya Kishia:

“Ni katika imani yetu ya kuwa yeyote aukataaye Uimamu wa Amirul-Muuminiyn (Sayidina ‘Aliy) na Maimamu baada yake ni sawa na yule anayekanusha Unabii wa Manabii.

“Ni katika imani yetu kuhusu yule anayeukubali (Uimamu wa) Amiri-l-Muminiyn lakini anakataa yeyote kati ya mmojawapo wa Maimamu, ya kuwa ni sawa na yule anayeamini Manabii wote lakini anakataa Unabii wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Maimamu baada yangu ni kumi na mbili. Wa kwanza ni Amirul-Muminiyn ‘Aliy ibn Abi Twaalib na wa mwisho ni Qa’im (Mahdi). Utiifu Kwao ni utiifu kwangu, na kutowatii wao ni kutonitii mimi. Hivyo yeyote amkataaye mmoja wao amenikataa mimi”.

 

Yeyote anayefanya kosa la kudai Uimamu ni dhalimu aliyelaaniwa. Yeyote atakayeweka Uimamu pahala pasipo hifadhi yake ni dhalim aliyelaaniwa. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema “Yeyote atakayemnyima ‘Ali Uimamu baada yangu atakuwa amekanusha Unabii wangu, na yeyote atakayeukanusha Unabii wangu atakuwa ameukanusha Uungu wa Allaah.” Imam Ja’far as Swaadiq amesema: “Yeyote atakayeshuku ukafiri wa maadui zetu basi yeye mwenyewe atakuwa ni kafiri.”3

 

Mwanafunzi wake Shaykh Mufid (aliyefariki 413 AH) ameandika:

Wameafikiana miongoni mwa Maimamu (Ithna ‘Ashari au Ja’fari Shia) ya kwamba yeyote atakayekataa Uimamu wa yeyote kati ya Maimamu, na akakataa wajibu wa kuwatii ambao umeamrishwa na Allaah, mtu huyo atakuwa ni kafiri, amepotea, na anastahiki adhabu ya kudumu Motoni (Jahanam).4

 

Abu Ja‘far at-Tusi, alimtaja Shaykh at-Ta’ifah, (aliyefariki 460AH), ambaye ni mwandishi wa vitabu viwili kati vitabu vinne vya hadith vinavyotegemewa na Mashia, alikuwa na hili la kusema:

Kutoukubali Uimamu ni Ukafiri, kama vile ambavyo kutoukubali Unabii ni ukafiri.5

 

Yule aliyeupa nguvu Ushia katika karne ya nane baada ya Hijra, Ibn Mutahhar al-Hilli (aliyefariki 726AH) alielezea maoni yanayofanana kama ifuatavyo:

Uimamu ni rehema ya wote (lutf ‘aam) wakati Unabii ni rehema maalum (lutf ‘khaas), kwa sababu inawezekana ya kuwa katika muda makhsusi pasiwepo na Nabii, na hili halipatikani kwa Maimamu (haiwezikani kutowepo Imamu katika zama fulani). Kukataa rehema ya wote ni mbaya zaidi kuliko kukataa rehema maalum.6

 

Rai hii ndiyo inayoshikiliwa na wanavyuoni wanne maarufu wa Kishia, na tukiitazama kwa mtazamo wa msimamo, ni rai iliyopendekezwa sana. Lakini ukimuuliza Mshia wa leo (haswa wale walioingia Ushia siku za karibuni) kama wanaamini Masunni ni Waislamu au la, watakutazama kwa mshangao, hata wanaweza kuonyesha hasira kwa kwa kuulizwa swali kama hilo. Ama kuhusiana na walioingia Ushia hivi karibuni, hili linatarajiwa kwao, kwani ni juu ya propaganda yoyote ile baadhi ya hoja ziwe ni siri kwa wafuasi wapya. Ama kwa wale wenye elimu ya ufundi wa kishia, wanajua mbele ya Mashia kuna tofauti kati Muslim na Mu-umin. Watu wote wenye kuukubali Uislamu kidhahiri ni Waislamu: Masuni, Mazaydiya, Mu`tazila, na madhehebu yote mengine. Ama Muumini ni yule tu ambaye anayeamini Maimamu Kumi na mbili. Kwa ujanja wao huu Mafuqahaa wa Kishia wanawaua ndege wengi kwa jiwe moja. Kwa kuyakubali madhehebu yote kuwa ni Waislamu, wanajilinda wenyewe dhidi ya istihizai ya kuwatoa 90% ya waumini wao nje ya Uislamu, na wale walioutawanya Uislamu katika kona nne za ardhi. Na wakati huo huo wanaepusha uhasama na Massuni na wengineo, na inawasaidia katika kuwapata wafuasi wapya. Kwa upande mwingine, kwa kutumia uerevu wa kupambanua kati ya Muislamu na Muumini wanatekeleza azma ya kuwatenga wapinzani wao. Muislam ni yule ambaye anahukumiwa kwa sheria ya kiislamu hapa duniani tu. Inaruhusiwa kuoana nao, kuswali nyuma yao, kula machinjo yao n.k., ambapo Wauumini ni wale ambao uokozi utakuwa ni wao tu huko akhera, na hili litapatikana tu kwa mtu kuwa na imani juu ya Maimamu Kumi na mbili. Upambanuzi huu kati ya Muislamu na Muumini unaweza kupatikana popote katika maandiko ya Kishia. Faqihi wa karne ya saba Yahya ibn Sa‘id al-Hilli (aliyefariki 690AH), kwa mfano ameandika katika kitabu chake cha fiqhi, al-Jami‘ lish-Shara’i‘:

