002-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Usharia Wa Kiapo

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

02- Usharia Wa Kiapo

 

 Alhidaaya.com

 

 

 

Usharia wa kiapo umethibiti katika Qur-aan, Sunnah na Ijma’a.

 

1-  Katika Qur-aan, ni Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَلَا تَنقُضُوا الْأَيْمَانَ بَعْدَ تَوْكِيدِهَا"

 

“Na wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha.  [An-Nahl (16:91)].

 

Na Neno Lake:

 

"قدْ فَرَضَ اللَّـهُ لَكُمْ تَحِلَّةَ أَيْمَانِكُمْ"

 

“Allaah Amekwishakufaridhishieni ukomboaji kwa viapo vyenu”.  [At-Tahriym (66:2)].

 

Na Allaah ‘Azza wa Jalla Amemwamuru Nabiy Wake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aape katika mwahala patatu katika Kitabu Chake.  Akasema:

 

"وَيَسْتَنبِئُونَكَ أَحَقٌّ هُوَ ۖ قُلْ إِي وَرَبِّي إِنَّهُ لَحَقٌّ"

 

53.  Na wanakuuliza:  Je, hiyo (adhabu na Qiyaamah) ni kweli?   Sema:  Ndio!  Naapa kwa Rabb wangu!  Hakika hiyo bila shaka ni kweli.  [Yuwnus (10)]. 

 

Na:

 

"قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتَأْتِيَنَّكُمْ"

 

“Sema:  Bali la!  Naapa kwa Rabb wangu!  Bila shaka itakufikieni”.  [Sabai (34:3)].

 

Na:

 

"قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ"

 

“Sema:  Bali hapana!  Naapa kwa Rabb wangu, bila shaka mtafufuliwa”.  [At-Taghaabun (64:7)].

 

2-  Na katika Hadiyth, ni neno lake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

" وَالَّذِيْ نَفْسُ مُحَمَّدٍ بِيَدِهِ إِنِّي لأَرْجُو أَنْ تَكُونُوا نِصْفَ أَهْلِ الْجَنَّةِ"

 

“Naapa kwa Ambaye nafsi ya Muhammad iko Mkononi Mwake, hakika mimi kwa yakini ninatumai mtakuwa nusu ya watu wa Peponi”.  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6528) na Muslim (221)].

 

Na neno lake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

" فَوَالَّذِيْ لَا إِلَهَ غَيْرَهُ إِنَّ أَحَدَكُمْ لَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ الْجَنَّةِ حَتَّى مَا يَكُونُ بَيْنَهُ وَبَيْنَهَا إِلَّا ذِرَاعٌ فَيَسْبِقُ عَلَيْهِ الْكِتَابُ ...."    

 

“[Basi naapa kwa Ambaye hakuna mungu mwingine ila Yeye tu], hakika mmoja wenu atakuwa akifanya ‘amali ya watu wa Peponi mpaka ikafikia kati yake na Pepo kubakia dhiraa moja, na hapo yaliyoandikwa azali yakamtangulia..”.  [Hadiyth Swahiyh.  Muslim ameikhariji kwa tamko hili (2643), na At-Tirmidhiy (2137).  Na kwa Al-Bukhaariy haina tamko la kiapo (3208)].

 

Na neno lake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

"مَا بَالُ أَقْوَامٍ يَتَنَزَّهُونَ عَنِ الشَّىْءِ أَصْنَعُهُ، فَوَاللَّهِ إِنِّي لأَعْلَمُهُمْ بِاللَّهِ وَأَشَدُّهُمْ لَهُ خَشْيَةً"

 

“Wana nini watu hawa wanaacha jambo ninalolifanya?  Basi naapa kwa Allaah, hakika mimi kwa yakini ndiye nimjuaye zaidi Allaah kuliko wao, na ndiye mwenye kumwogopa zaidi kuliko wao”.  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6101) na Muslim (2356)].

 

Toka kwa Ibn ‘Umar amesema: “Kiapo cha Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kilikuwa:

 

"لاَ وَمُقَلِّبِ الْقُلُوبِ"

 

“Laa, naapa kwa Mpinduaji wa nyoyo”.  [Al-Mughniy (11/160 pamoja na Ash-Sharhul Kabiyr].

 

Kuna viapo vingine vingi ambavyo tutavigusia baadhi yake katika kitabu hiki In Shaa Allaah.

 

3-  Ama kwa ‘Ijmaa, Umma wote umekubali usharia wa viapo na uthibiti wa hukmu zake.

                       

 

 

 

Share