 

Ni sawa kwa Muislamu kutoa wakfu (waqf) kwa Waislamu. Waislamu ni wale ambao wanatamka shahada mbili, na watoto wao. Lakini mtu akiazimia wakfu kwa Muumini, itakuwa ni khaswa kwa wenye itikadi ya Uimamu wenye kuamini Maimamu Kumi na mbili.7

 

Karne nane baadaye, mtazamo kama huu unaletwa tena na Khomeini. Katika kitabu chake cha fiqhi, Tahrir al-Wasilah anasema:

“Kama mtu akitoa wakfu kwa Waislamu itakuwa ni haki ya wote wale wenye kutoa shahada mbili … kama waumini waki-Imamia wakitoa wakfu kwa Muumin wakfu huo utakuwa ni kwa Ithna ‘Ashariya pekee.”8

 

Baadhi kati ya wazungumzaji wa Kishia, kama vile Kashif al-Ghita, wameonelea hata huo uerevu pekee hautoshelezi. Hivyo amevumbua namna nyingine ya kuelezea. Anazungumza kuwepo kwa Muumini maalum, na Muumini wa kawaida. Yeyote atakayeamini Maimamu atatambulikana ya kuwa ni Muumini maalum, na wale wasioamini watatambulikana ni Waumini wa kawaida, matokeo yake ni kuwa zile sheria zote za Kiislamu hapa duniani zitatumiwa juu yao. Upambanuzi wa tofauti hizi utabainika Siku ya Kiyama, kulingana na hadhi, ukaribu wa utukufu na heshima watakayopewa wale wenye kuuamini Uimamu.9

 

Kwetu inatubainishia zaidi ya mtunzi alivyokusudia, kuwa pale Mshia asemapo Masunni ni Waislamu, anamaanisha ni wa hapa duniani tu. Katika masuala ya kesho akhera, Masuni wasioamini Maimamu Kumi na mbili ni kama Mayahudi, Wakristo, Mabudha, Mabaniani au kama wengine wowote wenye kuukataa Unabii wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Sababu pekee ya kusema Masuni ni Waislamu ni kwa lengo na manufaa yao. Bila ya kubeba rai hii Mashia wangeingia mafichoni na kutengwa na jamii yote ya Kiislamu duniani. Sababu hii imetolewa na Sayyid ‘Abdullah Shubbar (aliyefariki 1232AH) katika maelezo ya az-Ziyarat al-Jami‘ah,

Kitabu cha dua kinachosomwa kwenye ziara za makaburi ya Maimamu. Katika sehemu ya ziara inasomeka hivi:

“Yeyote akukataaye ni kafiri”

anatoa maelezo juu yake, akisema:

Kuna hadithi nyingi zinaonyesha wapinzani kuwa ni makafiri. Kuziandika zote kunahitajia kitabu kingine. Kulinganisha hizi hadithi na vile ijulikanayo kuhusu Maimamu, yaani walikuwa wakiishi, wakila na walishirikiana nao kijamii, kunatupelekea kuhukumu ya kuwa wao (wapinzani) ni makafiri, na wataingia motoni milele, lakini katika hii dunia sheria ya kiislamu itatumika juu yao kama ishara ya huruma na fadhila kutoka madhehebu ya kweli (Mashia), kutokana na kwamba haiwezekani kuepukana nao.10

 

 

Utaratibu Wa Madaraka Wa Maimamu

Kwenye nukta hii itatosheleza tukisema Mashia wamewatwika Maimamu wao ukamilifu na ufanikishaji wa Manabii na hata zaidi yao. Haiwezekani kuziandika hadithi zote hapa ambazo zinahusiana na hadhi ya Maimamu, lakini itatosheleza tukitaja milango ambamo zimetajwa sifa zao katika kitabu kilichoelezewa ya kuwa “Ukweli wa taarifa ya elimu ya Maimamu”. Bihaar al-Anwaar ya Mwanachuoni Muhammad Baqir al-Majlisi (aliyefariki 1111AH), kinachotambulikana kuwa ni kitabu maarufu kilichowaathiri wasomi wa Kishia wa zama za Safwid. Wakati wa uhai wake alikuwa na wadhifa wa sheikh al-Islam katika mji mkuu Safwid ambao ni Isfahan, na hata leo hii kazi yake ni ya kutegemewa sana na wanachuoni wa Kishia na wafuasi wao. Tunakutajieni hapa majina ya milango na idadi ya Hadithi katika kila mlango:

1.     Maimamu wana elimu zaidi ya manabii (zipo hadiyth 13 kuhusiana na hili) 11

 

2.     Maimamu ni bora kuliko Manabii na kuliko viumbe vyote. Mkataba wa maimamu ulichukuliwa na Manabii, na Malaika, na viumbe wote. Wale (Mitume wakuu wajulikanao kama) ulul-‘Azm (Nuh, Ibrahim, Musa na ‘Isa) wameupata huo u- ulul-‘Azm kwa mapenzi yao juu ya Maimamu. (hadithi 88)12

 

3.     Dua za Manabii zilijibiwa kwa sababu waliomba kupitia (wasila) wa Maimamu. (zipo hadiyth 16)13

 

4.     Maimamu wanaweza kumhuisha aliyekufa. Wanaweza kumtibu kipofu na mwenye mbalanga. Wanamiliki miujiza yote ya Manabii (zipo hadiyth 4)14

 

5.     Hakuna elimu yeyote iliyoko Mbinguni, Ardhini, Peponi wala Jahanam ifichikanayo kwao. Walionyeshwa Ufalme wa Mbingu na Ardhi. Wanajua yaliyotendeka na yatakayotendeka mpaka Siku ya Kiyama. (zipo hadiyth 22)15

 

6.     Maimamu wanaujua ukweli wa imani ya mtu au unafiki wake. Wanamiliki kitabu ambacho kina majina ya wakazi wa Peponi, na majina ya wafuasi wao na yale ya maadui zao. (zipo hadiyth 4 juu ya habari hii)16

 

 

Vichwa vya habari vya milango hivi vinatudhihirishia picha wazi kuhusu hadiyth ambazo Mashia wanaegemeza imani yao. Hivyo tunaona madaraka ya Maimamu si ya kuongoza ummah pekee. Maimamu si viongozi wa kidola wenye haki ya utukufu wa utawala pekee. Wao ni wenye kumiliki nyanja zote za kielimu na pia kumiliki ukamilifu waliokuwa nao Manabii. Kuwepo kwa dunia kunategemea kuwepo kwao. Wao ndio njia ya maombi yetu kukubaliwa na hata maombi ya Manabii. Kutokana na hili mtu anaweza kufahamu sababu ya Khomeini kuandika jumla hii katika kitabu al-Hukumat al-Islamiyyah, ambacho falsafa ya mapinduzi yanakitegemea:

Haiwezi kukanushwa ya kuwa ni mafundisho ya imani yetu kuwa Maimamu wetu wana hadhi mbele ya Allaah ambayo hakuna Malaika wala Mtume anaweza kuipata.17

Baada ya utangulizi huu juu ya fikra ya Uimamu, utaratibu wa uteuzi wa Maimamu na namna waendeshavyo madaraka yao, tunauliza swali: Je, imani kuhusu fikra hii imethubutu na kuungwa mkono na Qur-aan? Ukweli ni kwamba imani yenye msukumo, wa ibara ya imani yenye matokeo, ambayo ni bora zaidi kuliko Manabii, ni lazima machimbuko yake yametokana ndani ya Qur-aan. Kitabu ambacho kimeteremshwa na Allaah:

Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinachobainisha kila kitu, na ni uongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu (an-Nahl:89)       

Na ni kwa lengo la kujibu swali hili makala haya yameandikwa.

 

 

Uimamu Na Unabii Ndani Ya Qur-Aan

Ndani ya makala haya tunachunguza kwenye Qur-aan misingi ya Kishia kuhusu fikra ya Uimamu. Kwa kutafiti utumikaji wa neno Imamu (imaam) na uwingi wake Maimamu (a-immah) ndani ya Qur-aan na tutachunguza kama Qur-aan inatoa msingi wowote kuhusu nadharia ya Uimamu kama ilivyoelezwa na pote la Kishia.

 

Kwa uchunguzi wetu kuhusu Qur-aan tu, si kwamba Sunnah haina athari yeyote kuhusu nadharia hii. Isipokuwa, ni kule kutaka kutoa shaka ya kuwa nadharia kama ya Uimamu, ambayo imani ya Kishia inaiweka juu ya Manabii, lazima ipatikane maandiko kwenye Qur-aan. Isitoshe suala linalofuatia baada Uimamu nayo ni Unabii lina dalili ya kutosha ndani ya Qur-aan. Hakuna mtu yeyote baada ya kusoma Qur-aan iliyo wazi na isiotatanisha ambapo Allaah Anawataja Mitume na Manabii Wake, na hadhi zao,

Na wote tuliwafadhilisha juu ya walimwengu wote (al-An‘aam: 86)

 

Visa vyao,

Na je! Imekufikia hadithi ya Musa? (Twahaa: 9)

Na wasomee khabari za Ibraahiym. (ash-Shu'araa: 69)

Sisi Tunasimulia simulizi nzuri kwa kukufunulia Qur-aan hii (Yuusuf: 3)

 

Majina yao yanatajwa kwa uwazi,

Na hizo ndizo hoja Zetu Tulizompa Ibraahiym kuhojiana na watu wake. Tunamnyanyua kwa vyeo Tumtakaye. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwenye hekima na Mwenye ujuzi. Na Tukamtunukia (Ibrahim) Is-haaq na Ya'aquub. Kila mmoja wao Tulimwongoa. Na Nuuh Tulimwongoa kabla. Na katika kizazi chake Tulimwongoa Dawuud na Sulaymaan na Ayuub na Yuusuf na Musa na Haaruun. Na hivi ndivyo Tunavyo walipa wafanyao wema. Na Zakariya na Yahya na 'Iysa na Ilyaas. Wote walikuwa miongoni mwa watu wema. Na Isma'iyl, na Al Yasaa, na Yuunus, na Luut. Na wote Tuliwafadhilisha juu ya walimwengu wote.  (al-An‘am : 83-86)

 

na umuhimu wa kuwaamini kama sehemu ya imani ya Kiislamu,

Na anayemkataa Allaah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Mitume Wake, na Siku ya Akhera, basi huyo amekwisha potelea mbali. . (an-Nisaa : 136)

 

Hatuna shaka yoyote ya kuwa Qur-aan inatilia mkazo, au inaamrisha, imani juu ya Manabii. Swali sasa ni: Je, tunaweza kusema vivi hivi juu ya Uimamu? Ikiwa Uimamu ni bora kuliko Unabii, kama ifundishavyo itikadi ya Shia Ithna ‘Ashari, ni mategemeo yetu tudhaniye Qur-aan itazungumzia kwa uwazi juu ya Uimamu; na ikiwa si hivyo, basi hata picha iliyo wazi pasi na utatanishi juu Uimamu ni nini na ni nani hao Maimamu, itapatikana ndani ya Qur-aan.

 

 

Matumizi Ya Neno Imamu Ndani Ya Qur-aan

Kinachofuata ni uchunguzi wa jinsi neno Imaam na wingi wake A-immah lilivyotumika ndani ya Qur-aan. Namna Allaah Alivyolitumia ndani ya Qur-aan itaangaliwa kama fikra ya Kishia kuhusu Uimamu tulivyoelezea hapo juu inapata kigezo chochote ndani ya Qur-aan.

 

 

Kitabu

Neno Imaam linajitokeza mara 7 ndani ya Qur-aan, wakati wingi wake, A-immah, linajitokeza mara 5. Mara 3 ya hizo inaelezea kwa uwazi ya kuwa ni Kitabu.

Na kabla yake kilikuwa Kitabu cha Muusa kilichokuwa mwongozi na rehema. (Huud: 17)

Na kabla yake kilikuwapo Kitabu cha Muusa, kuwa chenye uongozi na rehema. (al-Ahqaaf: 12)

Hakika Sisi Tunawahuisha wafu, na Tunaziandika zile amali zao wanazozifanya zikawacha taathira zao nyuma. Na kila kitu Tumekihifadhi katika daftari (Letu) linalobainisha (kila kitu). (Yaasiyn: 12)

 

 

Mabigwa Wa Ukafiri

Katika sehemu 2 inaelezea mabingwa wa ukafiri;

Basi piganeni na waongozi wa ukafiri. (at-Tawbah: 12)

 

Na tuliwafanya ni waongozi waitao kwenye Moto. (al-Qaswas: 41)

 

 

Njia

Na nchi mbili hizi ziko kwenye njia iliyo wazi. (al-Hijr: 79)

                                                                                      

 

 

Vongozi Wa Wana Wa Israeli

Sehemu sita zilizobakia ambapo neno linatumika, linatumika kwa maana yake haswa. Nayo ni uongozi. Katika Surah al Anbiyaa imeelezea:

Sisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibraahiym! Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi Tukawafanya wao ndio waliopata khasara. Na Tukamwokoa yeye na Luut Tukawapeleka kwenye nchi Tuliyoibariki kwa ajili ya walimwengu wote. Naye Tukampa Is-haaq, na Yaaqub kuwa ni ziada. Na wote Tukawajaalia wawe watu wema. Na Tukawafanya Maimamu wakiongoa watu kwa amri Yetu. Na Tukawafunulia watende kheri, na washike Swalah, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu. (al-Anbiyaa: 69-73)

 

Katika aayah hii, ambayo inabidi tuipanue ili msomaji aweze kuona maana kamili ya neno a-immah lilivyotumika, mtu ataona uhusiano ulio wazi ya kuwa Nabii ni kiongozi wa watu, anayewaongoza ummah wake kumjua Mola wao. Huku kuweka wazi kusiko na maana nyingine ya kuwa a-immah hapa ni Manabii kunatupelekea tuseme aayah hii katika Surah as-Sajdah, inaelezea Manabii na wala si aina nyingine ya watu.

Hakika Sisi Tulikwishampa Musa Kitabu. Basi usiwe na shaka kuwa kakipokea. Na tukakifanya kuwa ni uongofu kwa Wana wa Israili. Na Tukawafanya miongoni mwao waongozi wanaoongoa watu kwa amri Yetu, waliposubiri na wakawa na yakini na Ishara Zetu. (as-Sajdah: 23-24)

 

Hata kama tukilipanua neno a-immah katika aayah hii tuwaingize watu wasio kuwa Manabii, hakuna kinachojuzisha utambulisho wa kiundani kuhusu nadharia ya Uimamu kama inavyoeleweka na Mashia.

 

Katika aayah hii ya tatu Allaah Anazungumza mipango yake kuhusu wana wa Israeli waliodhoofishwa nchini Misri:

Na Tukataka kuwafadhili waliodhoofishwa katika nchi hiyo na kuwafanya wawe waongozi na kuwafanya ni warithi.  (al-Qaswas: 5)

 

Ili tuone neno a-immah lina uhusiano gani ndani ya aayah hii, mtu anatakiwa aangalie ni nani wale ambao waliotimiziwa bishara hii. Wa kwanza alikua ni Nabii Musa na halafu Manabii-Wafalme wa Kibanii Israeli kama vile Nabii Dawuud na Nabii Sulaymaan (‘Alayhimus salaam), kwa hiyo huo ndio uongozi unaowakusudia katika aayah hii ambao ndio waliokuja kabidhiwa. Kama kuna nyakati walitawaliwa na wasio kuwa Manabii, hadhi ya hao viongozi haikuwa bora kuliko daraja ya Manabii. Aayah kama hizo tatu hapo juu, mbali ya kuwa zinahusiana tu na Manabii wa wana wa Israeli, hazitoi dalili yoyote zionyeshazo kupatikana daraja ya Uimamu kama ielewekavyo na Mashia.

 

 

Kiongozi Wa Watu

Na Mola wake Mlezi Alipomjaribu Ibrahiym kwa kumpa amri fulani, naye akazitimiza, Akamwambia: Hakika Mimi nitakufanya uwe Kiongozi wa watu. Akasema: Je, na katika vizazi vyangu pia? Akasema: Ahadi yangu haitawafikia wenye kudhulumu. (al-Baqarah: 124)

Aayah hii haihitaji maelezo ya ziada inatubainikia wazi Kiongozi aliye kusudiwa ni Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam)

 

 

Viongozi Wa Wacha Mungu

Na wale wanaosema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe Viongozi kwa wacha Mungu. (al-Furqaan: 74)

Aayah hii inazungumzia watu wa kawaida ambao hawapo katika daraja kama ya Manabii, wanamuomba Allaah Awafanye Maimamu, wakimaanisha mfano bora wa wema, ambao mfano huo wengine watajitahidi kuiga. Inaonyesha wazi kabisa haimaanishi “Maimamu walioteuliwa kwa wahyi”, kwa sababu ya kwamba Maimamu kutawazwa kwao mpaka kufikia daraja ya Uimamu si kwa ajili ya ibada zao. Ni kwamba uteuzi wao, kama ule wa Manabii, inatarajiwa ni wa ki-wahyi kwa chanzo chake, na hili halipatikani kwa kiasi chochote cha ibada.

 

Ni jambo la kupendeza kuona aayah hii ilikuwa tonge gumu kumeza kwa baadhi ya Mashia wa zamani kiasi ikawapelekea kusema kuwa aayah hii imepotoshwa. Hadithi hii inapatikana kwenye tafsiyr ya ‘Ali ibn Ibrahim al-Qummi, mwalimu wa Abu Ja‘far al-Kulayni:

Ilisomwa kwa Abu ‘Abdillah (yaani Imam Ja‘far as-Swaadiq):

…na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamungu.

Akasema: “Ni jambo kubwa sana kwao kumuomba Allaah Awafanye wawe Maimamu wa wacha Mungu.” [Itikadi ya Kishia ikikusudiwa, hivyo inaeleweka, Maimamu wanachaguliwa, Na haiwezekani kuupata Uimamu kwa kuuomba.]

Kisha mtu akamuuliza; “Ni vipi aayah hii ilivyoteremshwa, ewe mtoto wa Mtume wa Allaah?”

Akajibu : Iliteremshwa:

…na utuujalie kwetu viongozi miongoni mwa wacha Mungu.18

 

Hadithi hii imeorodheshwa katika tafsiri miongoni mwa tafsiri za mwanzoni zenye kutegemewa na Mashia (tafsiri ambayo imeelezewa na mhariri wa karne ya ishirini ya kuwa “Ama kwa uhakika ni maoni ya Imamu al-Baqir na Swaadiq,"19 na kila mmoja wa wapokezi wake ni wenye kutegemewa na wataalam wa hadithi wa Kishia,20 ambao wameithibitisha kwa vipimo vya Kishia) na hii inaondosha haja ya kuingia mjadala katika maana ya neno Imamu kama ilivyo katika aayah hii.

 

 

Katika Siku Ya Qiyaamah

Hivyo imetubakia sehemu moja ndani ya Qur-aan ambapo neno Imamu limetumika. Ipo ndani ya Surah al-Israa ambapo Allaah Amesema:

Siku Tutapowaita kila kikundi cha watu kwa mujibu wa wakifuatacho (al-Israa: 71)

 

Imamu aliyezungumziwa ndani ya aayah hii anatambulika kulingana na wafasiri wa ki-Ahlus-Sunnah ni aidha kitabu cha matendo au Mtume ambaye ni wa zama za wafuasi. Maana ya kwanza ndio yenye kupendelewa na Ibn Kathiyr,21 ambaye amesema haya kwa kuegemezea na aayah ambazo zimetumia Imamu kama kitabu (tazama hapo juu). Maana hii inapewa uzito na sehemu iliyobakia katika aayah hii:

Basi watakaopewa daftari zao kwa mikono ya kulia, basi hao watasoma daftari zao (kwa furaha) wala hawatadhulumiwa hata chembe. (al-Israa: 71)

 

Maana ya pili pia inaungwa mkono vya kutosha ndani ya Qur-aan. Katika aayah nyingine Allaah Anasema:

Basi itakuwaje pindi Tukiwaletea kutoka kila umma shahidi, na Tukakuleta wewe kuwa shahidi wa hawa? (an-Nisaa: 41)

 

Kutokana na namna ya wadhifa wa Nabii (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) unavyolinganishwa na wadhifa wa “Mashahidi” wa Ummah zingine tunaweza tukasema mnasaba wa aayah hii ni wa Manabii. Hivyo inafuatia kwamba Ummah zote wataitwa kwa majina ya Manabii wao. Ummah zilizotangulia kuitwa kwa majina ya Manabii waliotumwa kwao ni kitu cha kawaida katika Qur-aan na Sunnah. Kwa mfano ‘Aad waliitwa kama “watu wa Huud”, kama vile Wana wa Israeli waliitwa “watu wa Musa”. Kumtambulisha Imaam aliyetajwa ndani ya aayah hii inayojadiliwa na Nabii ni jambo lililoruhusiwa na Qur-aan na Sunnah.

 

Ama kwa madai ya Mashia ya kwamba inaelezea Maimamu Kumi na mbili22 madai haya mbali ya kutokuwa na ushahidi ndani ya Qur-aan yananapunguza jumla ya uwezo (mawanda) wa aayah hii. Kutokuwepo na ushahidi wa Qur-aan ni wazi katika mjadala hapo juu wa neno Imamu lilivyotumika ndani ya Qur-aan. Ufinyu wa jumla ya uwezo wa aayah hii unatokana na tofauti ya mpangilio baina wakati walioishi Maimamu Kumi na mbili, na ule wakati Ummah zilizotangulia. Kama tukisema Ummah zote zitaitwa kwa majina ya Maimamu Kumi na mbili, vipi kuhusu Ummah zilizokuwepo kabla yao? Wataitwa kwa jina la nani? Ingawaje, aayah inasema watu wote wataitwa kulingana na viongozi wao.

 

Tukitia nyongeza, hebu na tuseme aayah hii ina maana ya Maimamu Kumi na mbili, hivyo itatuacha na hali isiyokubaliana. ‘Aliy (radhiya Allaahu ‘anhu), Imamu wa kwanza alifariki katika mwaka wa 40. Mwanawe l Hasan (radhiya Allaahu ‘anhu) alifariki miaka tisa baada yake, mwaka wa 49. kama ‘Ali (radhiya Allaahu ‘anhu) ni Imamu wa watu wa wakati wake, l Hasan (radhiya Allaahu ‘anhu) atabakiwa na watu wale waliozaliwa katika kipindi chake cha miaka tisa. Watu wote waliokuwa hai katika kipindi cha utawala wa baba yake watakuwa ni wafuasi wa baba yake na si wafuasi wake. Utawala wa Imamu wa 3 ulidumu kwa miaka 22; Imamu wa 4 ulidumu miaka 34; wa 5 miaka 19; wa 6 miaka 34; wa 7 miaka 35; wa 8 miaka 20; wa 9 miaka 17; wa 10 miaka 34 na wa 11 miaka 6, Ama Imamu wa 12 Mahdi anayengojewa, ana utawala ambao sasa uko kwenye miaka 1200. Tukitoa mfano, kundi litakaloitwa kwa jina la Imamu wa kumi na mbili , kundi hili litajumuisha wale waliozaliwa wakati wa utawala wa Uimamu wake ambao ulikuwa mwaka wa 254 mpaka 260, ambapo idadi ya wale wakatakaoitwa kwa jina la Imamu wa kumi na mbili itakuwa haina hesabu.

 

Linganisha hali ya mapishano haya na ule mpangilio na mfumo wa Qur-aan wa kuwa Umma zote wataitwa kwa majina ya Manabii wao Siku Ya Kiyama, na ule upuuzi wa kutumia aya 71 katika Sura al-Isra’ kuthibitisha itikadi ya Uimamu kama inavyodaiwa na Mashia uwazi utakubainikia. Hapana shaka ya kuwa neno Imamu katika aayah hii halielezei Maimamu Kumi na mbili.

 

 

MUKHTASARI

Tumejadili hapa kila pahala ndani ya Qur-aan ambapo neno Imaam na wingi wake A’immah lilivyotumika ndani ya Qur-aan. Imeoonyeshwa namna gani Allaah Ta’ala Alivyotumia neno hili Akimaanisha mara kuwa ni:

Kitabu (mara tatu)

Mabingwa wa ukafiri ( mara mbili)

Njia ( mara moja)

viongozi wa wana wa Ki-Israeli (mara tatu)

Kiongozi wa Watu

Viongozi wa wacha Mungu

Manabii au Kitabu

 

Majaribio yoyote ya Mashia kulinganisha hoja ya Uimamu na ule Uimamu wa Qur-aan haviendani kabisa. Kile wanachoweza kufanya ni kuchukua uwiano kati ya Maimamu wao na viongozi wa Kisraeli. Ingawaje uwiano huo utakanushwa papo hapo mtu akikumbuka ya kuwa uongozi huu unaonyeshwa wazi ndani ya Qur-aan kuwa ni Manabii wa Wana wa Ki-Israeli. Qur-aan haitoi nafasi yoyote kabisa kuutambulisha uongozi wa Wana wa Ki-Israeli na yeyote isipokuwa Nabii. Si ajabu kumpata Mshia akitaja aayah ya 5 ya Sura al-Qaswas kuthibitisha itikadi yao ya Uimamu. Kama wangelichukuwa taabu ya kusoma aayah kikamilifu bila ya kuongeza ziada ya itikadi yao, wataona ya kuwa haviendani. Kwa mfano katika al-Qaswas:5 inaelezea kwa uwazi ni Mtume Musa (‘Alayhis salaam) na watu wake. Ni mshangao ulioje kuona aayah hiyo Mashia wanadai kuwa inamuelezea ‘Aliy ibn Abi Twaalib (radhiya Allaahu ‘anhu) na Maimamu kumi na moja kutoka katika kizazi chake.

 

Majaribio ya kuleta uwiano kati ya Uongozi ndani ya Qur-aan wa wacha Mungu na ule Uimamu wa Kishia kadhalika umejaa matatizo. Imeonekana ya kuwa aina ya uongozi huu ni fadhila inayoombwa kutoka kwa Allaah na waja wake wema. Uimamu wa Kishia kwa Mashia, kwa upande wao ni kama Manabii, wanatawazwa kwa wahyi, na hawezi mtu kuomba akaupata. Kukosekana kwa mpangilio baina ya aina ya Uongozi na Uimamu wa Kishia hakukubainika wazi kama vile ulivyoletwa na hadithi sahihi iliyopokelewa kutoka kwa  Imamu Ja‘far as-Swaadiq ambayo inasema ya kuwa Qur-aan imepotoshwa ndani ya mikono ya Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) ndio sababu ya tofauti.

 

Maana pekee iliyobakia ndani ya Qur-aan ya neno Imamu kwa Mshia ni ile aayah inayoashiria Siku Ya Kiyama, wakati kila umma itakapoitwa kwa “viongozi” wao. Je inawezekana hapa neno “Imamu” kumaanisha itikadi ya Uimamu? Nawasikitikia Mashia kuwa hiyo haiwezekani, kwa mara nyingine tena haiwezekani. Haiwezekani, kwa sababu mbili:

 

Kwanza, sababu ikisomwa kwa ujumla aayah zinazotangulia kabla ya aayah yenyewe, pamoja na aayah zingine za Qur-aan zinalenga bila makosa ya kuwa Imamu anayekusudiwa hapa ni Nabii, ambaye kwa jina lake watu wake wataitwa Siku Ya Kiyama, na hata ndani ya Qur-aan na Sunnah pia, au kwenye vitabu vyao vya amali zao ambao wao watakuwa wenye kuulizwa.

 

Pili, ni kwa sababu ya kuitambulisha aayah na itikadi ya Mashia ndio kunatupelekea kwenye tatizo kubwa la ugawanyikaji wa ummah wa Maimamu kwa kila mmoja wao, yaani kila Imamu awe na ummah wake!

 

Kwa kukhitimisha, utumikaji wa neno “Imaam” ndani ya Qur-aan, hakupatikani kitu chochote kabisa cha kuelezea imani ya Uimamu kama ielewekavyo na Mashia.

 

___________________________

MAREJEO

1. Asl ash-Shi‘ah wa-Usuluha uk. 58 (Mu’ssasat al-A‘lami, Beirut)

2. al-Kafi mjalada. 8 (Rawdat al-Kafi) uk. 167 (Dar al-Adwa’, Beirut, 1992)

3. Risalat al-I‘tiqad uk. 111-114, imenukuliwa na al-Majlisi: Bihar al-Anwar mjalada. 27 uk. 62 (Dar al-Kutub al-Islamiyyah, Tehran, 1387)

4. al-Masa’il, imenukuliwa ndani ya Bihar al-Anwar mjalada. 8 uk. 366

5. Talkhis ash-Shafi mjalada. 4 uk. 131 (Dar al-Kutub al-Islamiyyah, Qum, toleo la 3. 1394)

6. al-Alfayn uk. 3 (al-Maktabah al-Haydariyyah, Najaf, toleo la 3. 1388)

7. al-Jami‘ lish-Shara’i‘ uk. 371 (Mu’assasat Sayyid ash-Shuhada’ al-‘Ilmiyyah, Qum, 1405)

8. Tahrir al-Wasilah mjalada. 2 uk. 72 (Mu’assasat Isma‘iliyan, Qum 1408)

9. Asl ash-Shi‘ah wa-Usuluha uk. 58-59

10. al-Anwar al-Lami‘ah Sharh az-Ziyarat al-Jami‘ah uk. 176 (Mu‘assasat al-Bi‘thah, Mashhad, toleo la 1. 1457)

11. Bihaar al-Anwaar mjalada. 26 uk. 194-200

12. Kitabu hicho hicho, mjalada. 26 uk. 267-318

13. Kitabu hicho hicho, mjalada. 26 uk. 319-332

14. Kitabu hicho hicho, mjalada. 27 uk. 29-31

15. Kitabu hicho hicho, mjalada. 26 uk. 109-107

16. Kitabu hicho hicho, mjalada 26 uk. 117-132

17. al-Hukumat al-Islamiyyah uk. 52 (Wizara ya Uongozi, Iran)

18. Tafsir (‘Ali ibn Ibrahim) al-Qummi mjalada 1 uk.  10 (ed. Sayyid Tayyib al-Musawi, toleo la 2, Kitabfarosh ‘Allameh, Qum 1968)

19. Tafsir (‘Ali ibn Ibrahim) al-Qummi, utangulizi wa mhariri.

20. Abu Talib at-Tajlil at-Tabrizi: Mu‘jam ath-Thiqat uk. 224 (Mu’assasat an-Nashr al-Islami, Qum 1404AH). Ndani ya kitabu hiki mtunzi anaorodhesha idadi ya wapokezi wa hadithi wenye kuaminika wa Kishia. Moja kati ya alikonukuu ni kwenye tafsiri ya al-Qummi. Katika ibara ya tatu ndani ya kitabu hiki anatoa orodha ya wapokezi wa hadithi ambao al-Qummi amewategemea katika kunukuu khabari zilizopo ndani ya tafsiri yake, akitaja kauli ya al-Qummi kwenye utangulizi wa kitabu chake isemayo “tutataja na kuwajulisha kile ambacho kilichotufikia, ambacho washauri wetu na wapokezi wenye kuaminika walivyotunukulia”. Kisha anamnukuu mtunzi wa Wasa’il ash-Shi‘ah ambaye amesema kuwa “Ali ibn Ibrahim al-Qummi anashuhudia ya kuwa tafsiri yake imepokelewa kutoka kwa Maimamu na wapokezi wenye kuaminika. (Wasa’il mjalada 3 uk. 524)

21.Tafsir Ibn Kathir mjalada 3 uk.  52 (Maktabah Dar at-Turath, Cairo)

22. Ndani ya mjalada wa kwanza wa al-Kafi aya hii imetumika mara tatu kuhusiana na Maimamu.

 

 

Share